SERENGETI BOYS WAANZA KAMBI

March 13, 2017
Timu ya taifa ya mpira wa miguu ya vijana wenye umri wa miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys imeanza mazoezi rasmi leo Machi 12, 2017 kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Serengeti Boys itakuwa kambini Dar es Salaam hadi Machi 26, mwaka huu ambako itakwenda Bukoba mkoani Kagera kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa kujiandaa na michuano Afrika ambayo sasa itaanza Mei 14, 2017 badala ya Mei 21, mwaka huu.

Michezo ya kirafiki ya kimataifa itakuwa ni dhidi ya timu za vijana za Rwanda (Machi 28, 2017), Burundi (Machi 30, mwaka huu) na Uganda Aprili 2, mwaka huu). Michezo yote itafanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.

Timu hiyo itarejea tena Dar es Salaam Aprili 3, mwaka huu ambako siku inayofuata itaagwa kwa kupewa bendera na mmoja wa viongozi wa nchi kabla ya kusafiri Aprili 5, mwaka huu kwenda Morocco kwa ajili ya kambi.

Timu hiyo itaunganisha kwenda Cameroon Mei mosi, mwaka huu ambako Mei 3, 2017 itacheza mechi ya kwanza na Cameroon kabla ya kurudiana Mei 6, mwaka huu na siku inayofuata itakwenda Gabon.

Serengeti Boys ni timu ya vijana ambayo imefuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14, mwaka huu. Timu hiyo imepangwa Kundi ‘B’ pamoja na mabingwa watetezi Mali, Niger na Angola. Ina lalengo ya kurejea na Kombe la Afrika kwa vijana.

La ikitokea imekosa nafasi hiyo angalau ikafika nusu fainali ambako kwa mafanikio hayo itakuwa tayari ina tiketi mkononi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia huko India, Novemba, mwaka huu.

Kikosi cha Serengeti Boys kinaundwa na Makipa: Ramadhan Kabwili, Samwel Edward na Kelvin Kayego.

Walinzi:  Kibwana Ally Shomari, Nickson Kibabage, Israel Mwenda, Dickson Job, Ally Msengi, Issa Makamba na Enrick Vitalis Nkosi.

Viungo: Kelvin Nashon Naftali, Ally Ng’anzi, Mohamed Rashid, Shaaban Ada, Mathias Juan, Najim Mussa, Marco Gerald, Abdulhamis Suleiman, Saidi Mussa na Cyprian Benedictor Mtesigwa.

Washambuliaji:  Muhsin Malima Makame, Yohana Mkomola, Ibrahim Abdallah, Assad Juma na Abdul Suleiman. 

Benchi la Ufundi:
Bakari Shime (Kocha Mkuu)
Oscar Mirambo (Kocha Msaidizi)
Muharami Mohamed (Kocha wa makipa)
Kim Poulsen (Mshauri wa Ufundi)
Edward Evans (Mtunza Vifaa)
Shecky Mngazija (Daktari wa timu)
Gomez Dardenne (Mtaalamu wa saikolojia)
DK.SHEIN AREJEA KUTOKA DODOMA

DK.SHEIN AREJEA KUTOKA DODOMA

March 13, 2017
REE
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akifuatana na Mkuu wa Wilaya Dodoma Mjini Christina Mndeme (kushoto) pamoja na ujumbe aliofuatana nao wakati alipokuwa akiondoka katika uwanja wa ndege wa Dodoma leo baada ya kumalizika kwa Vikao vya Chama cha CCM Ukiwemo Mkutano Mkuu maalum uliofanyika juzi katika ukumbi wa mpya wa Kiwete Hall uliopo nje ya Mji wa Dodoma,
REE 1
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Viongozi wengine  waliofika kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar akitokea Dodoma katika Mkutano Mkuu malaaum uliofanyika juzi,[Picha na Ikulu.] 13/03/2017.

MAYANGA ATANGAZA KIKOSI CHA TAIFA STARS

March 13, 2017


Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Salum Mayanga leo Jumatatu Machi 13, 2017 ametangaza majina ya wachezaji 26 watakaounda kikosi hicho.

Taifa Stars, inatarajiwa kucheza na Botswana Machi 25, 2017 kabla ya kuivaa Burundi Machi 28, mwaka huu katika michezo kirafiki wakati huu wa Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika leo Makao Makuu ya TFF, yalioko Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam, Mayanga aliwataja wachezaji hao kuwa ni walinda milango, Aishi Manula (Azam FC), Deogratius Munishi (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).

