UWEKEZAJI MAHIRI MAENEO YA KIMKAKATI YA TAWA KUIINGIZIA SERIKALI ZAIDI YA DOLA ZA KIMAREKANI MILIONI 314

January 03, 2024

 Na Beatus Maganja, Dar es Salaam


Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema Serikali inatarajia kupata mapato yanayokadiriwa kufikia dola za Kimarekani milioni 314 katika kipindi cha miaka 20 kutokana na uwekezaji mahiri katika maeneo saba (7) yaliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA

Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo Januari 03, 2024 katika hafla ya utiaji saini mikataba ya uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas - SWICA) kati ya TAWA na Makampuni manne ya uwekezaji yanayofanya shughuli za utalii ndani na nje ya nchi iliyofanyika chuo cha utalii cha Taifa (NCT) Jijini Dar es Salaam.

Amesema kupitia uwekezaji huo unaokadiriwa kuwa na thamani ya TZS bilioni 696 wawekezaji watawajibika kuwekeza kwenye miundombinu katika maeneo yao ya uwekezaji na kuhakikisha wananchi wanaozunguka maeneo hayo wananufaika na kuona umuhimu wa aina hiyo ya uwekezaji.

Aidha amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania kwa kufanya filamu maarufu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imeleta matokeo makubwa kwa kuleta ongezeko kubwa la watalii nchini

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesema baada ya upembuzi yakinifu uliofanywa katika nchi za SADC kuhusu uwezekano wa modeli hii ya biashara (SWICA), uzoefu ulionesha kuwa modeli hii inajulikana kwa uwezo wake wa kuwezesha Mamlaka za eneo lililohifadhiwa kuzalisha mapato endelevu kwa ajili ya uhifadhi na maendeleo.

Aidha amesema mapato yanayotarajiwa kuzalishwa kwa mwaka ni mara tisa (9) ya mapato yaliyokuwa yakipatikana awali kwa shughuli za utalii zilizokuwa zikifanyika maeneo hayo, hivyo ongezeko hili la mapato linaashiria kwamba mpango wa biashara wa SWICA ni chaguo zuri la kufikia matumizi bora na endelevu ya rasilimali ya wanyamapori kwa manufaa ya kiuchumi

Aidha amesisitiza kuwa TAWA imejipanga vyema kuhakikisha inatekeleza vyema miradi yote ya SWICA katika maeneo husika kwa kushirikiana na wawekezaji

Maeneo ya kimkakati ya uwekezaji mahiri yanayotajwa kuwekezwa ni Pori la Akiba Mkungunero (Dodoma), mapori ya akiba Ikorongo na Grumeti (Mara) pamoja na Pori la Akiba Maswa (Kimali, Mbono na Kaskazini) Mkoani Simiyu.

Aidha, Makampuni yaliyowekeza katika maeneo hayo ni Bushman Safari Trackers Ltd (Maswa GR North), Grumeti Reserves Ltd (Grumeti na Ikorongo GR), Mwiba Holdings Ltd (Maswa GR Mbona na Maswa GR Kimali) pamoja na Kampuni ya Magellan General Trading LLC (Mkungunero GR).

Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula(Mb), Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko

Wengine ni Makamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Uhifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), baadhi ya watendaji na maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na TAWA pamoja na wadau mbalimbali wa uhifadhi.



 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akizungumza wakati wa utiaji saini wa mikataba sita ya uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji wa Wanyamapori (Special Wildife Investment Concession Areas – SWICA).
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Dunstan Kitandula akizungumza katika hafla hiyo kabla ya kumkaribisha Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Angella Kairuki.













 Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwindaji ya Bushman Safari Trackers Ltd, Talal Abood akitoa shukurani zake kwa serikali kwa kampuni yake kusaini mkataba huo na wizara ya Maliasili akisema hiyo inafungua milango kwa wafanyabiashara kuwekeza katika sekta ya Utalii.





