PSSSF YAPEWA TUZO YA KIMATAIFA

May 30, 2023

 

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, DAR ES SALAAM

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Umepewa tuzo na Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Jamii (International Social Security Association-ISSA)kutokana na mafanikio iliyoyapata katika kipindi kifupi baada ya kuunganishwa (Merge) kwa mifuko minne ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF, PPF, GEPF NA LAPF na kuwa PSSSF.

Akizungumzia tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema sababu nyingine iliyoifanya ISSA kutoa tuzo kwa Mfuko huo ni pamoja na jinsi Mfuko ulivyoweza kupunguza gharama za uendeshaji na ulipaji wa mafao kwa wakati.

“Kwenye suala la kuunganisha mifuko yapo mambo manne ambayo ISSA imeyaona na kuona ni mafanikio ambayo ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji, kutoa mafao yanayofanana kwa wanachama wa Mfuko licha ya kutoka kwenye mifuko tofauti, kukabiliana na madeni kabla ya mifuko kuunganishwa na pia suala la uwekezaji hususan katika viwanda.” Alisema

CPA Kashimba aliishukuru Bodi ya Wadhamini kwa usimamizi mzuri na hivyo kuufanya Mfuko huo kufanya vizuri.

“Kazi kubwa ya kusimamia zoezi hili la kuunganisha mifuko mmeifanya ninyi Bodi kwa maelekezo ya serikali, sehemu nyingi duniani wanasema karibu asilimia 85 ya kampuni zilizoungana huwa zinashindwa lakini muunganiko wetu sisi umeendelea kufanya vizuri hadi kuivutia taasisi hii kubwa kuifanya PSSSF kuwa mfano wa kuigwa.” Alisema CPA Kashimba.

Alisema tayari Mfuko umeanza kupokea wageni KUTOKA sehemu mbalimbali wakihitaji kujifunza kutoka PSSSF.

“Juzi kamati ya bunge ya Uganda wao wanaanzisha Mfuko wa Watumishi wa Umma na walikuja kujifunza na wameridhishwa na elimu tuliyowapatia.” Alifafanua.

Alisema tuzo hiyo ni zawadi kwa Bodi na sio Menejimenti pekee na mfuko uko kwenye mikakati ya kuhakikisha unaendelea kutoa huduma bora kwa Wanachama na Wastaafu kwa ujumla.

Awali Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbarouk Magawa alidokeza kuwa eneo lingine ambalo liliwavutia watoa tuzo ni jinsi mfukoulivyofanya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma kwa wastaafu na wanachama. 

"Suala la Huduma kwa wananchama, jinsi tunavyokusanya michango, tunavyolipa mafao, kutoka kwenye matumizi ya hundi kulipa mafao, lakini jinsi tunavyohakiki wastaafu wetu, haya yote yaliwavutia." Alifafanua Bw. Magawa.

Aidha Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma (PSSSF) Bw. James Mlowe alisema PSSSF ilikabidhiwa tuzo hiyo jijini Abidjan Ivory Coast Mei 17, 2023 na kwamba ifikapo Agosti Mosi, 2023 PSSSF itafikisha miaka mitano tangu kuundwa kwake baada ya kuunganishwa kwa mifuko (merge), Agosti Mosi, 2018.

“Majukumu ya mfuko yanatekelezwa vizuri, uwezo wa mfuko unazidi kuimarika, watumishi wanazidi kuwa kitu kimoja na kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kwakweli mafanikio haya ndiyo yamewavutia ISSA kuweza kutoa tuzo hii” Alisema

“Tunajisikia faraja kwa tuzo hii na hii imekuwa chachu ya  kuendelea kutekeleza majukumu yetu sawasawa kuendelea kuwahudumia wanachama wetu na wastaafu kikamilifu.” Alitoa hakikisho.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF),  Dkt. Aggrey Mlimuka (kulia) akipokea tuzo ya Kimataifa inayotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Jamii (International Social Security Association-ISSA) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba katika hafla fupi iliyofanyika Makao Makuu ndogo ya PSSSF jijini Dar es Salaam Mei 30, 2023. PSSSF ilipewa tuzo hiyo na ISSA kwa kutambua mafanikio iliyopata PSSSF katika kipindi kifupi ndani ya muundo mpya wa mifuko kuunganishwa (merging).

Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbarouk Magawa, akielezea mchakato uliopelekea PSSSF kupewa tuzo hiyo.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma PSSSF, Bw. James Mlowe, akionesha tuzo hiyo.


