KAGERA, GEITA KUANZA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA AGOSTI 5,2024

July 24, 2024

 

Makamu Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Julai 24, 2024 Mjini Bukoba Mkoani Kagera.Wadau hao ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Bi. Giveness Aswile akiwasilisha mada.
*******************
Na. Waandishi Wetu, Geita na Kagera
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Geita na Kagera utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 05 hadi 11 Agosti, 2024 ambapo vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Geita leo tarehe 24 Julai, 2024.

Mkutano kama huo mkoani Kagera umefunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Juji Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk. Mikutano hiyo inafanyika ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo.

“Mzunguko wa pili wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utajumuisha mkoa huu wa Geita na Kagera ambapo uboreshaji utaanza tarehe 5 hadi 11 Agosti, 2024. Vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,” amesema Jaji Mwambegele.

Ameongeza kuwa mikoa hiyo inafanya uboreshaji kwenye mzunguko wa pili baada ya mzunguko wa kwanza ambao umejumuisha mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora ambako uboreshaji umeanza tarehe 20 Julai, 2024 na unatarajiwa kukamilika tarehe 26 Julai, 2024.

“Tume tayari imeanza zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo uzinduzi ulifanyika mkoani Kigoma tarehe 20 Julai, 2024 na mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB). Uzinduzi huo umeenda sambamba na kuanza kwa mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi. Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo unaendelea hadi tarehe 26 Julai, 2024,” amesema.

Akizungumza mkoani Kagera, Mhe. Jaji Mbarouk amesisitiza kuwa kadi za wapiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 ni halali na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo. Hivyo, amewataka wadau wa uchaguzi kwenye mkoa huo kuwaelimisha wapiga kura wenye kadi hizo wasiende kuboresha taarifa zao kwa kuwa zoezi hilo haliwahusu.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 zenye jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni halali na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo. Hivyo, zoezi hili la uboreshaji wa Daftari haliwahusu wapiga kura wenye kadi hizo,” Jaji Mbarouk amesema.

Akizungumzia teknolojia ya uandikishaji wa wapiga kura wakati wa kuwasilisha mada, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhan amesisitiza kuwa wapiga kura wanaoboresha taarifa zao wanaweza kuanza mchakato wa awali kwa kutumia simu janja au kiswaswa na kompyuta kupitia mfumo ujulikanao kama Online Voters Registration System (OVRS) au kwa kubobya *152*00#, kisha namba 9 na kufuata maelekezo.

”Mtumiaji wa huduma hii, atatakiwa kufika kituo anachokusudia kujiandikisha ili akamilishe hatua za kupigwa picha, kuweka saini na kupatiwa kadi yake ya mpiga kura,” amesema Bw. Kailima.

Meza kuu ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk (katikati) Mjumbe wa Tume, Mhe. Magdalena Rwebangira (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Bi. Giveness Aswile



Viongozi wa kimila ni miongoni mwa wadau muhimu wa Uchaguzi hivyo Tume iliwashirikisha viongozi hao kutoka Kagera.

Wadau kutoka makundi mbalimbali ya wanawake na vijana nao walishiriki.

Wahariri kutoka Vyomb0 vya habari nao walishiriki.
Vyama vya siasa nao walishiriki
Viongozi wa Dini nao walishiriki

Makamu Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk akiongoza majadiliano wakati wa Mkutano huo.






Maswali na maoni mbalimbali yaliulizwa na kutolewa na wadau na kupatiwa majibu.Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Bi. Giveness Aswile akifafanua jambo.



Maswali na maoni mbalimbali yaliulizwa na kutolewa na wadau na kupatiwa majibu.

JESHI LA ZIMAMOTO TANGA WAJA NA PROGRAMU MBALIMBALI ZA KUELIMISHA UMMA NAMNA KUKABILIANA NA MAJANGA YA MOTO

July 24, 2024

Na Oscar Assenga,TANGA

JESHI la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tanga wameanzisha program mbalimbali za kuielimisha Umma kuweza kuwa na utambuzi ili majanga ya moto yanapotokea waweze kukabiliana nayo.

