WAZIRI KAIRUKI AMSIMAMISHA KAZI MKUU WA CHUO CHA UTUMISHI WA UMMA

February 22, 2016

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais; Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angella Kairuki akitoa taarifa mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma leo katika Ukumbi wa Utumishi iliopo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Waandishi wa Habari na viongozi mbalimbali wakisikiliza taarifa toka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais; Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angella Kairuki kuhusu kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma leo katika Ukumbi wa Utumishi iliopo Jijini Dar es Salaam.
(Picha na Benedict Liwenga-Maelezo)
………………………………………………………………………………………
Na. Lilian Lundo – Maelezo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah  Kairuki amemsimamisha  kazi aliyekuwa mkuu wa chuo cha Utumishi wa Umma Said Nassoro kutokana na kushindwa kusimamia watumishi walioko chini yake
Mhe. Kairuki ametoa maamuzi hayo leo jijini Dar es Salaam  katika mkutano na waandishi  wa  habari katika moja ya kumbi zilizopo katika ofisi za Utumishi wa Umma.
“Namsimamisha Bwana Said Nassoro aliyekuwa mkuu wa chuo hiki kwa kushindwa kusimamia watumishi walioko chini yake  na kupelekea suala zima la usimamizi wa shughuli za chuo hususani katika matawi yake mbalimbali yaliyoko mikoani kuathirika,” alisema Mhe. Kairuki.
Mhe. Kairuki aliongeza kwa kusema kuwa usimamizi  wa Bw. Nassoro  ambao haukuwa wa ufanisi umetoa mwanya kwa viongozi mbalimbali wa matawi kufanya ubadhilifu wa mali za Umma ambapo mwaka  2011 na 2013 aliyekuwa mkurugenzi wa chuo upande wa tawi la Mtwara Silvanus Ngata aliongeza gharama za ujenzi.
Aidha taarifa kutoka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na TAKUKURU zilithibitisha ubadhilifu huo lakini mkuu huyo wa chuo hakuweza kuchukua hatua yoyote badala yake alimuhamisha Bw. Ngata kwenda kwenye tawi la Tabora na kuendelea na wadhifa wake.
Kutokana na ubadhilifu huo imempelekea Mhe. Kairuki  kumsimamisha kazi Bw. Ngata ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma tawi la Tabora na Bw. Joseph Mbwiro kutokana na matumizi mabaya ya fedha za malipo ya ada kiasi cha shilingi bilioni moja ambazo zilikuwa zikilipwa na wanafunzi kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Mhe. Kairuki ameendelea kueleza kuwa  bado wanaendelea kuondoa watumishi wa Umma ambao hawafuati   mifumo na miongozo ya Utumishi wa Umma ili kuwabakiza  watumishi ambao wanaonyeshe taswira nzuri na kufuata mifumo na miongozo  ya Utumishi wa Umma kwa ukamilifu wake.
BODI YA TSN YAMSIMAMISHA KAZI MHARIRI MTENDAJI

