CMSA YATAKA TAASISI ZICHANGAMKIE FURSA KUJIENDELEZA KIUCHUMI

December 15, 2023

 Na Mwandishi Wetu - Michuzi Tv


OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama, amezitaka kampuni za uwekezaji, zikiwemo benki za biashara, benki za wananchi, kampuni za bima na mashirika ya umma kutumia vyema fursa za kujiongezea kipato.

Amezitaka kutumia fursa zilizopo katika sekta ya masoko ya mitaji, ikiwemo kuuza hisa na hatifungani kwa umma na hatimaye kuorodheshwa katika soko la hisa kwa lengo la kuongeza uwezo wa rasilimali fedha.

Mkama ameyasema hayo Desemba 14, 2023 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuorodheshwa kwa Hisa za upendeleo millioni 72 za Kampuni ya Uwekezaji ya TCCIA Investment Plc kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

"Ndugu wageni waalikwa, natoa wito kwa kampuni za uwekezaji, benki za biashara, benki za wananchi, kampuni za bima na mashirika ya umma kutumia fursa zilizopo katika sekta ya masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kuuza hisa na hatifungani kwa umma na hatimaye kuorodheshwa katika soko la hisa ili kuongeza uwezo wa rasilimali fedha," amesema.

Ametoa rai kwa wadau wa masoko ya mitaji kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia CMSA katika kutekeleza mikakati ya kuendeleza masoko ya mitaji nchini ikiwemo kuleta bidhaa mpya katika masoko ambazo zitaorodheshwa katika Soko la Hisa.

"Kwa kufanya hivyo tutawezesha masoko ya mitaji kuendelea kuwa injini ya kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi yetu," amesisitiza.

Pia, aliikumbusha na kutoa msisitizo kwa bodi ya Wakurugenzi na uongozi wa TCCIA Investment Plc kwamba wawekezaji walionunua hisa zinazoorodheshwa leo wamewapa jukumu kubwa la kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la thamani katika uwekezaji wao ndani ya TCCIA kufaidika kiuchumi kutokana na uwekezaji huo.

"Miongoni mwa faida hizo ni kama vile kupata gawio la faida itakayopatikana kutokana na utendaji wa kampuni, kupata hisa zaidi za upendeleo (rights issue shares) na kupata hisa za bakshishi (bonus issue shares)" amesema.

Ameongeza hiyo tawezekana ikiwa TCCIA pamoja na mambo mengine itahakikisha kuwa inatekeleza maelekezo ya Serikali kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwamba kiasi kilicho patikana kutokana na mauzo ya hisa kinatumika kuwekezwa kwa mujibu wa sera za uwekezaji zilizopitishwa na Bodi na kuidhinishwa na Mamlaka.

Pia uwekezaji sahihi utaiwezesha TCCIA kuongeza ufanisi wa kampuni na kupata faida na hivyo kuongeza thamani ya uwekezaji kwa wanahisa huku akisisitiza Mamlaka hiyo itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi ili kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi na shughuli za maendeleo.

Ameongeza ambapo ni pamoja na kuuza hisa kwa umma, hatifungani za miundombinu (infrastructure bonds), hatifungani Rafiki wa mazingira (green bonds), hatifungani za bluu (blue bonds), na hatifungani za taasisi za Serikali (subnational bonds).

Pamoja na hayo amesema utoaji wa hisa za upendeleo unatoa fursa kwa wanahisa kuongeza uwekezaji wao kwa bei nafuu na hivyo kufaidika na punguzo la bei; na ni miongoni mwa njia zinazotumiwa na kampuni kuongeza mtaji.

Aidha, uorodheshwaji wa hisa za upendeleo za TCCIA Investment Plc katika soko la hisa unawapatia fursa wawekezaji kuuza hisa zao pale wanapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi mengine; kujua thamani halisi ya hisa zao; na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hisa hizo.