Hayo yalibainishwa leo na Afisa Operesheni wa Jeshi hilo mkoani Tanga Mrakibu Msaidizi wa Jeshi hilo Yusuf Msuya wakati akizungumza na kuhusu namna walivyojipanga kukabiliana na matukio ya moto kwa wananchi.

Alisema katika kuzuia ajali za moto wameamua kuja na mpango huo ambao wanaamini utakuwa na mafanikio makubwa ambao utakwenda sambamba na

ukaguzi wa kinga na tahadhari kwa majanga katika maeneo mablimbali yakiwemo ya biashara,makazi na vyombo bya usafiri na usafirishaji.

“Lengo la ukaguzi huu ni kutambua yale mapungufu na risk zilizopo kwenye majengo ambayo ni hatari na kuyawasilisha kwa mmiliki ikiwemo kumpa mapendekezo na hatua za kufanya ili kuzuia moto usitokee “Alisema

Msuya alisema na endapo moto unapotokea madhara yake yawe machache kwa maisha ya wakazi wa Jengo au wafanyakazi wa eneo husika na ambaye atakidhi vigezo vya kukabuliana na majanga ya moto watatoa cheti kutoka Jeshi hilo cha kuonyesha eneo limekaguliwa na kukidhi vigezo vya usalama wa moto .

,”Katika kulipambanua hili nitoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Tanga kufika kwenye ofisi zetu zilizopo maeneo mbalimbali kwa ajili ya kupatiwa wataalamu kwa lengo la kwenda kukagua vyombo vyao vya usafiri iwe nchi kavu au majini pamoja na maeneo ya Biashara na ya makazi uli kuimarisha usalama dhidi ya majanga ya moto kwenye maeneo yao”Alisema

Awali akizungumzia mpango huo Mfanyabiashara katika soko la Mgandini Jijini Tanga Rashidi Said Kihondo alisema kwamba iwapo wataanzisha mpango huo utawasaidia kuweza kukabiliana na moto hivyo kupunguza majanga hayo katika maeneo yao.

“Huko nyuma tuliwahi kukutana na janga la moto na soko liliungua kutokana lakini kwa sasa kutokana na baadhi ya elimu ya kukabiliana na majanga hayo ya moto tulianza kuchukua tahadhari na hayajaweza kujitokeza tena”Alisema

Naye wa upande wake Mfanyabiashara wa soko Makorora Jijini Tanga Mwanahamisi Bakari alisema kwamba elimu hiyo iwapo elimu hiyo itatolewa kwa wafanyabiashara itawawezesha kukabiliana na majanga ya moto na kuweza kuyadhibiti pindi yanapojitokeza na hivyo kutokuwa na adhari kubwa kwao.

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA WAHASIBU AFRIKA

July 24, 2024

 Na. Peter Haule na Joseph Mahumi, WF, Arusha


Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Wahasibu Barani Afrika (African Association of Accountants General Meeting (AAAG)) utakaofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 3 hadi 5 Disemba Mwaka 2024, ukiwahusisha zaidi wa washiriki 2,000 kutoka takriban nchi 55 za Bara la Afrika.

Hayo yameelezwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari jijini Arusha, uliolenga kuujulisha umma kuhusu mkutano huo na fursa za kiuchumi na kijamii kwa watanzania.

CPA Mkude alisema kuwa mkutano huo unatarajia kuleta manufaa makubwa kiuchumi na kijamii pamoja na kuitangaza sekta ya utalii ya Tanzania, hususan kwa wajumbe kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko katika ukanda wa Kaskazini.

Alizitaja faida nyingine za mkutano huo kuwa ni pamoja na kuwa na Afrika yenye mafanikio yenye msingi wa ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu, Bara jumuishi lililounganishwa kisiasa na kwa kuzingatia maadili ya Pan-Africanism.

Aliyataja manufaa mengine kuwa ni pamoja na kuwa na maono ya Mwamko wa Afrika na Afrika yenye utawala bora, demokrasia, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria, Afrika yenye amani na usalama na Afrika yenye utambulisho thabiti wa kitamaduni, urithi wa pamoja na maadili.

