DK.BITEKO:KANUNI UNUNUZI MAFUTA KITUO CHA GBP MKOANI TANGA KUANZA KUTUMIKA FEBRUARI

January 26, 2024



NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk.Dotto Biteko amesema kanuni ya kuwataka wafanyabiashara wa mafuta kununua mafuta yao katika kituo cha GBP Tanga zimekamilika na zitaanza kutumika rasmi Februari mwaka huu.

Dk.Biteko ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baaa ya kutemebela mradi wa bomba la mafuta wa Afrika ya Mashariki (EACOP), Flow Meter inayomilikiwa na Mamlaka ya Bandari na baadaye kituo cha kuhifadhi mafuta cha GBP.

"Kanuni zilirekebishwa mwezi uliopita na wafanyabiashara wote wa Kanda ya Kaskazini waache kwenda Dar es Salaam kununua mafuta hayo kwani ndiko kunasababisha kuongeza bei ya mafuta na muda.

" Nia ya Serikali ni kuhakikisha wafanyabiashara wa mafuta Kanda ya Kusini wanachukua mafuta yao Mtwara na wale wa Kaskazini na hata wale ambao wanatoka nchi jirani ya Kenya kuchukulia mafuta mkoani Tanga, "amesema.

Dk.Biteko ametoa mwito kwa taasisi za Serikali, Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA), EWURA, Wakala wa Uagizaji Mafuta na Shirika la Viwango (TBS) zote kwenda kasi ili kutekeleza agizo hilo ili taratibu za kushusha mafuta Tanga zianze mara moja.

Akizungumzia kuhusu Bandari ya Tanga Dk. Biteko amesema shughuli za badari zinatarajiwa kungezeka kutokana na Serikali kusaini kanuni inayoelekeza wanunuzi wa mafuta wa Kanda ya Kaskazini kununua bidhaa hiyo Tanga,

Dk Biteko amesema Serikali inathamini uwekezaji unaofanywa na kampuni ya GBP namipango yake ya kuinua uwekezaji huo na iko tayari kuhakikisha kuwa uwekezaji huuo hauna hasara,

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Gulf Bulk Petroleum (GBP) ya Tanga Badari Seif Masoud amesema kampuni hiyo iliyoanza shughuli zake mwaka 2001 sasa hivi inauwezo kwa kuhudumia malori 12 kwa mpigo kwa muda wadakika 30 na mabehewa 20 kwa muda wa dakika 45.

Ameongeza kampuni hiyo ambayo ina uwezo wa kuhifadhi lita million 203 inampangplo wa kupanua shughuli zake kwa kujenga sehemu ya kupakia na kupakua mafuta katika kina cha bahari cha mita 20 ili kuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa zenye uzito wa tani 100,000.

Amesema kampuni ina mpango kwa kujenga mtambo wa kuzalisha vilainishi, mtambo wa gesi na wa kupokelea lami kutoka melini huku akisisitiza haja ya kuwepo na akiba kubwa ya mafuta.

Wakati huo huo, Meneja wa Bandari, Tanga, Masoud Mrisha amesema tangu kufungwa kwa flow mita katika badandari hiyo mwaka 2020 Serikali imefanikiwa kudhibiti upotevu wa mafuta uliokuwa ukitokea awali.