BODI YA TSN YAMSIMAMISHA KAZI MHARIRI MTENDAJI

February 22, 2016

DI1
Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya magazeti ya serikali (TSN) Prof Moses Warioba(wa kwanza kushoto) akitoa tamko la kumsimamisha kazi Mhariri mtendaji wa kampuni ya magazeti ya serikali Bw.Gabriel Nderumaki (hayupo pichani) kutokana na utendaji usiorizisha.Wengine pichani ni wajumbe wa Bodi hiyo  Dkt Evelyn Richard na Bw.Alfred Nchimbi(Picha na Daudi Manongi)
DI2
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo mhe Nape Nnauye akiongea na vyombo vya Habari kuhusu maagizo aliyoyatoa kwa Bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya magazeti ya serikali TSN ikiwemo sababu za wafanyakazi wengi kuacha kazi katika shirika hilo.
DI3
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akitembezwa kuonyeswa mazingira ya kampuni ya magazeti ya serikali(TSN) leo jijini Dar es Salaam.Kulia ni mhariri mtendaji wa kampuni hiyo ya magazeti ya serikali Bw.Gabriel Nderumaki ambaye amesimamishwa kazi kutokana na utendaji usiorizisha  na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya magazeti ya serikali (TSN) Prof Moses Warioba.
DI4
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akipata maelezo jinsi gazeti linavyotengenezwa kutoka kwa mchapaji msaidizi wa magazeti ya serikali (TSN) Bw.Paul Kasele alipofanya ziara katika shirika hilo leo jijini Dar es Salaam.
DI5
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea kampuni ya magazeti ya serikali TSN leo jijini Dar es Salaam.
………………………………………………………………………………………………………………….
Na Shamimu Nyaki-WHUSM.
Bodi ya wakurugenzi wa magazeti ya Serikali,(TSN) imemsimashisha kazi Mhariri Mtendaji wa magazeti hayo  Bw Gabrieli Nderumaki kupisha uchunguzi kutokana  na utendaji usioridhisha  ndani ya kampuni hiyo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw Prof Moses Warioba amesema hatua za kumsimamisha kazi Mhariri Mtendaji huyo umetokana na kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambapo nafasi yake itachukuliwa na Naibu Mhariri Bi Tumma Abdalah.
“Kumekuwa  na mambo mengi yanayofanyika bila kufuata utaratibu ndani ya kampuni hii ikiwemo wafanyakazi kutoelewana na menejimenti katika kulipwa stahili zao, pamoja na wafanyakazi kupewa  majukumu ambayo hawana uwezo wa kuyatekeleza”.Alisema Prof Warioba.
Aidha Prof Warioba  ametengua uteuzi wa Bw Felix Mushi aliyekuwa Meneja mauzo na masoko katika kiwanda cha uzalishaji kwa kukosa sifa na utendaji mbovu uliopelekea kampuni kushuka katika uzalishaji.
Hatua hiyo  ya kuwawajibisha watendaji hao imetokana na Ziara ya Mhe. Nape Nnauye  Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo katika  Kampuni hiyo  ambapo pia hakuridhiswa na utendaji mbovu uliopelekea    wafanyakazi 21  kuacha kazi.
“Nataka Bodi itafakari juu ya  malalamiko yaliopo kwa wafanyakazi na wachukue hatua kabla mimi sijakutana na wafanyakazi hao wiki ijayo ili kujua mapungufu yako wapi.”Alisema Mhe Nape.
Hata hivyo Bodi hiyo ya wakurugenzi inaendelea kutafuta namna ya kuboresha utendaji ndani ya kampuni  ili iendane na kasi iliyopo katika uzalisahaji wa magazeti kwa kiwango kikubwa
GAVANA AZINDUA MWONGOZO WA KWANZA WA KITAIFA WA ELIMU NA ULINZI KWA MTUMIAJI WA HUDUMA ZA FEDHA” (N-FEF).

GAVANA AZINDUA MWONGOZO WA KWANZA WA KITAIFA WA ELIMU NA ULINZI KWA MTUMIAJI WA HUDUMA ZA FEDHA” (N-FEF).

