March 24, 2014

KATIBU MKUU OFISI YA MAKAMU WA RAIS, SAAZ SALULA, AKAGUA MIRADI YA HIFADHI YA ZIWA TANGANYIKA MKOANI RUKWA

Safari ya msafara wa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Ndugu Saaz Salula mwishoni mwa juma katika kukagua miradi inayofadhiliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira pamoja na wahisani wengine katika Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa haikuwa rahisi kutokana na kukabiliwa na changamoto ya barabara kutokana na mvua kubwa kunyesha na hivyo kupelekea magari ya mizigo inayokwenda nchi jirani za Burundi na DRC kupitia bandari ya kasanga kukwama na kuziba njia. Juhudi za ziada kwa kushirikiana na wananchi pamoja na mkandarasi anaejenga barabara hiyo ya Sumbawanga – Kasanga kwa kiwango cha lami zilisaidia katika kuhakikisha magari yote yaliyokwama pamoja na msafara wa katibu Mkuu yanavuka salama.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Ndugu Saaz Salula (watatu kulia) akiwa na msafara wake wakielekea kagua wadi ya kujifungulia kinamama kijiji cha Samazi Wilayani Kalambo ikiwa ni sehemu ya mradi unaosimamiwa na mradi wa hifadhi wa ziwa Tanganyika uliopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira pamoja na miradi mingine ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya msingi Muzi na ujenzi unaoelekea kukamilika wa daharia (bweni) katika shule ya sekondari Kasanga. Katika msafara wake aliambatana na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu Smythies Pangisa (wa nne kulia)
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Ndugu Saaz Salula akizungumza na mhudumu wa afya katika wadi ya wazazi Samazi juu ya huduma na mahitaji ya kituo hicho kipya ambacho kinategemewa kuanza kazi siku za hivi karibuni.

RAIS JK ASIMAMISHA ZIARA YAKE KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI HANDENI.

March 24, 2014
NA OSCAR ASSENGA,HANDENI.
RAIS Jakaya Kikwete jana alilazimika kusimama na kusikiliza kero za wananchi waliyobomolewa nyumba zao kupisha ujenzi wa barabara ya Mkata Handeni kwa kusimamisha msafara wake mara tano ili kujibu hoja za wananchi hao waliyotaka kujua hatma ya kuvunjwa kwa makazi yao.

Alikumbana na adha hiyo baada ya wananchi wa maeneo ya vijiji vya Sua,Mazingara, Amani,Kwachaga na Magamba kuzuia msafara huo na kumtaka rais kuwaeleza hatma ya fidia zao ambazo wanadai kutokana na kupisha ujenzi wa barabara hiyo.

Wananchi hao walidai kuwa pamoja na mambo mengine lakini hawaridhishwi na utaratibu uliyotumika katika uendeshwaji wa zoezi hilo wa fidia hizo kulipwa kiupendeleo ambapo baadhi yao hajawalipwa kabisa.

Wenyeviti wa serikali za  vijiji  vya Sua, Said Magoma,Kwachaga, Miraji Kamwende,Magamba, Mzingara na Amani wote kwa nyakati tofauti  walimueleza rais  Kikwete kwamba kero kubwa katika vijiji hivyo pamoja na maji lakini suala la fidia ni zaidi.

Hata hivyo wenyeviti hao kila mmoja alieleza ukubwa wa tatizo hilo na kutaka kauli ya rais kuhusiana na malipo ya fidia kwa waliyobomolewa nyumba zao ili haki iweze kutendeka pamoja na kuwawezesha wakazi hao kujipanga kimaisha.

Rais  Kikwete ambaye alikuwa akitokea Mkoani Pwani na kupokelewa katika kijiji cha Manga  ambapo alizidua mradi wa maji wenye  thamani ya zaidi ya  tsh million 800 wa Mkata Magharibi, akiwa njiani kuelekea Handeni mjini alilazimika  kusimama kwa kila kijiji  kuhutubia kutokana na wananchi waliyojipanga barabarani kumzuia.

Akihutubia akiwa ndani ya gari katika vijiji hivyo,rais Kikwete aliwahakikishia wananchi waliyovunjiwa nyumba zao kupisha mradi wa barabara watalipwa fidia kila mmoja kulingana na stahiki zake.

Alisema suala hilo halina mjadala hivyo serikali haiwezi kukaa kimya juu ya haki za wananchi wake hivyo atahakikisha kila moja analipwa stahili yake ambapo atakaa na viongozi wake kuangalia namna ya kuzipatia ufumbuzi kero hizo.

Aidha aliwaahidi wakazi wa Handeni kwamba kero ya fidia itapata ufumbuzi na kwamba atamuagiza Waziri wa Ujenzi, John  Pombe Magufuli kuhakikisha kuwa wananchi hao wanalipwa bila ya upendeleo wowote.

Awali akizindua mradi wa bwawa la maji la Mkata magharibi, Kikwete alisema kuwa lengo la serikali ni kupunguza kama siyo kuondoa kabisa kero ya maji inayowakabili wakazi wa Wilayani Handeni kama ilivyowaahidi \.

Awali Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Khalfan Haule alimueleza rais kuwa mradi huo uliyoanza  julai mwaka jana unatekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya zaidi ya tsh million 819 ambapo mpaka sasa umeshatumia zaidi ya tsh million 361 nguvu za wananchi zikiwa ni tsh million 37.

 Akiwa katika ziara ya siku ya kwanza Mkoani Tanga, rais mbali ya mradi wa bwawa hilo  lakini pia alizindua barabara ya Mkata-Handeni na shamba la mifugo la Msomelwa  ambapo kesho (leo) atakuwa Wilayani Korogwe kwa siku moja kabla ya kurejea Jijini Dar.