JUMIA TRAVEL YATOA TUZO KWA HOTELI ZINAZOFANYA VIZURI NCHINI TANZANIA

November 18, 2016
 Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee (kushoto), akielezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na kampuni hiyo.
 Hafla ikiendelea.
 Wadau wakiwa kwenye hafla hiyo.
 Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee (kulia), akimkabidhi tuzo Flora Rwehumbiza katika hafla hiyo.
Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee akimkabidhi tuzo ya  Ushirikiano Mkubwa mwaka 2016 kwa Meneja wa Huduma za Hoteli ya Amaan Bungalows, Daudi Fundi (kushoto). Hafla ya sherehe hizo zilifanyika jana katika ukumbi wa Mayfair jijini Dar es Salaam.
 Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee (kulia) akikabidhi tuzo ya Mshirika Bora Katika Biashara mwaka 2016 kwa Mtendaji wa Mauzo wa Hoteli ya Serena ya jijini Dar es Salaam,  Emma Sizya. 

Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee (kushoto), akizungumza na wanahabari.




Na Dotto Mwaibale

MTANDAO unaoongoza kwa huduma za hoteli kwa njia ya mtandao barani Afrika wa Jumia Travel umetoa tuzo kwa hoteli na washirika wake wakati wa hafla fupi iliyofanyika siku ya Alhamisi katika ukumbi wa hoteli ya Mayfair jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa sherehe za utoaji wa tuzo hizo zilizofanyika Dar es Salaa jana, Meneja Mkaazi wa Jumia Travel Tanzania Fatema Dharsee alibainisha kuwa tuzo hizo zimelenga kuleta chachu katika matumizi ya huduma za hoteli mtandaoni nchini na kupanua wigo wa huduma kwa wateja.

“Leo hii tumejumuika hapa kuzitambua na kuzitunuku hoteli zinazotoa huduma nzuri pamoja na kupendwa na wateja wa ndani na nje ya nchi. Mbali na sababu hizo lakini kikubwa zaidi ni kwa hoteli hizi kuendana na mabadiliko ya teknolojia kupitia mtandao wa intaneti ambao unawezesha huduma zao kufikiwa na mtu yeyote duniani,” alisema Dharsee.

“Hoteli zote zilizojiunga au kujumuishwa kwenye mtandao wetu wa ‘Extranet’ zinazo fursa kubwa za kuongeza ufanisi na thamani ya biashara yao kwani hazitegemei tena wateja wanaokwenda moja kwa moja kutafuta huduma kwenye meza zao za maulizo. Kupitia mtandao wetu ambao unapatikana kwenye kompyuta, tabiti na simu, unamwezesha meneja wa hoteli au mapokezi mahali popote walipo mbali na vituo vyao vya kazi kupokea maombi ya wateja kisha kuthibitisha au kubatilisha upatikanaji wa huduma husika,” aliongezea Dharsee

Aliendelea mbele kwa kufafanua zaidi kuwa vipengele vya tuzo za Jumia Travel Tanzania vilivyokuwa vikiwaniwa ni pamoja na:

Chaguo la Wasafiri – hii ilitolewa kutokana na maoni ya wateja au wageni wengi walioitembelea; Hoteli Iliyoonesha Ushirikiano Mkubwa – hii ilitolewa kwa kigezo cha kuthamini mchango na ushirikiano wake; Hoteli Bora Inayochipukia – hii ilitolewa kutokana na juhudi na jitihada zilizooneshwa katika sekta nzima kwa ujumla; Hoteli Iliyopokea Maombi Zaidi Kutoka Kwa Wateja – hii ilitolewa kwa mujibu wa kuwa na maombi mengi kutoka kwa wateja; na Mshirika Bora Katika Biashara – hii ilitolewa kwa kutuunga mkono na mchango mkubwa katika biashara.

“Ningependa kutoa shukrani za dhati kwa hoteli zote zilizokubali wito na kuhudhuria hafla hii. Uwepo wenu hapa jioni ya leo unaonyesha kutuamini na kuunga mkono jitihada za kuinua sekta ya utalii na ukarimu nchini hususani kuhamasisha kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani,” alihitimisha Meneja Mkaazi huyo wa Jumia Travel nchini Tanzania.

