PROFESA KITILA MKUMBO ATEMBELEA MTAMBO WA KUZALISHIA MAJI WA RUVU JUU

April 20, 2017

Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji ametembelea Tenki la Maji la terminal lilipo karibu na chuo kikuu cha ardhi ambalo linapokea maji kutoka mtambo wa Ruvu na chini.

Pia ametembelea tenki kubwa jipya la Maji lilipo Kibamba Luguruni ambalo linapokea maji kutoka mtambo wa Ruvu juu na ametembelea Ofisi za Dawasco Mkoa wa Kibaha na kumalizia ziara yake kwa kutembelea mtambo wa kuzalishia Maji wa Ruvu juu ambapo umeanza kuzalisha maji mapya leo.
 Katibu mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo akiwa ameambatana na Ofisa Mtendaji mkuu Dawasco,mhandisi, Cyprian Luhemeja katika ziara ya kutembelea   Mtambo Ruvu juu uliopo mkoani Pwani.
 Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa DAWASA, mhandisi Romanus Mwangingo, akitoa maelezo mafupi kwa Katibu mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo kuhusu tenki jipya la Maji lilipo Kibamba Luguruni ambalo linapokea maji kutoka mtambo wa Ruvu juu mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea Mtambo huo wa uzalishaji Maji wa Ruvu juu uliopo Mlandizi, mkoani Pwani. Picha na Emmanuel Massaka, Globu ya jamii.
 Ofisa Mtendaji mkuu Dawasco, mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa maelezo mafupi kwa Katibu mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo katika ziara ya kutembelea Mtambo Ruvu juu uliopo mkoani Pwani.
 Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji

HIVI NDIVYO INTANETI INAVYOATHIRI MAISHA YAKO YA KILA SIKU

April 20, 2017



Na Jumia Travel Tanzania

Hakuna kitu kinachoudhi kama kuwa sehemu na marafiki, familia au ndugu lakini unakuta kila mtu ameinamia skirini ya simu yake! Kwa kiasi kikubwa kuja kwa mtandao wa intaneti kumewafanya watu kujikita zaidi na simu zao badala ya watu au kufaidi mazingira yanayowazunguka.

Kuna tafiti nyingi zimekwishafanyika na kuthibitisha kuwa muda mwingi unaotumika kwenye intaneti una madhara kama vile ya kimwili na kiakili. Mbali na kuwepo kwa faida lukuki za mtandao huo, Jumia Travel ingependa kukujulisha kuwa yafuatayo yanaweza kukumba endapo utautumia vibaya: 
Intaneti husababisha hali ya kujisikia vibaya, kukosa furaha na wivu. Mtu anaweza kushangaa na kujiuliza hii inaweza kutokeaje. Jibu ni rahisi sana. Mambo tunayoyaona kwenye mitandao ya kijamii yanayowekwa na watu maarufu, ndugu, jamaa au marafiki wa karibu huweza kukukosesha furaha kwa namna moja ama nyingine. Hebu jaribu kufikiria unamuona rafiki yako wa karibu ameweka picha zake akiwa amesafiri sehemu ambayo wewe hujawahi kufika au chakula usichowahi kukila utajisikiaje? Ingawa sio wote wanaoweza kujisikia vibaya lakini kwa asilimia kubwa wengi wao hupatwa na wivu au kusononeka nafsi kuona kwamba inawezakana wao wasije kuwa na maisha kama yale. 
Intaneti husababisha watu wengi kujihisi kuwa wanapitwa na wakati. Tangu enzi za kale kila nyakati zimekuwa na mitindo tofauti ya maisha hapa duniani. Kwa bahati mbaya sio watu wote ambao wanao uwezo wa kuendana na mitindo au fasheni zilizopo. Hali hii imewafanya wengi kujihisi kupitwa na wakati endapo wasipoishi kama wanavyoona kwenye mitandao. Kupitia mitandao ya kijamii kama vile Instagram watu wanaweza kuwashirikisha wenzao picha na video za namna wanavyoishi kuendana na wakati. Ambapo mara nyingi yale yanakuwa sio uhalisia wa maisha yao.    