Walinzi wa pembeni upande wa kulia aliwataja Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael (Azam FC).

Mayanga aliwataja walinzi wa kati Vicent Andrew (Yanga SC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Erasto Nyoni (Azam FC) ilihali aliwataja viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude (Simba SC).

Kadhalika wako viungo wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC), Frank Domoyo (Azam FC) na Muzamil Yassin (Simba) wakati viungo wa kulia waliotajwa ni Simon Msuva (Yanga SC) na Shizza Kichuya (Simba SC).

Viungo wa kushoto ni Farid Mussa (Teneriffe, Hispania) na Hassan Kabunda (Mwadui FC) wakati washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Thomas Ulimwengu na AFC Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu(Kagera Sugar) na Abdul-Rahman Mussa (Ruvu Shooting).

Pia Mayanga aliwataja wasaidizi wake kuwa Kocha Wa Makipa, Patrick Mwangata wakati Meneja wa timu upande wa ufundi atakuwa mwenyewe Mayanga na upande wa mipango mingine atakuwa Danny Msangi; Mtunza Vifaa, Ally Ruvu wakati Daktari wa timuatakuwa Richard Yomba huku Daktari wa viungo akiwa ni Gilbert Kigadya.

Timu hiyo itaingia kambini Machi 19, 2017 kwenye Hoteli ya Urban Rose, Dar es Salaam na mara baada ya michezo hiyo kambi itaahirishwa Machi 29, mwaka huu.

JK AZINDUA RASMI TAASISI YA MAENDELEO YA JAKAYA MRISHO KIKWETE (JMKF)

March 13, 2017
 Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete (kulia), akizungumza alipokuwa akizindua rasmi Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) ikiwa ni sehemu pia ya uzinduzi wa taasisi hiyo kwenye Hotel ya Hyatt Kempinsk The Kilimanjaro Dar es Salaam leo. Kikwete ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo.PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA;KAMANDA WA MATUKIO BLOG
 Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Jakaya Kikwete, alisema kuwa Taasisi hiyo pamoja na mambo mengine  itajihusisha na masuala ya Maendeleo ya Binadamu nchini, Afrika na Duniani.


Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete amesema kuwa anapenda kuendelea kufanya shughuli zinazosaidia kuleta maendeleo kwa watu na jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari  leo Jijini Dar es salaam, wakati alipokuwa  akizindua Taasisi yake ya Jakaya Kikwete (Jakaya Mrisho Kikwete Foundation)  alisema kuwa kwa muda mrefu amekua akipenda na kujihusisha na shughuli mbalimbali za maendeleo ya watu na hivyo Taasisi yake itamsaidia katika kufikia malengo yake.

“Nimetumia muda wangu kwa ajili ya maendeleo ya watu, baada ya shule, nilikitumikia Chama cha Mapinduzi(CCM), nilitumikia Jeshi na baadae Serikali, kwangu Taasisi hii imekuwa chombo kitakachonisaidia kuendeleza maono yangu na kutimiza ndoto zangu katika kuendelea kusaidia watu” alisema Dkt. Kikwete.

Akiizungumzia taasisi hiyo Kikwete alisema kuwa, Taasisi yake ina wajumbe 9 kutoka sehemu mbalimbali duniani wenye nyadhifa na heshima kubwa katika nchi zao.

Ameongeza kuwa Taasisi hiyo imejikita kusaidia jamii katika maeneo makubwa manne, maendeleo ya jamii  hasa katika kujikita kuondoa umaskini, mabadiliko ya hali ya nchi na kilimo  kwa wakulima wadogo.

Pia Taasisi hiyo imejikita katika huduma za afya, kutokomeza malaria na afya ya mama na mtoto.

Maeneo mengine ambayo Taasisi hiyo inajihusisha nayo ni  ni elimu kwa  vijana ili  kukuza vipaji vyao na kuwapa mafunzo kuhusu uongozi bora, usawa wa kijinsia na namna ambavyo Serikali inavyotoa huduma kwa wananchi.

Aidha, alisisitiza kuwa Taasisi yake itaisaidia Serikali, mashirika na Taasisi mbalimbali ili kushirikiana kuwaletea maendeleo watanzania na watu mbalimbali duniani.

Dkt. Kikwete amewataja Wajumbe wa Bodi ya Udhamini ya Taasisi yake kuwa ni Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Profesa Rwekaza Mukandala Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Willium Mahalu Mhadhiri Mwandamizi  katika Chuo Kikuu cha Tabibu cha Bugando.

