Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania au Kamati ya
Saa 72, ilifanya kikao chake juzi Ijumaa Aprili 7, 2017 jijini Dar es Salaam na
kufikia uamuzi ufuatao.
Kuhusu kupulizwa dawa vyumbani Uwanja wa Kambarage
Daktari wa Uwanja wa Kambarage, Dk. Abel Kimuntu amekataa
kuwasilisha taarifa yake kuhusu tuhuma za kupuliziwa dawa kwenye chumba cha
kubadilishia nguo cha timu ya Majimaji katika mechi namba 170 ya Ligi Kuu ya
Vodacom dhidi ya wenyeji Stand United. Klabu ya Majimaji iliwasilisha
malalamiko yake kwa Bodi ya Ligi kuhusu suala hilo.
Hivyo, Kamati imeagiza suala la daktari huyo lipelekwe kwenye
Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya
hatua za kinidhamu dhidi yake kutokana na kukataa kutoa ushirikiano kwa
mwendeshaji wa Ligi juu ya jambo hilo. Kamati ya Nidhamu inatarajiwa kukaa
wakati wowote wiki ijayo.
Kuhusu Mchezaji Abdi Banda Mechi namba 194 Kagera Sugar 2 vs Simba 1). Beki wa Simba, Abdi Banda jezi namba 24
amesimamishwa kucheza Ligi Kuu wakati akisubiri suala lake la kumpiga ngumi
kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla jezi namba 15 wakati akiwa hana mpira
kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF).
Alifanya kitendo hicho ambacho hakikuonwa na waamuzi katika
mechi hiyo iliyofanyika Aprili 2, 2017 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Uamuzi wa Kamati umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.
Pia Kamati ilibaini kuwa Banda alifanya kitendo cha aina hiyo
kwenye mechi namba 169 kati ya Simba na Yanga iliyofanyika Februari 25, 2017
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, Klabu ya Kagera Sugar iliwasilisha malalamiko dhidi ya
kitendo cha beki wa Simba, Abdi Banda kumpiga ngumi kiungo wao George Kavilla
wakati akiwa hana mpira, na Mwamuzi wa mechi hiyo kutochukua hatua yoyote.
Kwa vile kosa hilo ni la kinidhamu, Kamati imemsimamisha Abdi
Banda kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) wakati akisubiri suala lake kusikilizwa na
kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF). Kamati ya Nidhamu inatarajiwa kukaa wakati wowote wiki ijayo.
Kadhalika Klabu ya Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe
ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na timu ya Kagera Sugar
kumchezesha mchezaji Mohamed Fakhi Gharib wakati akiwa na kadi tatu za njano
katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini
Bukoba.
Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, imeahirisha shauri hilo
hadi Alhamisi Aprili 13, 2017 kwa vile bado inafuatilia baadhi ya vielelezo
kuhusu malalamiko hayo kabla ya kufanya uamuzi.
Mechi namba 195 (Yanga 1 vs Azam 0). Yanga haikuingia kwenye chumba chake cha
kubadilishia nguo, kutokana na kuwa na maji yaliyomwagwa na wanachama wa klabu
hiyo (makomandoo) muda mfupi kabla ya timu hiyo kuwasili uwanjani.
Kamati imeelekeza klabu ya Yanga iandikiwe barua ya onyo, na
kuitaka kuhakikisha wanachama wake wanaacha mara moja mtindo wa kumwaga maji
vyumbani baada ya kuwa vimeshafanyiwa usafi na wafanyakazi wa uwanja tayari kwa
ajili ya matumizi ya timu yao.