SERIKALI HAITAWAVUMILIA WAWEKEZAJI WENYE VIWANDA WANAOCHAFUA MAZINGIRA – MPINA

September 19, 2017

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe . Luhaga Mpina kushoto akimsikiliza Mratibu wa Kanda ya Mashariki kutoka NEMC Bwana Jafari Chimgege alipokuwa akizungumzia suala la utunzaji wa mazingira na ukiukwaji wa sheria ya Mazingira katika eneo la Viwanda Mikocheni jijiniDar es Salaam.
Sehemu ya taka ya vyuma chakavu katika kiwnda cha Iron and Steel Limited jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina akiongea na vyombo vya habari baada ya ziara ya ukaguzi wa baadhi ya viwanda jijini Dar es Salaam Leo.

NA ; EVELYN MKOKOI,  DAR ES SALAAM
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Masuala ya Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina, amesema Serikali haitawavumilia wawekezaji wenye viwanda wanaokiuka sheria za nchi hasa ya uchafuzi wa mazingira.

Mpina ameyasema hayo leo alipokuwa katika ziara  ya kikazi jijini Dar Es Salaam ya uzingatiaji wa sheria ya Mazingira alipotembelea eneo la viwanda mikocheni katika kiwanda cha Iron and Steel Limited, BIDCO limited na Basic elements Limited.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo Mpina alisema  yeye na team yake katika ziara hiyo wamebaini uvunjifu mkubwa wa sheria katika uchafuzi wa mazingira kwenye viwanda hivyo na kiwanda cha Iron Steel na Basic Limited , kila kimoja kimetozwa faini ya sh. Milioni 10 inayotakiwa kulipwa ndani ya wiki mbili na kutakiwa kufanya marekebisho ya mfumo.
Katika kiwanda cha utengenezaji bidhaa ya  Unga wa ugali cha Basic Element alisema kwa kushirikiana na wataalamu wa mazingira wamebaini wamiliki wa kiwanda hicho wamekiuka kanuni kwa kuziba mfereji wa maji taka.
“Kilichofanyika hapa hakikubaliki na hakiwezekani kufumbiwa macho walichokifanya wamiliki wa kiwanda hiki ni ukiukwaji wa sheria na wamesababisha wananchi wengi waishi katika mazingira hatarishi haiwezekani kuziba mfereji mkubwa kama huu ambao maji taka mengi yalitakiwa kusafiri ikiwemo kutoka viwanda vingine ni hatari,”alisema.
Alisema awali kabla ya kiwanda hicho kujengwa ulikuwepo mfereji huo hivyo ni vyema wenye kiwanda wangeshirikiana na Baraza la Mazingira NEMC kutafuta njia bora ya maji hayo kusafirishwa Kwenye mfumo wa majitaka wa DAWASCO bila kuathiri mazingira.
“Lengo  ni kukomesha kabisa uchafuzi wa mazingira kwa wenye viwanda utokanano na majitaka na moshi viwandani , kwani una athari kubwa kwa mazingira na viumbe hai vingine.” Alisisitiza Mpina.
Kwa upande wake Mratibu wa Mazingira Kanda ya Mashariki kutoka Baraza la taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Bw. Jaffar Chimgege alisema kuwa katika kiwanda cha Iron Still Limited imebainika kuwa wafanyakazi  wa kiwanda hicho hawana  vifaa vya vya usalama kazini kitendo ambacho kinatishia afya zao.

Aidha alisema kiwanda hicho kinatakiwa kurekebisha mfumo wa utoaji moshi kiwandani hapo pamoja na kupima moshi kiwango cha ubora wa hewa pamoja na kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa mazingira ya robo mwaka NEMC, Pamoja na kuajiri Afisa mazingira atayewashauri kuhusu masuala yote ya mazingira.
Baadhi ya wakazi wa Eneo la Mikocheni ‘B’ akiwemo Kanali Mstaafu wa Jeshi Bw. Lameck Meena alisema kuwa kama mkazi wa eneo hilo ana mashaka na wasi wasi wa afya ya familia yake na mazingira kwa ujuma kutokana na sababu kuwa moshi majitaka na vumbi linatoka katika baadhi ya viwanda hivyo siyo rafiki na kushauri wamiliki wenye viwnda hivyo kukaa karibu na wataalamu kuona namna ya kuweza kutatua changamoto hizo na kunusuru maisha ya wakazi na mazingira
TANZANITE YAREJEA KUJIPANGA DAR

TANZANITE YAREJEA KUJIPANGA DAR

September 19, 2017
Timu ya Taifa ya wasichana wenye umri wa chini ya miaka 20 (Tanzanite), imewasili salama nchini ikitokea Nigeria ambako ilicheza mechi ya awali dhidi ya wenyeji Nigeria katika mchezo wa kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Ufaransa.
Timu hiyo iliwasili saa 9.00 usiku wa kuamkia Jumanne Septemba 19, 2017 na kulakiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Kidao Wilfred; Bw. Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano, Bw. Jonas Kiwia na Ofisa Habari wa TFF, Bw. Alfred Lucas.

