BILIONI 161.4 ZA RAIS DKT SAMIA ZAIWEZESHA TANGA UWASA KUTEKELEZA MIRADI 20 YA KIMKAKATI

March 22, 2024

MKUU wa wilaya ya Muheza Zainabu Abdallah wa kwanza kushoto akikapata utepe kuashiria makabidhiano ya mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Maji Taka wilayani Muheza pamoja na kukabidhi Vyoo vilivyojengwa ikiwa ni sehemu ya Ujenzi wa Mradi huo kwa shule ya Sekondari Bonde,Shule ya Msingi Mdote na Soko la Majengo wilayani Muheza uliotekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) Kulia Diwani wa Kata na anayefuatia ni Kaimu Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Rashid Shabani

MKUU wa wilaya ya Muheza Zainabu Abdallah akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo
Kaimu Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Rashid Shaban akizungumza kuhusu mradi huo

Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Bonde akieleza taarifa yake wakati wa makabidhiano hayo
Sehemu ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Bonde wakiwa kwenye halfa hiyo ya makabidhiano

Na Oscar Assenga, MUHEZA

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa ) wamesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt Samia Suluhu Serikali imewawezesha ujenzi wa miradi ya kimkakati 20 ya maji safi yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 161 ambayo imekuwa chachu kubwa kuwezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na hivyo kuondokana na changamoto walizokuwa nazo awali.

Hayo yalisemwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) Mhandisi Rashid Shaban wakati wamekabidhi mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Maji Taka wilayani Muheza pamoja na kukabidhi Vyoo vilivyojengwa ikiwa ni sehemu ya Ujenzi wa Mradi huo kwa shule ya Sekondari Bonde,Shule ya Msingi Mdote na Soko la Majengo wilayani Muheza.

Mhandidi Shaban alisema pamoja na hilo pia ipo miradi 6 ya maji taka yenye thamani ya Bilioni 4.2 ukiwemo wa ujenzi wa miundombinu ya kupokea na kuchakata majitaka wenye thamani ya Bilioni 1 ambao umetekelezwa na hivyo kusaidia kuondosha kero ambayo ilikuwa ikiwkumba wananchi.

Alisema kutokana na uwezeshwaji huo kwa sasa mamlaka hiyo inatoa huduma ya maji safi na salama kwa wastani wa asilimia 92.5 ya wakazi wa Jiji la Tang (96.1%), Pangani (70%) na Muheza (71%) ambapo miaka mitatu iliyopita kabla ya utawala wa Serikali ya awamu ya sita huduma ya maji ilikuwa inapatikana kwa wastani wa asilimia 83.2 ya wakazi hao (Tanga 89%, Muheza 33% na Pangani 60%).

Aidha alisema hivi sasa maji safi yanapatikana kwa wastani wa saa 15 kwa siku katika miji ya Muheza ambapo miaka mitatu iliyopita huduma ya maji ilikuwa inapatikana kwa wastani wa masaa matatu na wakati mwengine siku moja baada ya Juma Zima.

Akizungumzia huduma ya uondoshaji wa maji Taka, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema huduma hiyo hufanywa kupitia mtandao wa mabomba unaowahudumia wakazi wapatao 20,615 sawa na asilimia 5.2 ya wakazi Tanga Mjini, Maeneo ya Muheza, Pangani na maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Tanga ambayo hufanywa kwa kutumia mifumo mingine ya uondoshaji majitaka ikiwemo vyoo vya shimo na vyoo vya kunyonywa na magari vikishajaa.

Hata hivyo akielezea ujenzi wa vyoo na ombi la kukabidhi kwa watumiaji ,Mhandisi Rashid alisema kwamba kwa kua mradi huo unahusiana na usafi wa mazingira,Tanga Uwasa iliona ijenge aina hiyo ya vyoo ili kuonesha mfano wa vyoo bora vinavyotakiwa kujengwa katika jamii ikiwemo faida ambazo zinapatikana kupitia mradi huo.

Alisema faida ni kuwaepusha uchafuzi wa maji ya ardhini, uwepo wa huduma karibu na wananchi kupitia gari la kunyonya majitaka toka na hivyo kuondoa changamoto ya utupaji mbali na wakati mwengine katika maeneo yasiyorasmi.