Wengine ni Balozi Mwanaidi Maajar aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Abubakar Bakhresa, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Makampuni ya Bakhresa, Genevieve Sangudi  Mtaalamu wa Masuala ya kibishara ya Kimataifa kutoka Marekani.

 Pia wapo Dato’ Sri  Idris Jala, Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu nchini Malyasia,  Balozi Charles R. Stith aliyekuwa Balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania pamoja na Dkt. Carlos Lopes ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taaisi ya Mafunzo na Utafiti ya Umoja wa Mataifa (UNITAR).

Taasisi ya Maendeleo ya Jakaya Kikwete ilisajiliwa tarehe 17, Februari 2017, na hii ni mara ya kwanza kwa wajumbe wa bodi ya wadhamini kukutana tangu kuanzishwa kwake.
 Kikwete akizungumza na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi yake ya JMKF
 Jakaya Kikwete akikumbatiana na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi hiyo, Balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania, Charles Stith
 Mwenyekiti wa Taasisi ya JMKF, Jakaya Kikwete akisalimiana na mjumbe wa Bodi hiyo, Mfanyabiashara maarufu Mtanzania aishie Marekani, Genevieve Sangudi

MALINZI AWAPA MAAGIZO MAZITO MAKOCHA WAPYA

March 13, 2017

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amewazawadia makocha wapya 27 waliofuzu kozi ya ukocha kwamba kila mmoja mmoja atampa koni 20 na vizibao 22 kwa ajili ya mazoezi.

Rais Malinzi alitoa ahadi hiyo wakati wa hafla ya kufunga kozi ya ukocha ngazi ya ‘Intermidiate’ kwa makocha waliohitimu. Rais Malinzi alialikwa na waratibu kuwa mgeni rasmi ambaye awali, alishangazwa kwa namna ilivyoratibiwa kwa kufuata miongozi ya TFF na CAF.

Katika hotuba yake, Rais Malinzi aliwataka waamuzi hao kuzingatia weledi wakiwa ni mabalozi wa kupinga matumizi ya dawa za kulevya lakini zaidi wajiepushe kwa njia yoyote ile kupanga matokeo.

Rais Malinzi alifurahishwa na idadi kubwa ya makocha waliohitimu kwani kabla walikuwa ni wachezaji wa timu kubwa na kongwe mbalimbali, “Hilo sasa linanisukuma kuwapa kila mmoja wenu koni 20 na bips (vizibao) 22,” alisema Rais Malinzi.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kuwaombea dunia Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Chilla Tenga ambaye anawania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji wa FIFA kwa nchi zinazozungumza Kiingereza ambako anapambana na Kwesi wa Ghana.

Pia katika mkutano huo Mkuu wa CAF utakaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia ukihusisha nchi 53 kati ya 54 wanachama wa CAF, pia watapiga kura kuichagua Zanzibar kuwa mwanachama kamili wa shirikisho hilo.

Kozi hiyo iliendeshwa na Wilfred Kidao - Mkufunzi anayetambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), akisaidiwa na Manyika Peter aliyefundisha programu au mtaala kwa makocha wa makipa; Dk. Nassoro Ally Matunzya aliyewanoa makocha hao kuhusu tiba za wanamichezo/wanasoka na Mkufunzi wa muda mrefu wa soka, Hemed Mteza.

Wahitimu wa kozi hiyo walikuwa Doris Malyaga ambaye ni Mwanamke pekee kati ya wanafunzi 27 walisoma kozi hiyo kwa kipindi cha siku 14 cha mwanzo wa mwaka. Doris ni mwanahabari za michezo aliyehudhuria kozi hiyo. Anaandikia gazeti la MwanaSPOTI linalotolewa na Kampuni ya Magazeti ya Mwananchi (MCL).

Wengine ni nyota wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ waliopata kuchezea klabu kongwe na kubwa nchini. Wanafunzi hao ni Boniface Pawasa, Fred Mbuna, Innocent Haule, Herry Morris, Ivo Mapunda, Nizar Khalfan na Mussa Hassan Mgosi.

Wengine ni Omar Kapilima, Amosi Mgisa, Uhuru Mwambungu, Yussuf Macho, George Minja, Haruna Adolf, Selemani Omari, Ally Ruvu, Masoud Selemani, Haji Mustapha, Mhasham Khatib, Issa Ndunje, Salum Kapilima, Said Salum, Julio Elieza, Hassan Mwakami, Rajab Mponda, Ally Mbonde na Evod Mchemba.