Mara baada ya kurejea, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sebastian Nkoma, amesema walipoteza mchezo wa awali kwa kufungwa mabao 3-0 kwa sababu Nigeria ni timu bora na Tanzanite kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

“Kwa kuwa tulionesha kiwango bora, ni matumaini yangu kwamba tutafanya vema kwenye mchezo wa marudiano hapa nyumbani na tutasonga mbele,” amesema Nkoma ambaye ndoto zake ni kuipeleka Tanzanite Ufaransa mwakani.

Mchezo wa marudiano utafanyika Oktoba mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam, ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

Wakati timu ikionekana ina ari ya kufanya vema kwenye mchezo wa marudiano, Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Kidao Wilfred aliwapa shime kufanya vema kwenye mchezo wa kirafiki na kusisitiza kambi kuendelea mpaka mchezo wa maruadiano.

Mkuu wa Msafara, Bi. Amina Karuma, alisema kuwa mapambano bado yanaendelea na anaamini kikosi chake kitashinda katika mechi ya marudiano itakayochezwa baada ya wiki mbili. Karuma pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Tanzania (TWFA).
NAIBU WAZIRI ATEMBELEA TFF, SERENGETI BOYS

NAIBU WAZIRI ATEMBELEA TFF, SERENGETI BOYS

September 19, 2017
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Anastazia Wambura jana Jumatatu Septemba 18, 2017 ametembelea Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
Mhe. Naibu Waziri Anastazia Wambura ambaye aliongozana na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Bw. Mohammed Kiganja alilakiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Kidao Wilfred.

Mhe. Naibu Waziri Anastazia Wambura alifanya mazungumzo na Kidao kwa muda ambako alijifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ripoti ya utendaji katika mwezi mmoja tangu uongozi mpya wa TFF uingie madarakani.

Mhe. Naibu Waziri baada ya kupata maelezo ya Utendaji kwa Uongozi mpya amepongeza Uongozi mpya kwa kuanza vizuri na ameridhishwa na mipango ya Uongozi mpya katika program za Vijana na Soka la Wanawake.

Pia amepongeza zoezi la Ugawaji wa mipira 100 kwa mikoa yote ya Tanzania na kusema muhimu ni kutumika ilivyokusudiwa. Anaamini mwanzo mzuri wa Rais Wallace Karia ni dalili njema za kuleta maendeleo makubwa katika soka.

Mbali ya kuzungumza na Kaimu Katibu Mkuu, Naibu Waziri Wambura alikuwa shuhuda wa mazoezi ya jioni ya Timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Mara baada ya mazoezi hayo, Naibu Waziri Anastazia alikaribishwa kuzungumza na vijana wa Serengeti Boys, ambako awali kabisa alitaka vijana hao ambao wengi wao wana umri wa chini ya miaka 15 kwa sasa kuwa ni wenye thamani.

“Mtakumbuka kamba kwee Umitashumta mlikuwa wengi, ila mmebaki ninyi. Nataka mjue kuwa Serikali iko hapa na tunafuatilia. Tunataka matunda kutoka kwenu,” amesema Naibu Waziri, huku akiwapa salamu za Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dk. Harrison Mwakyembe.

Akaongeza: “Nawapongeza sana kwa kuonesha mnaweza. Ila fanyeni mazoezi kwa juhudi, chezeni mpira kwa uhodari, ila msisahau kuzingatia pia masoma. msifanye masihara hata kidogo. Mkizingatia masomo na kucheza mpira, mtafanya makubwa zaidi.

“Naamini baada ya kambi hii mtakuwa vizuri. Je, kwenye mashindano yajayo mtashika namba gani?” alihoji Naibu Waziri Wambura kabla ya vijana kwa pamoja kujibu: “Namba moja.”
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), liliiteua Tanzania kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tayari Tanzania imeanza kuandaa timu.

PROF. MAGHEMBE ATOA SIKU 40 KWA WALIOLIMA NDANI YA HIFADHI YA TAIFA YA ARUSHA WAONDOKE KWA HIARI

September 19, 2017
Na HAMZA TEMBA - WMU
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa ya Arusha kuhakikisha kuwa wananchi wote waliolima ndani ya eneo la hifadhi hiyo kinyume cha sheria wanaondoa mazao yao pamoja na kusitisha kabisa shughuli zozote za kibinadamu ndani ya hifadhi hiyo.  

Prof. Maghembe ametoa agizo hilo jana wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyopo wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na hifadhi hiyo ikiwemo maeneo yenye mgogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.

