MARUFUKU UCHAPAJI HOLELA WA VITABU VYA KUFUNDISHIA NA KUJIFUNZIA - MAJALIWA

December 02, 2016


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imepiga marufuku uchapaji holela wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia kwa wachapaji binafsi na badala yake uchapaji huo utasimamiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) ili kuthibiti ubora.

Amesema mbali na kudhibiti wa ubora pia uamuzi huo unalenga kuwa na kitabu kimoja kwa kila somo kwa kila mwanzfunzi kwa nchi nzima ili kuweka uwiano mzuri katika ufundishaji na upimaji wa wanafunzi .

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Desemba 2, 2016) wakati akizungumza na walimu wa halmashauri ya Jiji la Arusha na wilaya ya Arusha kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Ziara hiyo inalenga kukagua utelelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,Utendaji wa Serikali, kusikiliza na kujionea kero zinazowakabili wananchi  wa Mkoa huo kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa ili kuweza kuzitafutia suluhisho.

Amesema kipindi cha nyuma vitabu vilikuwa vinachapwa na watu mbalimbali hivyo kusababisha malalamiko makubwa kutokana na vitabu hivyo kuwa na makosa mengi. “Sasa vitabu vikibainika kuwa na makosa tutaibana Taasisi ya Elimu Tanzania,”.

Aidha, amesema Serkali itahakikisha kila mtoto anakuwa na kitabu chake ili kuwawezesha kusoma vizuri na kuwa na uelewa wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuwarahisishia walimu katika ufundishaji.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu madeni ya walimu, ambapo  amewataka Wakurugenzi wa  Halmashauri zote nchini kutenga fedha katika mapato yao kwa ajili ya kulipa madai ya watumishi mbalimbali katika maeneo yao wakiwemo walimu.

Awali Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Jiji na wilaya ya Arusha na kumuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Arusha kumchunguza Ofisa Utumishi wa wilaya ya Arusha, Bi. Imelda Isosi kufuatia tuhuma za rushwa, ufisadi, unyanyasaji kwa watumishi zilizotolewa dhidi yake.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada watumishi hao kupewa fursa ya kumuuliza maswali ambapo mhudumu wa Chumba cha kuhifadhia maiti wa Hospitali ya  Ortumet Wilayani Arusha, Bw. Bernard Mtei kudai kwamba halmashauri ya wilaya ya Arusha inanuka ufisadi na rushwa hususan katika sekta ya afya.

Baada ya kutoa madai hayo Bw. Mtei alimkabidhi Waziri Mkuu nyaraka mbalimbali zenye uthibitisho wa madai hayo, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo amuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watafanya uchunguzi wa kina dhidi ya tuhuma hizo na zikithibitika wahusika watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria

Wakati huo huo Waziri Mkuu ameitaka Idara ya Uhamiaji kudhibiti wahamiaji haramu kwa kuanza kufanya misako katika nyumba za kulala wageni ili kuwabaini wageni wanaoingia nchini bila ya kibali kwani ni chanzo cha kuingiza silaha haramu nchini.
Amesema inashangaza kuona silaha za aina nyingi katika maeneo mbalimbali ambazo Tanzania hakuna ambazo zinadaiwa kuingia nchini kupitia maeneo ya mpakani. “Hivyo ni lazima Idara ya Uhamiaji ihakikishe wanadhibiti uingiaji wa wahamiaji kwenye mipaka mbalimbali nchini,”.

Waziri Mkuu amesema Serikali haizuii wageni kutoka mataifa mengine kuingia nchini ila ni lazima udhibiti wa wageni hao ufanyike ikiwa ni pamoja na kujiridhisha sababu za kuja nchini na muda watakao kuwepo.

Hata hivyo aliwasihi watumishi wa idara mbalimbali za Serikali kuhakikisha wanafanya kazi kwa nidhamu, weledi, uadilifu na kuwatumikia wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali hata kama wamekosea kuuliza katika maeneo yao.

Amesema “baadhi ya wananchi  hawana uelewa juu ya wapi wapeleke malalamiko yao lakini kwa kuwa wewe ni mtumishi wa umma unapaswa kumsikiliza na kumwelekeza aende wapi badala ya kumtolea maneno yasiyofaa,”.
CHAMA CHA TBN CHATOA SHUKURANI KWA BENKI YA NMB KWA KUKUBALI KUWA MDHAMINI WA MKUTANO WAO.

CHAMA CHA TBN CHATOA SHUKURANI KWA BENKI YA NMB KWA KUKUBALI KUWA MDHAMINI WA MKUTANO WAO.