Intaneti imekuwa ni chanzo kikubwa kwa watu wengi kutokuwa na utulivu wa akili. Nadhani hii hali inawakuta watu wengi katika maisha yao ya kila siku katika ulimwengu wa sasa wa intaneti. Kuna wakati unajaribu kujikita kwenye suala fulani lakini shughuli zinazoendelea mtandaoni kupitia simu yako ni kikwazo kikubwa. Kwa mfano, unataka kukamilisha kazi uliyopewa na bosi wako, mara ujumbe wa Whatsapp umeingia, hujatulia Facebook, Twitter na Instagram nazo zote zinakujulisha kuwa unapitwa huku. Kwa hali hii sidhani kama kuna jambo ambalo mtu anaweza kulikamilisha kwa ufanisi na usahihi unaohitajika.
Intaneti inawanyima watu fursa ya kufurahia maisha halisi yanayowazunguka. Kwa sasa ni jambo la kawaida kabisa sasa kuona familia imekwenda hotelini kupata chakula pamoja na kubadilisha mazingira ya nyumbani lakini ukakuta kuanzia watoto mpaka wazazi wote wameinamisha nyuso zao kwenye skirini za simu zao. Hakuna tena ile hali ya zamani kwamba muda wa chakula ndipo familia hukutana kwa pamoja, kuzungumza, kucheka na kubadilishana mawazo juu ya yale waliyoyapitia siku nzima. Kwa hali ilivyo sasa hivi huwezi kusikia tena vicheko au gumzo kwenye familia nyingi kwani vyote hivyo vimeamia kwenye simu. Usishangae ukamuona mtu anacheka mwenyewe ukadhahania ni punguani, hapana, ni mambo ya intaneti hayo.

Intaneti imekuwa ni chanzo kikubwa cha watu kutokuwa wabunifu katika masuala mbalimbali. Hebu jaribu kufikiria ingekuwaje kama hizo video unazozitazama kupitia YouTube, habari unazoziona Facebook au Twitter, au picha unazoziona kupitia Instagram; vyote hivyo ungevipataje kama waliogundua nao wangekuwa wanatumia muda wao kwenye intaneti kupitia kazi za wenzao. Hii inamaanisha kwamba hatupaswi kutumia muda mwingi kuwa watumiaji wa vitu vya kwenye intaneti badala yake nasi tuwe wazalishaji ili kuwanufaisha na wengine zaidi. Unaweza kukuta mtu tangu siku inaanza mpaka inaisha yeye anaimaliza kwenye mitandao ya kijamii akipitia, kutazama na kusoma habari za watu wengine.
Yaliyozungumzwa katika makala haya ndio maisha ya wengi kwa sasa jinsi yalivyoathiriwa na kuja kwa intaneti. Lakini zipo mbinu kadhaa za kuweza kujiepusha na madhila hayo yote. Jumia Travel inashauri kwamba jukumu la mtu kuepukana na uraibu wa matumizi ya intaneti ni la kwake mwenyewe. Kwa mfano, kujiwekea au kutenga muda maalumu wa kuingia mtandaoni, kuzima ishara zitokanazo na mitandao ya kijamii au kuzima kabisa intaneti kwenye simu yako mpaka muda fulani inaweza kusaidia pia.   

Mshindi wa Biko apokea fedha zake

April 20, 2017
Ofisa wa Benki ya NMB kushoto akimkabidhi kadi yake ya benki mshindi wa shindano la bahati nasibu ya Biko baada ya kushinda Sh Milioni 10 za shindano hilo nchini Tanzania. Anayeshuhudia kulia ni Meneja Masoko wa Biko, Goodhope Heaven. Makabidhiano hayo ya fedha na kadi ya benki kwa mshindi huyo yalifanyika Makao Makuu ya benki ya NMB kama sehemu ya kumuandaa mshindi wa Biko kuzitumia fedha zake kwa uangalifu ili zimnufaishe kiuchumi.

Mshindi wa Biko Milioni 10 apokea fedha zake na elimu NMB

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSHINDI wa shindano la bahati nasibu ya Biko ‘Ijue Nguvu ya Buku’, Christopher Mgaya, jana amepokea fedha zake sambamba na kupewa elimu ya kifedha kutoka Benki ya NMB ambapo alifunguliwa akaunti ya kuhifadhia fedha hizo.

Mgaya alitangazwa mwishoni mwa wiki katika droo ya kwanza ya kumtafuta mshindi wa Sh Milioni 10, droo iliyochezeshwa na Balozi wa Biko Tanzania, Kajala Masanja akishirikiana na mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Juhudi Ngolo, jijini Dar es Salaam.

