Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt Asha
Mahita akieleza mkakati wa kukabiliana na upungufu wa damu kwa wajumbe
Mratibu wa afya ya mama na mtoto Mkoa wa Tanga
Dorothy Lema akionesha hali ya vifo vya kina mama tangu mwaka 2010 -2013
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Pangani Dkt Dennis
Ngaromba akichangia mjadala jinsi ya kukabiliana na vifo vitokanavyo na uzazi .Habari
& picha na Fatna Mfalingundi- Afisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.
Madaktari Mkoani Tanga kwa
pamoja wameazimia kuchukua hatua za tahadhari ikiwemo kubuni njia mbadala zitakazowezesha kuokoa maisha ya mama na
mtoto pindi wanakapokumbana na vikwazo vya
dharura wakati wa mama kujifungua ili kufikia lengo la nne la dunia la kukabiliana na vifo vya uzazi,watoto
wachanga na walio chini ya umri wa miaka mitano.
Madaktari hao walifikia
hatua hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa kikao
cha pamoja cha Sekta ya Afya kilichofanyika Wilayani Lushoto na kuwajumuisha
ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa, Waganga Wakuu wa Wilaya ,Wenyeviti wa Bodi za Afya,
Wadau wa Sekta ya Afya wakiwemo MSD,NHIF,WHO,kfw,WEI na GIZ kwa lengo la
kujadili changamoto na mikakati ya kuboresha Sekta ya Afya kwa mwaka 2014/2015.
Akitoa maelezo kuhusu
kukabiliana na changamoto ya upungufu wa damu salama katika benki za damu ambayo
ilitajwa kuwa ni miongoni mwa sababu kubwa zinazopelekea vifo vingi vya
wajawazito, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga
Dkt Asha Mahita, alisema kuwa miongoni mwa mikakati waliyojiwekea ni pamoja na
kuifanya hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo kuwa kituo cha kusambaza damu kwa
hospitali za Wilaya badala ya kila wilaya kuomba na kusubiri damu kutoka hospitali ya rufaa ya
KCMC.
“Tumeshaiandikia Wizara kuiombea hospitali ya Mkoa ya Bombo
kuwa kituo cha kusambaza damu kwa Halmashauri zake, tunaamini kwa kufanya hivyo
tunaweza kupunguza tatizo la upungufu wa damu na vifo vya kinamama”.Alisema Dkt
Mahita.
Akichangia mjadala Mganga Mkuu wa Wilaya ya Pangani Dkt Dennis
Ngaromba, aliwashauri madaktari wenzake kuachana na rufaa za ghafla na kuwataka
kuwafuatilia wajawazito wanaowapatia
rufaa ya kwenda kujifungulia mahali kwingine kwa kuanzisha utaratibu wa kujaza
fomu tatu ambayo moja itabaki mahali alipofungulia kadi,nyingine itakwenda
alikopewa rufaa na nyingine kubaki katika ofisi za kijiji au mtaa ambapo
utaratibu huo utakwenda sambamba na mawasiliano ya simu lengo likiwa ni kutoa
historia ya Mjamzito ili hatua stahiki za haraka zichukuliwe.
“Pangani tumeweza kupunguza
vifo vya uzazi kwa kuachana na rufaa za fumanizi na tumeweka
utaratibu wa kuwatambua wanaofariki kutokana na uzazi kwa kuzishirikisha vyema
ofisi za Serikali za vijiji”.Aliongeza Dkt Ngaromba.