“Pia kupungumza changamoto ya ufinyu wa vyoo katika shule za Msingi Mdot,Shule ya Sekondari Bonde na Soko la Majengo ambapo gharamaa nafuu kwani kutumia eneo dogo la ardhi na hudumu muda mrefu pia upatikanaji wa mbolea inayoweza kutumika kwa kilimo lakini tunaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kuwezesha ujenzi wa mradi huu”Alisema

“Sisi Tanga Uwasa tumeona ujenzi wa vyoo umekamilika na vipo tayari kutumika tunadhani hakuna haja ya kuendelea kusubiri hadi ujenzi wa miundombinu pale Kilapula ukamilike ikiwa wanafunzi na wananchi sokoni wanauhitaji mkubwa hivyo tunakuomba ukabidhi vyoo hivi kwa uongozi wa shule ya Sekondari Bonde, Shule ya Msingi Mdote na Soko la Majengo vianze kutumika na hivyo kusaidi kupunguza changamoto iliyopo ya uhitaji wa matundu ya vyoo”Alisema

Awali akizungumza mara baada ya kupokea mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Maji Taka wilayani Muheza pamoja na kukabidhi Vyoo vilivyojengwa ikiwa ni sehemu ya Ujenzi wa Mradi huo kwa shule ya Sekondari Bonde, Shule ya Msingi Mdote na Soko la Majengo wilayani Muheza, Mkuu wa wilaya ya Muheza ZainabuAbdallah alisema miaka mitatu ya nyuma hali ya upatikanaji wa maji ilikuwa ni asilimia 33 lakini miaka mitatu sasa hivi himefikia 71 hiyo ni kazi kubwa anayoifanya Rais Dkt Samia Suluhu.

Katika miaka mitatu ya Rais Dkt Samia wamefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya kikamkati 20 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 161.4 ya Maji Safi na Maji Taka miradi sita yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 4.2 ambapo hiyo ni kazi kubwa na nzuri inayofanya na Rais Samia.

Alisema wamefika katika hafla hiyo kuungana na Tanga Uwasa katika tukio hilo huku akimpongeza Waziri wa Maji Jumaa Aweso kutokana na kazi kubwa anayofanya kuhakikisha huduma ya maji kwenye mkoa wa Tanga inakuwa nzuri na Muheza wanatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya maji taka wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 1 ambapo kwenye mradi ho wamepata gari la maji taka, gari ya usimamizi wa mradi na wamepata matundu ya vyoo,shule ya sekondari na Msingi pamoja na Soko .

MWisho


MAKAMU WA RAIS AKIWASILI ZAMBIA KUSHIRIKI MKUTANO WA SADC

MAKAMU WA RAIS AKIWASILI ZAMBIA KUSHIRIKI MKUTANO WA SADC

March 22, 2024

 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda, Lusaka nchini Zambia tarehe 22 Machi 2024. Makamu wa Rais anatarajia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Ushirikiano katika Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC Organ Troika) pamoja na Nchi zinazochangia vikosi katika jeshi la utayari la SADC lililopo nchini Msumbiji (SAMIM) na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SAMIDRC).


JESHI LA POLISI TANGA LAWAFIKISHA MAHAKAMANI WATUHUMIWA 35 KWA MAKOSA MBALIMBALI

March 22, 2024

 




Na Oscar Assenga, TANGA

JESHI la Polisi Mkoani Tanga katika kuhakikisha wanaendelea kudhibiti uhalifu wamefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa (35) ambapo wamehukumiwa vifungo mbalimbali.

Akizungumza leo na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi alisema watuhumiwa hao waliofikishwa mahakamani na kuhukumiwa vifungo mbalimbali ni.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni wa makosa ya kubaka, ulawiti, wizi na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani ambapo watuhumiwa 20 walipatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo gerezani.

Kamanda Mchunguzi aliwataka waliohukumiwa vifungo vya maisha Jela ni Deogratius Alex (22), Samwel Ghamuga (25) wote kwa kosa la kubaka na Athumani Rajabu (19) akihukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kulawiti huku Anthony Agunstino na Twaha Rajabu wakihukumiwa miaka (30) jela kwa kosa la kubaka.

