JK AKUTANA NA MWENYEKITI WA SENETI WA LESOTHO

July 30, 2023

 Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akies ns Mwenyekiti wa Seneti wa Lesotho Mhe Mamonaheng Mokitimi   mjini Maseru siku ya Ijumaa. 


Mhe Kikwete yuko katika Ufalme wa Lesotho kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa Jopo la Wazee wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Jopo hili la Wazee wa SADC ambalo Makamu Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Paramasivum Pillay B. Vyapoory, Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Mauritius, limekutana na Serikali na wadau mbalimbali ndani ya Ufalme wa Lesotho, kama mwendelezo wa juhudi ya kusaidia upatitanaji wa utulivu wa kisiasa katika Ufalme huo.
 
Jopo limekutana na Mhe. Ntsokoane Samuel Matekane, Waziri Mkuu wa Ufalme wa Lesotho; Mhe. Nthomeng Justina Majara, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Sheria na Masuala ya Bunge; Mhe. Tlohang Sekhamane, Spika wa Bunge la Lesotho; Mhe. Mamonaheng Mokitimi, Mwenyekiti wa Seneti; Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Viongozi wa Vyama vya Upinzani; Uongozi wa Ofisi ya Mpito ya Mabadiliko ya Kitaifa (NRTO); Viongozi wa Umoja wa Machifu; na wadau mbalimbali.

MWENYEKITI WA CCM MKOA WA TANGA AKERWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI MKINGA ATOA MAAGIZO

July 30, 2023

Na Oscar Assenga,MKINGA

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Tanga Rajabu Abdurahman amekerwa na utekelezaji wa mradi wa Maji Wilayani Mkinga wenye thamani ya zaidi ya Shs Bil 3.1 huku akiumuagiza Waziri wa Maji Jumaa Aweso na Mkuu wa Mkoa Tanga Waziri Kindamba  kuutembelea mradi huo na kuchukua hatua za kinidhamu ikiwa kutabainika ubadhilifu wowote .

Mradi huo unaosimamiwa na wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilayani humo(RUWASA) ambao umeonekana hauna ufanisi wala tija kwa wananchi zaidi elfu kumi wanaokabiliwa na adha ya maji Wilayani humo.

Mwenyekiti huyo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki akiwa Wilayani Mkinga katika mwendekezo wa ziara yake iliyokuwa na lengo la kukiimarisha chama hicho pamoja na kukagua miradi ya maendeleo na kusema watendaji watakaobainika kufanya ubadhirifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.

Alisema ni lazima wanyooshane mapema hasa kwa wale watumishi wazembe ambao wanashindwa kutekeleza wajibu wake na kupelekea kukipa chama chetu  taabu wakati wa kampeni hivyo hawatakubaliana nao na wanaanza kuchukua hatua kabla ya kukutana na maswali toka kwa wananchi.

Aidha alisema kitendo kinachofanywa na Mamlaka hiyo ya Maji Wilayani Mkinga cha kujenga Tank la maji kwa ajili ya kuyasambaza kwa wananchi bila ya kuwa na chanzo cha uhakika wa maji ni uchonganishi wa Rais na wananchi wake.

Alisema alitegemea kuona mradi huo wa ujenzi wa tank hilo la maji mbali ya utekelezaji wa miundombinu ya kupokea maji,kusafirisha na kusambaza maji hayo ungekwenda sambamba na ukarabati wa bwawa la maji la Gombero ambalo ndio chanzo kikuu cha upatikanaji wa huduma hiyo.

Aidha alisema kilichoonekana kwenye mradi mradi huo tanki maji lipo lakini hakuna uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo mwisho wa siku Serikali inamlipa mkandarasi pesa nyingi huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma hiyo.

Alisema Rais,Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanahangaika mchana na usiku kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo itakayowasaidia wananchi kuondokana na kero mbalimbali jambo la kusikitisha watendaji waliopewa dhamana hiyo hawatekelezi walichoagizwa.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi juu ya bwawa hilo Meneja wa RUWASA Wilayani Mkinga Thomas Kaijage (TM) alisema bwawa hilo linachangamoto na linahitaji kufanyiwa ukarabati ili liweze kutunza maji ya kutosha yatakayoweza kuhudumia Wananchi hao na kuongeza kuwa wanategemea kupata fedha kwa bajeti ya mwaka 2023/2024.

Kaijage alisema kwa mujibu wa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo kazi ya ukarabati wa bwawa hilo zitafanywa na wakala wa uchimbaji wa mabwawa na visima (DDCA) baada ya usanifu kukamilika.