"Nimefurahi kuona mikakati madhubuti iliyowekwa na Bodi na Uongozi wa TCCIA Investment Plc juu ya matumizi sahihi ya fedha zilizopatikana kupitia mauzo ya hisa, ambapo, fedha hizo zitatumika kukuza uwekezaji wa kampuni hii katika dhamana mbalimbali za masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika hisa za kampuni, hatifungani na vipande katika mifuko ya uwekezaji wa pamoja.

"Hatua hii itaiwezesha TCCIA Investment Plc kutimiza malengo yake ya kimkakati ya kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wake; na kuiwezesha kampuni hii kuwekeza zaidi katika masoko ya mitaji hapa nchini, Afrika Mashariki (EAC) na Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC)." alisema CPA Mkama.
 OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama akigonga Kengele kuashiria kuorodheshwa kwa Hisa za upendeleo millioni 72 za Kampuni ya Uwekezaji ya TCCIA Investment Plc kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).


OFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA Nicodemus Mkama akizungumza kwenye hafla ya kuorodheshwa kwa Hisa za upendeleo millioni 72 za Kampuni ya Uwekezaji ya TCCIA Investment Plc kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE),iliyofanyika Disemba 14,2023 jijini Dar es Salaam.






DAKIKA 40 CHUMBA CHA WANAOZALIWA KABLA YA WAKATI

December 15, 2023
Novemba 17, 2023, Dunia iliadhimisha siku ya Mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati, siku moja kabla, nilibahatika kufika katika Wodi maalumu kwenye mojawapo ya vyumba vya kutunza Watoto hao katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na kujenga msingi wa simulizi hii.

Ni kijichuchumba kidogo chenye nafasi, makadiliyo ya mita 5 kwa 2.5 za mraba, nilikaribishwa na joto la wasitani, macho yakavutwa na vitanda mithili ya minara ya kuonesha, ngazi tatu kila kimoja, ya kwanza ikihifadhi vifaa, ya pili ni kijiboksi kilichozingwa kwa kingo za plastic inayoonesha kilicho ndani, yatatu ilisimama kama paa yenye mkonga wa kusaidia kuegesha drip.

Ndani ya viboksi ngazi ya pili kulikuwa na vichanga wakirusha miguu na mikono, kwa haraka sikufahamu ilikuwa ishara ya furaha ya kuja duniani au maumivu, jambo nililokuwa na uhakika nalo, vitendo vile vilithibitisha Uhai.

Baadhi ya vichanga viliwekwa vifaa kwenye ngozi kufuatilia mapigo ya Moyo na upumuaji, vifaa vingine viliwekewa kwenye mguu au mkono kusoma kiwango cha Oksijeni na Joto la Mwili.

Harakati za huduma ziliendelea, Muuguzi akimsaidia mama kukumbata mtoto katikati ya kifua chake, nikaambiwa ni ulezi-Kangaroo hufanyika kumsaidia kichanga apate joto la mama.

Pembezoni mwa mojawapo ya vitanda hivyo, alisimama Muuguzi, mama wa kichanga akiwa kitako pembeni yake wakishirikiana kumlisha chakula kichanga kwa kutumia mpira maalumu wa kulishia.

Ingawa, sura za kina mama waliyokuwa katika Wodi hiyo zilisawajika, macho na matamshi yao yalikuwa yenye matumaini na upendo mkubwa.

Vichanga wale walikuwa wadogo kwa umbo na mwonekano, hawakuwa sawa na vichanga wanaozaliwa wakiwa wametimiza umri wa kukaa tumboni yaani wiki 37, hivyo walizaliwa na uzito pungufu, gram 700 hadi 900 kwa niliyobahatika kupata taarifa zao.

Ifahamike kuwa, kisayansi mtoto hupaswa kukaa tumboni kwa mama kwa takribani wiki 37, afikishe uzito wa kilo 2 hadi 3.5 ndipo akamilike kujiumba na kuwa tayari kukabiliana na hali ya Dunia.