Aidha aliwataja watuhumiwa wengine ambao ni Omari Mganga na Hussein Amiry (41) wamehukumiwa kifungo cha miaka nane jela kwa kosa la wizi pamoja ana Salim Jumbe ambaye amehukumiwa miaka 27 jela kwa kosa la kubaka.

Akizungumzia kwa upande wa makosa ya usalama barabarani madereva wawili wameondolewa madaraja kwenye leseni zao za udereva na 1 amefungiwa leseni ya udereva ambapo wengine wamelipa faini mahakamani kwa makosa ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

Hata hivyo Kamanda Mchunguzi alisema ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia mwezi February 21 hadi Machi 21 Jeshi hilo katika Operesheni ya kuimarisha doria na misako wamefanikiwa kukamata watuhumiwa 94 wakiwa na makosa mbalimbali ikiwemo makosa ya uvunjaji,mauaji,kujeruhi,kusafirisha wahamiaji haramu,kuharibu mali pamoja na kupatikana na silaha sita aina aya Gobole.

 

RAIS SAMIA AZIDI KUUFUNGUA MKOA WA SIMIYU KWENYE MIRADI YA BARABARA NA MADARAJA

March 22, 2024

 Serikali kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) imeendelea kuufungua Mkoa wa Simiyu kwa kutekeleza zaidi ya miradi mikubwa mitano ya Kitaifa ya ujenzi wa Miundombinu ya Barabara na madaraja


Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Simiyu, Mha. Boniface Mkumbo ameyasema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi.

Amesema Serikali kupitia TANROADS imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa awamu ya tatu ya kipande cha barabara ya Bariadi-Maswa yenye urefu wa Km 49.7 pamoja na Barabara ya mchepuo ya Maswa ( Maswa Bypass) sehemu ya Lamadi-Bariadi-Maswa - Wigelekelo hadi Mwigumbi upande wa Shinyanga na Daraja la Malampaka lenye mita 12.5.

Amesema miradi mingine ambayo ipo kwenye utekelezaji wa kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami ni pamoja na Barabara ya Bariadi - Salama - Gh’aya- Magu (Km 76) ambayo itaunganisha mkoa wa Simiyu na Mwanza, Barabara ya Nyashimo - Ngasamo - Ndutwa (km 48), na mradi mkubwa wa ujenzi wa Barabara ya Karatu-Mbutu - Hydom - Mto Sibiti - Meatu - Lalago - Maswa yenye Jumla ya kilometa 339.

Amesema madaraja zaidia 20 yamejengwa katika mtandao wa barabara kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5.6 na Ujenzi wa Daraja kubwa la Itembe lenye urefu wa mita 150 unaendelea ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75 ambalo linaunganisha Mkoa wa Singida, Mikoa mingine ya Kanda ya kati na kanda ya kaskazini.

Amesema katika kipindi cha miaka 3 cha Serikali ya awamu ya sita zaidi ya taa 569 za barabarani zimefungwa kwenye miji na Vijiji vikubwa ili kuwafanya wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii hata giza linapoingia.

Pia, ameishukuru Serikali kwa kuweza kuwajali Wakandarasi Wazawa ambapo Mkoa wa Simiyu ni Moja kati ya Mikoa ambayo kazi nyingi wamepewa Wakandarasi wa ndani na kuwapa Kipaumbele Wanawake ili kuweza kuwawezasha kupewa upendeleo ili kuwakuza kiuchumi.

Mha. Mkumbo ametoa wito kwa Wananchi kutunza Miundombinu ya Barabara kwani Serikali inatumia fedha kuhakikisha wananchi wanapita kwenye Miumbombinu iliyo na viwango vinavyokubalika.

Naye, Msimamizi wa idara ya Matengenezo TANROADS Simiyu, Mha. Amiri kwiro ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kutenga fedha za matengenezo mkoa humo ambazo pia kwa kiasi kikubwa zimesaidia kuepuka madhara ya mvua za Elnino zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali Nchini.







