STARTIMES RAUNDI YA 12 WIKIENDI

STARTIMES RAUNDI YA 12 WIKIENDI

January 29, 2016
Vita ya kuwania kupanda daraja msimu ujao itaendelea wikiendi hii kwa michezo 12 ya Ligi daraja la kwanza nchini (Startimes League) kuchezwa katika viwanja mbalimbali kwa makundi A, B, C, kwa kila timu kusaka pointi tatu muhimu.

Jumamosi uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, wenyeji Polisi Dodoma watakua wenyeji wa Africa Lyon, Kiluvya United wakiwakaribisha Mji Mkuu (CDA) katika uwanja wa Mabatini Mlandizi, Polisi Morogoro dhidi ya Kimondo FC uwanja wa Jamhuri, huku Kurugenzi ikiwakaribisha Burkinafaso kwenye uwanja wa Wambi mjini Mafinga.

JKT Mlale watawakaribisha Njombe Mji uwanja wa Majimaji mjini Songea, Panone dhidi ya Mbao FC uwanja wa Ushirikia Moshi, Polisi Mara watakua wenyeji wa Rhino Rangers uwanja wa Karume mjini Musoma, huku JKT Oljoro wakiwaribisha JKT Kanembwa uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Ligi hiyo ya StarTimes itaendelea siku ya Jumapili kwa michezo minne kuchezwa, Friends Rangers watakua wenyeji wa Ashanti United uwanja wa Karume, Polisi Dar dhidi ya KMC uwanja wa Mabatini Mlandizi, Lipuli wakicheza dhidi ya Ruvu Shooting uwanja wa Wambi Mafinga huku Polisi Tabora wakicheza dhidi ya Geita Gold uwanja wa Ali Hassani Mwinyi mjini Tabora.
MWILI WA SWAI KUSAFIRISHWA LEO

MWILI WA SWAI KUSAFIRISHWA LEO

January 29, 2016
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) linapenda kuwajulisha wapenzi, wadau, wa mpira wa miguu nchini kuwa, mwili wa aliyekua Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Simiyu, Epaphra Swai utaangwa leo saa 9 alasiri katika hosiptali ya Muhimbili, na baadae saa 11 jioni itaanza safari ya kuelekea mkoani Kilimanjaro.

Ibada ya kuuaga mwili wa marehemu itafanyika leo Ijumaa saa 9 alasiri katika hospitali ya Muhimbili, ambapo ndugu, jamaaa, marafiki na wadau wa mpira wa miguu nwatapana nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa marehemu Epaphra Swai, na baadae majira ya saa 11 jioni itaanza safari ya kuelekea Machame mkoani Kilimanjaro.

Mazishi ya marehemu Epaphra Swai yatafanyika kesho Jumamosi mchana nyumbani kwako Machame Kilimanjaro.

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) inatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki, wadau wa mpira wa miguu pamoja na familia ya marehemu, na kusema wako pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombelezo ya msiba huo.

Marehemu Epaphra Swai alifariki dunia jana asubuhi katika hospital ya taifa ya Muhimbili.

MGODI WA BULYANHULU WATOA ZAIDI YA MILIONI 300 KWA HALMASHAURI YA WILAYA YA NYANG'WALE KAMA USHURU WA HUDUMA.

January 29, 2016
Meneja Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu Graham Crew akiwa na wafanyakazi wengine wa Bulyanhulu Gold Mine wakikabidhi mfano wa hundi kwa kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Nyang'wale Venance Ngeleuya ,Wengine wanaoshuhudia tukio hilo ni Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale Ibrahim Marwa .

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu Graham Crew akiteta jambo na mkuu wa idara ya Mahusiano ya Jamii wa Mgodi  huo Sara Terri wakati wa hafla ya kukabidhi hundi.
Madiwani wa halmashauri ya Nyang’wale wakishuhudia makabidhiano ya hundi hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Nyangwale Venance Ngeleuya akizungumza wakati wa makabidhiano ya hundi hiyo.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu Graham Crew akizungumza na baadhi ya viongozi na madiwani wa halmashauri ya Nyang’wale (hawapo pichani)wakati wa kukabidhi hundi kwa halmashauri hiyo.
Viongozi wa Mgodi wa Bulyanhulu  wakiwa kaika picha ya pamoja na Viongozi wa seriali pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Nyang'wale.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu umekabidhi hundi yenye thamani ya Shilingi Milioni Mia Tatu Thelathini na Nne, Laki Sita na Elfu Themanini na Sita kwa Halamashauri ya Wilaya ya Nyang’wale.