"Naagiza, kuanzia leo ni marufuku mtu yeyote kuonekana akilima katika eneo hili, wekeni askari hapa, atakayeonekana piga pingu, hatuwezi kushuhudia watu wanalima ndani ya hifadhi tukae kimya, ni lazima tuchukue hatua. Watangaziwe na wapewe muda wa kuondoa mazao yao, ndani ya siku 30 au 40 wawe wameshaondoka", alisisitiza Prof. Maghembe baada ya kukagua eneo hilo.

Awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa Waziri Maghembe, Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga alisema eneo hilo ambalo pia linajulikana kama shamba namba 40 na 41 limekuwa na mgogoro tangu mwaka 1990 baada wananchi wa Kijiji cha Olkung'wado kuvamia eneo hilo huku wakitoa hoja kadhaa ikiwemo madai kuwa shamba hilo ni maeneo yao ya asili waliyokuwa wakimiliki tangu zamani.

Alisema hoja nyingine wanazozitoa ni kuwa walipewa mashamba hayo na Serikali wakati wa operesheni ya uanzishwaji wa vijiji mwaka 1975 na 1976, Aidha, hoja nyingine ni kuwa hawakushirikishwa kwenye mchakato wakati wa ugawaji wa mashamba hayo na kwamba TANAPA pia haina hati miliki ya mashamba hayo.

Ngada alisema hoja zote hizo zilikinzana na ukweli ya kwamba shamba hilo lilimilikishwa kwa TANAPA tangu mwaka 1980 baada ya kutolewa tangazo kwa wadau wanaoweza kuliendeleza kufuatia muwekezaji wa awali, James Preston Mallory kushindwa kuliendeleza na hivyo kufutiwa hati miliki na Mhe. Rais mnamo mwaka 1979.

“Wadau mbalimbali waliomba umiliki wake ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Halmashauri ya Kijiji cha Olkung'wado, lakini Kamati ya Ushauri ya Ardhi ya Mkoa wa Arusha ikaishauri Serikali mashamba hayo yamilikiwe na TANAPA na hivyo tukaandikiwa barua rasmi ya kukubaliwa kupewa shamba na Idara ya Ardhi Mkoa” alisema Ndaga.

Alisema TANAPA ilinunua eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 966 kwa lengo la kupanua hifadhi ya Taifa ya Arusha ambapo baada kupewa shamba hilo, iliagizwa kulipa fidia ya mali zilizokuwepo, mwaka 1983 tathmini ikafanyika na malipo yakalipwa Serikalini hatimaye TANAPA ikapewa barua ya kumiliki ardhi mwaka 1988. Alisema kwa upande wa Kijiji hicho cha Olkung'wado hakuna nyaraka yeyote inayoonesha shamba hilo kupewa kijiji hicho. 

Mhifadhi huyo alisema baada ya mgogoro wa muda mrefu, wataalam wa TANAPA walifanya survey katika shamba hilo ili kubaini maeneo yaliyo na shughuli nyingi za kibinadamu na yale yenye umuhimu zaidi kiikolojia, mapendekezo yalitolewa kuwa maeneo yenye shughuli nyingi za kibinadamu yaachwe kwa wananchi na yale yenye umuhimu kiikolojia yaendelee kuhifadhiwa, Bodi ya TANAPA iliridhia ekari 366 zipewe wananchi na ekari 600 ziendelee kuhifadhiwa.

“Baada ya kikao cha wadau wa uhifadhi kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru tarehe 11 Mei, 2017 ambacho kilijumuisha Madiwani, mwakilishi wa Mbunge, katibu tarafa, watendaji wa kata, wenyeviti na watendaji wa vijiji, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na wataalam wa halmashauri, ilifikiwa maazimio ambapo wajumbe waliridhia maamuzi ya Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kuwapa wananchi ekari 366 ya shamba hilo na kubakiwa na ekari 600” alisema Ndaga.

Aliongeza “Kikao hicho pia kiliridhia TANAPA kuweka vigingi vya mpaka katika shamba hilo ambapo tarehe 14 Mei, mwaka huu, 2017 zoezi hilo lilianza na jumla ya vigingi 26 viliwekwa”.

Alisema hata hivyo kumekuwepo na taarifa kuwa baadhi ya wanakijiji wa Kitongoji cha Momella walifungua kesi mahakamani wakidai wakidai kuwa kijiji cha Olkung'wado kimenyang'anywa ardhi yao na TANAPA, hata hivyo Serikali hiyo ya Kijiji imekana kwa maandishi kuhisika na ufunguzi wa kesi hiyo wakidai imefunguliwa na mtu binafsi na sio Serikali ya Kijiji hicho.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi alimuhakikishia Waziri Maghembe kuwa maagizo yote aliyoyatoa ya kusitisha shughuli za kibinadamu ndani ya eneo hilo yatafanyiwa kazi na atapewa mrejesho wa utekelezaji wake.

