Jovina Bujulu-MAELEZO.
Sekta
ya kilimo nchini ni kitovu cha maendeleo ya viwanda kwa kutoa masoko na
malighafi za viwandani ambapo inaajiri Watanzania wengi takribani zaidi
ya asilimia 67.
Katika
utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, Serikali inaendelea
kuimarisha mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya kilimo ikiwemo
kuimarisha masoko ya kilimo ili sekta hiyo iendelee kuwa na tija kwa
wakulimananchi na taifa kwa ujumla.
Hivi
karibuni Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilitangaza
kufuta ada na tozo mbalimbali katika baadhi ya mazao ya biashara ili
kumpa unafuu mkulima wakati wa kuuza mazao yake.
Hatua
hiyo ni mwanzo mzuri wa kuimarisha sekta hiyo hasa wakati huu ambapo
Serikali ya Awamu ya Tano imetangaza nia yake ya kuimarisha uchumi wa
kati na viwanda.
Serikali
iliamua kufuta na kupunguza ada na tozo imedhamiria kumaliza kero na
kilio cha muda mrefu cha wakulima ambao wamekuwa wakilalamikia tozo hizo
kwa madai kuwa zinawanyonya.
Aidha,
uamuzi huo unategemea kuwapunguzia mzigo mkubwa wa malipo ambao umekuwa
ukiwaelemea wakulima hao, hivyo kuwapa unafuu mkubwa na kuwapatia
faida.
Akiwasilisha
hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba alizitaja baadhi ya tozo
zilizofutwa katika zao la tumbaku kuwa ni mchango wa ushirika wa mkoa,
mchango kwa ajili ya gharama za masoko ya ushirika na chama cha msingi
cha ushirika, dhamana ya benki kuu ya Tanzania na fomu ya maombi ya
leseni za tumbaku.
Ada
na tozo nyingine zilizotajwa kuwa ni kodi ya leseni ya kununua tumbaku
kavu na mbichi kiwandani, leseni ya kuuza tumbaku nje ya nchi na tozo ya
Baraza la Tumbaku.
Pamoja
na kufuta tozo na ada katika baadhi ya mazao, Serikali pia imetoa
punguzo katika zao la tumbaku ambapo kodi ya leseni ya tumbaku kavu
itakuwa dola za kimarekani 2,000 badala ya dola 4,000.
Aidha,
leseni ya kusindika tumbaku imepungua kutoka dola za kimarekani 10,000
hadi 5,000 ambapo Serikali imechukua hatua hizo ili kuhakikisha wakulima
wananufaika na kilimo wakiwemo wakulima wadogo.
Kupitia
bodi ya mazao, Serikali itaendelea kuimarisha soko la mazao ya asili
hasa mazao ya jamii ya mikunde ili kukidhi mahitaji ya zao hilo katika
soko la India na zao la muhogo kwa ajili ya soko la China.