HAKUNA USAFIRISHAJI HARAMU WA WATOTO NA WENYE ULEMAVU NAMANGA - KATAMBI

January 03, 2024

 Na. Mwandishi wetu, Arusha - Namanga.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amethibitisha kutokuwepo kwa usafirishaji haramu wa biashara ya binadamu katika mpaka wa Namanga na Kenya hususani kwa watoto na wenye ulemavu. 
 
Mhe. Katambi amethibitisha hayo Januari 3, 2023 Jijini Arusha katika Wilaya ya Longido alipofanya ziara katika mpaka wa namanga kwa ajili ya kukagua hali ya utoaji huduma kwa abiria.

Amesema taarifa ambazo hivi karibuni zimesambazwa katika mitandao ya kijamii juu ya watoto na wenye ulemavu kusafirishwa kinyume na sheria na kupelekwa nchini kenya kwa ajili ya kutumikishwa zipuuzwe kutokana na hali ya ulinzi na usalama uliopo katika mpaka huo.

Ametoa rai kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kudhibiti vipenyo visivyo halali ikiwa ni pamoja na kuweka polisi jamii ili kuwachukulia hatua watakao bainika wanapita bila kufuata utaratibu
.
Aidha, amesema Serikali ya Mhe, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mfumo  wa kielekroniki wa kupata hati ya kusafiria kwa muda mfupi hivyo hakuna sababu ya kusafiri bila kufuata utaratibu.




 

EFTA YATENGA BILIONI 3.5/- KUKOPESHA VIJANA KUKU BILA DHAMANA

January 03, 2024

 Na Mwandishi Wetu Arusha, Tanzania


Taasisi ya EFTA inayojishughulisha na utoaji wa mikopo ya mashine na magari bila dhamana kwa wajasiriamali na wakulima nchini, imetenga Zaidi ya shilingi Bilioni 3.5 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa lengo la kuwawezesha vijana na wanawake nchini kupata mikopo ya vifaranga vya kuku, chakula Pamoja na mahitaji mengine muhimu ya ufugaji wa kuku bila dhamana.

Mpango wa mkopo wa vifaranga vya kuku kwa wakulima na hususani vijana na wanawake wasiokuwa na ajira au wanaotaka kujipatia kipato cha ziada ni wa kwanza na wa aina yake kwa taasisi ya kifedha nchini kuutoa kwa wakopaji.

EFTA imezindua mpango huu ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dr Samia Suluhu Hasan, ambaye amekuwa akijipambanua katika kuhakikisha kuwa watanzania na hususani vijana na wanawake wanawezeshwa kiuchumi kwa kuwawezesha kupata mikopo ya aina mbalimbali ambayo itawasaidia kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Kwa muda sasa kundi la vijana na wanawake nchini Tanzania, ni miongoni mwa makundi ambayo yamekuwa yakitajwa kuwa na idadi kubwa ya watu wasiokuwa na ajira rasmi hatua ambayo imekuwa ikichangia kuongezeka kwa umasikini miongoni mwa kundi hili.

Serikali kupitia mpango wa Jenga Kesho Bora unaojulikana kama “Built Better Tomorrow – Youth initiative for Agribusiness (BBT-YIA), umewezesha vijana wengi nchini kupata fursa ya mafunzo na mikopo ya kuanzisha na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji hapa nchini.

Kampuni ya EFTA katika kuunga mkono jitihada hizo za serikali nayo imeamua kuanzisha mpango wa majaribio wa mkopo wa kuku kwa vijana na wanawake bila dhamana. Hatua ambayo itawezesha makundi haya kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uzalishaji kupitia uwezeshwaji wa mkopo huu bila dhamana, hatua ambayo itakuwa imeondoa ile kadhia ya vijana na wanawake kutokukopesheka katika taasisi mbalimbali za kifedha kwa kukosa dhamana.

Haya yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa EFTA, Bwana Nicomed Bohay wakati alipokuwa akiutambulisha mpango huu wa mkopo wa Kuku kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, katika hafla iliyofanyika katika kiwanda ya kuzalisha kuku cha Silverland kilichoko USA-River jijini Arusha.