Mshindi wa Sh Milioni 10 wa mchezo wa kubahatisha wa Biko, Christopher Mgaya, akisikiliza wakati Meneja Masoko wa Biko Tanzania, wachezeshaji wa bahati nasibu ya Ijue Nguvu ya Buku, Goodhope Heaven, wakati anafanya mazungumzo na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam. Fedha hizo alikabidhiwa jana Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam sambamba na kupewa elimu ya kifedha ili fedha hizo zimnufaishe kiuchumi na kubadilisha maisha yake.


Nia ya kufunguliwa akaunti katika tawi la NMB Makao Makuu jijini Dar es Salaam sambamba na kupatiwa elimu ya kifedha kwa mshindi huyo limetokana na kiu ya kumuandaa kijana huyo ili aweze kuzitumia ipasavyo fedha zake kwa ajili ya kumuinua kiuchumi kutokana na uwapo wa mchezo wa bahati nasibu huo unaochezwa kwa kufanya miamala ya kifedha kwenye Tigo Pesa, Mpesa na Airtel Money.


Ofisa wa NMB akimkabidh mshindi wa Biko kadi yake ya ATM ya benki hiyo tayari kwa matumizi yake.

Mshindi wa Sh Milioni 10 wa mchezo wa kubahatisha wa Biko, Christopher Mgaya, akipokea fedha zake alizoshinda baada ya kutangazwa mwishoni mwa wiki na kukabidhiwa mapema jana Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam sambamba na kupewa elimu ya kifedha ili fedha hizo zimnufaishe kiuchumi na kubadilisha maisha yake. Kulia kwake ni Meneja Masoko wa Biko Goodhope Heaven.

Akizungumza katika ufunguzi wa akaunti ya mshindi wao huyo jana jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko wa Biko, Goodhope Heaven, alisema kwa mshindi wao wa Sh Milioni 10 wameona wasimuache hivi hivi badala yake wakaamua kumfungulia akaunti NMB sanjari na kupatiwa elimu ya kifedha ili zimuendeleze kimaisha.

“Biko ushindi ni nje nje kwa kuwa lengo letu ni kuwafanya Watanzania wafanikiwe kimaisha kwa kuutumia vema mchezo wetu huu kwa kuingia kwenye kipengele cha lipa bili kwenye simu zao za Mpesa, Tigo Pesa na Airtel Money kisha kuingiza namba ya kampuni 505050 na kumalizia namba ya kumbukumbu ambayo ni 2456.

“Biko tunalipa kwa haraka kwa zawadi za papo kwa hapo kuanzia Sh 5000, 10,000, 20,000, 50,000, 100,000, 500,000 na sh Milioni moja, huku zawadi ya ushindi wa Sh Milioni 10 inayopatikana kwa kuchezeshwa droo kila mwisho wa wiki italipwa kwa njia ya hundi na kumuingizia fedha zake benki kama tulivyofanya kwa mshindi wetu Mgaya aliyeibuka na ushindi kutokea Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam,” Alisema.

Naye Mgaya alisema kwamba anawashukuru Biko kwa kumpatia zawadi yake kwa haraka sambamba na kumpeleka NMB ili apatiwe elimu namna gani atazitumia fedha hizo ili zimuendeleze badala ya kuzitumia kwa matumizi yasiyokuwa ya lazima.

“Wakati nashiriki kucheza Biko sikutaraajia kama ningeshinda, lakini baada ya awali kushinda pia Sh 5000, nilihamasika na kuendelea kucheza ambapo Jumapili sikuamini baada ya kupigiwa simu na Kajala akinitaarifu kuwa nimeshinda Sh Milioni 10, ushindi ambao hakika utanitoa sehemu moja kwenda nyingine hususan kwa kukamilisha ujenzi wa nyumba.

“Nawashukuru Biko huku nikiwakumbusha Watanzania wenzangu kuchangamkia fursa ya bahati nasibu ya Biko kwa sababu haiitaji kujua lolote zaidi ya kucheza kwa njia ya ujumbe wa simu na kuingiza miamala kiasi cha Sh 1000 na kuendelea, huku kila Sh 1000 tunayolipa ikitupatia nafasi mbili, zawadi za papo kwa hapo pamoja na nafasi ya kuingia moja kwa moja kwenye droo ya kubwa ya wiki yakuwania Sh Milioni 10,” Alisema Mgaya.

Bahati nasibu ya Biko imeanza kwa kasi kubwa nchini Tanzania, ambapo mbali na kumpatia zawadi yake ya Sh Milioni 10 mshindi wao, pia inaendelea kulipa fedha mbalimbali walizoshinda washiriki wao kwa haraka hali inayoongeza msisimko mkubwa kwa washiriki na Watanzania kwa ujumla.