Fedha hizo ni malipo ya ushuru wa huduma kwa kiwango cha asilimia 0.3 (0.3%) ya mapato ghafi ya mgodi huo kwa halmashauri ambapo Bulyanhulu inalipa kwa halamashauri ya Nyang’wale kutokana na makubaliano ya mwaka jana kwamba asilimia 35 ya malipo hayo yaende kwa wilaya hiyo na asimia nyingine kwa Halamashauri ya Msalala ambayo ndiyo mwenyeji wa Mgodi wa Bulyanhulu kwa asilimia kubwa.

Akipokea hundi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale Mheshimiwa Ibrahim Marwa amesema, “Leo wenzetu wa Mgodi wa Bulyanhulu wamefunga safari kuja kutuletea hundi ya ushuru wa huduma kwa ajili ya halmashauri ya Nyangw’ale huo ni mwanzo mzuri, sasa tumepata chanzo kizuri cha mapato kutoka mgodi wa Bulyanhulu.”
“Lakini hiyo haitoshi tukijenga mahusiano vizuri watatusaidia zaidi, kuna eneo lao ambalo kuna wachimbaji wadogo wamevamia eneo hilo na baadhi ya viongozi wanawatetea, sasa ni lazima tuwe wa kweli kwenye mambo haya ya msingi, tunataka huku ushuru halafu huku tunataka kutetea wavamizi wa eneo lao ambalo wanalimiliki kwa leseni halali ya uchimbaji, hivi mtu akija nyumbani kwako akavamia akasingizia kwamba ana njaa ivi hiyo ni sababu.”
“Tutachukua hatua za juu ili tuwaondoe wale wachimbaji waliovamia katika kijiji cha mwasabuka wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita”
Akizungumza baada ya kukabidhi hundi, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Bulyanhulu Graham Crew amesema, “Ninashukuru sana kwa ushirikiano kutoka jamii na wilaya zinazozunguka mgodi wa Bulyanhulu, nashukuru pia kuona serikali ya awamu ya nne inahamasisha hapa kazi nafikiri hilo ni jambo zuri tuendelee kushirikiana ili kwa pamoja tulete maendeleo kwa taifa zima. Ijapokuwa bei ya dhahabu imeshuka lakini mgodi wetu wa Bulyanhulu bado umejidhatiti kuhakikisha kuchangia juhudi za maendeleo ya huduma za maendeleo ya jamii kadiri itakavyowekzekana.
Malipo ya ushuru wa huduma kwa kiwango cha asilimia 0.3 (0.3%) ya mapato ghafi ya mgodi yanafuatia makubaliano kati ya Serikali na Kampuni zinazomiliki migodi husika kufanya marekebisho kwenye Mikataba ya Maendeleo ya Uchimbaji Madini (Mining Development Agreement – MDA) baina ya Serikali na Migodi ikiwemo wa Bulyanhulu, kuhusu ulipaji wa ushuru wa 0.3% ya uzalishaji kulingana na Sheria ya Local Government Finance Act, Cap.290 Revised Editions of 2002 badala ya Dola za Marekani 200,000 kwa mwaka zilizokuwa zikilipwa awali.

MTEJA AILALAMIKIA TANESCO CHARAMBE KWA KUCHELEWA KUMUWEKEA UMEME

January 29, 2016
Mteja Ambwene Kyoga


Dotto Mwaibale

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) Wilaya ya Charambe Temeke jijini Dar es Salaam limelalamikiwa na mteja wake mmoja kwa kushindwa kumfungia umeme kwa wakati licha ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Mhongo kuagiza wateja wapya kufungiwa umeme katika kipindi kifupi.

Malalamiko hayo yametolewa na mteja wa shirika hilo Ambwene Kyoga ambaye amelipa sh. 320,960 kwa ajili ya kuwekewa umeme na kupatiwa lisiti namba TDB 16841 kwa ajili ya nyumba yake iliyopo Mbagala Kuu Bucha.

Ambwene alisema sasa anaingia mwaka wa pili bado haja fungiwa umeme kwani mwaka jana mwanzoni alipeleka maombi yake ofisi za shirika hilo za Kurasini lakini alipofuatilia aliambiwa faili lake limepotea hivyo aende ofisi za Charambe ambapo alilipa fedha hizo Desemba 28 mwaka jana tangu hapo licha ya kupelekewa nyaya amekuwa akizungushwa kwa kuambiwa nguzo inayotakiwa achukulie umeme imeoza ingawa inaendelea kutumika.