RAIS SAMIA AHITIMISHA ZIARA YAKE YA KITAIFA NCHINI INDONESIA KWA KUTEMBELEA KIWANDA CHA INDESSO AROMA

January 26, 2024

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Januari Makamba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo pamoja na viongozi wengine wakifuatilia wasilisho la historia ya Kiwanda cha Karafuu cha Indesso Aroma nchini Indonesia wakati akihitimisha ziara yake nchini humo tarehe 26 Januari, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Afisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Karafuu cha Indesso, Robby Gunawan kuhusu mchoro maalum unaoashiria mchakato mzima wa utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na Karafuu nchini Indonesia tarehe 26 Januari, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Afisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Karafuu cha Indesso, Robby Gunawan kuhusu moja ya bidhaa zitokanazo na Karafuu ambazo zinatengenezwa na Kiwanda hicho nchini Indonesia tarehe 26 Januari, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo kuhusu kazi mbalimbali zinazofanyika katika Kiwanda cha Karafuu cha Indesso Aroma wakati akihitimisha ziara yake nchini Indonesia tarehe 26 Januari, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo kuhusu kazi mbalimbali zinazofanywa katika Kiwanda cha Karafuu cha Indesso Aroma nchini Indonesia wakati alipohitimisha ziara yake tarehe 26 Januari, 2024. Kiwanda hicho kikubwa kinatengeneza bidhaa mbalimbali kutokana na malighafi ya zao hilo la Karafuu



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Mkurugenzi wa Ubunifu na uendeshaji wa Kiwanda cha Indesso Bi. Rosalina Privita mara baada ya kukagua shughuli mbalimbali za Kiwanda hicho cha Karafuu nchini Indonesia tarehe 26 Januari, 2024.

RAIS DKT. MWINYI AZINDUA RASMI JEZI YA TIMU YA TAIFA YA ZANZIBAR

January 26, 2024

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, leo amezindua rasmi Jezi ya Timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) zilizotengenezwa na mbuifu wa mitindo nchini, Sheria Ngowi kwa udhamini wa Benki ya CRDB, katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Viwanja vya Nyamanzi, Uguja Zanziar.





TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI YASHIRIKI MAONESHO YA WIKI YA SHERIA-DODOMA

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI YASHIRIKI MAONESHO YA WIKI YA SHERIA-DODOMA

January 26, 2024

 

 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi-NEC inashiriki katika maonesho ya wiki ya Sheria yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Utaratibu huu wa kushiriki katika maonesho mbalimbali nchini ni sehemu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kutoa elimu ya Mpiga Kura endelevu ambapo wadau mbalimbali wa Tume hufika katika Banda hilo na kupata elimu hiyo.

Maonesho haya ambayo huandaliwa na Mahakama ya Tanzania ikiwa ni kuelekea kilele cha siku ya sheria na kuanza kwa mwaka mpya wa Mahakama. 

Mwaka huu maonesho haya yamebeba kauli mbiu isemayo "Umuhimu wa Dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa:Nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha mfumo Jumuishi wa Haki Jinai" yameanza tarehe 24 Januari,2024 na yanatarajia kumalizika tarehe 30 Januari, 2024.

WAZIRI MKUU ATOA AGIZO WASIMAMIZI MJI WA SERIKALI

January 26, 2024

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wasimamizi na wataalamu wa ujenzi wa Mji wa Serikali jijini Dodoma wahakikishe matarajio ya ujenzi huo yanafikiwa kama ilivyokusudiwa.


Ametoa agizo hilo wakati akizungumza na Mtawala wa Mamlaka ya Kusimamia Uendelezaji wa Mji wa Serikali wa Korea Kusini, Mheshimiwa HyeongRyeol Kim.

Amekutana na kiongozi huyo leo Ijumaa, Januari 26, katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni Jijini Dar es Salaam, baada ya hafla ya utiaji saini mikataba ya makubaliano kati ya taasisi za Korea Kusini na Tanzania.

Makubaliano hayo yanahusu kubadilishana uzoefu juu ya usimamizi na uratibu wa uendelezaji wa makao makuu na mji wa Serikali pamoja masuala ya ujenzi vikiwemo viwanda, hoteli.

Utiwaji saini huo umefanyika kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi Uendelezaji wa Mji wa Segong na kampuni ya Heerim ya Korea Kusini katika masuala ya usanifu na ubunifu wa ujenzi kwenye Mji wa Serikali na Makao Makuu jijini Dodoma.

“Serikali ya Tanzania na Korea Kusini zina mahusiano mazuri ya kidiplomasia, hivyo matarajio yetu ni kuona Makao Makuu na Mji wa Serikali jijini Dodoma unakuwa mzuri.”

