Na Oscar Assenga, Tanga.
KOCHA Mkuu wa timu ya Coastal Union ,Hemed Morroco amesema
watahakikisha wanajipanga vyema ili kuweza kuchukua pointi tatu muhimu kwenye mechi yao ya
ufunguzi wa Ligi kuu Tanzania bara dhidi yao na JKT Oljoro itakayochezwa Agosti
24 katika uwanja wa Sheirh Amri Abeid mkoani Arusha.
Morroco alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na blog hii ambapo alisema mechi za majaribio walizocheza zimempa mwanga mzuri wa
kujua kikosi chake kinahitaji kitu gani kabla ya kuanza msimu mpya wa ligi kuu.
Alisema kutokana na usajili mzuri ambao ulifanywa na timu
hiyo matumaini yake ni kuchukua ubingwa wa ligi hiyo ili kuweza kucheza kombe
la shirikisho kwani hayo ni malengo yake ya kucheza kombe hilo siku zijazo.
Morroco alisema wanatarajia kuondoka mkoani hapa siku moja
kabla ya mechi yao na Oljoro JKT na kueleza watakachokwenda kukifanya mkoani
Arusha ni kufuata pointi tatu muhimu.
Wakati huo huo,Timu ya 3 Pillars ya Nigeria na Coastal Union
ya Tanga jana zilishindwa kutambiana baada ya kulazimishana sare ya
kutokufungana katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Mkwakwani
mjini hapa.
Mchezo huo ulianza kwa kasi ambapo kila timu ilikuwa
ikilishambulia lango la mwenzie kwa zamu ambapo mpaka kipindi cha kwanza
kinamalizika timu hizo zilitoka nguvu sawa licha ya Coastal Union kuonekana
kukosa mabao ya wazi kutokana na wachezaji wake kukosa umakini.
Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mechi hiyo baadhi ya
wadau wa soka mkoani hapa waliojitokeza walisifu kiwango kilichoonyeshwa na
timu ya Coastal Union ambacho kilicheza vema licha ya kushindwa kufunga mabao.