"Watu wa dharura wamekwisha toa taarifa kuhusu nguzo hiyo lakini bado haijabadilishwa jambo linaloweza kuleta maafa iwapo ikianguka na kibaya zaidi wamekuwa na maneno mengi badala ya kazi sijui wanataka kujenga mazingira ya rushwa" alilalamika Kyoga.

Kyoga alisema waziri wao Mhongo anafanya kazi kwa kujituma na alimsikia katika vyombo vya habari akiagiza kuwa ndani ya wiki moja mwombaji wa umeme awe amefungiwa lakini anashangaa Tanesco Charambe jinsi wanavyofanya kazi kwa kusuasua.

Msemaji wa Tanesco ofisi za  Charambe ambaye alifahamika kwa jina moja la Mugaya alipopigiwa simu jana ili kuzungumzia suala hilo simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila ya kupokewa hata hivyo gazeti ili linaendelea kumtafuta.


MAHAKAMA KUU KANDA YA MWANZA YAFUTA KESI YA KUPINGA MATOKEO JIMBO LA TARIME VIJIJINI.

January 29, 2016
Kulia ni Mwl.Chacha Heche ambae ni Katibu wa Chadema Mkoani Mara akiongea na wanahabari nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.
Na:George Binagi-GB Pazzo @BMG
Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza jana imeitupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Novemba 25 mwaka jana, katika Jimbo la Tarime Vijijini Mkoani Mara, iliyofunguliwa na aliekuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Christopher Ryoba Kangoye.

Katika kesi hiyo, wajibu maombi walikuwa ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mhe.John Heche (Chadema), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo mtoa maombi alikuwa akiiomba Mahakama kutengua matokeo ya Uchaguzi Mkuu katika Jimbo hilo kwa kuwa haukuwa huru na haki.

Baada ya Mahakama hiyo kupitia kwa Jaji Lameck Mlacha kusikiliza utetezi wa pande zote, iliamua kuifuta kesi hiyo ambayo ilikuwa ni nambari nne ya mwaka 2015 kutokana na hoja za mleta maombi kuwa na kasoro mbalimbali ikiwemo kutoainisha majina ya waliokuwa wakilalamikiwa kuvuruga uchaguzi Jimboni humo.

Wakili wa mleta maombi Costantine Mutalemwa pamoja na Wakili wa mjibu maombi Paul Kipeja aliekuwa akisaidiana na Wakili Tundu Lisu katika kesi hiyo, wameelezea kuridhika na maamuzi ya Mahakama hiyo.

Nae Mwl.Chacha Heche ambae ni Katibu wa Chadema Mkoani Mara, ameelezea kuwa na imani na Mahakama kutokana na maamuzi iliyoyatoa katika kesi hiyo pamoja na kesi nyingine zilizowahi kuamuliwa Mahakamani hapo na kuongeza kuwa sasa kazi imebaki moja kwa Mhe.Heche ambayo ni kuwatumikia wakazi wa Jimbo la Tarime Vijijini.

Kwa upande wake Mrimi Zabloni ambae ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, ameelezea furaha kwa wananchi wa jimbo hilo huku akiwasihi kuweka imani na Mahakama hapa nchini katika kutoa maamuzi ya kesi mbalimbali.

Wananchi wengi Mahakamani hapo kutoka Jimboni Tarime Vijijini walikuwa ni wafuasi wa Chadema na wameonyesha kuyapokea maamuzi ya mahakama hiyo kwa furaha kubwa na kwamba wao waliamua ushindi wa Heche tangu Novemba 25 mwaka jana kwenye daftari la kupigia kura.


Kesi hiyo ilisikilizwa January 19,2016 mwaka huu na kuahirishwa hadi juzi January 27,2015 kwa ajili ya kutolewa maamuzi, lakini pia iliahirishwa hadi jana January 28,2016 ambapo maamuzi yameweza kutolewa.
Mrimi Zabloni (Katikati) ambae ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini akiongea na wanahabari
Wakili wa mjibu maombi Paul Kipeja akihojiwa na wanahabari
Wakili wa mleta maombi Costantine Mutalemwa  akihojiwa na wanahabari
Mwl.Chacha Heche ambae ni Katibu wa Chadema Mkoani Mara na wafuasi wengine wa Chadema wakifurahia baada ya maamuzi ya Mahakama
Mahakamani kabla ya mashauri kutolewa
Mahakamani kabla ya mashauri kutolewa
Mahakamani kabla ya mashauri kutolewa