Bohay amesema, mpango huu wa mkopo wa kuku kwa vijana na wanawake bila dhamana pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali lakini unakwenda sambamba na malengo ya uanzishwaji wa taasisi yake wa kuwawezesha wajisiriamali na wakulima na hususani kutoka katika makundi hayo kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo ya EFTA inayotolewa bila dhamana.



“Vijana na wanawake wengi hawakopesheki katika taasisi zetu za kifedha kwa sababu wengi wao hawana dhamana ya kuwawezesha kupata mikopo hiyo, ndio maana sisi baada ya kuiona changamoto hii, tuliamua kuja na mpango wa kuwakopesha vifaranga vya kuku bila dhamana, Na tumechagua kuku kwa sababu uwekezaji wake ni wa muda mfupi na mkopaji ndani ya miezi michache anaanza kuona matunda ya uwekezaji wake”

“Kwa mfano kwa kuku hawa tunaowakopesha wakopaji wataweza kuanza kuwauza baada ya siku sitini, hii ni aina ya uwekezaji ambao unaweza kuona matunda yake ndani ya muda mfupi na ndio maana tunawahimiza vijana wengi na wanawake wajitokeze kuchangamkia fursa hii” amesema Bohay.

Bohay ameongeza kuwa katika mwaka wa kwanza wa mpango huu EFTA inategemea kutoa mkopo wa kuku 250,000 nchi nzima, ambapo mpaka sasa wamekwisha kabidhi zaidi ya Kuku 30,000 kwa wafugaji kutoka maeneo mbalimbali nchini.

“Tayari tumeanza mafunzo kwa wafugaji walio tayari kukopa na kwa waliohitimu mafunzo tayari tumeisha wakabidhi katika awamu ya kwanza ambayo wafugaji takribani 30, wamenufaika kwa kupata mkopo wa kuku zaidi 30,000. Hivyo niwahimize vijana wengi zaidi wajitokeze mikopo hii ni kwa ajili yako” Amesisitiza Bohay

Kwa kushirikiana na wazalishaji wa vifaranga vya kuku kama vile Silverland Ltd, na wengine EFTA itamwezesha mkopaji kupata mahitaji yote muhimu kama vile chakula, madawa na vifaa mbalimbali kama mkopo kwa wakati wote mpaka atakapokuwa tayari kuwapeleka kuku wake sokoni.

Kwa upande wake Meneja Masoko wa Silverlands Ltd, Bi.Mwanamvua Ngocho, ambao ni mojawapo wa wazalishaji wa vifaranga vya kuku ambao EFTA itashirikiana nao katika mpango huu kuhakikisha wafugaji wanapata vifaranga bora, chakula na chanjo ili kumhakikishia mfugaji anapata matokeo chanya kwa wakati.

"Hapo awali, wateja wetu walikuwa wafugaji wenye uzoefu na mitaji mikubwa. Lakini sasa, kwa ujio wa EFTA, fursa zaidi kwa vijana na wanawake zitafunguka, na sisi kwa kweli tuko tayari kuhakikisha kwanza tunatoa mafunzo makini ya namna ya kufuga kisasa, lakini pia kuzalisha vifaranga vya kuku vyenye ubora zaidi," alibainisha Ngocho.

“Tunatamani kuona watu wetu wanaimarika kiuchumi kwa kuwa wafugaji wa kuku, lakini pia afya ya jamii yetu ikiimarika zaidi kwa kula nyama na mayai ya kuku bora kutoka kwa wafugaji wetu, Na hii sasa ndio fursa ambayo naamini hakuna kijana wala mwanamke anaehitaji kujiajiri ataiacha impite” ameongeza Ngocho

Kwa upande wake kaimu katibu tawala msaidizi mkoa wa Arusha anaeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, Bwana Daniel Loroku, ameishukuru taasisi ya EFTA na kampuni ya Silverland kwa kuja na mpango huu wa kusaidia vijana na wanawake kupitia mikopo ya vifaranga vya kuku bila dhamana.