WADAU MSD KANDA YA MTWARA WAHIMIZWA KUSIMAMIA MATUMIZI SAHIHI YA TAKWIMU KATIKA BIDHAA ZA AFYA

March 22, 2024

 WADAU  wa afya wa Bohari ya Dawa(MSD) Mtwara wamehimizwa kusimamia matumizi sahihi ya takwimu za mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, ili ziwawezeshe kufanya maamuzi sahihi kuhusu bidhaa hizo katika maeneo yao.

Akifungua kikao cha wadau na wateja wa MSD kanda ya Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Masasi Lauteri Kanoni amesema uwepo wa takwimu sahihi unaiwezesha MSD kuagiza kwa usahihi bidhaa za afya na kuboresha upatikanaji wa bidhaa hizo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya. 

Amewashauri MSD kuhakikisha utaratibu wa vikao  vya mwaka vya wadau ni muhimu kwa pande zote mbili, yaani Bohari ya Dawa (MSD) yenyewe na wadau ili kwa pamoja kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya, kwa kujadili changamoto na kuzitafutia utatuzi.

Kwa upande wake Meneja Kanda ya Mtwara Tea Malay ameeleza kwa sasa Kanda ya MSD Mtwara inahudumia vituo vya kutolea huduma za afya 631, na inasambaza bidhaa za afya kila baada miezi miwili.

Awali Meneja Huduma kwa Wateja na Miradi Dkt. Pamella Sawa ameeleza kuwa vikao vya MSD na wadau wake kuanzia sasa vitakuwa endelevu kila mwaka.

Amefafanua kwamba MSD Kanda ya Mtwara inahudumia mikoa ya Lindi,Mtwara na Wilaya ya Tunduru.

Wakati huo huo, Halmashauri ya Mji wa Masasi,mkoani Mtwara wameitambua Kanda ya MSD Mtwara kwa kuboresha huduma za afya, hasa katika jukumu la msingi la kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya umeimarika katika halmashauri hiyo.

Tuzo hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Masasi Dkt.Salum Gembe kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi.




TRA YAPELEKA ELIMU YA MLANGO KWA MLANGO KWA MLIPA KODI SHINYANGA

March 22, 2024

 Timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wamefunga kambi katika mkoa wa Shinyanga lengo likiwa ni kutoa Elimu ya mlango kwa mlango kwa wafanyabiashara wa mkoani hapo mjini pamoja na vijijini.


Zoezi hilo linaenda sambamba na ukusanyaji wa maoni na changamoto na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara hao kwa lengo kwenda kuyafanyia kazi kwa lengo la kuboresha zaidi na hatimae kurahisisha ulipaji kodi kwa hiyari.

Miongoni mwa changamoto zilizoripotiwa ni pamoja na umbali wa upatikani wa huduma, ambapo wafanyabiashara wanapotaka huduma za TRA wanalazimika kusafiri kwa masafa marefu kufuata huduma hiyo jambo linalowaongezea gharama wanazotumia katika usfari na muda mwingi.

Aidha, baadhi ya wafanyabiashara wamefurahishwa na zoezi hilo ambalo limewasaidia kufamahu mambo mbali mbali ya kodi na kushauri zoezi hilo liwe endelevu ili waendelee kujifunza zaidi.





REA NA TANESCO KUTUMIA BILIONI 48 KUUFIKISHA UMEME KWENYE NYUMBA 5,000 ZA KIJIJI CHA MSOMERA, SAUNYI NA KITWAI B MKOANI TANGA

March 22, 2024

 Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Tarehe 21 Machi, 2024 wameingia kwenye ubia ili kuanza utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa kusambaza umeme kwenye nyumba 5,000 katika kijji cha Msomera, Saunyi na Kitwai B, wilayani Handeni, mkoani Tanga ambapo Mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 48.


Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema, Mradi huo utakuwa endelevu na kuongeza kuwa licha kuwafikishia Wananchi huduma ya umeme katika vijiji hivyo lakini pia utawaunganisha Wananchi na huduma ya umeme (Wiring) moja kwa moja kwenye nyumba zao bila ya wao kulipia huduma hiyo.

“Nyumba 5,000 zitasambaziwa umeme pamoja na kufanyiwa “wiring”. Lengo la Serikali ni kuhakikisha Wananchi katika vijiji hivyo, mnapata umeme lakini pia mnaishi vizuri na kufanya shughuli zenu za kiuchumi”. Amesema Naibu Waziri Kapinga.