Katika hafla hiyo hoteli zilizojinyakulia tuzo hizo ni pamoja na Serena ambayo ilitunukiwa tuzo ya Mshirika Bora Katika Biashara; Tanzanite Executive Suites ilitunukiwa tuzo ya Chaguo Bora la Wasafiri; Amaan Bungalows ilitunukiwa tuzo ya Hoteli Iliyoonesha Ushirikiano Mkubwa; Harbour View Suites ilitunukiwa tuzo ya Hoteli Iliyopokea Maombi Zaidi Kutoka Kwa Wateja; na Slipway ambayo yenyewe ilitunukiwa tuzo ya Hoteli Bora Inayochipukia.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo Mtendaji wa Mauzo kutoka Hoteli ya Serena ya jijini Dar es Salaam Emma Sizya amesema kuwa amefarijika kupokea tuzo hiyo na kuipongeza kampuni ya Jumia Travel Tanzania kwa kuja na kitu hiki cha kipekee.

“Kwanza ningependa kuipongeza Jumia Travel Tanzania kwa kuja ni hizi tuzo ambazo ninaamini kuwa zitaleta mchango mkubwa katika kuhamasisha sekta ya hoteli nchini. Tumekuwa tukiona sekta mbalimbali zikiwa na tuzo zao lakini yetu ikiwa imelala kidogo, huu ni mwanzo mzuri na ninaamini waandaaji hawataishia hapa,” alisema na kumalizia Sizya kwamba, “Serena siku zote tunajivunia kuwa mbele katika kuunga mkono jitihada za wadau mbalimbali wanaofanya kazi na sisi. Lengo letu kubwa ni kuona kuwa kwa pamoja tunashirikiana katika kuwashawishi wateja kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ambapo sasa hivi kupitia kampuni kama hii unaweza kupata huduma zetu mtandaoni.”


Hafla hiyo imeambatana na kuadhimisha miaka mitatu tangu Jumia Travel kuanzishwa pamoja na kampeni maarufu ya mauzo inayoendelea kwa jina la ‘Black Friday’ ambayo  imeanza Novemba 14 mpaka Novemba 25, 2016. Matarajio ya kampuni kwa wiki hizi mbili za mbili ni makubwa ambapo imelenga kuwapatia wateja fursa ya kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma za awali kwa ajili ya msimu wa sikukuu kwa gharama nafuu. 

ENDELEENI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI – MAJALIWA

ENDELEENI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI – MAJALIWA

November 18, 2016
majaliwa1
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Kichangani, Magomeni jijini Dar es salaam Novemba 18, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
majaliwa2
………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Waislamu nchini waendelee kushirikiana na Serikali kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.
Aidha, amewasihi waislam kuimarisha umoja ,upendo ,mshimano miongoni mwao kwa kushirikiana na jamii zinazowazunguka bila kujali tofauti zao za kiimani.
Ametoa wito huo leo mchana (Ijumaa, Novemba 18, 2016) wakati akishiriki sala ya Ijumaa katika msikiti wa Kichangani, Magomeni jijini Dar es Salaam.
Amesema uwepo wa dini umewezesha nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu hivyo kila mmoja ahakikishe suala hilo linaendelezwa.
Pia amewashauri waumini na viongozi wa dini kuzingatia maadili ya dini ili kuepusha migongano isiyo ya lazima hasa taasisi zinapokuwa na miradi.
Waziri Mkuu alitolea mfano msikiti huo wa Kichangani chini ya Sheikh  Walid umeweza kusuluhisha hitilafu wenyewe bila kukimbilia Serikalini au mahakamani kusuluhishwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Waislamu wana jukumu la kuwafunza elimu ya dini watoto wao na kuhakikisha wanakua kwenye imani na kujengeka katika maadili mema.
Amesema dini inajenga maadili mema kwa mtoto na kumwezesha kukua katika misingi ya uvumilivu na inamuwezesha kumtambua Mwenyezi Mungu.
“Nimefarijika kuona vijana wengi wameshiriki katika sala hii ya Ijumaa. Nawaomba wazazi waendelee kuelimisha watoto umuhimu wa kufanya ibada,” amesema.
“Tuendelee kuwafundisha vijana wetu umuhimu wa kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kidini ili wakikua waweze kuiendeleza kwa vizazi vijavyo,” amesema.
Waziri Mkuu amewaomba waumini hao waendelee kuwaombea viongozi wa kitaifa ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao na kufikia malengo yanayotarajiwa na wananchi.

TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF

November 18, 2016


YAHYA HAMAD KAIMU MWENYEKITI KAMATI YA SAA 72 YA TFF 

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kunashukuru wanafamilia wa soka kwa salamu mbalimbali za rambirambi kutokana na msiba wa Mwenyekiti wa Azam FC na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu, Sheikh Said Muhammad aliyefariki dunia Novemba 7, 2016 katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Hayati Sheikh Said Muhammad kualikuwa hazina katika mpira wa miguu nchini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutoa mchango ya mawazo na miongozo katika Kamati ya Utendaji ya TFF. 

Itakumbukwa kwamba Sheikh Muhammad aliongoza Klabu ya Azam kwa mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ianzishwe.

Kutokana na kufariki kwa Sheikh Muhammed, Rais wa TFF, Jamal Malinzi amempendekeza Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Bwana Yahya Hamad - kukaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji Ligi (Kamati ya Saa 72) ili kushughulia masuala yote ya mechi zilizochezwa tangu mwanzo wa Novemba, 2016 baada ya kifo cha Sheikh Muhammad.

Tunachukua nafasi hii kutoa wito kwa klabu kumpa ushirikiano Bwana Hamad katika majukumu yake mapya akiongoza kamati hiyo yenye wajumbe ambao ni Baruan Muhuza (Azam Tv), Boniface Wambura (Mtendaji Mkuu Bodi ya Ligi), Jonas Kiwia (Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano TFF), Philemon Ntahilaja (Mdau wa Mpira wa Miguu), Charles Ndagala (Katibu Kamati ya Waamuzi ya TFF), Kanali Mstaafu wa JWTZ, Isaron Chacha na Steven Mnguto ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya ligi. 


KUMEKUCHA AZAM SPORTS FEDERATION CUP

Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayoshirikisha timu 86 msimu huu, itaanza rasmi kesho Novemba 19, 2016 kwa uzinduzi rasmi utakaofanyika mkoani Tanga kwa kuzikutanisha Bingwa wa Mkoa wa Tanga, Muheza United na Sifa Politan ya Temeke, Dar es Salaam kwenye  Uwanja wa Mkwakwani jijini humo.

Siku hiyo kabla ya mchezo kutakuwa na shamrashamra kupamba michuano hiyo ambako wachezaji wa zamani wa Coastal Union na African Sports za Tanga zitachuana kabla ya kuanza kwa mchezo huo wa uzinduzi. Timu hizo za maveterani, zitachezwa kuanzia saa 8.00 mchana.

Pia kutakuwa na shamrashamra za wasanii walioandaliwa na Wadhamini Azam Tv ambayo kwa msimu wa 2016/17 zimeongezwa timu 22 kutoka mabingwa wa mikoa-- Muheza na Sifa Politan ni miongoni mwa timu hizo. Ongezeko hilo tofauti na msimu uliopita ambako kulikuwa na timu 64.

Mwaka huu kuna timu 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL); timu zote 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), timu zote 24 za Daraja la Pili (SDL) na timu 22 za mabingwa wa mikoa. Mashindano hayo yatakuwa ni ya mtoani na yataendeshwa kwa raundi tisa (9).

Raundi ya Kwanza itashirikisha timu zote 22 za Mabingwa wa Mikoa katika makundi manne ya timu sita na timu tano ambako timu mbili za juu zitaingia raundi ya pili.Raundi ya Pili itashirikisha timu nane zilizofuzu za RCL katika raundi ya kwanza na kujumlisha timu 24 za Daraja la Pili (SDL) kufanya jumla ya timu zote kuwa 32 kwa hatua ya pili.

Raundi ya Tatu itashirikisha timu 16 zilizofuzu hatua ya pili kushindana ili kupata timu nane zitakazoingia hatua ya nne.Raundi ya Nne itashirikisha timu zote za Daraja la Kwanza (24) na kumulisha timu nane (8) zilizoshinda Raundi ya Tatu (3) kufanya timu zote kuwa 32.

Raundi ya Tano, itashirikisha timu 16 zilizofuzu Raundi ya Nne (4) na kumuisha timu zote 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kufanya timu zote katika raundi hii kuwa 32.Raundi ya Sita itashirikisha timu zote 16 zilizofuzu katika Raundi ya Tano na mzunguko huo utaitwa Hatua ya 16 Bora.

Raundi ya Saba (7) itashirikisha timu nane zilizofuzu katika raundi ya sita na mzunguko huo kutambuliwa kuwa Nane Bora au Hatua ya Robo fainali .Raundi ya Nane ambayo itashirikisha timu nne zilizofuzu Raundi ya Saba (Robo Fainali) na mzunguko huo utatambuliwa kuwa ni Nusu Fainali.

Raundi ya Tisa itashirikisha timu mbili zilizofuzu Raundi ya Nane na washindi hao wa Nusu Fainali na kumpata Bingwa wa Azam Sport Federation Cup kwa msimu wa 2016/2017.

………………..…………………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

MAJALIWA ATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA NYUMBA MAGOMENI KOTA

November 18, 2016

  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mshauri wa Wakala ya Majengo Tanzania (TBA), Edwin Nnuduma  kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Nyumba, Magomeni Kota jijini Dar es salaam wakati alipotembelea mradi huo Novemba 18, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mshauri wa Wakala ya Majengo Tanzania (TBA), Edwin Nnuduma  kuhusu Mradi wa Ujenzi wa Nyumba, Magomeni Kota jijini Dar es salaam wakati alipotembelea mradi huo Novemba 18, 2016. Wapili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally  Happy.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokagua Mradi wa Ujenzi wa Nyumba, Magomeni Kota jijini Dar es salaam Novemba 18, 2016.  Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Happy. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wajenzi wakati alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Nyumba, Magomeni Kota jijini Dar es salaam kukagua mendeleo ya mradi huo Novemba 18, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

TANZANIA KUENDELEA KUSIMAMIA HISTORIA YA UKOMBOZI WA BARA LA AFRIKA

November 18, 2016


Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye (kulia) akieleza jambo kwa Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa   Afrika ya Kusini Ndg. Nathi Mthehwa(kushoto) ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi kwa siku tatu yenye lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo kupitia Sanaa na Utamaduni ikiwemo kuhifadhi historia ya ukombozi wa Afrika ya Kusini leo Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Prof.Elisante Ole Gabriel (kulia) akisalimiana na Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Afrika ya Kusini Ndg.Nathi Mthehwa (Kushoto) leo Jijini Dar es Salaam alipotembelea Wizara hiyo kwa ajili ya mazungumzo ya kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo katika sekta za Sanaa na Utamaduni, katikati ni Balozi wa Afrika ya Kusini Nchini  Thamsanga Dennis Mseleku.
Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye  akiongea na waandishi wa habari (hawapo katika Picha) leo Jijini Dar es Salaam kuhusu ziara ya Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa Afrika ya Kusini Ndg. Nathi Mthehwa  ambaye yupo nchini kwa siku tatu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo kupitia sekta ya Sanaa na Utamaduni ikiwemo kuhifadhi historia ya ukombozi wa Afrika ya Kusini.
Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa   Afrika ya Kusini Ndg. Nathi Mthehwa (kulia) akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ziara yake ya siku tatu nchini leo Jijini Dar es Salaam (kushoto) ni Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye . 
Mshauri Mtaalamu wa Urithi wa Utamaduni Dkt.Daniel Ndagala akichangia hoja  wakati wa kikao baina ya Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye na Waziri wa Sanaa na Utamaduni wa   Afrika ya Kusini Ndg. Nathi Mthehwa leo Jijini Dar es Salaam.

RAIS MAGUFULI AMTEUA DIWANI ATHUMAN KUWA RAS KAGERA, PIA AMETEUA WENYEVITI WA BODI KATIKA TAASISI ZA SERIKALI AKIWEMO JAJI WARIOBA.

November 18, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 18 Novemba, 2016 amemteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Bw. Diwani Athuman kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.Uteuzi wa Bw. Diwani Athuman unaanza mara moja.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Wenyeviti wa Bodi katika taasisi tano za Serikali kama ifuatavyo.

Kwanza, Rais Magufuli amemteua Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jaji Joseph Sinde Warioba kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)

Uteuzi huu umeanza tarehe 16 Novemba, 2016.

Pili, Rais Magufuli amemteua Dkt. Jones A. Kilimbe kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na amemteua Bw. Sylvester M. Mabumba kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Uteuzi huu umeanza tarehe 17 Novemba, 2016

Tatu, Rais Magufuli amemteua Prof. Patrick Makungu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo (TEMDO).

Uteuzi huu umeanza tarehe 16 Novemba, 2016.

Nne, Rais Magufuli amemteua Bw. Martin Madekwe kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi.

Uteuzi huu umeanza tarehe 17 Novemba, 2016.

Tano, Rais Magufuli amemteua Prof. Raphael Tihelwa Chibunda kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kitropiki Tanzania (TPRI)

Uteuzi huu umeanza tarehe 17 Novemba, 2016.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

18 Novemba, 2016
MJUE MNYAMA TEMBO NA SIFA ZAKE

MJUE MNYAMA TEMBO NA SIFA ZAKE

November 18, 2016
index
Na Pamela Mollel,Mikumi
 
Tembo ni mnyama kubwa kuliko wote lakini sio mrefu kama twiga,kuna aina mbili ya tembo.tembo w a bara la Afrika na  bara la Asia
 
Ukitaka kujua tofauti zao wa bara la Afrika ni wakubwa ,na maskio yao yanamuonekano wa ramani ya bara la afrika lakini tembo bara la Asia wanamasikio madogo na pia wanaweza kufundishwa kulima na michezo mbalimbali
 
 Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mnyama huyo (Tembo)Afisa wa shirika la Tanapa katika hifadhi ya Mikumi Abdalla Choma alisema kuwa Tembo hao wa  wa bara la Afrika wapo katika makundi mawili,
1.      Tembo wa msituni wanameno ambayo  yamenyooka kwaajili ya kuwawezesha kupita katika msitu
2.       Tembo wa Savana, meno yao yamepindapinda wanapenda kuishi katika familia moja wanaweza kuishi kwanzia wawili hadi 45 kwa familia
Alisema Tembo wauwezo mkubwa wa kusikia na wanakumbukumbu ya kutosha
 
Akizungumzia kuhusu uzazi wa tembo mzee Chuma alisema kuwa tembo wanauwezo wa kubeba mimba na kuzaa kwa miezi 18-20
 
Tembo huyo hunyonyesha mtoto wake kwa takribani miaka miwili hadi mitatu na mtoto wa tembo huyo akishafikisha miaka 15 huhesabika ameshakuwa na kutakiwa kuondoka katika familia hiyo na kwenda kujitegemea
 
Tembo huishi kwa miaka 60-75 kwa sasa lakini miaka ya nyuma walikuwa na uwezo wa kuishi miaka 80-120 .
“Sababu za kuishi miaka michache kwa miaka hii ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi “alisema mzee Mchoma
 
CHAKULA CHA TEMBO
 
Anapenda kula matawi ya miti na nyasi za chini alafu anakula kwa maasaa 16 kati ya masaa 24
Kiasi cha chakula anachokula ni kati ya 150-300 kg kwa tembo mkubwa na hunywa maji kati ya lita 200 hadi 250

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA AMALIZA ZIARA YA SIKU 5 MKOANI MWANZA

November 18, 2016
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wananchi wa Nyamagana kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa machinjio ya Nyakato.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo ya ujenzi  wa machinjio ya Nyamagana kutoka kwa Mhandisi wa jiji la Mwanza Ndugu Ezekiel Kunyalanyala (kushoto) kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa machinjio ya Nyakato.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi la ufunguzi wa Jengo la Utawala Manispaa ya Ilemela .
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikikabidhi madawati kwa Mbunge wa Nyamagana Mhe. Stanslaus Mabula ambayo yalitolewa na Ofisi ya Bunge ambapo zaidi ya madawati 1074 yalikabidhiwa kwa wilaya ya Nyamagana na Ilemela.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipanda mti wa kumbukumbu mara baada ya kufungua jengo la Manispaa ya Ilemela. 
                                   .............................................................................................. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa muda wa mwezi Mwezi Moja kuanzia leo tarehe 18-Nov-2016 kwa watendaji na viongozi waandamizi wa wilaya ya Ilemela wahamie kwenye wilaya hiyo haraka iwezekanavyo na waache tabia ya kukaa kwenye wilaya nyingine kwa kisingizio cha kukosa nyumba za serikali.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo katika hotuba yake kwa wananachi na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela waliojitokeza katika hafla ya uzinduzi jengo la utawala la Manispaa hiyo na kukabidhi madawati 1,074 yaliyotolewa na ofisi ya Bunge.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha kukerwa na tabia hiyo na amewataka viongozi hao wahamie karibu na maeneo yao ya kazi kabla ya muda aliotoa kwisha ili waweze kuwa karibu na wananchi katika kuwasaidia kutatua kero na matatizo yanayowakabili kwa haraka.


Akiwa katika wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza wakati anaweka jiwe la msingi katika mradi wa ukarabati wa mchinjio ya Nyakato jijini Mwanza, Makamu wa Rais ameuagiza uongozi jiji la Mwanza kusimamia kikamilifu mradi wa ukarabati wa machinjio  ya Nyakato na watendaji watakaobainika kuhujumu mradi ambao utagharimu zaidi ya shilingi bilioni Tatu wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwa wananchi na watendaji wa jiji la Mwanza waliohudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ukarabati wa machinjio ya Nyakato unaohusisha uboreshaji wa jengo la machinjio,tanki la kuhifadhi maji,ujenzi wa vyumba vya baridi vya kuhifadhi nyama na ujenzi wa mtambo wa kutibu majitaka yanayotoka kwenye machinjio hiyo.


Makamu wa Rais katika hotuba yake, amesema hategemei hata kidogo ukarabati wa machinjio hiyo ufanyike chini ya kiwango kwa sababu ni mradi wa kibiashara ambao ukikamilika na kuanza kufanya kazi utasaidia jiji la Mwanza kupata mapato yatakayosaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Makamu wa Rais pia amemwagiza Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella ahakikishe anasimamia uundaji wa menejimenti ya machinjio hiyo ambayo itafanya kazi vizuri na sio kuingiza watu ambao hawana uwezo ambao watakwamisha utendaji kazi wa machinjio hiyo.


Kuhusu ukusanyaji wa kodi, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewahimiza watendaji wa Halmashauri zote za mkoa wa Mwanza waongeze kasi ya ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa njia ya kielekroniki kutoka kwenye vyanzo mbalimbali fedha ambazo zitasaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi mkoani humo.

Makamu wa Rais pia ametoa wito maalum kwa wananchi nchini wahakikishe wanadai risiti wanaponunua bidhaa mbalimbali kwani kufanya hiyo watasaidia kuongeza mapato yake ambao yataelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.


Katika Mkutano wake wa Majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya Siku Tano mkoani Mwanza na viongozi wa mkoa wa Mwanza, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewasisitiza viongozi na watendaji wa mkoa wa Mwanza wafanye kazi kwa bidii katika kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za umma.

Ameonya kuwa serikali ya awamu ya Tano haitasika kuwachukulia hatua kali viongozi na watendaji ambao watakwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma kwenye maeneo yao ya kazi.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa mkoa wa Mwanza kusimamia kikamilifu katika kulinda hali ya amani na Utulivu na wachukue hatua  kali kwa watu wanaotaka kuharibu  amani ya nchi.

Makamu wa Rais amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku Tano mkoani Mwanza kwa kukagua,kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya mbalimbali ya maendeleo katika wilaya za Ilemela,Misungwi, Kwimba, Magu na Nyamagana.

BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI
WAZIRI MKUU AWATAKA WAKAZI WA JIJI LA DAR KUANZISHA VIWANDA KWA KUTUMIA FULSA YA UMEME ULIOPO UMEME

