Magreth Sinyangwa wa Kilosa Morogoro apokea Milioni 20 za Biko

June 16, 2017
Meneja Masoko wa Biko, Goodhope Heaven kulia akiwa katika makabidhiano ya Sh Milioni 20 kwa mshindi wao wa Kilosa, mkoani Morogoro, Magreth Senyangwa aliyeibuka kidedea katika droo kubwa iliyofanyika Jumatano iliyopita. Kushoto ni mume wa Magreth, Bahati Ramadhani na mwingine ni Ofisa wa NMB Tawi la Kilosa, akiwa kwenye makabidhiano hayo.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro
MJASIRIAMALI mwanamke mwenye umri wa miaka 26, Magreth Sinyangwa amekabidhiwa jumla ya Sh Milioni 20 za ushindi wa bahati nasibu ya Biko, aliyoupata katika droo kubwa iliyochezeshwa juzi Jumatano, jijini Dar es Salaam, huku akiwa mwanamke wa kwanza kuibuka na ushindi huo.

Sinyangwa amekabidhiwa fedha hizo Kilosa katika benki ya NMB, mkoani Morogoro na Meneja Masoko wa Biko, Goodhope Heaven, ambaye pamoja na mambo mengine, alimpongeza mshindi huyo na kumtaka azitumie fedha zake kwa uangalifu pamoja na kuboresha maisha yake ya kila siku.

Mshindi wa donge nono la Sh Milioni 20 kutoka Kilosa, mkoani Morogoro, Magreth Senyangwa akiwa ameshika fedha zake baada ya kukabidhiwa kutoka kwa waendeshaji wa bahati nasibu ya Biko.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Heaven alisema ni wakati wa kutajirika kwa kutumia vyema bahati nasibu ya Biko, ‘Ijue Nguvu ya Buku’ iliyozidi kuchanja mbuga na kutoa mamilioni ya Sh kwa washindi wa droo kubwa zinazofanyika Jumatano na Jumapili, sanjari na zawadi za papo kwa hapo.

MBUNGE WA PANGANI AWEKA MIKAKATI YA UJENZI WA SOKO LA KISASA LA SAMAKI PANGAN

June 16, 2017
MBUNGE wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso amesema mkakati mkubwa alionao hivi sasa ni ujenzi wa soko la kisasa la Samaki katika wilaya hiyo ili kuwakomboa wavuvi kiuchumi wao na jamii zao kutokana na kukosa sehemu sahii ya kufanyia shughuli zao.
Hayo aliyasema wakati akizungumza na mtandao huu ambapo alisema wilaya ya Pangani shughuli za uvuvi zimekuwa ndio kazi kubwa kwa jamii hiyo lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa soko maalumu la kufanyia biashara zao.

Alisema kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo anakusudia kupelekea ombi kwa serikali kwenye vikao vya bunge ili serikali ione namna ya kuwajengea soko la kisasa wananchi wake ili waweze kuondokana na adha wanayoipata mara baada ya kuvua samaki hao.

“Miongoni mwa majukumu niliyoyabeba kwa wananchi wake na kuyafikisha bungeni ni pamoja na suala la kujengwa soko la kisasa la samaki ambalo ndio mkombozi wa kuinua kiuchumi kwa jamii ya wakazi wa Jimbo la Pangani kwani limezungukwa mto Pangani ikiwemo bahari ya hindi “Alisema.

“Kama unavyojua Jimbo langu la Pangani asilimia kubwa wananchi wake wanajishughulisha na shughuli za uvuvi hivyo lazima tutawekee miundombinu imara ikiwemo soko la kuuzia na kuhifadhia samaki wanaovuliwa kwa ajili ya kuuzwa “Alisema.

Kauli ya Mbunge huyo inatokana na kuwepo ombi kutoka kwa wavuvi wilayani humo wakiitaka Serikali ya awamu ya tano chini ya Dokta John Magufuli kuangalia namna ya kuwajengea soko la kisasa la kuuzia samaki ili kuweza kuondokana na adha ambayo wamekuwa wakikumbana nayo hivi sasa.

Akizungumza jana mmoja wa wavuvi hao, Shamba Baakari alisema kutokana na kutokuwepo kwa soko hilo linapelekea wavuvi kukosa uhakikisha wa mahali sahihi ya kufanyia shughuli zao ikiwemo kusaidia kulipa kodi.

“Ukosefu wa soko la uhakika la kufanyia shughuli zetu limekuwa kikwazo cha kushindwa kufikia malengo yao hivyo tunaamini kilio hiki cha uwepo wa soko la kisasa utafanyiwa kazi na mamlaka husika kwa lengo la kuongeza tija kwa wavuvi “Alisema.

Naye kwa upande wake,Mahamud Rubonzo ambaye ni mkazi wa wilayani alisema asilimia kubwa ya vijana wilayani  humo wanategemea ajira zao kutokana na shughuli za uvuvi hivyo kutokuwepo kwa soko kunazorotesha shughuli hiyo na kuongeza ugumu wa maisha kwa vijana wengi Wilayani humo.