Naibu Waziri Kapinga amewaambia, wakandarasi wanaotekeleza Mradi huo kuongeza kasi katika kazi hyo pamoja na kutanguliza weledi (Professionalism) katika majukumu yao.

“Tekelezeni Mradi huu kwa wakati ili Wananchi wapate umeme kwa wakati, tunawategemea mfanye kazi kwa weledi, (Sisi) Viongozi wa Wizara ya Nishati, tupo pamoja nanyi ili kuhakikisha Miradi hii yote, inakamilika kwa wakati”. Amekaririwa Naibu Waziri, Kapinga.

Mradi huo mkubwa utatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia mkandarasi, kampuni ya China Railways Construction and Electrification Bureau Group Company Ltd (CRCEBG) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia kampuni yake tanzu ya ETDCO.

Katika mkabata huo, kampuni ya CRCEBG itajenga miundombinu ya umeme katika maeneo ya Mradi wa ujenzi wa nyumba 5,000 kwa shilingi bilioni 14.2 ambapo, mkandarasi huyo atajenga umeme wa msongo wa kati wenye urefu wa kilomita 281 pamoja na kufunga mashine umba (Transformer) 190.

Kwa upande wa kampuni ya ETDCO, nayo itajenga miundombinu ya katika maeneo yaliyobaki ya Mradi huo pamoja na kuwaunganishia Wananchi na huduma ya umeme (Wiring) kwa nyumba hizo 5,000 kwa gharama ya shilingi bilioni 33.8 na kufanya jumla ya shilingi bilioni 48 kwa Mradi wote.

Katika taarifa yake ya awali kwenye hafla hiyo; Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, kutoka REA, Mhandisi, Jones Olotu amesema katika kijiji cha Msomera, REA imekuwa ikitekeleza Mradi wa REA III (Mzunguko wa Pili) ambapo kupitia mkandarasi huyo huyo, kampuni ya CRCEBG, imejenga miundombinu ya umeme wa msongo wa kati wa kilomita 49.4, msongo mdogo wa kilomita 146 pamoja na kuunganisha Wateja wa awali 557 ambapo jumla ya shilingi bilioni 3.7 zimetumika kugharamia Mradi huo na kuongeza kuwa Mradi utakamilika, Tarehe 31 Machi, 2024.

“Mkandarasi anaendelea kuunganisha umeme kwenye nyumba 375 ambazo hapo awali hazikuunganishwa (Wiring), mpaka sasa amejenga “line” ya umeme ya msongo mdogo ili kuunganisha nyumba 340 kati ya nyumba 375”.

“Mkandarasi, anataraji kukamilisha kazi ya kuunganisha umeme kwenye nyumba zote 375 mwezi Machi, 2024”. Amesema, Mhandisi, Olotu.

Nao wananchi wa kijiji cha Msomera wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuwafikishia huduma ya umeme, wakiongea katika nyakati tofauti, wamesema kuhamishwa kutoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kumewafungulia fursa ya kuanza maisha mapya na mazuri tofauti na hapo kabla.

“Naishukuru Serikali kwa kutuhamisha kutoka Ngorongoro na kuja hapa Msomera, hapa Mimi na familia yangu, tunatumia umeme kwa matumizi, tofauti na nilipokuwa Ngorongoro, kule nilikuwa natumia vibatali, kwenye eneo la hifadhi hauruhusiwi kutumia umeme, ila hapa natumia umeme nyakati za usiku, natumia umeme kupata taarifa kwa njia ya televisheni”. Amesema Mama, Veronica Mathulda, mkazi wa kijiji cha Msomera.

Naye Bwana Yamati Masinde amesema umeme kwenye kijiji cha Msomera ni fursa kwake na kuahidi kuutimia kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

“Ngorongoro tulikuwa hatuwashi umeme, hata umeme wa kutumia mionzi ya jua (Solar), nilikuwa siruhusiwi, kule hatukuwa na fursa ya umeme kabisa ila hapa, tuna umeme, nitautumia umeme kwa ajili ya maendeleo yangu”. Amesema Bwana Masinde.