Aidha alisema mradi huo unaojengwa Wilayani humo unakwenda sambamba na ujenzi wa Tank la maji litakaloweza kuhifadhi mita za ujazo 300,vituo 28 vya kuchotea maji,Ofisi ya Chombo Cha watoa huduma ngazi ya jamii(CBWSO),Machujio ya Maji(treatment Plant),uchimbaji na ulazaji wa mabomba na ufukuaji wa mitaro mita 48,000 na ukarabati wa Nyumba ya Pampu(pump house).

Kwa upande wake Mbunge wa wilaya hiyo ya Mkinga Dastan Kitandula alisema Rais ameridhia kata ya Gombero Wilayani humo kuboreshewa miundombinu ya usambazaji wa maji na ujenzi wa tank ili kuweza kuwahudumia wananchi wanaokabiliwa na adha ya Maji Wilayani humo.

Aidha alisema upo mradi wa maboresho ya Bwawa la Gombero amabalo ndio chanzo kikuu cha maji utakaogharimu Shs Bil 4,na mradi mkubwa utakaotoa maji mto Zigi kuelekea Horohoro ambao utagharimu zaidi ya Shs Bil 34 na kuifanya Wilaya hiyo kuondokana na adha hiyo ya maji.

Ziara ya Mwenyekiti huyo itadumu kwa takriban siku 20 ambapo atatembelea Wilaya za Mkinga,Muheza,Korogwe Mji na Korogwe Vijijini na Wilayani Lushoto kama alivyoahidi kuzitembelea Wilaya zote za Mkoa Tanga mara baada ya kuchaguliwa na kushika wadhifa huo.

MBUNGE SEKIBOKO ATEMBELEA VIKUNDI VYA WAKINA MAMA VILIVYONUFAIKA NA FEDHA ZA ASILIMIA 10 YA MAPATO YA JIJI LA TANGA

July 30, 2023

Mbunge Husna Sekiboko (kishoto) akizungumza katika mkutano wa Mabokweni alipotembelea chanzo cha maji. Akiwa na Mwenyekiti wa UWT Jiji la Tanga Moza Shilingi

 NA MASHAKA MHANDO, Tanga


MBUNGE wa viti maalumu mkoani Tanga, Husna Sekiboko, ametembelea vikundi vya akina mama vilivyokopeshwa fedha kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ya Jiji la Tanga.


Mbunge huyo ambaye amekuwa karibu na Umoja wa Wanawake (UWT) mkoa wa Tanga kutokana na kufanya kazi kwa pamoja na Jumuiya hiyo, alitembelea vikundi vya ufugaji kuku, usagaji nafaka pamoja na uuzaji wa unga wa chakula.


Akizungumza na akina mama hao katika kikao kilichofanyika kata ya Mnyanjani na kisha mkutano kule Mabokweni ambako alizungumza na wananchi wa kata za  Nguvumali na Chumbageni, alisema mikopo waliyopewa vikundi hivyo vya ujasirimali watumie pesa hizo kujenga uchumi wao na kupiga hatua.


Alisema fedha walizopewa zinatakiwa zirejeshwe ili ziweze kukopesha wajasirimali wengine kwa kuwa dhamira ya serikali ni kuwasaidia ili waweze kuinuka kiuchumi.


Hata hivyo, alisema mikopo hiyo inayotolewa na serikali asilimia nne vijana na wanawake na asilimia mbili makundi ya watu Wenye ulemavu, kwasasa imesitishwa ili kuboresha kwa makundi hayo tofauti na awali.


Mbunge huyo aliipongeza halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kuweza kutoa fedha nyingi za mikopo tofauti na wilaya nyingine alizopita baada ya kukuta kikundi kimoja kimepewa mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 40.


"Kiukweli nimetembea wilaya nyingine na hata kule kwetu Lushoto hakuna mjasiriliamali ambaye halmashauri imeweza kumkopesha fedha kama hizi sana sana huko wanawakopeshwa shilingi milioni mbili au tatu," alisema mbunge.


Alisema fedha hizo wasione zinatolewa tu kwa bahati mbaya bali  ni usimamizi mzuri wa mbunge wa jimbo la Tanga Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya.


"Muungeni mkono mbunge wenu (Ummy) ni kiongozi makini na ndiyo maana ameaminiwa na kupewa uongozi, mnaweza msione umuhimu wake lakini nawaambia mshikeni sana mbunge wenu," alisema Sekiboko.


Mbunge huyo alisema kuwa ziara yake katika jimbo la Tanga, ni kukutana na wanachi kujua changamoto zao lakini pia kuwaomba wananchi wamuunge mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri anayoifanya nchini ikiwemo mkoa wa Tanga.


Alisema akina mama wanao wajibu mkubwa wa kumuunga mkono Rais licha ya kuwa mwanamke mwenzao lakini ametekeleza miradi mingi ya maendeleo nchini katika sekta za afya, elimu, maji na miundo mbinu.


Mwisho