CPA Mkude alisema kuwa Mkutano huo utawaleta Wahasibu wakuu wa Serikali Afrika watakaoambatana na Wahasibu Wakuu wa Wizara, Taasisi za umma na Wahasibu na wadau wengine ambao watapata fursa ya kusikiliza mada za masuala mbalimbali ya kitaaluma na kubadirishana mawazo na kujua fursa zinazopatikana katika nchi za Afrika.

Alisema wageni kutoka nje watakuja na fedha za kigeni ambazo watazitumia hapa Tanzania kwa kuwa watatembezwa kwenye mbuga za Wanyama na vituo mbalimbali vya utalii na hivyo kuunga mkono dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuutangaza Utalii wa Tanzania.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wa nyumba za wageni (hoteli), usafiri, mamalishe na jamii kwa ujumla kuchangamkia fursa hiyo ya ujio wa wageni ili kunufaika kiuchumi na kijamii.

“Natoa wito kwa Maafisa Masuuli wa Wizara na Taasisi zote kuwaruhusu Wahasibu, wakaguzi na wadau wengine watakaoomba kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Pili wa Wahasibu wakuu wa Serikali Afrika, African Association of Accountants General (AAAG) utakaofanyika jijini Arusha mwezi Desemba, 2024”, alisema CPA Mkude

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wahasibu wa Afrika, ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa nchi ya Lesotho, Bi. Malehlohonolo Mahase, alisema Mkutano wa Wahasibu Afrika unafanyika Tanzania kwa kuwa ni mwanachama anayeaminika na amekuwa mshiriki mwaminifu katika umoja huo, na kwamba wajumbe wa mkutano huo wanakuja kujifunza namna Tanzania ilivyopiga hatua kubwa katika matumizi ya mifumo ya fedha.

Alisema kuwa Tanzania ipo vizuri katika kutekeleza viwango vya kimataifa vya kihasibu, imekuwa ya mfano katika ukuaji wa Uchumi, imeimarika katika suala la ukarimu wa wageni, maendeleo katika teknolojia ya Habari na Mawasiliano na ni miongoni mwa nchi zenye vivutio vingi vya utalii hivyo wanachama kuna mambo mengi ya kujifunza.

Aidha alieleza kuwa Mkutano huo utakao wakutanisha pia Jumuiya za wafanyabiashara watapata fursa ya kujua ni namna gani Afrika ipo tayari katika suala la uwekezaji na namna ya kuripoti hali ya Uchumi ya Afrika, jambo ambalo litaongeza uwazi na uwajibikaji.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Bi. Christine Mwakatobe alisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wageni wanapokuja wanapata huduma bora kwa kuwa wanaamini watakuwa mabalozi wa Tanzania na watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

Alisema anamshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuitangaza nchi yetu Duniani na kwamba hauo ni matunda ambayo Taasisi za Serikali kwa ujumla zinafaidi kwa kazi yake anayoifanya, huku Kituo chake cha Mikutano kikihudumia mikutano mingi ya Kitaifa na Kimataifa.

Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Leonard Mkude (Katikati), akizungumza na wanahabari katika ukumbi wa Mikutano katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kuhusu ujio wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika (African Association of Accountants General-AAG Meeting) unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Disemba Mwaka huu, katika Kituo hicho , ambapo washiriki zaidi ya 2,000 kutoka nchi za Afrika na unalenga kujenga Imani ya umma katika Mifumo ya Usimamizi wa Fedha za Umma kwa Ukuaji Endelevu. Kushoto ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wahasibu Wakuu wa Afrika, Bi. Malehlohonolo Mahase, na Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Bi. Christine Mwakatobe.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA. Leonard Mkude, akizungumza na wanahabari katika ukumbi wa Mikutano katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kuhusu ujio wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika (African Association of Accountants General-AAG Meeting), unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Disemba Mwaka huu, katika Kituo hicho cha AICC, na utawashirikisha zaidi ya washiriki 2,000 kutoka nchi za Afrika na mkutano huo unalenga kujenga Imani ya umma katika Mifumo ya Usimamizi wa Fedha za Umma kwa Ukuaji Endelevu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wahasibu Wakuu wa Afrika ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Lesotho, Bi. Malehlohonolo Mahase, akizungumza wakati wa Mkutano na wanahabari katika ukumbi wa Mikutano katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kuhusu ujio wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika (African Association of Accountants General-AAG Meeting) unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Disemba Mwaka huu, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), ambapo amesema kuwa Mkutano huo utakawakutanisha pia Jumuiya za wafanyabiashara na watapa fursa ya kujua ni namna gani Afrika ipo tayari katika suala la uwekezaji na namna ya kuripoti hali ya Uchumi ya Afrika, jambo ambalo litaongeza uwazi na uwajibikaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Bi. Christine Mwakatobe, akizungumza kuhusu fursa ambazo Tanzania na wakazi wa mkoa wa Arusha watapata wakati wa Mkutano na wanahabari katika ukumbi wa Mikutano katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kuhusu ujio wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika (African Association of Accountants General-AAG Meeting) unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Disemba Mwaka huu, katika Kituo cha AICC, ambapo amesema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wageni wanapokuja wanapata huduma bora na watakua mabalozi wazuri wa Tanzania.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, akiongoza Mkutano wanahabari katika ukumbi wa Mikutano katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kuhusu ujio wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika (African Association of Accountants General-AAG Meeting) unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Disemba Mwaka huu, katika Kituo hicho cha AICC, ambapo Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, Mwenyekiti wa Umoja wa Wahasibu wa Afrika, ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Lesotho, Bi. Malehlohonolo Mahase na Mkurugenzi Mkuu wa AICC, Bi. Christine Mwakatobe, wamewaeleza wanahabari kuwa mkutano huo unatarajia kuleta manufaa makubwa kiuchumi na kijamii pamoja na kuitangaza sekta ya utalii ya Tanzania, kwa wajumbe kutembelea vivutio vya utalii, hususan vilivyoko katika ukanda wa Kaskazini.
Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Wizara ya Fedha, Bw. Renatus Msangira (Kulia) na Mhasibu Mkuu Msaidizi wa Serikali, Bw. Victus P. Tesha, wakifuatilia Mkutano na wanahabari katika ukumbi wa Mikutano katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kuhusu ujio wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika (African Association of Accountants General-AAG Meeting) unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Disemba Mwaka huu, katika Kituo hicho cha AICC, ambapo Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, Mwenyekiti wa Umoja wa Wahasibu wa Afrika, ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Lesotho, Bi. Malehlohonolo Mahase na Mkurugenzi Mkuu wa AICC, Bi. Christine Mwakatobe, wamewaleza wanahabari kuwa mkutano huo unatarajia kuleta manufaa makubwa kiuchumi na kijamii pamoja na kuitangaza sekta ya utalii ya Tanzania, hususan kwa wajumbe kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko katika ukanda wa Kaskazini.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude (Katikati), Mwenyekiti wa Umoja wa Wahasibu wa Afrika, ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa nchi ya Lesotho, Bi. Malehlohonolo Mahase (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mikutano wa Kitamaifa (AICC), Bi. Christine Mwakatobe, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Mkutano wao na wanahabari katika ukumbi wa Mikutano katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kuhusu ujio wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika (African Association of Accountants General-AAG Meeting) unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Disemba Mwaka huu, katika Kituo hicho, ambapo wamewaeleza wanahabari kuwa mkutano huo unatarajia kuleta manufaa makubwa kiuchumi na kijamii pamoja na kuitangaza sekta ya utalii ya Tanzania, kwa wajumbe kutembelea vivutio vya utalii hususan vilivyoko katika ukanda wa Kaskazini.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude (kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Wizara ya Fedha, Bw. Renatus Msangira, wakiteta jambo wakati wanawasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kufanya Mkutano na wanahabari, kuhusu ujio wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Wahasibu Wakuu wa nchi za Afrika (African Association of Accountants General-AAG Meeting) unaotarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 5 Disemba Mwaka huu, katika Kituo hicho, ambapo wamewaeleza wanahabari kuwa mkutano huo unatarajia kuleta manufaa makubwa kiuchumi na kijamii pamoja na kuitangaza sekta ya utalii ya Tanzania, kwa wajumbe kutembelea vivutio vya utalii hususan vilivyoko katika ukanda wa Kaskazini.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Arusha)