Alisema iwapo soko hilo litakuwepo litasaidia wavuvi kushindwa kupata hasara ya kuharibikiwa na samaki hasa wale ambao wanakuwa hawajauzika kwa siku husika kwani wanaweza kupata sehemu pa kuhifadhiwa .

Save the Children yaadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika Dar

June 16, 2017
Shirika la Save the Children nchini limeadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika kwa kukutana na Watoto mbalimbali wa shule za Msingi na Sekondari za Manispaa ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam. Katika maadhimisho hayo Walimu na Maafisa wa Ustawi na Maendeleo ya Jamii walishiriki na kuchangia mijadala iliyoibuliwa na watoto wenyewe kuhusu malengo ya usawa na haki ya jinsia ifukapo mwaka 2030. Katika tukio hilo baadhi ya shughuli walizofanya watoto ni pamoja na kuibua mijadala ya Haki na Wajibu wa Mtoto, Unyanyasaji na changamoto za kurepoti kesi za unyanyasaji. Watoto walipata majibu jinsi ya kuripoti kesi za ukatili na unyanyasaji katika kituo cha dawati la jinsia kwenye kituo cha Polisi karibu nao. Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bi. Halili Katani wakati wa kufungua mjadala wa Siku ya Mtoto wa Afrika, alieleza kuwa, Watoto wana haki na wajibu wa kusaidiwa pamoja na kulindwa kama wajibu wa Serikali na Jamii yote. Alitoa wito na rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa, haki za watoto zinatimizwa na kulindwa na kuwafikia watoto zikiwemo za elimu, ulinzi na malezi bora. Aidha, aliwataka watoto hao wakawe mabalozi wazuri wa kutoa elimu kwa wenzao kwa kuwapa elimu waliopata katika siku ya Mtoto wa Afrika. Bi Halili aliwataka watoto Manispaa ya Kinondoni na maeneo mengine kuhakikisha wanaripoti matendo ya kikatili pindi watakapofanyiwa huko mitaani ama na walezi wao kwa kutoa taarifa kwa watu wanaowaamini ikiwemo Walimu, Maafisa wa Ustawi wa jamii na madawati ya Jinsia katika ngazi mbalimbali ikiwemo kwenye Kata, Vituo vya Polisi na sehemu zingine. Naye Meneja wa Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki kwa vijana na watoto, Bi. Ellen Otaru amesema kuwa, watoto wenyewe wamebaini kutokuwa na usawa katika malezi yao huku wakilalamika kuwa wamekosa upendo kutoka kwa wazazi / walezi kutokana na aina ya maisha ya baadhi ya familia. “Shughuli hii ni maalum kwa watoto wa Manispaa ya Kinondoni ambapo watoto wenyewe pamoja na walimu wao wameweza kuelezea hali halisi wanayopambana nayo huko majumbani na mashuleni hivyo changamoto hizo zimepokelewa na walimu wenyewe pamoja na maafisa Maendeleo ya Jamii hatua zaidi ya utekelezaji zimewekwa bayana hapa.” Alieleza Bi. Ellen. Aidha, amewasihi wazazi kuwa na desturi ya kufuatilia watoto wao hasa mienendo ya maisha na makuzi yao kwani watoto wamekuwa na maisha mabaya katika makuzi yao. Shughuli zingine kwenye tukio hilo ni pamoja na watoto hao kuonyesha igizo maalum, mijadala ya wazi ya wao kwa wao pamoja na kuamsha mijadala ya kujifunza kutoka kwa maafisa wengine waliokwemo . Kwa mwaka huu Siku ya Mtoto wa Afrika Kitaifa inatarajia kufanyika hapo kesho Juni 16.2017, Mkoani Dodoma huku ikiwa na kauli mbiu “Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto”. Katika maadhimisho hayo, Jumla ya shule 10 za Manispaa hiyo ya Kinondoni ziliweza kushiriki huku baadhi ya shule hizo ni pamoja na : Mbezi Ndumbwi, Salasala, Mikocheni A, Ushindi, Mikocheni B Sekondari, Nakasangwe, Changanyikeni, Makongo Juu na nyinginezo. Tazama hapa tukio hilo:
Meneja wa Mradi wa Elimu ya Afya ya Uzazi na Haki kwa vijana na watoto, Bi. Ellen Otaru akitoa elimu katika tukio hilo la siku ya Mtoto wa Afrika 2017, ambapo maadhimisho hayo yamefanyika mapema leo Juni 15, Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Mratibu wa Ulinzi kwa Watoto wa Save The Children, Bi. Haika Harrison.

Baadhi ya watoto waliokuwa kwenye shughuli hiyo ya siku ya Mtoto wa Afrika iliyofanyika Manispaa ya Kinondoni leo Juni 15.2017.