“Jukumu la serikali ni kuona kila mmoja wetu wetu anashiriki katika ujenzi wa taifa kwa kuchangia pato kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi tunazozifanya, hata hivyo changamoto ya mitaji kwa baadhi ya watanzania imekuwa ni kikwazo cha wao kuwa sehemu ya wachangiaji wa pato la Taifa” Amesema Bwana Loroku.

“Ujio wa EFTA na aina hii mpya ya mkopo wa vifaranga vya kuku bila dhamana, kwa kweli kwetu kama serikali ni fursa muhimu sana maana itasaidia kuwezesha kundi hili la vijana na wanawake kuweza kujikwamua kiuchumi maana sasa wataweza kuwa na shughuli za kufanya na ambazo zitawapatia kipato ndani ya muda mfupi” Ameongeza Bwana Loroku

Kwa upande wake Flora Danford Sando, mmoja wa wanufaika wa mpango huu, anaelezea namna ambayo fursa hii itakavyomsaidia katika kuyabadili Maisha yake na hasa baada ya kutafuta ajira kwa muda mrefu bila mafanikio.

"Baada ya kuhitimu masomo yangu, nilitafuta ajira, lakini kwa Bahati mbaya sikufanikiwa kupata kazi. Nilijaribu pia kutafuta mikopo katika mabenki ili nianze biashara lakini huko nako sikufanikiwa maana nilitakiwa kuwa na dhamana, Nikiwa katika hali ya kukata tamaa ndio nikapata Habari za uwepo wa mkopo huu kutoka EFTA bila dhamana” Anasimulia Sando

“Haraka sana niliwatembelea EFTA na wakanielezea taratibu zao ambazo nilizifuata, na baada yapo walinipeleka Iringa katika Chuo cha Ufugaji wa Kuku cha Silverlands, ambapo nilipata elimu ya namna bora ya kufuga kuku kisasa, Na leo Nimekabidhiwa rasmi vifaranga zaidi ya miatano ambavyo nitavifuga kwa siku 60, na kisha nitaviingiza sokoni, ambapo baada ya kuuza ndio nitakuja kulipa mkopo wangu” anaeleza Frola kwa furaha.

Mpango huu wa mkopo kwa wafugaji wa kuku nchini utakuwa ni sehemu ya mwarobaini wa changamoto ya ajira kwa vijana na wanawake maana utatoa fursa nyingi kwa vijana kujiajiri na hivyo kuwafanya vijana wengi kuwa sehemu ya wachangiaji katika uchumi wa Taifa.



Mkurugenzi wa EFTA, Bwana Nicomed Bohay akiwakabidhi, baadhi ya wanafufaika wa mkopo wa vifaranga vya kuku ambao kampuni hiyo imevitoa kwa wafugaji mbalimbali bila dhamana. Jumla ya vifaranga 30,000/= vimekabidhiwa kwa wafugaji wa kuku wapatao thelathini katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Bi Mwanamvua Ngocho, Meneja Masoko wa Kampuni ya Silverlands Tanzania Ltd, wazalishaji wa vifaranga bora vya kuku ambao wanahusika na kuzalisha vifaranga vinavyotolewa kwa mkopo na EFTA kwa wakulima mbalimbali nchini, akimuongoza mkurugenzi mtendaji wa EFTA, kutembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa vifaranga hivyo.

Mkurugenzi wa EFTA, Bwana Nicomed Bohay akiwakabidhi, baadhi ya wanafufaika wa mkopo wa vifaranga vya kuku ambao kampuni hiyo imevitoa kwa wafugaji mbalimbali bila dhamana. Jumla ya vifaranga 30,000/= vimekabidhiwa kwa wafugaji wa kuku wapatao thelathini katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Baadhi ya wanufaika wa mkopo wa vifaranga vya kuku kutoka EFTA, wakiwa katika picha ya pamoja na mkurugenzi mtendaji wa EFTA Bwana Nicomed Bohay, baadhi ya maafisa kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha, wakati wa hafla ya kuzindua utoaji wa mikopo ya kuku kwa wafugaji nchini. Picha na mpiga picha wetu.