Hata hivyo, hali huwa tofauti miongoni mwa vichanga 13.4 ( UN 2020) wanaozaliwa kabla ya kufikisha wiki 37 kote dunia, hivyo kuzaliwa wakiwa na changamoto mbalimbali na hata kufariki kabla ya kufikisha siku 28.

Dkt. Julieth Kabengula, Bingwa wa Magonjwa ya Watoto na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Watoto BMH, anasema Watoto hao hupitia changamoto za kiafya kwa kuwa huzaliwa kabla viungo mbalimbali havijakamilika kujiumba.

“Hupatwa na changamoto ya upumuaji kwa sababu mapafu hayajakomaa, miili yao haiwezi kudhibiti joto hivyo mara nyingi joto hushuka chini ya kiwango na kuhatarisha uhai, na wakati mwingine hawawezi kugandisha damu, na wanaweza kupungukiwa na sukari mwilini” Dkt. Kabengula.

Asilimia 11 ya wanawake wanaojifungua kila mwaka nchini hupata Watoto kabla ya wakati, huku vifo 50,000 vikiwakabili Watoto wenye umri chini ya siku 28 ambapo asilimia 27 ya vifo hivyo huwakabili Watoto waliyozaliwa kabla ya wakati.

Dkt. Kabengula anasema, vifo hivyo vinaweza kuepukika ikiwa Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati watapatiwa huduma mapema.

“Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati wanaweza kuishi kama wengine endapo tutadhiti visababishi vinavyokatisha uhai wao, ikiwemo kudhiti sukari, joto, maambukizi na kutokwa damu” Alisema Dkt. Kabengula.

Takwimu za BMH zinaonesha kuwa asilimia 95 ya Watoto waliyozaliwa kabla ya wakati na kufikishwa kwenye Wodi maalumu ya Uangalizi Hospitalini hapo hupata nafuu na kuruhusiwa.

Hata hivyo, nilipata shauku ya kuwatafuta kina mama waliyowahi kupita katika wodi hiyo maalumu. kujionea Uso kwa Macho maendeleo ya Watoto hao baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Nilianza kwa kusafiri umbali wa kilometa 19 mwendo wa nusu saa kwa gari kwenda Mtaa wa Kikuyu hapa jijini Dodoma, huko nilimfuata Bi. Olabeth Nikanoni Martine, aliyepata Watoto mapacha kabla ya wakati.

Hadithi ya Bi. Olabeth ni chungu tamu, kama mama yeyote alikuwa na shauku ya kupata mtoto, hata hivyo ujauzito ukawa kizungumkuti ukamlazimisha kulala kidandani hadi utakapofikisha wiki 37, lakini safari ya kulala bila kujali ugumu aliyoupata ilikoma baada ya wiki 26.

“Niliona kitu kama maji yanatoka sehemu za siri, tukakimbia Hospitali ambako niliambiwa napaswa kujifungua, nikapelekwa chumba cha kujifungua, nikajifungua Watoto mapacha wa kike na wa kiume, watoto walikimbizwa wodi maalumu” Alisimulia Bi. Olabeth kwa Uchungu.

Akiwa katika kilele cha furaha ya kupata watoto, ndipo habari aliyoitaka iwe, haikuwa, kama alivyotarajia watoto baada ya wiki 37 za ujauzito, akaishia wiki 26 ndivyo ilivyokuwa alipoalikwa kutambulishwa kwa wanae katika wodi maalumu (Chumba cha Joto).

“Niliambiwa Kulwa alifariki kwa kushindwa kupumua,tumaini langu likabaki kwa Doto, lakini nilivyomwona nilishituka, niliumia kwa sababu alikuwa ni mdogo, mwenye gram 900, anayepumua kwa kutumia msaada wa mashine” Bi. Olabeth alisimulia kwa Uchungu.

Safari, ya wiki 7 kuishi na mwanae katika Wodi maalumu ya kulelea Watoto waliyozaliwa kabla ya wakati (Chumba cha Joto) ikaanza, anasema haikuwa tambarare alipanda vilima na milima, akashuka mabonde na vibonde.