Hifadhi ya Taifa ya Arusha ilianzishwa mwaka 1960 wakati huo ikiitwa Ngurdoto na ina ukubwa wa kilomita za mraba 322. Hifadhi hiyo ni maarufu kwa utalii wa magari, kutembea kwa miguu, kupanda milima (mlima Meru), utalii wa farasi, mitumbwi ya kuogelea, baiskeli na wa utalii wa kutumia farasi. Katika mwaka wa fedha uliopita 2016/2017 hifadhi hiyo ilivunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 12 ambapo ilikusanya Shilingi bil. 5.4.
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akiingia kwenye ofisi kuu ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha jana Mkoani Arusha katika ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi.
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisalimiana na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga alipowasili katika ofisi kuu ya hifadhi hiyo jana Mkoani Arusha kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
 Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga (wa pili kulia) akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi.
Prof. Maghembe akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi (kushoto) akizungumza kutambulisha viongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha kwa Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo jana Mkoani Arusha ambapo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) na wajumbe wa kikao hicho wakifuatilia taarifa kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Arusha ambayo iliwasilishwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Steria Ndaga.
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akiongea na viongozi wa TANAPA kuhusu eneo lililolimwa na wananchi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha kinyume cha sheria wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi, aliagiza wananchi hao waondolewe ndani ya siku 40. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi na Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga (kulia). 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) akisikiliza ufafanuzi wa jambo kutoka kwa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga (kushoto) wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
 Baadhi ya wanyamapori (Twiga na Pundamilia) wakionekana wakijivinjari ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 

TUME YA TAIFA YA MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI(NLUPC) YATOA TATHIMINI YA UTAFITI WALIOFANYA KORIDO YA MNGETA NA UKANDA WA UDZUNGWA-MGOMBELA-SELOUS,KILOMBERO-MOROGORO

September 19, 2017
 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Dkt. Stephen Nindi (aliyesimama)akitoa maneno ya utangulizi kwa wadau wa Korido ya Mngeta na ukanda wa Magombela-Selous-Udzungwa wilayani Kilombero juu ya utafiti uliofanywa na wataalam kutoka Tume hiyo wakishirikiana na Asasi ya kiraia ya African Wildlife Foundation uliolenga maeneo ya uhifadhi wa Mazingira,Matumizi bora ya Ardhi, Hati miliki za Kimira na Bioanuai katika Korido ya Mngeta na ukanda wa Udzungwa-Mgombela-Selous, iliyofanyika Wilayani Kilombero.
 Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero (DAS)  Mh.Robert Selasela(aliyesimama) akifungua mkutano huo kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Kilombero uliohusu uhifadhi wa Mazingira,Matumizi bora ya Ardhi, Hati miliki za Kimira na Bioanuai katika Korido ya Mngeta na ukanda wa Udzungwa-Mgombela-Selous
Bw. Eugine Cylilo mtaalam kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi akitoa tathimini ya tafiti iliyofanywa na wataalamu kutoka Tume wakishirikiana na African Wildlife Foundation(AWF) ambayo ilionesha hali halisi ya usimamizi wa mipango ya Ardhi katika Korido ya Mngeta na ukanda wa Udzungwa-Mgombela-Selous juu ya,utunzaji wa Mazingira na Bioanuai,Mipango ya matumizi ya Ardhi na hati miliki za kimila na migogoro ya ardhi.
 Wadau wakimsikiliza Bw. Eugine Cylilo mtaalam kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi akiwasilisha utafiti huo.
 Bi. Jane Mkinga Afisa mradi wa jumuiko la maliasili Tanzania akichangia maswala juu ya maliasili

RAIS DKT. MAGUFULI ATOA RAMBIRAMBI MSIBA WA SHEHE SAAD ZUBEIR ALLY KINONDONI JIJINI DAR ES SALAAM

September 19, 2017

Msaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Kanali Mkeremy akibidhi Rambirambi(kwa niaba ya Mhe. Rais) kwa Mufti wa Tanzania Shekhe Aboubakar Zubeir ambaye amefiwa na Kaka yake Shekhe Saad Zubeiry Ally ambaye amefariki katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam
 
 
Msaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Kanali Mkeremy akizungumza jambo na Mufti wa Tanzania Shekhe Aboubakar Zubeir ambaye amefiwa na Kaka yake Shekhe Saad Zubeiry nyumbani kwa Marehemu Kinondoni Mtaa wa Ufipa jijini Dar es Salaam. Wakwanza kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu.

Msaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Kanali Mkeremy akiagana na Shekhe wa mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum mara baada ya kuwasilisha Rambirambi kwa niaba ya Mhe. Rais katika msiba huo uliopo Kinondoni mtaa wa Ufipa jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU