VETERAN SC yaanza vema Kombe la Takukuru Cup.

June 24, 2013

Na Oscar Assenga, Tanga.
TIMU ya Veteran leo imeanza vema mashindano ya ligi ndogo ya Takukuru Cup baada ya kuilaza Makorora Star mabao 4-2 katika mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo mchezo uliochezwa uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa kusisimua kutokana na timu zote kuonekana kucheza kwa kukamiana ambapo mpaka timu zote zinakwenda mapumziko timu ya Makorora Stars ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-1.

Mabao ya Makorora Star yakifungwa na Hussein Salim ambaye alifunga mabao mawili kwenye dakika ya 6 na 45
Huku bao la Veteran FC la kwanza likipatikana kwenye dakika ya 9 kupitia Sadiq Rashid ambaye alitumia uzembe wa mabeki kupachika wavuni bao hilo.



Kipindi chaa pili kilianza kwa kasi kwa kila timu kuingia uwanjani hapo ikiwa na hari na nguvu mpya baada ya kufanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji wake ambapo, Veteran Sc walionekana kujipanga na kutaka kulipa kisasi.

Wakicheza kwa kusikilizana Veteran Sc waliweza kuongeza bao la pili ambalo lilifungwa na Tinath Tsungi katika dakika ya 55 huku Anderson Solomoni akiipatia timu hiyo bao la pili ambalo lilipatikana kwenye dakika ya 58 kwa njia ya penati.

Baada ya kuingia mabao hayo,Veteran waliweza kuongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Makorora na kufanikiwa kuandika bao lao la nne kupitia Faridini Hemed dakika ya 84 ambalo lilihitimisha karamu ya mabao kwenye mchezo huo.




Mashindano hayo yamefunguliwa leo na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Tanga ,Edson Makallo na yanashirikisha timu 4 ambazo ni Makorora Star,Magomeni Sc,Bomboka Sc na Veteran yenye lengo la kuhamasisha mapambano dhidi ya rushwa kupitia michezo mkoani Tanga.

Mwisho.

Tukidhibiti rushwa michezoni tutapata mafanikio.

June 24, 2013

 Na Oscar Assenga, Tanga.
MKUU wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Tanga, Edson Makallo amesema endapo watanzania tutafanikiwa kudhibiti rushwa kwenye michezo itasaidia kupata wachezaji wazuri wenye uwezo wa kuliletea sifa taifa letu siku zijazo.

.Makallo alitoa rai hiyo jana wakati akifungua Mashindano ya Vijana ya Takukuru  Cup yaliyoanzishwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na chama cha soka wilaya ya Tanga (TDFA) yenye lengo la kukuza na kuibua vipaji vya wachezaji wachanga mkoani Tanga

Alisema rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo ya soka hapa nchini kutokana na kuwa mara nyingi huzifanya timu kushindwa kufanya maandalizi ya kutosha huku zikitegemea kupata ushindi wa kupewa badala ya kutumia jitihada zao binafsi wanapokuwa uwanjani.


Mkuu huyo alisema kuanzishwa kwa ligi hiyo ni kuhamasisha mapambano dhidi ya rushwa kupitia michezo ambapo taasisi hao wakiwa kama wadau muhimu wanawajibu wa kukuza vipaji vya vijana ambao ndio nguvu kazi kubwa katika taifa lolote lile duniani.

Aidha alisema wanatarajia kuanzisha ligi kubwa lengo kubwa likiwa ni kutoa elimu juu ya mapambano dhidi ya rushwa kupitia michezo ili wachezaji wafahamu kuwa rushwa ina athari gani katika jamii na inavyochangia kurudisha nyuma maendeleo ya soka hapa nchini.

Makallo alisema mashindano hayo yalianza jana yakishirikisha timu nne kutoka maeneo mbalimbali wilayani hapa na kuzitaja timu hizo kuwa ni Makorora Sc,Veteren Sc,Bomboka Sc na Magomeni ambazo zitachukua ili kuweza kumpata bingwa wa mashindano hayo.

Mshindi wa kwanza kwenye mashindano hayo atapata kombe na jezi seti moja,mshindi wa pili atapata kitita cha sh.100,000,mshindi wa tatu atapata sh.50,000 huku mshindi wa nne akipata sh.30,000.

  


 “Suala la rushwa michezoni hudumaza maendeleo ya soka hapa nchini hivyo wanamichezo wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupiga vita kwani ndio silaha yao ya kufikia malengo yao siku zijazo na Tanzania bila rushwa michezoni inawezekana “Alisema Makallo.

Mwisho.

RAMBIRAMBI MSIBA WA MATHIAS KISSA

June 24, 2013
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji wa zamani wa timu za Cosmopolitan na Taifa Stars, Mathias Kissa (84) kilichotokea leo alfajiri (Juni 24 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani enzi zake, Kissa akiwa na timu ya Tabora alitamba katika michuano ya Kombe la Taifa wakati huo ikiitwa Sunlight Cup. Alikuwa akicheza katika nafasi ya ulinzi.

Baadaye alijiunga na Cosmoplitan ya Dar es Salaam, na pia kuwa mchezaji wa timu ya Taifa ambapo enzi zake akiwa na wachezaji kama Yunge Mwanansali wakiiwakilisha Tanganyika na baadaye Tanzania Bara walitamba katika michuano ya Kombe la Chalenji wakati huo ikiitwa Gossage, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

Kissa ambaye alipata tuzo ya mchezaji bora wa karne kwa upande wa Tanzania, tuzo inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) alikuwa ndiye mchezaji msomi kupita wote wakati akichezea timu ya Taifa akiwa amehitimu elimu ya Darasa la Kumi.