“Kuna wakati mtoto anashindwa kupumua anawekewa mashine, hawezi kula, akila tumbo linajaa, inabidi awekewe drip, anabadilika kila mara, kama mama nilikuwa nakosa nguvu” Alikumbuka Bi. Olabeth, akipepesa macho kama anayezuia machozi.

Mkasa wa Bi. Olabeth hautatosha kwenye Makala hii pekee una ngano nyingi zilizosheheni ujasili, uvumilivu na ustahimilivu wa mama, niliachana naye na kuelekea Mtaa wa Ihumwa nje kidogo ya jiji la Dodoma mwendo wa zaidi ya kilometer 20.

Ihumwa nilimfuata mama mwingine, Bi. Anne Mlei au mama Mikaela kama anavyopenda kuitwa, alijifungua mtoto wiki ya 29, huku akipitia changamoto nyingi wakati wa ujauzito.

“Nilikuwa nalazwa mara kwa mara kwa sababu ujauzito ulitishia kutoka, mara ya mwisho nilikuwa kliniki, nikahisi kama kutokwa na maji, nikalazwa kwa siku tano ambapo ililazimika nifanyiwe upasuaji wa kumtoa mtoto”

Kama ilivyokuwa kwa Bi. Olabeth, mama Mikaela alijikuta katika wakati mgumu alipokutana na Mikaela kwa mara ya kwanza.

“Nilipoletewa mtoto wangu, nilishangaa sana, alikuwa tofauti na Watoto wengine, alikuwa ni mdogo sana, nikasema Mungu wangu nimezaa nini hiki, niliogopa mno, alikuwa tofauti na Watoto niliyozoea kuwaona” Alinisimulia Mama Mikaela kwa hisia zilioaksi kumbukizi ya siku husika.

Pamoja na simulizi nzito, jambo nililoliona wazi na la pekee kwa Bi. Olabeth na Mama Mikaela ni upendo, Moyo wa shukrani na furaha ya kuwa na mtoto. Lakini je, kwanini mama ajifungue kabla ya wakati?

Kwa mujibu wa Dkt. Kabengula, kuwa na maambukizi wakati wa ujauzito, lishe duni, upungufu wa damu, shinikizo la juu la damu, au sababu nyingine ikiwemo kuwa na ujauzito wenye mtoto zaidi ya mmoja ni baadhi ya visabishi.

“Njia rahisi ya kumsaidia mama asijifungue kabla ya wakati ni kwa wanandoa kuzingatia lishe bora, kufika Hospitali mapema mama anapopata ujauzito, ili kufuatiliwa kwa karibu kwa kufanya vipimo vya damu, kutibiwa maambukizi na kudhibiti shinikizo la juu la damu” Alisema Dkt. Kabengula.

Serikali imepiga hatua kuhakikisha huduma za Afya hasa kwa mama na Mtoto zinaboreshwa na kupatikana kote nchini, kwa kujenga vituo vingi vya kutolea huduma, kusomesha wataalamu, na kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinakuwepo.

Hatua hizo zinapunguza vifo vya Watoto kabla ya siku 28 baada ya kuzaliwa, Ushahidi wa utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria Tanzania 2021-2022, unaonesha kina mama wengi wanapokea usaidizi wa kitaalamu wakati wa kujifungua kutoka asilimi 66, 2015-16 hadi asilimia 85, 2021-2022.


Mwandishi wa Makala haya ni Raymond Mtani

Afisa Uhusiano wa Hospitali ya Benjamin Mkapa-Dodoma.

0767074991.
Pichani, Mama waliyojifungua watoto kabla ya wakati wakiwakumbatia kifuani vichanga kuwasaidia kupata joto na kukua kwa haraka (Kangaroo motherhood) katika moja ya Wodi maalumu ya uangalizi wa watoto hao.

WADAU WAJADILI MITAALA YA UHANDISI MAJI NA MAENDELEO YA JAMII JIJINI MWANZA.