MALINZI AMLILIA SIR GEORGE KAHAMA

March 13, 2017


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi, ametuma rambirambi kwa familia ya marehemu Sir George Kahama aliyefariki dunia Jumapili akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Rais Malinzi amesema taifa limepoteza mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa katika kupigania maendeleo ya mpira wa miguu baada ya kupigania Uhuru ambao Watanzania leo wanajivunia amani.

Pamoja na familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki, Rais Malinzi Dkt Magufuli amewapa pole wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi, akisema ni kielelezo cha kiongozi aliyetukuka.

“Kabla ya Uhuru Mzee wetu, Mzee Kahama alikuwa kiongozi shupavu na mzalendo, alama ambayo ametuachia sisi Watanzania leo hii tunajivunia amani,” alisema Rais Malinzi.

Rais Malinzi ambaye katika vikao vyake vya jana hapa Dar es Salaam, alikuwa akitoa nafasi ya kumkumbuka Sir George, akisema msiba huo pia ni wa TFF kwa kuwa mmoja wa watoto wake, Joseph ni Mjumbe wa Mfuko wa Bodi ya Maendeleo ya Mpira wa Miguu wa TFF.

Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.

WADAU WA BARABARA WATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA KUDHIBITI AJALI NCHINI

March 13, 2017


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wadau wa usafirishaji kuweka mikakati dhabiti ya kupunguza ajali za barabarani nchini ili kuokoa maisha ya watanzania wanaofariki dunia kila mwaka kutokana na ajali hizo.

Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo alipofungua mkutano maalumu wa kanda wa kujadili na kutathmini changamoto za usalama barabarani na jinsi ya kuzikabili unaofanyika jijini Dar es salaam.

Profesa Mbarawa amesema kuwa ajali za barabarani zimekuwa zikikatisha maisha ya watanzania wengi kila mwaka ambao wengi wao ni vijana na nguvu kazi ya taifa hivyo ni jukumu la wadau kubadilisha hali ya usalama barabarani.

“Kama tukijifunza vizuri na kuyafanyia kazi mafunzo haya tunaweza kubadili hali ya usalama barabarani kwani inaumiza kuona vifo vya watu wengi vinavyotokana na ajali za barabarani hivyo ni wakati wa Jeshi la Polisi, na Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu na Majini SUMATRA kushirikiana kukomesha ajali hizi”. Amesisitiza Profesa Mbarawa.

Ameongeza kuwa Serikali itatoa kipaumbele kwa yale yatakayojadiliwa na kuamuliwa katika mkutano huo ili kuongeza kasi ya udhibiti wa ajali za barabarani hapa nchini na kupunguza idadi ya ajali zinazoepukika.

Naye Mwenyekiti wa Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule amesema kuwa Bodi hiyo inashirikiana na taasisi nyingine katika kuhakikisha ubora wa miundombinu ya barabara inakuwa salama na kupitika wakati wote.

Kwa upande wake Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani hapa nchini Mohamed Mpinga amesema kikosi cha usalama barabarani kitaendelea kuhakikisha kuwa ajali za barabara zinadhibitiwa.

“Suala la ajali za barabarani ni jukumu letu sote kwa pamoja hivyo tukiungana kwa pamoja na kushirikiana tutaweza kupunguza ajali hizi kwa kiwango kikubwa”. Amesema Kamanda Mpinga.

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo jijini Dar es salaam umewakutanisha wadaau mbalimbali wa kimataifa wa masuala ya ujenzi na usimamizi wa usalama wa watu na mali wawapo barabarani .
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wadau waliohudhuria mkutano wa siku mbili wa Usalama barabarani katika ukumbi wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB) Bw. Joseph Haule akitoa taarifa ya udhibiti wa ajali za barabarani kwenye mkutano wa wadau wa usalama barabarani uliofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akiongea na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano wa Namibia Mhe. Sankwasa James Sankwasa wakati wa mkutano wa siku mbili wa kutathmini usalama barabarani, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa Chama cha Kimataifa kinachoshughulika na masuala ya barabara Dkt. Kiran Kapila wakati wa mkutano wa siku mbili wa kutathmini usalama barabarani, Jijini Dar es salaam.
Mmoja wa wanafunzi aliyeshinda tuzo ya uchoraji wa picha ya usalama barabarani Veronica Shirima akitoa maelezo kwa wadau wa usalama barabarani, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Wanne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Usalama barabarani mara baada ya kufungua mkutano huo, Jijini Dar es salaam.