Kwa upande wake, Mheshimiwa HyeongRyeol Kim amesema utiaji saini wa makubaliano hayo ni fursa muhimu ya kuendeleza ushirikiano baina ya mataifa hayo.

Pia, Mheshimiwa Kim amemshukuru Waziri Mkuu kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na amemuhakikishia kwamba nchi yao itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuliendeleza jiji la Dodoma.


MWAROBAINI WA MIUNDOMBINU KOROFI SERENGETI WAPATIKANA

January 26, 2024


Kamishna Kuji atoa maelekezo mahususi Serengeti



Na. Edmund Salaho/Serengeti.


Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA Juma Kuji leo amefanya ziara ya kukagua miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuiagiza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kushughulikia mara moja maeneo korofi ya barabara ndani ya hifadhi hiyo, ili watalii wafikie adhma yao ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Akizungumza baada ya kukagua maeneo hayo Kamishna Kuji, ameielekeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kurekebisha maeneo yote korofi na kuhakikisha kuwa hakuna maeneo ambayo hayatapitika licha ya uwepo wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ili kupunguza adha kwa wageni.

“Licha ya changamoto ya mvua kubwa zinazoendelea hatuwezi kusubiri ziishe tumeazimia kushughulikia kwa haraka maeneo yote korofi ikiwa ni hatua za haraka, lakini lengo kuu ni kuhakikisha barabara hizi zinakuwa na tabaka gumu, haya ni maagizo yangu kwa menejimenti kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote”.

Aidha,Kamishna Kuji alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchi nzima.

Vile vile, Kamishna Kuji amebainisha kuwa TANAPA imejipanga kuhakikisha miundombinu yote katika Hifadhi za Taifa Tanzania inaboreshwa ili kukidhi matamanio ya wageni wanaotembelea Hifadhi za Taifa zilizosheheni sifa lukuki za kuwa na utajiri mwingi wa bayoanuai.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu Mhandisi. Dkt. Richard Matolo alibainisha kuwa Shirika limekuwa likitumia teknolojia mbalimbali kutafuta mwarobaini wa changamoto za barabara na kubainisha kuwa mwaka huu hali imekuwa tofauti kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha tofauti na miaka mingine.

“Shirika limefanya majaribio mbalimbali na kuja na teknolojia ambazo zitapelekea barabara hizi hususani hii ya Naabi iwe inapitika wakati wote tafiti nyingi zilionekana haziwezi kuleta matokeo chanya katika maeneo haya kutokana na asili ya udongo wa hifadhi zetu hivyo kutokana na stadi zote imethibitika kuwa tunaweza kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizi”

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moronda Moronda amesema, Menejimenti ya Serengeti imejipanga kuhakikisha maeneo korofi yanarekebishwa na kutoa rai kwa waongoza watalii kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali katika Hifadhi ikiwemo alama mbalimbali za barababra ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza hasa wakati huu wa mvua.

Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mkuu anayeshughulikia Mawasiliano Catherine Mbena, alisema
"Lengo letu kama Shirika ni kuhakikisha wageni wetu(watalii) wanapofika maeneo yetu wanaondoka na kumbukumbu nzuri, ndio maana timu nzima ya TANAPA iko hapa kuhakikisha kipande hiki korofi kinapitika na tumekuwa na mipango ya muda mrefu na mfupi na yote tutaitekeleza lengo likiwa ni wageni wetu wafurahie vivutio hivi vya kipekee duniani"

Hifadhi ya Taifa Serengeti hivi karibuni imekumbwa na changamoto ya barabara kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Tanzania na nchi jirani, hivyo ukarabati wa miundombinu ya barabara hizo unaofanywa na TANAPA utaondoa adha hiyo na kuzifanya barabara za hifadhi za Hifadhi ya Taifa Serengeti kupitika mwaka mzima.