Kwa mujibu wa binti yake, Erica, marehemu ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi (stroke) alioupata miaka mitano iliyopita, na kisukari. Baadaye alipata kidonda ambacho ndicho kilichosababisha kifo chake.

Msiba uko nyumbani kwa marahemu, Masaki, Mtaa wa Ruvu karibu na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST). Maziko yatafanyika keshokutwa, Jumatano (Juni 26 mwaka huu) kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kisa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Cosmopolitan na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Kisa mahali pema peponi. Amina

Mwisho.
Kwamichi Fc yaitambia Mirado Fc

Kwamichi Fc yaitambia Mirado Fc

June 24, 2013

IMEWEKWA saa 01:44.

Na Mwandishi Wetu,Tanga.

TIMU ya soka Kwamichi Fc juzi ilifanikiwa kuchukua pointi tatu muhimu kwenye mechi yao na Mirada Fc baada ya kuibamiza mabao 3-0,ikiwa ni muendelezo wa michuano ya kombe la Sheshe Cup inayoendelea kutimua vumbi uwanja wa Chuda relini jijini Tanga.

Katika mchezo ambao ulikuwa na upinzani mkubwa licha ya Kwamichi Fc kuonekana kuutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa na kupata bao lao la kwanza dakika ya 6 kupitia Omari Daiyo bao ambalo lilidumu mpaka timu zote zinakwenda mapumziko.

Mpaka timu zote zinakwenda mapumziko,Kwamichi walikuwa wakiongoza ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa kutokana na timu zote kufanya mabadiliko.

Wakionekana kuukamia mchezo huo,Kwamichi waliweza kujipanga na kuweka safu imara ambayo iliweza kuwadhibiti wachezaji wa Mirada Fc hali iliyopelekea kuwachezesha nusu ya uwanja.

Kutokana na hali hiyo,Kwamichi waliweza kufanya shambulio la nguvu langoni mwa wapinzani wao na kuweza kufanikiwa kuandika bao la pili kwenye dakika ya 75 ambalo lilifungwa na Omari Bakata baada ya kutumia uzembe wa mlinda mlango wa timu ya Mirada na kuweka wavuni mpira huo.

Katika dakika ya 85 Yasini Baba Yero aliweza kuwainua kwenye vitini mashabiki wa timu ya Kwamichi mara baada ya kuifungia bao la tatu ambalo liliweza kuihitimisha karamu ya mabao.

Mratibu wa Ligi hiyo,Mbwana Sir Ride aliliambia gazeti hili lengo la kuanzishwa mashindano hayo ni kutaka kuibua vipaji vya wachezaji wachanga na kuinua kiwango cha soka.

MWisho.
UFINYU wa BAJETI katika mradi wa Damu.

UFINYU wa BAJETI katika mradi wa Damu.

June 24, 2013

Na Oscar Assenga, Tanga.
IMEWEKWA JUNE 24 saa 12:11
UFINYU wa Bajeti ya kutosha katika mradi wa uhamasishaji jamii kuhusu uchangiaji damu kwa hiari katika wilaya za Korogwe, Mkinga na Tanga ni miongoni mwa changamoto zilizojitokeza wakati wa zoezi hilo likiwa linafanyika katika maeneo hayo hali ambayo ilipelekea kutokufikia malengo yaliyokusudiwa.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoani Tanga,(TPC)Hassani Hashimu hivi karibuni wakati akisoma taarifa ya uhamasishaji huo kwa waandishi wa habari kwenye majumuisho ya uchangiaji wa damu yaliyofanyika katika viwanja vya Tangamano jijini Tanga .

Hashimu alisema katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huo ulifanikiwa kukusanya uniti 210 za damu kati ya makadirio ya kukusanya uniti 450 ambapo kati yao wanaume waliochangia ni 183 na wanawake walikuwa 27.

Aliongeza kuwa kutokana na uhamasishaji huo uliofanywa na chama hicho katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huo kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje ya mkoa wa Tanga wataalamu wa damu salama kutokana kanda ya kaskazini wameweza kukusanya uniti 450 kati ya lengo walilojipangia la kukusanya uniti 1000.

Alisema kikwazo kingine ni kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa uchangiaji wa damu ndani ya jamii sambamba na kukosekana kwa msukumo kutoka kwenye mamlaka husika katika kuvifanya vilabu vya wachangiaji damu kuwa endelevu.

Aidha aliiomba serikali ya mkoa wa Tanga kupitia mganga mkuu wa mkoa kuweka utaratibu mzuri ambao utawezesha wachangiaji damu wanaojitolea kwa hiari kutambulika na kupewa huduma kwenye hospitali bila kikwazo pale inapohitajika.

“Tunaaamni kuwa huduma bora hiyo itawafanya wachangiaji damu kuwa na ari ya kuendelea kujitolea kutokana na kuwa na uhakika wa kupata huduma wakati wote wanapokuwa wakihitaji wao pamoja na ndugu zao “Alisema Hashimu.

Alisema ombi hilo linatokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wachangiaji damu kuwa wamekuwa wakikosa huduma stahiki na ikibidi kununua damu hasa wanapohitaji huduma hiyo kwenye hospitali za mkoani hapa.

Kampeni hiyo ilizinduliwa mei 23 mwaka huu ambapo lengo kuu ilikuwa ni kukabiliana na changamoto ya upungufu wa damu unaozikabili benki za damu katika hospitali za mkoa wa Tanga hususani hospitali ya rufaa ya mkoa ambayo ni Bombo.

Mradi huo ulianzishwa na Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Tanga( Tanga Press Club) kwa kufadhiliwa na Kampuni ya simu za Mikononi ya Vodacom kwa kiasi cha shilingi milioni sita 6,000,000.

Mwisho.