BENKI YA CRDB YATUNUKIWA TUZO YA UBORA KUHUDUMIA WAJASIRIAMALI WADOGO NA JARIDA LA EUROMONEY

July 24, 2024

 

Mkurugenzi wa Biashara ya Awali na Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul (kulia) akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Benki ya CRDB, Toyi Ruvumbagu mara baada ya Benki ya CRDB kutangazwa taasisibora ya kuhudumia biashara ndogo na za kati katika hafla iliyofanyika jijini London nchini Uingereza mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kutokana na ubunifu na umahiri wake katika mikakati tofauti ilinayo katika kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake pamoja na wadau wengine, Benki ya CRDB imetunukiwa tuzo ya kimataifa ya benki bora Tanzania inayohudumia biashara ndogo na za kati kwa mwaka 2024 na Jarida la Euromoney la nchini Uingereza.

Tuzo hizo zinazotolewa kwa miaka 30 sasa, huzitambua benki na taasisi za fedha zenye mchango mkubwa kwa jamii inazozihudumia kwa namna tofauti hivyo kuchangia uchumi wa mataifa yao na dunia kwa ujumla.

“Euromoney ni jarida kubwa duniani linalofanya utafiti wa kina kabla ya kuitambua na kutunuku benki tuzo yake. Wanao uzoefu mkubwa wa zaidi ya miaka 30 ya kuandaa tuzo za benki dunia nzima. Najisikia furaha kwa Benki yetu ya CRDB kushinda tuzo za Euromoney kwa mwaka wa tatu mfululizo sasa,” amesema Bonaventura Paul, Mkurugenzi wa Biashara ya Awali na Kati wa Benki ya CRDB aliyepokea tuzo hiyo.

Paul amesema Benki ya CRDB imeongeza juhudi katika kuwahudumia wajasiriamali nchini kwa kubuni bidhaa zinazoendana na mahitaji yao jambo lililowawezesha wafanyabiashara kuimarisha kipato na kukuza miradi yao pamoja na kukuza mchango wao kwenye pato la taifa. Kati ya juhudi hizo, mkurugenzi huyo amesema ni utaratibu wa kuwaruhusu wajasiriamali kukopa kwa kutumia taarifa za mtiririko wao wa mzunguko wa fedha za biashara bila kuhitaji kuwa na dhamana.

“Mfanyabiashara mwenye hati ya ununuzi anaweza kupata mkopo kutoka Benki yetu ya CRDB. Tunashirikiana na wadau tofauti kufanikisha hili. Mwaka jana kwa mfano, tulishirikiana na kampuni ya Silent Ocean kuwawezesha wafanyabiashara wanaoingiza mzigo nchini kutoka nje ya nchi kwa kuwakopesha hadi dola 63,000 za Marekani (zaidi ya shilingi milioni 170) kugharimia usafiri, gharama za bandari pamoja na kodi,” amesema Paul.

Mwaka 2023 Benki ya CRDB ilikopesha zaidi ya trilioni 8.9 na asilimia 12 ya kiasi hicho kilielekezwa kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati. Tengo hili limekuwa likiongezeka kila mwaka kwani mwaka 2022 ilikuwa asilimia 11 ya mikopo yote tuliyoitoa.

Matumizi ya teknolojia hasa katika malipo, Paul amesema yameongeza ufanisi katika biashara za wajasiriamali wengi. Wajasiriamali wamekuwa wakiunganishwa na mifumo ya kidijitali ya upokeaji na ufanyaji wa malipo kwa urahisi ikiwamo mfumo wa LIPA Namba na msimbomilia (QR Code), Huduma za benki kupitia mtandao (Internet banking), na huduma ya SimBanking zinazowawezesha kusimamia kwa urahisi akaunti zao.

Ili kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi, Paul amesema benki imetanua wigo kwa kuwahusisha wafanyabiashara wachanga ambao nao hunufaika kwa mafunzi na elimu ya fedha inayotolewa kupitia majukwaa tofauti. Hali hiyo, amesema imeifanya benki iongeze fungu inalolitenga kwa ajili ya kundi hili.