Mratibu wa Ulinzi kwa Watoto wa Save The Children, Bi. Haika Harrison akiwaimbisha watoto nyimbo mbalimbali

Watoto hao wakitoa burudani

Afisa wa Save the Children kutoka Sweden- Award Manager, SCS, Bwana. Olle Kvist akizungumza na watoto hao wakati wa tukio hilo

Afisa wa Save the Children kutoka Sweden- Award Manager, SCS, Bwana. Olle Kvist akizungumza na watoto hao wakati wa tukio hilo

Afisa mipango wa Save the Children, Mzee John Komba 'JK' Kijana akizungumza jambo katika tukio hilo

Baadhi ya walimu wakifuatilia tukio hilo

Baadhi ya watoto wakitoa maelezo namna ya michoro yao katika mradi maalum wa watoto katika baadhi ya shule unaoendeshwa na Save the Children

RC MASENZA AFUTULISHA ZAIDI YA WATU MIA MBILI (200)

June 16, 2017
 Mkuu wa mkoa wa Iringa bi Amina Masenza akiwa sambamba na katibu tawala wa mkoa wa Iringa bi wamoja Ayoub wakiwa katika viwanja vya Ikulu ndogo wakifurahia jambo baada ya futari ya pamoja wa watu zaidi ya miambili
Baadhi ya watu waliojitokeza kushiriki futari pamoja na mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza.

Na Fredy Mgunda, Iringa

Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina masenza amefutulisha futari  watu zaidi ya mia mbili katika eneo la Ikulu iliyopo kata ya gangilongo kwa lengo kudumisha amani na upendo.

Akizungumza baada ya futari Mkuu wa mkoa masenza aliwataka waumini wote wa dini ya kiislamu na wakristo kuwa makini katika maeneo ya ibada ili kuepukana na kutoka kwa shambilio lolote lile ambalo litasababisha maafa.

"Tumeona nchi nyingine kipindi hiki cha ramadhan kukitokea milipiko mingi ya kujitoa mhanga kwa baadhi ya watu wenye itikadi kali hivyo tunapaswa kuwa makini mno mwezi huu hata miezi mengine yote kwa kudumisha amani yetu"alisema Masenza

Masenza aliwaomba wananchi wote wa mkoa wa Iringa kuwafichua waalifu wanaofanya shughuli hiyo kwa njia yoyote ile ili kuendelea kudumisha tunu tuliyokuwa nayo toka wakati tunapata Uhuru hadi hii Leo.

Aidha Masenza aliwaomba watanzania kuendelea kumuunga mkono na kuombea Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr John pombe Magufuli katika vita hii ya kukuza uchumi kutoka hapa tulipo hadi uchumi wa kati kwa kuwa vita hii sio lelemama.

"Ni kitu kigumu sana unapogusa maslai ya mtu binafsi kwa maslai ya wanyonge huwa inakuwa vita kubwa kupambana nayo lakini Rais wetu mpendwa anafanikiwa hilo hivyo lazima tuwe tunamuombe na kumuunga mkono ili tuendelee kumpa moyo kwenye vita hii" alisema Masenza

Niwaombe wananchi wa mkoa wa Iringa kuwapuuza viongozi wanaopotosha ukweli wa mambo ambayo serikali inayafanya kwa manufaa ya wananchi wa kipato cha chini,kati na wale wenye kipato kikubwa pasipo kumnyang'a au kumdhulumu mtu haki yake.

Katika futari hiyo kulihudhuriwa na wakuu wa wilaya zote za mkoa wa Iringa kama Kilolo iliwakilishwa na mh Asia Abdalah,Mufindi Jamhuri William na wilaya ya Iringa Richard Kasesela.

Lakini mkuu wa wilaya ya Kilolo Asia Abdalah aliwataka wananchi na viongozi kutunza amani na kuacha kufanya uharifu kipindi hiki cha ramdhan hata baada ya kuisha ramadhan ili kuendelea kuweka nchi kwenye utulivu uliopo sasa.

"Unakutana na mtu kipindi hiki anajifanya kafunga lakini matendo yake hayaendani ya wakati uliopo lakini kuna wengine saizi wametulia ila ramadhan ikiisha tu anaanza matendo ya uvunjifu wa amani hivyo niwaombe tena na tena wananchi kutunza amani iliyopo "alisema Abdalah

Abdalah alimshukuru mkuu wa mkoa wa Iringa bi Amina masenza kwa futari ambayo imewakutanisha watu mbalimbali kukaa pamoja na kubadilisha mawazo japo kwa muda mchache hivyo kuwaomba wakuu wenzake wa wilaya zote za mkoa wa Iringa kuiga mfano wa mkuu wa mkoa.

Nao baadhi ya viongozi wa dini waliofika eneo la futari walimpongeza mkuu wa mkoa kwa kufutulisha watu mbalimbali ambao imekuwa fursa ya kufanya wabadilishane mawazo ya kujenga tofauti na kila mmoja angefuturu kwake.

"Hili ni jambo jema sana kwa kiongozi wetu wa mkoa maana leo tumekutana na viongozi kutoka dini mbalimbali hata wengine sio viongozi lakini tumebadishana mawazo na hili ni jambo jema kwetu sisi kwa ukweli tumejifunza mambo mengi leo mungu ambariki mheshimiwa mkuu wa mkoa" walisema viongozi wa dini