February 22, 2016

bot1
Meza kuu ikifuatilia kwa makini yanayojiri katika kikao cha uzinduzi wa Mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF).
bot2
Baadhi ya wadau waliohudhuria uzinduzi huo.
bot3
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania akieleza jambo wakati wa uzinduzi Mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF).
bot4
Bi. Susan Rutledge, Mtafiti na Mshauri wa masuala ya fedha, akieleza umuhimu wa elimu ya masuala ya fedha kuelekezwa kwa wananchi.
……………………………………………………………………………………………………………………………………..
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Kifedha Tanzania (FSDT), imezindua Mwongozo wa taifa wenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu elimu ya mambo ya fedha kwa wananchi.
Uelimishwaji wa wananchi kuhusu mambo ya fedha utatekelezwa kupitia “Mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF).
Gavana Prof. Beno Ndulu ameuzindua rasmi mwongozo huu ambao utajikita katika kutatua changamoto zilizobainishwa katika utafiti uliopima uelewa wa mambo ya fedha kwa watu wazima nchini Tanzania. Utafiti huu unaitwa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014.
Utafiti huo umebainisha kuwa watanzania wengi hawana elimu na ujuzi mahususi wa  masuala ya mambo ya fedha kwa ujumla, hivyo kuwanyima fursa ya kutumia huduma za kifedha kwa faida yao.
Katika utafiti huo imeonyeshwa kuwa upatikanaji wa huduma za fedha umekuwa na changamoto katika maeneo mengi huku zile zitolewazo kwa njia ya mitandao bado hazikidhi matarajio ingawa zinawafikia  wateja wengi kwa sasa.
Sambamba na hilo kumekuwa na uhaba wa nyenzo na miundombinu ya kuhifadhi na kufikisha taarifa za fedha kwa watumiaji wa huduma hizo  kwa kuzingatia namna sahihi ya kutoa taarifa, kuwaelimisha na kuwalinda.
Kutokana na utafiti wa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014 wananchi kutoka makundi mbalimbali katika jamii hawana ujuzi wa hesabu za kawaida  ambao ndiyo msingi mkuu katika nadharia ya masuala yahusuyo mambo ya fedha. 
Elimu msingi katika masuala ya fedha umekuwa kikwazo kwa waliowengi  hasa katika uandaaji wa bajeti, kutunza kumbukumbu ya matumizi, kupanga fedha kwa matumizi yasiyotegemewa ama ya ziada na muhimu zaidi kutunza kiasi kwa ajili ya matumizi ya uzeeni (baada ya kustaafu).
Inaonekana kuwa upatikanaji wa taarifa za masuala ya fedha hutegemea zaidi vyombo vya habari kama redio, televisheni na magazeti lakini vyombo hivi kwa sehemu kubwa,  hufikisha zaidi taarifa za biashara na masoko kuliko ambavyo vinaelimisha jamii kuhusu matumizi na upangaji wa mapato yao.
 “Haya ndiyo masuala mahususi ambayo  mwongozo huu wa taifa kuhusu elimu ya huduma za fedha unalenga kushughulika nayo,” alisema Prof Ndulu.
Pamoja na kuwepo ongezeko la upatikanaji wa huduma za kifedha, mpaka asilimia 58  mwaka 2013 kutoka kiwango cha asilimia 17 mwaka 2009, miongoni mwa watu wazima nchini, bado mwongozo huu ni muhimu ili kuleta mfumo imara wa sekta ya fedha na Zaidi sana ili kuleta ustawi wa maisha ya watanzania kwa ujumla.
Prof. Ndulu anasema kutatua changamoto za kielimu kwa ujumla na hususan elimu ya huduma za fedha italiwezesha taifa kuwa katika mwelekeo mzuri wa kukabiliana na umasikini na kufikia malengo ya kukuza uchumi.
 “Tunapaswa kujiuliza: ni kwa namna gani wananchi hasa wale masikini na wasiokuwa na elimu za kifedha  za wanapambana kuendeleza biashara zao katika mazingira ya soko huria na lenye ushindani kila uchwao” alisisitiza Prof. Ndulu.
Hivyo, mwongozo huu utahakikisha watanzania wapata elimu sahihi na ya uhakika ya huduma za kifedha pamoja na njia anazoweza nazo kujilinda katika ushindani huu.
Vilevile mwongozo huu umeundwa ili kutatua changamoto za kifedha zinazohusiana na maamuzi miongoni mwa watumiaji wa huduma hizi na kuwa jumuishi na wenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Mwongozo wa taifa kuhusu elimu ya huduma za fedha umeandaliwa kwa kujumisha washikadau kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Unabainisha changamoto zinazohusuana na uwezo wa kifedha ambazo zinahitaji kutatuliwa kwa uwepo wa elimu ya fedha. Pia, unatoa taratibu wakufanikisha utekelezaji wa elimu ya fedha, na mwongozo wa kitaifa wa kuratibu elimu ya fedha nchini.
Lengo la mwongozo wa elimu ya huduma za fedha ni kuwa na wananchi na kaya zenye uwezo kifedha nchini.

RAIS MHE. DKT MAGUFULI APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO WA MABALOZI KUTOKA CONGO DRC, NAMIBIA PAMOJA NA KUZUNGUMZA NA MABALOZI MBALIMBALI IKULU JIJINI DAR ES SALAAM.

February 22, 2016

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini Bi. Dianna Melrose Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Uingereza hapa nchini Bi. Dianna Melrose Ikulu  jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana Balozi Mteule wa Namibia hapa nchini Bi Theresia Samaria mara baada ya kupokea Hati ya Utambulisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Balozi Mteule wa Namibia hapa nchini Bi Theresia Samaria mara baada ya kupokea Hati ya Utambulisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi Mteule wa Namibia hapa nchini Bi Theresia Samaria mara baada ya kupokea Hati ya Utambulisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Balozi wa Misri hapa nchini Mohamed Yasser El Shawaf Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Misri hapa nchini Mohamed Yasser El Shawaf Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati ya Utambulisho kutoka kwa Balozi mteule kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jean Pierre Mutamba Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati ya Utambulisho kutoka kwa Balozi mteule kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jean Pierre Mutamba Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Balozi wa Afrika Kusini hapa nchini Thamsanqa Mseleku Ikulu jijini Dar es Salaam. 
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam. 
Picha na IKULU.

RC MAHIZA AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI (NHIF) LEO MJINI TANGA.

February 22, 2016


Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mwantumu Mahiza akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,Michael Mhando akizungumza Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mwantumu Mahiza

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,Michael Mhando kushoto akiingia kwenye ukumbini wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mwantumu Mahiza

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,Michael Mhando akisisitiza jambo kwa wafanyakazi wa mfuko huo wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mwantumu Mahiza na wa mwisho kulia ni Meneja wa NHIF Mkoa wa Tanga,Ally Mwakababu.
MKURUGENZI wa Huduma na Uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ya Jamii Tanzania, NHIF, Eugine Mikongoti akifuatilia kwa umakini hotuba ta mkuu wa mkoa wa Tanga,Mwantumu Mahiza wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya uliofanyika leo mjini Tanga.

 MKURUGENZI wa Huduma na Uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ya Jamii Tanzania, NHIF, Eugine Mikongoti wa kwanza kushoto akiimba nyimbo ya solidarite na wafanyakazi wenzake wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya uliofanyika leo mjini Tanga.

Baadhi ya wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wakifuatilia mambo mbalimbali wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya uliofanyika leo mjini Tanga.

Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)wakiwa mkutanoni leo

 

 Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mwantumu Mahiza akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya leo mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi kulia kwake ni Kaimu Mkuu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Michael Mhando
Kaimu Mkuu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Michael Mhando akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga mara baada ya kufungua mkutano wa
Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,
Picha na Tanga Raha Blog
WAZIRI MUHONGO AITAKA TANESCO na TPDC KUFANYA KAZI KISASA

WAZIRI MUHONGO AITAKA TANESCO na TPDC KUFANYA KAZI KISASA

February 22, 2016

HON1
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna ( wa pili kutoka kulia) akielezea majukumu ya kampuni hiyo mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo pamoja na watendaji wa Wizara  ya Nishati na Madini pamoja na  Taasisi zilizopo chini yake.
HON2
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akielezea fursa za uwekezaji katika sekta ya gesi nchini.
HON3
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna akisisitiza jambo katika kikao hicho.
HON4
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna (kushoto) na Mwenyekiti wa Kampuni ya Pan African Energy Nchini Patrick Rutabanzibwa (kulia) wakinukuu maelekezo  kutoka  kwa Wiziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani)
………………………………………………………………………………………….
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Waziri wa  Nishati na  Madini Profesa Sospeter Muhongo amelitaka  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la  Maendeleo  ya Petroli Nchini (TPDC) kufanya kazi katika  mtindo wa kisasa ili nishati ya umeme iweze kuwa  ya  uhakika kwa maendeleo  ya uchumi wa nchi.
Profesa Muhongo aliyasema hayo katika kikao chake na Kampuni ya Pan African Energy kilichofanyika jijini Dar es Salaam  kilichoshirikisha pia watendaji kutoka wizara ya nishati na madini, TANESCO, TPDC na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Alisema  mahitaji ya gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme wa uhakika ni makubwa, hivyo hakuna sababu  ya  kuwepo  kwa upungufu wa nishati ya umeme  nchini wakati kuna gesi ya uhakika.
Alifafanua kuwa haiwezekani shirika la TPDC likadai kuwa kuna gesi ya kutosha kwa ajili ya kuzalisha umeme, wakati kuna upungufu wa umeme nchini.
Alisema  serikali ina mpango wa kuhakikisha kuwa  wananchi wote hasa waishio vijijini  wanaunganishwa na umeme wa uhakika kupitia Wakala wa Nishati Nchini (REA) hivyo ni jukumu la mashirika hayo kuhakikisha yanabuni miradi na kukaribisha wawekezaji mbalimbali  katika uzalishaji wa umeme  wa uhakika ili wananchi wote waweze kuunganishwa na huduma ya umeme.
Alisisitiza kuwa amekwishawaalika wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya kuwekeza kwenye uzalishaji  wa  Megawati 1000 za umeme  kwa ajili ya kuingizwa kwenye  gridi ya  taifa, hivyo ni vyema shirika la TPDC likahakikisha   gesi ya uhakika inapatikana ili  umeme uweze kuzalishwa mara moja.
“  Lengo la  serikali kupitia  Wizara ya Nishati na Madini ni kuhakikisha kuwa ifikapo  mwaka 2025 Megawati 10,000 zinazalishwa, hivyo sekta ya nishati  kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kutoka kwenye  kundi la nchi masikini duniani  na kuingia kwenye kundi la nchi za  kipato cha kati, kama   Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, inavyofafanua,”alisema Profesa Muhongo.
Wakati huo huo, Profesa Muhongo aliitaka kampuni ya Pan Afrian Energy  kuhakikisha inatatua changamoto zote  inazozikabili  kwa kipindi cha miezi mitatu kabla ya kukutana naye  Juni 01 mwaka huu kwa ajili ya kupokea mapendekezo ya kampuni hiyo katika kuzalisha  gesi ya uhakika.
Alisisitiza kuwa kutakuwepo na utaratibu wa kukutana na kampuni hiyo kila baada ya miezi mitatu kwa ajili ya kujadili utendaji kazi wa kampuni hiyo, na serikali ipo tayari kutoa msaada pale kampuni itakapokwama.
Aidha, Profesa Muhongo aliitaka kampuni hiyo kuweka utaratibu wa kuajiri  vijana wa kitanzania wanaomaliza masomo ndani na nje  ya nchi baada ya kupata ufadhili kutoka serikalini.
“ Kwa sasa tuna  vijana wengi waliohitimu mafunzo  kwa ngazi  ya shahada za uzamili katika masuala ya mafuta na gesi katika  vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi kama Norway, Uingereza na China, hivyo ni vyema  wakapata ajira katika kampuni ya  Pan African Energy, ili nao waweze kufaidika na elimu na uwepo wa uwekezaji katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Naye  Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna, akielezea mafanikio ya uwekezaji kupitia  kampuni yake, alieleza kuwa kampuni hiyo imefanikiwa kutoa  ajira 87 kwa watanzania na kuboresha huduma  za jamii kama vile kutoa huduma ya umeme  bure katika eneo la Kilwa kilipo kituo chake za kuzalisha gesi.
Aliendelea kusema kuwa kampuni ya Pan African Energy imejenga  zahanati pamoja na kutoa mafunzo kwa waajiriwa wake lengo likiwa ni  kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inakuwa na wataalam wazawa.
ZAIDI YA TRILIONI ZAKUSANYWA KWA MWEZI FEBRUARI-DKT.LIKWELILE

ZAIDI YA TRILIONI ZAKUSANYWA KWA MWEZI FEBRUARI-DKT.LIKWELILE

February 22, 2016

MPO1
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile (kushoto) akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam ambapo amesema kuwa wizara hiyo imeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na katika kipindi cha mwezi Februari mwaka huu zimekusanywa zaidi ya Sh. trilioni 1 tofauti na mwanzo ambapo zilikuwa zkikusanywa Sh.bil 850. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Waziri wa Afya, Maendeleo, Jinsia, Watoto na Wazee Mpoki Ulusubisya.
MPO2
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata akifafanua kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam jinsi Mamlaka hiyo ilivyofanikiwa kukusanya mapato kutoka trilioni 1.2 kwa mwezi Disemba mpaka trilioni 1 na bilioni 79 kwa mwezi Januari na kwa mwezi Februari wanatarajia kukusanya trilioni 1.013 na tayari wamefikia nusu ya malengo waliyojiwekea.
MPO3
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi,Teknologia na Ufundi Tarishi Kibenga amesema Wizara yake itazitumia fedha walizopewa mwezi huu kulingana na malengo yaliyokusudiwa ikiwemo fedha za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa Diploma na wanafunzi wa chuo kikuu. Wa kwanza kushoto ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata.
MPO4
Katibu Mkuu Wizara ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee akifafanua namna Wizara yake ilivyojipanga kuzitumia fedha walizopata mwezi huu ambapo amesema zitatumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa ikiwemo fedha za mradi wa ujenzi wa Chuo cha Tiba cha Kimataifa cha Muhimbili eneo la Mloganzila nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
MPO5
Baadhi ya Waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam ambapo amesema kuwa wizara hiyo imeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na katika kipindi cha mwezi Februari mwaka huu zimekusanywa zaidi ya Sh. trilioni 1 tofauti na mwanzo ambapo zilikuwa zkikusanywa Sh.bil 850.
(Picha na Eleuteri Mangi- MAELEZO)
………………………………………………………………………………………………………………………
Na Nyakongo Manyama –MAELEZO-Dar es salaam
Serikali imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwezi huu tofauti na zilizokuwa zikukusanya hapo awali za bilioni 850 kwa kipindi cha mwezi mmoja na kuzielekeza fedha hizo kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.
Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango  Dkt. Servacius Likwelile wakati akitoa taarifa ya hali ya mapato kwa kipindi cha mwezi Februari mwaka huu.
Amesema kuwa kati ya fedha hizo ,sekta ya elimu imepewa shilingi bilioni 18.7  kwa ajili ya utekelezaji wa utoaji wa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za awali hadi kidato cha Nne ambapo fedha hizo ni kwa ajili ya malipo ya ada,chakula pamoja na ruzuku.
Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa Mkoa wa Dar es salaam  imeongezewa shilingi bilioni 2 ili kupanua uwezo wa udahili kama Rais alivyoahidi katika mkutano wake na Wazee wa Mkoa huo.
Aidha, Dkt. Likwelile amesema kuwa ili kuwajengea uwezo walimu walio masomoni na wakufunzi wao  ,Wizara imetoa shilingi Bilioni 1.65  kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.
Kati ya fedha hizo  wakufunzi wamepatiwa shilingi milioni 431.6 walimu walio masomoni wametengewa  shilingi milioni 249.2 kwa ajili ya vifaa vya kufundishia, posho na nauli.
Ameongeza kuwa fedha nyingine kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 573.7 zimetolewa kwa ajili ya  mishahara ya watumishi wa Umma  , ulipaji wa deni la taifa kwa mwezi huu zimetolewa shilingi bilioni 842.1 na Mifuko ya hifadhi za Jamii zimetolewa shilingi bilioni 81.13.
Fedha kwa ajili ya shughlui mbalimbali za maendeleo zimetolewa kiasi cha Shilingi Bilioni 166.2  ambapo chuo kipya cha Sayansi kilicho katika hatua ya ujenzi cha Mlunganzi la kimepatiwa Shilingi Bilioni 18 na Kiasi cha Shilingi Bilioni 13.6 kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya juu.
Mamlaka ya Elimu (TEA) imepatiwa shilingi Bilioni 23.078, Mpango wa Maji vijijini Bilioni l7.1, maendeleo ya ujenzi wa barabara zimetolewa shilingi bilioni 58.8, miradi ya umeme vijijini zimetengwa shilingi  bilioni 20.2, Reli shilingi bilioni 2.034, Serikali za mitaa zimepatiwa shilingi bilioni 4.5, na Mahakama zimepatiwa shilingi bilioni 12.3.
Naye Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata amesema kuwa makusanyo yameongeza kutoka shilingi trilioni 1.2  kwa mwezi Disemba hadi kufikia trilioni 1.79 kwa mwezi Januari
MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA UJUMBE WA WATU WA CHINA NA MWENYEKITI WA SHELL DEEPWATER

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA UJUMBE WA WATU WA CHINA NA MWENYEKITI WA SHELL DEEPWATER

February 22, 2016

ras1
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia suluhu Hassan  akizungumza na Ujumbe wa kampuni ya Gezhouba kutoka China kuhusu masuala ya uwekezaji. Kushoto ni kiongozi wa msafara huo Mhandisi Hu pend.
ras2
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia suluhu Hassan  akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa kampuni ya Gezhouba kutoka China.
ras3
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia suluhu Hassan  akizungumza na Mwenyekiti wa Shell Deepwater Tanzania BV Alex Knope walipokutana leo ofisini kwake Ikulu kwa ajili ya kumsalimia.

BAYPOT YAZINDUA MIRADI SITA YA MIKOPO YA VIWANJA,SERIKALI YAPONGEZA

February 22, 2016
Mkurugenzi Mkuu wa Bayport Financial Services, John Mbaga, kulia akizungumza jambo katika uzinduzi wa huduma mpya wa mikopo ya viwanja vinavyotolewa na taasisi yao katika maeneo sita ambayo ni Kilwa, Bagamoyo, Kigamboni, Chalinze, Kibaha na Morogoro. Kulia kwake ni Zahra Moore kutoka kwenye kampuni yao ya BlackWood na Mwanasheria wao Ntiiba Muganga. Picha na Story kwa Hisani ya Bayport Financial Services.


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAASISI ya Kifedha ya Bayport Financial Services inayojihusisha na mikopo, imezindua miradi sita mipya ya mikopo ya viwanja katika maeneo ya Kibaha, Bagamoyo, Chalinze, Temeke, Kilwa na Morogoro, ikiwa ni mwendelezo wa utoaji huduma bora za viwanja baada ya ule wa Vikuruti kuungwa mkono Watanzania wengi.

Kuzinduliwa kwa huduma hizo mpya za viwanja huku wakiongozwa na Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Temeke, Martha Minga, kunatanua wigo wa urahisishaji wa maisha ya Watanzania, hususan katika suala la ardhi linalozidi kupanda thamani siku hadi siku, jambo linalohitaji juhudi za taasisi kama Bayport za kuwasaidia wananchi wake kupata maeneo ya makazi kwa utaratibu rahisi na nafuu.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya Temeke, Bi Martha Minga, aliyesimama akizungumza katika uzinduzi wa hudumaya viwanja inayotolewa na taasisi ya kifedha ya Bayport Financial Services, leo mchana katika Ukumbi wa Ramada Encore, Posta, jijini Dar es Salaam. Anayeshuhudia ni mwanasheria wa Kampuni ya BlackWood, Ntiiba Muganga na Mkurugenzi wa Uzalishaji wa BlackWood Zahra Moore.

Akizungumza katika uzinduzi wa miradi hiyo mipya ya viwanja, Mkurugenzi Mkuu Bayport Financial Services, John Mbaha, alisema huduma zao zitakuwa na njia rahisi kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wote kuchangamkia fursa ya upatikanaji wa viwanja hivyo.
Meneja Masoko na Mawasilianowa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo kushoto akibadilishana mawazo na Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya Temeke, Bi Martha Minga.
Mkurugenzi Mkuu wa Bayport Financial Services, Jonh Mbaga, akipiga picha ya pamoja na Mbunge wa Kigamboni, Mheshimiwa Faustine Ndugulile katika uzinduzi wa huduma ya mikopo ya viwanja, uliofanyika leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni mwakilishi wa Mkuu wa wilaya Temeke, Bi Martha Minga.
Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo akizungumza katika uzinduzi huo wa huduma ya mikopo ya viwanja.
Meneja Biashara wa Bayport Financial Services, Thabit Mndeme, akimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mkuu wa taasisi yao John Mbaga kulia kwake wakati anazungumza na wageni waalikwa katika uzinduzi wa huduma yao ya mikopo ya viwanja.

Alisema njia hizo ni pamoja na ununuaji wa kiwanja kwa pesa taslimu ambapo mteja anatakiwa kulipia fedha zote za kiwanja kwenye akaunti ya Bayport, kukabidhi nakala za nyaraka za malipo hayo kwenye ofisi za Bayport na kusubiri ndani ya siku 90 ili akabidhiwe hati yake baada ya kukamilisha malipo yote.

“Kwa wateja wa mkopo wa upande wa ujasiriamali na watumishi wa kampuni binafsi, wanatakiwa kulipia malipo ya awali ya mita za mraba walizochagua, huku Bayport ikikamilisha malipo yaliyosalia na wateja hao kupatiwa nyaraka zao baada ya kukamilisha mkopo wao, ambapo thamani ya viwanja hivyo vikianzia sh Sh 550,000,” Alisema Mbaga.

Naye Meneja Biashara wa Bayport Financial Services, Thabit Mndeme, alisema watumishi wa umma hawatakuwa na gharama za awali, badala yake wakichagua maeneo watakayo, wataingizwa kwenye kundi la mkopo na kutakiwa kulipa mkopo huo kila mwezi kwa kipindi cha miaka mitatu, huku makato yakikadiliwa kuwa Sh 73,684.49 kila mwezi.

“Bado tunaendelea kutanua wigo kwa watu wote kama vile watumishi wa umma, watumishi wa kampuni binafsi, bila kusahau kundi kubwa la wajasiriamali ambalo limeendelea kujumuishwa kwenye miradi yetu ya viwanja, tukiamini gharama ya makato ya kila mwezi ya Sh 102,855 ni rahisi na yanaweza kuwa mkombozi wa maisha ya watu wengi,” alisema Mndeme.

Kwa mujibu wa Mndeme, huduma za viwanja zinapatikana katika maeneo ya Bagamoyo na mita moja za mraba zitauzwa kwa Sh 10,000 tu na (Boko Timiza) Kibaha mita moja za mraba itauzwa kwa Sh 9,000 na (Kibiki na Mpera) Chalinze mita moja za mraba zitauzwa Sh 4500, huku (Tundi Songani) Kigamboni mita moja ya mraba itanunuliwa kwa Sh 10,000 na (Msakasa) Kilwa mita ya mraba itapatikana kwa Sh 2000, bila kusahau (Kiegea) mita moja ya mraba Sh 3500 tu.

Naye Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, alisema kwamba hakuna Mtanzania atakayelalamika kushindwa kujenga nyuumba, kama watafanyia kazi juhudi za taasisi yao yenye dhamira na malengo makubwa ya kuwakwamua watu wote ili wawe na vitu vya thamani kama vile nyumba na viwanja.

Kwa upande serikali kwa kupitia mwakilishi wa Mkuu wa wilaya Temeke, Martha Minga, aliitaka Bayport kushirikiana na serikali katika mambo yao hususan ya viwanja ili kuhakikisha kwamba wananchi wanafanikiwa kwa dhati na kuepusha migogoro hususan katika suala zima la hati ambalo ndio muhimu katika mambo yanayohusiana na ardhi.


Naye Mbunge wa Kigamboni Faustine Ndugulile alisema kwamba amefurahishwa mno na huduma ya viwanja vya Bayport sambamba na kuguswa kwa jimbo lake la Kigamboni, jambo linaloweza kuiweka eneo hilo katika nafasi za juu.
Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya BlackWood Zahra Moore kushoto akizungumza jambo katika uzinduzi wa huduma ya viwanja ya Bayport Financial Services.
Mwanasheria wa Kampuni ya BlackWood Ntiiba Mungana akizungumza jambo kwenye uzinduzi huo wa huduma ya mikopo ya viwanja.
Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, akipiga picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Uzalishaji wa kampuni ya BlackWood, Bi Zahra Moore.