Paul ameongezea kuwa katika mkakati wake wa muda wa kati wa miaka mitano 2023 -2027, Benki ya CRDB imetoa kipaumbele kikubwa katika uwezeshaji wa wajasiriamali wadogo, na kati (MSMEs). Paul amesema katika nusu ya mwaka huu tayari Benki ya CRDB imesha toa mikopo yenye thamani ya jumla ya takribani Shilingi trilioni 1.5.

Hivi karibuni Benki ya CRDB iliadhimisha Siku ya Wajasiriamali Duniani, ambapo pamoja na maadhimisho hayo ilizindua akaunti maalum kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na wa kati iliyoboreshwa zaidi na inayoendana na mahitaji halisi ya wateja ijulikanayo kama ‘Biashara Account.’

Kila mwaka, zaidi ya benki na taasisi za fedha 600 kutoka zaidi ya nchi 100 duniani kote hushiriki tuzo za Euromoney zinazoheshimika zaidi katika sekta ya benki na fedha kutokana na utafiti unaofanywa dhidi ya washindi pamoja na ushauri elekezi kwa washiriki wote ambao umekuwa msaada mkubwa wa kuboresha huduma za benki nyingi ulimwenguni kote.

KETI JIFUNZE YA BENKI YA CRDB YAIFIKIA SHULE YA WANAFUNZI MAALUM, MAJIMOTO KATAVI

July 24, 2024

 

  
Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga  (watatu kulia) akipokea sehemu ya msaada wa magodoro, viti na meza kutoka kwa Meneja wa Benki Uhusiano wa Benki ya CRDB Kanda ya Nyada za Juu Kusini, Pascalia Bura, (katikati) kwa ajili ya Shule ya Msingi ya Majimoto (Shule Maalum), katika hafla ya makabidhiano hayo, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Wilayani ya Mpimbwe, mkoani Katavi. Wapili kulia ni Mbunge wa Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Geophrey Pinda, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mpimbwe, Shamimu Mwariko (watatu kushoto) pamoja na viongozi wengine mbalimbali.
 
========    ========    ========

Benki ya CRDB kupitia sera yake ya kurudisha kwa jamii sehemu ya asilimia moja ya faida yake, imeweza kutoa msaada wa magodoro 68 pamoja na viti 24 na meza 2 kwa matumizi ya wanafunzi wenye changamoto za usikivu na madawati 25 kwa ajili ya wanafunzi wenye changamoto ya uoni hafifu na viungo katika Shule ya Msingi ya Majimoto (Shule Maalum) , iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi.

Akipokea msada huo, Mkuu wa Wilaya ya Mlele anayesimamia pia Wilaya ya Mpimbwe, Majid Mwanga ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuona umuhimu wa kuisaidia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutatua changamoto mbalimbali za elimu hapa nchini. Ameishuru Benki ya CRDB kwa msaada huo wa magodoro, viti pamoja na meza.

Msaada huo ni muendelezo wa programu maalumu ya benki hiyo iitwayo 'Keti Jifunze' yenye lengo la kuwawezesha wanafunzi kujifunza wakiwa wameketi katika mazingira mazuri na salama. Shule Maalum ni zile zinazohudumia wanafunzi wenye changamoto mbalimbali kama vile uoni, usikivu na viungo.

Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga  (watatu kushoto), Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Geophrey Pinda (watatu kushoto), Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mpimbwe, Shamimu Mwariko (wapili kulia), Meneja wa Benki Uhusiano wa Benki ya CRDB Kanda ya Nyada za Juu Kusini, Pascalia Bura (wapili kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Benki ya CRDB na Halmashari wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wanafunzi Shule ya Msingi ya Majimoto (Shule Maalum) iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi.
Meneja wa Benki Uhusiano wa Benki ya CRDB Kanda ya Nyada za Juu Kusini, Pascalia Bura (watatu kushoto) akizungumza jambo wakati wa hafla ya kukabidhi magodoro, viti na meza


Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga akizungumza katika hafla hiyo.