December 15, 2023

 

Wadau wa fani ya uhandisi na maendeleo ya jamii wakiwemo kutoka mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA), mamlaka ya maji vijijini (RUWASA), mamlaka ya taifa ya umwagiliaji, wakufunzi wa vyuo vya uhandisi na maendeleo ya jamii wamekutana Misungwi mkoani Mwanza kujadili mapitio ya mitaala ya programu ya uhandisi maji na maendeleo ya jamii.

Majadiliano hayo ya siku moja yamefanyika Alhamisi Desemba 14, 2023 katika ukumbi wa chuo cha maendeleo ya jamii ufundi Misungwi (Misungwi CDTTI).

Makamu Mkuu Taaluma wa chuo hicho, Dongo Nzori amesema lengo ni kupitia hiyo na kutoa maoni ya mwisho kabla ya kuwasilishwa katika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa ajili ya kuidhinishwa.

Amesema kozi ya uhandisi maji na maendeleo ya jamii ikipitishwa na NACTVET itakuwa kozi ya pili katika vyuo vyao vya maendeleo yajamii ufundi Misungwi mkoani Mwanza na Mabughai kilichopo Lushoto mkoani Tanga ambapo itasaidia kuleta tija katika sekta ya umwagiliaji.

"Tumeamua kuleta huu mseto wa uhandisi maji na maendeleo ya jamii kwa sababu utasaidia kupunguza rasilimali watu, kuongeza ufanisi katika kusimamia miradi ya maji pamoja na kurahisisha ujenzi wa miundombinu ya maji" amesema Nzori.

Amesema kwa sasa kwenye kozi ya uhandisi ujenzi na maendeleo ya jamii ina wanafunzi zaidi ya 900 katika vyuo hivyo ambapo Misungwi kuna wanafunzi 600 na Mabughai 300 huku idadi ikitarajiwa kuongezeka baada ya kozi ya uhandisi maji na maendeleo ya majii kuanza kutolewa ambayo pia itazalisha wataalamu wanaohitajika katika soko la ajira.

Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Mabughai wilayani Lushoto, Erasmus Hipoliti amesema mtaala wa uhandisi maji na maendeleo ya jamii utasaidia vijana wengi kupata fursa za ajira kwa namna utakavyotoa wigo wa kushiriki katika masuala ya MMaendeleo ya Jamii na uhandisi maji.

Amesema bado kuna changamoto ya miradi ya maji katika jamii ndiyo maana wameanzisha kozi hiyo ili kuandaa wataalamu watakaoibua miradi ya maji hatua itakayosaidia kutatua changamoto zilizopo.

Kwa upande wake Mhandisi Willybert Bujiku kutoka MWAUWASA Kanda ya Misungwi, amesema kozi hiyo italeta manufaa makubwa kwa Serikali ambapo akiajiriwa mtu aliyesoma uhandisi maji na maendeleo ya jamii atafanya kazi kwa ufanisi mkubwa huku pia ikiongeza wigo kwa wahandisi kufanya kazi kwa weledi zaidi.

Awali akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju ameshauri maboresho ya mitaala ya uhandisi maji na maendeleo ya jamii kusaidia kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na weledi utakaosaoidia kuchochea maendeleo katika jamii.
Makamu Mkuu Taaluma Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Misungwi CDTTI, Dongo Nzori akizungumza kwenye warsha ya wadau kujadili mitaala ya programu za uhandisi maji na maendeleo ya majii iliyofanyika katika chuo hicho.
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi Mabughai mkoani Tanga, Erasmus Hipoliti akizungumza wakati wa warsha hiyo.
Wadau wa maji na maendeleo ya jamii wakiwa kwenye majadiliano ya mitaala ya programu ya uhandisi na maendeleo ya jamii.
Wadau wakiwa kwenye majadiliano.
Wadau wakiwa kwenye majadiliano.
Wadau wakiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju (katikati waliokaa).
Wadau wakiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju (katikati waliokaa).
PIA SOMA>>> HABARI ZAIDI HAPA