WAZIRI KAIRUKI AKAGUA MABANDA YA MAADHIMISHO YA SIKU YA MISITU DUNIANI NA SIKU YA UPANDAJI MITI KITAIFA

March 20, 2024

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) leo Machi 20, 2024 amekagua mabanda ya Maonesho yatakayotumika katika Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika Machi 21 ambapo Mgeni Rasmi katika Kilele hicho anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.


Akitembelea mabanda yaliyopo kwenye Maonesho hayo, Mhe. Kairuki ameipongeza Wizara pamoja na Wadau wa misitu waliojitokeza kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu majukumu yanayotekelezwa na taasisi zao ikiwemo elimu ya uhifadhi pamoja na kuonesha bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na mazao ya misitu.

Mhe.Kairuki ametumia fursa hiyo kuwataka Wakazi wote wa Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro pamoja na Mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho hayo.

Amesema maonesho hayo ni muhimu kwao kwani wataweza kujifunza masuala mbalimbali ikiwemo elimu ya ufugaji nyuki kibiashara pamoja na kujua fursa mbalimbali zinazopatikana katika mnyororo wa thamani ya mazao ya misitu.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji miti Kitaifa hufanyika kila mwaka Machi 21ambapo kwa mwaka huu Tanzania inaadhimisha Kilele hicho kwa kupanda miti pamoja na kutembelea maonesho ya bidhaa mbalimbali zitokanazo na misitu na nyuki.



PPRA YAANZISHA OFISI TANO ZA KANDA KUSOGEZA HUDUMA KWA WANANCHI.

March 20, 2024

 MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imefungua Ofisi katika kanda tano nchini na kuwa na jumla ya kanda sita, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusogeza huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika kusimamia sekta ya ununuzi wa umma.


Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bw. Eliakim Maswi katika kikao cha wafanyakazi wa Mamlaka kilichohudhuriwa na Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) ngazi ya Mkoa, kilichofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.

Amezitaja ofisi hizo za Kanda kuwa ni Kanda ya Ziwa (Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza), Kanda ya Kati (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora), Kanda ya Kaskazini (Jengo la PSSSF jijini Arusha), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Jengo la NHIF jijini Mbeya) na Kanda ya Kusini (Jengo la PSSSF mjini Mtwara). Orodha hiyo inafanya Mamlaka kuwa na jumla ya ofisi sita za kanda kwa kujumlisha na ofisi ya kanda ya Pwani iliyopo jengo la Wizara ya Fedha Jijini Dar es salaam iliyokuwepo awali.

‘’Naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Mamlaka kusogeza huduma kwa wananchi. Hii ni sehemu ya mafanikio ya miaka mitatu ya uongozi wake. Sasa wananchi hawatakuwa na ulazima wa kuja Dodoma ili wafike PPRA, kila kanda watahudumiwa kikamilifu,” alisema Bw. Maswi.

Ameongeza kuwa kila Kanda imewezeshwa kuwa na wafanyakazi wa idara zote ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji ya wananchi na wadau wa sekta ya ununuzi katika maeneo yao, akisisitiza kuwa wameweka nguvu pia kwenye utoaji wa huduma za Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST).

Aidha, amewasihi wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kuendelae kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia uzalendo ili kufanikisha malengo ya serikali ya kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana kwenye ununuzi wa umma.

“Ninawaomba watumishi wenzangu mwende mkatengeneze uhusiano mzuri katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka, hii itawasaidia kuendelea kuaminika kwa wananchi na mtapata ushirikiano mkubwa kwa viongozi wa mikoa hiyo,” amesisitiza.

Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Bw. Maulid Kipeneku ametoa rai kwa wafanyakazi PPRA kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi, kwa kuzingatia sheria na taratibu. Aliwapongeza wafanyakazi hao kwa jinsi wanavyotoa huduma kwa wananchi, na kwamba anaamini wafanyakazi hodari watapatikana ndani ya Mamlaka hiyo.

DKT. MOLLEL DARAJA LA MAENDELEO KWA WANANCHI WA SIHA

March 20, 2024

 Wananchi wa Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro wamempongeza Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Godwin Mollel kwa kuwa daraja la maendeleo kati ya wananchi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Hayo yamebainishwa na Baadhi ya wananchi wa Jimbo la Siha waliojitokeza wakati wa mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Siha, Dkt. Godwin Mollel wakusikiliza kero za wananchi wake katika viwanja vya Rex Sanya juu Machi 19,2024 wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro

Wamesema kuwa Dkt. Mollel amekuwa kiungo kizuri na imara kwenye kutatua changamoto kadha za Wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kwa wagonjwa wanaozuiliwa Hospitali kwa kushindwa kulipa gharama za matibabu wanazodaiwa.

Aidha wamempongeza kwa mchango wake wa hali na mali ambao umesaidia baadhi ya familia kuwatoa ndugu zao Hospitali kwa kudaiwa gharama za matibabu ambazo wameshindwa kulipa.

“Sisi wakazi wa Siha tuna kila sababu ya kukupongeza na kukuombea ili Mwenyezi Mungu aendelee kusimamia yale maono mema kwa watu wa Siha yaendelee kutimia” mwananchi ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Hata hivyo wamesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia akiwa madarakani shule mbali mbali ikiwemo shule ya wasichana ya Kilimanjaro, vituo vya Afya pamoja pamoja barabara zimejengwa na zinaendelea kujengwa pamoja na veta.

Naye Bi. Lilian Malya mmoja ya Wananchi hao amesema kupitia Dkt. Mollel mtoto wake Lilian Samweli Malya

Mtoto Nickson Emanuel (7) alimpeleka kupata matibabu ya moyo katika Taasisi ya moyo ya Jakaya (JKCI) Dar esalaam ambapo alitakiwa kulipia kiasi cha Shilinhgi Milioni 22 kwa ajili ya gharama za matibabu ya mtoto huyo.

“Pamoja na kusaidia gharama za matibabu pia ameahidi kumsomesha ni jambo la kumshukuru sana na Mungu amfanyie wepesi katika majukumu yake, hizi fedha ni nyingi ni msaada mkubwa amenisaidia na aendelee kuwasaidia wengine wenye uhitaji katika jamii”, ameeleza Bi. Liliani.

Naye Diwani wa viti maalumu Bi.Egger Nzao, amesema kwamba Mbunge Dkt. Mollel ameweza kuwasaidia wagonjwa wengi kwa kusimamia gharama za matibabu na kuhakikisha wale watu wanatoka Hospitali

“Kwa namna ya kipekee tunampongenza anafanya kazi kubwa na aendelee kuwasaidia watu wa Siha mbali na matibabu anadhamini watoto zaidi kupata masomo ndani ya jimbo la Siha”, amesema Bi. Egger

Mbunge wa Siha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka Wananchi kumuunga mkono katika majukumu yake ya kuwaletea maendeleao Wakazi wa Siha.