KLABU YA KWANZA YA MKONGE YAZINDULIWA

May 30, 2023


Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) kwa kushirikiana na Shule ya Sekondari ya Coastal ya jijini Tanga, zimezindua Klabu ya Mkonge kwa wanafunzi wa shule hiyo ambayo imelenga kuwafundisha vijana kuhusu kilimo cha Mkonge na Sekta ya Mkonge kwa ujumla hatua itakayowawezesha kujiajiri baada ya kumaliza masomo.

Akizindua klabu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TSB, Saddy Kambona amesema wazo la kuanzisha klabu hiyo lilizaliwa kwenye Mahafali ya kidato ya shule hiyo Machi mwaka huu, lakini baadaye ikaonekana isiwe klabu kwa ajili ya Shule ya Coastal pekee bali ianzishwe klabu itakayoshirikisha shule zote za Tanga na vizazi vinavyokuja kushiriki kwenye uchumi huu wa mkonge.

Amesema kwa muda mrefu imezoelekea kwamba elimu yetu haimuandai mwanafunzi kwenda kujitegemea anapomaliza shule, wengi wamekuwa na mtazamo kuwa kazi ya kuajiririwa ndiyo inafaa.

“Kwa hiyo sisi tulitazama wazo la kuwa na klabu za Mkonge kwa maana kama tunasema Mkonge ni Tanga na Tanga ni Mkonge, basi tunataka mtu akifika Tanga aone kweli kama Mkonge ni Tanga, tunategemea aone kwamba Mkonge ndiyo zao kuu la kibiashara.

“Yaani kuanzia anatua uwanja wa ndege anapotua anaona bidhaa za Mkonge barabarani hadi anapofika hotelini anakutana na mazuria ya Mkonge na bidhaa nyingine. Sasa sehemu ya kuanzia ni kuwa na klabu za kuhamasisha si tu kilimo cha Mkonge bali  pia kuhamasisha matumizi ya bidhaa za Mkonge lakini pia kushiriki kwenye kuzalisha hizo bidhaa.

“Baada ya hayo sasa Bodi inakuwezesha kupata elimu, utaalamu kuanzia shambani kulima Mkonge na uongezaji wa thamani, wataalamu wetu watatoa ujuzi huo kwa vijana wa Tanga na nje ya Tanga ili wanapomaliza shule huko wanakokwenda wakawafundishe na wengine,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Zao la Mkonge na Masoko, Olivo Mtung’e akizungumzia faida za Mkonge na somo la kuhamasisha wanachama wa klabu hiyo alisema mahitaji ya Mkonge kwa sasa yameongezeka ndiyo maana wanahamasisha wakulima kulima zao hilo.

“Nchi nyingi sasa zinahitaji Mkonge lakini kiasi ambacho tunakilima kwa sasa ni kidogo ndiyo maana baada ya kuingia kwenye kilimo cha wakulima wadogo sasa tunahamasisha na sisi kwenye familia zetu wenye mashamba ya eka moja hadi tatu walime Mkonge kwa sababu kwa sasa hali ya hewa inatusukuma kuelekea huko kwani zao la Mkonge linahimili hali za hew azote ili kuimarisha uchumi wa familia,” amesema.

Mkurugenzi Mtung’e anasema kutokana na hali hiyo, wahitimu hawana haja ya kutafuta ajira kwa sababu Mkonge wenyewe ni ajira kwani ukishapanda baada ya miaka mitatu unaanza kuvuna hadi kwa muda wa miaka 18.

Kwa upande wake mwanafunzi wa shule hiyo na mmoja wa wanachama wa klabu hiyo, Fatuma Mshashi amesema klabu hiyo yenye wanachama 50 ambao kati yao wavulana ni 23 na wasichana 27, inatekeleza malengo mbalimbali ikiwamo kufanya tafiti kuhusu kilimo cha zao la Mkonge ili kuona faida zake, kutoa elimu kwa wanafunzi, walimu, wadau wa elimu kuhusu umuhimu wa zao hilo, kuhamasisha jamii kutumia bidhaa za mkonge, kuwaandaa wanafunzi ili kuja kuwa wataalamu wazuri na wabobevu katika zao la Mkonge na nyingine nyingi.

“Ili kufanikisha malengo katika Klabu ya Mkonge katika shule yetu, tunaomba ofisi yako kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwalimu Mkuu itusaidie kukutanishwa na wataalamu wa zao la Mkonge ili kupata elimu na ujuzi wa zao hili, kuwezeshwa klabu kuwa na shamba darasa ambalo litakuwa la kujifunzia hatua zote za uandaaji hadi uvunaji ambapo shamba hilo mlitakuwa mradi wa klabu,” amesema.