WAZIRI MKUU AWATAKA WAKAZI WA JIJI LA DAR KUANZISHA VIWANDA KWA KUTUMIA FULSA YA UMEME ULIOPO UMEME

November 18, 2016
fuls1
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza kabla ya kuzindua Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Umeme jijini Dar es salaam kwenye Kituo cha TANESCO cha Mikocheni jijini Dar es salaam Novemba16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
fuls2
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo  akizungumza katika Uzindunduzi wa Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya umeme katika jiji la Dar es salaam uliofanywa na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa kwenye Kituo cha TANESCO cha Mikocheni jijini Dar es salaam Novemba 16, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
fuls3
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto kwake) wakitazama mfumo wa usambazaji umeme  kabla ya Waziri Mkuu kuzindua Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Umeme jijini Dar es salaam kwenye Kituo cha TANESCO cha Mikocheni jijini Dar es salaam Novemba 16, 2016.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam watumie fursa ya uwepo wa umeme wa uhakika kwa kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa ili waweze kujiongzea kipato.
Ametoa wito huo leo (Jumatano, Novemba 16, 2016) wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa uboreshaji miundombinu ya umeme jijini Dar es Salaam uliofanyika kwenye Ofisi za TANESCO zilizoko Mikocheni jijini humo.
Akizungumza kabla ya kubonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema: “Umeme ni mhimili mkubwa sana kwa maendeleo ya nchi yoyote ile. Tumepata umeme wa uhakika, tumieni fursa hii ya uwepo wa umeme wa uhakika kujiongezea kipato.”
“Hivi sasa tumepata umeme wa uhakika, fanyeni kazi kwa bidii ili mfaidi matunda ya kuwepo kwa umeme huo. Serikali inategemea kwamba sasa wananchi mtaanzisha na kukuza viwanda vidogo vidogo na vikubwa, biashara zitapanuka na kilimo bora huko vijijini kitaongezeka,” amesema.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa viwanda na moja ya nyenzo kuu ya kuendesha uchumi wa viwanda kwa tija na ufanisi ni upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika, na ndiyo maana kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha miundombinu ya  umeme inaboreshwa ili kuondoa tatizo la kukatika kwa umeme.
“Wataalam wamenieleza kuwa mradi huu ulihusisha ujenzi wa kituo kikubwa cha kupozea umeme cha MVA 100, ujenzi wa njia za usafirishaji umeme wa msongo wa kilovoti 132 katika maeneo mbalimbali ya Jiji kupitia chini ya ardhi, ujenzi wa njia za usambazaji umeme wa msongo wa kilovoti 33, pamoja na ujenzi wa ujenzi kituo cha udhibiti mifumo ya usambazaji umeme (Distribution SCADA System) katika msongo wa kilovoti 33 na 11.”
“Kukamilika kwa mradi huu kunaondoa adha zilizokuwepo awali kutokana na kukatika umeme mara kwa mara. Jiji la Dar es Salaam ni kitovu cha shughuli za biashara katika kuleta maendeleo ya Taifa ambapo upatikanaji wa umeme wa uhakika ni wa lazima,” ameongeza.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira iliyokuwepo, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amesema Wakala wa Jiolojia Tanzania kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia wa Finland wanaunda mpango wa pamoja wa kuibua madini ya kisasa ambayo yanatafutwa zaidi duniani kukidhi mahitaji ya kiteknolojia.
“Hivi sasa madini kama graphite na lithium yanahitajika zaidi kwenye teknolojia za kisasa kama za utengenezaji wa simu, tuachane na madini yaliyozoeleka kama vile dhahabu na Tanzanite,” alisisitiza.
Alitumia fursa kuuagiza uongozi wa TANESCO uhakikishe kuwa hakuna mgao wa umeme nchi nzima kwani Watanzania wamechoshwa na tabia ya kukatiwa umeme mara kwa mara. “Ili tujenge nchi ya viwanda, tunahitaji umeme wa uhakika, umeme unaotabirika na zaidi ya yote umeme wa bei nafuu,” alisema huku akishangiliwa.
Naye Waziri wa Biashara za Nje na Maendeleo wa Finland, Bw. Kai Mykkanen alisema Serikali yake imedhamini ujenzi wa mradi huo kwa vile inaamini kuwa umeme wa uhakika ni suluhisho la kuondoa umaskini kwa hiyo kukamilika kwa mradi huo kutaondoa adha ya kukatika umeme kila mara.
Aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika eneo la nishati ya umeme na nishati mbadala.
Katika hatua nyingine,  Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Eng. Felchesmi Mramba alisema ujenzi wa mradi huo umegahirimu sh. bilioni 74.6 ambapo kati ya hizo, sh. bilioni 63.56 zimetolewa na Serikali ya Finland na sh. bilioni 11.03 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kumewezesha sehemu kubwa ya Jiji la Dar es Salaam kuwa na njia za mzunguko (ring circuit) zinaoingizaa umeme. “Teknolojia hii iliyotumika itawezesha vituo vya kupozea umeme kuwa na njia mbadala ya kupata umeme endapo njia mojawapo inayopeleka umeme itapata hitilafu,” alisema.
Naye Meneja wa Kituo cha Kudhibiti Mifumo ya Usambazaji, Eng. Alex Kalanje alimweleza Waziri Mkuu kwamba kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kompyta, (distribution SCADA SYSTEM) kituo hicho cha udhibiti wa mifumo ya usambazaji umeme katika jiji la Dar es Salaam kitawasaidia watoa huduma wao waweze kufuatilia kwa haraka zaidi pale matatizo yanapotokea.
“Baada ya kukamilika kwa kituo hiki, lengo letu ni kujenga kituo kama hiki kwenye mjai ya Arusha, Mbeya, Dodoma na Mwanza,” alisema.