Na Okello Thomas
Wadau wanaojishughulisha na matumizi ya kemikali Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya wamehimizwa kuzingatia Sheria na Kanuni za matumizi ya kemikali ili kuondokana na athari ambazo hujitokeza endapo kemikali hazitotumika kwa kuzingatia usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Batenga alitoa wito huo wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi salama wa Kemikali kwa wadau wanaojihusisha na shughuli za kemikali katika mafunzo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika leo katika Hoteli ya Omary City iliyopo wilayani Chunya.
“Kemikali hutumika katika uchimbaji na uchakataji wa madini, hivyo kemikali hizi zinahitaji uangalifu katika kutumia, kutunza ili kuepuka kusababisha madhara mbalimbali kwa watumiaji, wauzaji, wanyama na mazingira,” alisema Mhe. Batenga.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo ya usimamizi salama wa kemikali kwani uchimbaji wa madini huchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo Mamlaka iendelee kutoa elimu ya kemikali kwani wadau wapo wengi.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Elias Mulima amewataka wadau walioshiriki mafunzo ya usimamizi salama wa kemikali kuwa mabalozi kwa jamii lakini pia ametoa wito kwa wadau ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo, kuwa mafunzo hayo ni endelevu hivyo wawe tayari kushiriki wakati Mamlaka itakapotangaza tena.
“Hii elimu tutaendelea kutoa mara kwa mara kwa wadau na kuhakikisha kwamba kemikali zinatumika vizuri na hazileti madhara kwa watumiaji wenyewe, lakini pia na jamii inayowazunguka, alisema Mulima.
Naye Omary Hamisi kutoka kampuni ya Small Scale Miners - Chunya, ameishukuru Mamlaka kwa kuwafikia na kuwapa elimu ya matumizi salama ya kemikali kwa sababu wamekutana na mambo mengi ya kigeni kwenye masuala ya matumizi ya kemikali ikiwemo kuzifahamu sheria, alama za kemikali, utunzaji na namna ya utumiaji wa kemikali hatarishi.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Batenga, (aliyesimama) akiongea wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi wa Kemikali kwa wadau mbalimbali wanaojishughulisha na kemikali katika Mkoa wa Kimadini Chunya, katika Hotel ya Omary City Chunya, Novemba 07, 2024
Meneja, Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Elias Mulima, akiongea kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, kufungua mafunzo ya Usimamizi wa Kemikali kwa wadau wanaojishughulisha na kemikali katika Mkoa wa Kimadini Chunya, yaliyofanyika katika Hotel ya Omary City Chunya, Novemba 07, 2024.
Meneja Mulima amesema kuwa mafunzo hayo siku mbili kuanzia Novemba 07-08, 2024 katika Mkoa wa Kimadini Chunya, yamelenga kujenga uelewa wa pamoja kwa wadau mbalimbali wanaoshughulika na matumizi ya kemikali kuhusu matumizi yaliyo salama ya kemikali kwa afya zao na Mazingira kwa ujumla.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Chunya, Eng. Laurent Mayale , akiongea kuwasalimu washiriki wa mafunzo ya Usimamizi wa Kemikali kwa wadau wanaojishughulisha na kemikali katika Mkoa wa Kimadini Chunya.
Mwenyekiti wa Wachimbaji madini Mkoa wa Mbeya, Saddam Kyando akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wengine wa mafunzo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Usimamizi wa Kemikali kwa wadau wanaojishughulisha na kemikali katika Mkoa wa Kimadini Chunya
Washiriki wa mafunzo kutoka Mkoa wa Kimadini Chunya, wakimsikiliza Mgeni rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Batenga (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya Usimamizi wa Kemikali kwa wadau wanaojishughulisha na kemikali katika Mkoa wa Kimadini Chunya.
Watumishi wa Mamlaka kutoka Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Georgina Kilindo, (picha ya juu) na Jansen Bilaro, (picha ya chini) wakiwasilisha mada wakati wa mafunzo ya Usimamizi wa Kemikali kwa wadau wanaojishughulisha na kemikali katika Mkoa wa Kimadini Chunya.
Munisi Jonas kutoka kampuni ya Anglo De Beer (pcha ya juu, aliyesimama) na Paschal Kalonga kutoka Kampilipili Gold Family (picha ya chini, aliyesimama) wakitoa maoni yao kwenye mafunzo ya Usimamizi wa Kemikali kwa wadau wanaojishughulisha na kemikali katika Mkoa wa Kimadini Chunya.
Washiriki wa Mafunzo ya Usimamizi wa Kemikali, Michael Makosa (picha ya juu aliyesimama) na Bahati Muhanga (picha ya chini aliyeshika kipaza sauti) wakiuliza maswali mbalimbali baada ya mawasilisho ya mada.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbaraka Batenga, (katikakati waliokaa) akiwa na wadau mbalimbali wanaojishughulisha na masuala ya kemikali katika Mkoa wa Kimadini Chunya baada ya kufungua mafunzo ya siku mbili ya Umsamizi wa kemikali Omary City Hotel Chunya, Novemba 07,2024