RAIS DOKTA MAGUFULI AFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS WA ZANZIBAR DKT SHEIN LEO

March 13, 2017
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein walipokutana kwa mazungumzo Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma leo Jumatatu Machi 13, 2017. Picha na IKULU


MAXCOM AFRICA (MAXMALIPO) INAWAKARIBISHA WATANZANIA KUSHIRIKI MANUNUZI YA HISA KWA NJIA YA MTANDAO

March 13, 2017
C:\Users\Deogratius Lazari\AppData\Local\Microsoft\Windows\Temporary Internet Files\Content.Word\IMG_4247.jpg
Mkuu wa kitengo cha Masoko na Ubunifu  Bwana. Deogratius Lazari Mosha akifafanua jambo kwa Waandishi wa habari (hawapo pichani)
Kampuni ya Maxcom Africa (Maxmalipo) inawakaribisha watanzania kushiriki manunuzi ya hisa za makampuni yaliyoorodheshwa kwenye Soko la hisa la Dar es salaam(DSE)  kwa njia ya mtandao (simu za kiganjani) na kufanya malipo kupitia kwa mawakala wa  Maxmalipo waliopo nchi nzima Tanzania.
Mkuu wa kitengo cha Masoko na Ubunifu  Bwana. Deogratius Lazari Mosha,  Leo 13/03/2017 amewaambia waandishi wa habari kwamba Maxcom Africa (Maxmalipo) ikishirikiana na soko la hisa la  Dar es Salaam(DSE) kwa kutumia mfumo madhubuti wa simu za viganjani unamwezesha Mtanzania kuweza kushiriki kwenye Manunuzi ya hisa  za makampuni yaliyoorodheshwa kwenye soko la awali  la mitaji (primary markets ) kwa kupiga *150*36#, ameongeza kwamba baadhi ya makampuni hayo kwa sasa ni Vodacom na TCCIA.
Akifafanua hili Bw. Deogratius Lazari amesema ili Mtanzania aweze kushiriki Manunuzi ya hisa kwa mfumo huu anatakiwa kubonyeza *150*36# kisha ataingia kwenye Menyu ya soko la hisa na Kuchagua IPO kisha atachagua kampuni anayotaka kununua hisa, baada ya kufanya hivyo mteja atalazimika kujisajili na kisha atapata nafasi ya kuainisha idadi ya hisa anazohitaji(zisizo pungua 100 katika awamu ya kwanza).
Bw. Deogratius Lazari ameongeza kwamba baada ya hatua ya uanishaji wa hisa, mteja atapokea ujumbe mfupi wa simu kutoka DSE wenye  nambari ya kumbukumbu ya malipo, idadi ya hisa na kiasi anachotakiwa kulipia. Ili kukamilisha  malipo haya mteja  atatakiwa kufika kwa wakala yeyote wa Maxmalipo aliye karibu naye na kufanya malipo kama ilivyo ainishwa kwenye ujumbe aliopokea kwenye simu yake. Mteja anahimizwa kuhakikisha kwamba anapatiwa risiti pindi anapolipia hisa kwa mawakala wa Maxmalipo ili kutunza kumbu kumbu zake.
Kwa kuongezea Bw. Deogratius Lazari ameeleza kwamba mfumo huu rafiki unamwezesha mteja kushiriki manunuzi ya hisa kadiri ya uwezo wake (Mfano, Mteja Anaweza kila siku akanunua hisa 100 kulingana na kipato chake au zaidi). Pamoja na mwakala wa Maxmalipo mteja anaweza  kulipia kwa kutumia mitandao ya simu.
Mfumo huu wa kununua hisa kwa simu za kiganjani  ( *150*36#) umetengenezwa na kampuni ya kitanzania ya Maxcom Africa (Maxmalipo) ikishirikiana na Soko la hisa la Dar es Salaam(DSE)  na ni mfumo rasmi wa kuuza na kununua hisa kwenye soko la hisa .
Bw. Deogratius Lazari ametoa wito kwa watanzania kushiriki ununuzi wa hisa kwa njia ya simu ya kiganjani na kuhakikisha wanafanya malipo mapema  kupitia kwa mawakala wa Maxmalipo  walioko nchi nzima  takribani Mawakala Elfu kumi na sita .