December 02, 2016
nbc
Ndugu Mwakilishi kutoka Benki ya NMB,

 Kwa niaba ya Chama cha Wamiliki/Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii nchini ‘Tanzania Bloggers Network’ (TBN) napenda kuwashukuru kwa kujitokeza katika mkutano huu muhimu. 

TBN inajua kuwa mnamajukumu mengi ya kuujuza umma masuala anuai, lakini mmechagua kuja kwetu ili kutusikiliza tulichowaitia na baadae tunaamini mtaujuza umma juu ya tukio letu.
TBN iliosajiliwa rasmi na Serikali mwezi Aprili, 2015 kwa kushirikiana na wataalam wa masuala ya habari na mitandao ya kijamii imeandaa semina kwa wanahabari hawa wa mitandao ya kijamii hasa ‘Bloggers’ itakayofanyika jijini Dar es Salaam. Semina hii maalumu ambayo itajumuisha mafunzo ya siku mbili yaani tarehe 5 na 6 ya Mwezi Desemba, 2016 kwa washiriki takribani 150 kutoka Tanzania nzima (Bara na Visiwani) itafuatiwa na mkutano mkuu kwa wanachama hai wa TBN kujadili masuala mbalimbali ya chama na tasnia nzima ya mitandao ya jamii.
Ndugu Wanahabari,
Katika mkusanyiko huu wanatasnia watapewa semina juu ya uendeshaji mitandao ya jamii kwa manufaa, upashaji habari kwa kutumia mitandao yao kwa kuziangatia maadili na namna ya kunufaika na mitandao hiyo kwa waendeshaji (kujipatia kipato) hasa ukizingatia kuwa wapo baadhi yetu tunaifanya kama ajira nyingine. Kimsingi lazima tukubali kuwa mitandao hii imekuwa tegemeo kubwa la kusambaza habari mbalimbali tena kwa muda mfupi tangu kutokea kwa tukio fulani, hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kuwapiga msasa wanaoiendesha ili kupunguza matumizi mabaya ya mitandao hii.
TBN inaamini njia pekee ya kupambana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ni kuendelea kutoa elimu kwa waendeshaji na watumiaji ili mwisho wa siku wasikubali kutumika vibaya au kuitumia vibaya mitandao hii katika kutoa taarifa. Kwa dunia ya sasa hakuna atakayepinga kuwa mitandao hii imekuwa ikielimisha umma, ikikosoa jamii na kiburudisha juu ya masuala anuai ya kijamii.
TBN inapenda kutoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Nne na Tano chini ya Mh. Rais John Pombe Magufuli kwa ushirikiano alioanza kuuonesha hasa kwa kutambua mchango wa mitandao hii ya kijamii na hata kuitumia katika utoaji wa taarifa zao. Kimsingi hii ni hatua nzuri na ya kuigwa hasa katika ulimwengu huu ambapo dunia imekuwa kama kijiji kutokana na hatua ya maendeleo ya habari na mawasiliano.
Ndugu Wanahabari,
Kwa kulitambua hili mnaweza kuona hata taasisi nyeti kama Ikulu nayo ina Blogu maalumu kwa ajili ya kutoa taarifa kwa umma, Idara ya Habari Maelezo nayo ina Blogu kwa ajili ya kutoa taarifa kwa umma juu ya masuala mbalimbali yanayopaswa kutolewa kitaarifa kwa jamii. Jambo la kujivunia zaidi kwa maendeleo ya mitandao hii hata Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Nape M. Nnauye amekuwa mstari wa mbele kuona umuhimu wa mitandao ya kijamii hasa blogu na hata kuzitumia katika kupasha habari umma. Hata katika mkutano wetu wa kesho kutwa ndiye tunayemtarajia kuwa mgeni rasmi atakayetufungulia mkutano huo.
Ndugu Wanahabari,
Kwa namna ya pekee TBN inapenda kutoa shukrani za pekee kwa Benki ya NMB kwa kukubali kuwa wadhamini wa kuu wa mkushanyiko huo wa ‘bloggers’ kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa yetu. Kitendo cha kujitolea kufanikisha jambo hili kinaonesha namna gani NMB inavyowajali wananchi katika masuala mbalimbali ikiwemo hili la upashanaji habari kwa jamii.
Kama hiyo haitoshi tunapenda kuwashukuru wadhamini wengine ambao ni NHIF, SBL, PSPF na Coca Cola ambao wamejitolea kuungana nasi katika kufanikisha tukio hili la kuwaleta pamoja bloggers na kutoa mafunzo kwao. Tunaamini tutakuwa nao siku zote katika masuala mengi ya maendeleo ya tasnia ya mitandao ya kijamii.
Imetolewa na; Mwenyekiti wa Muda wa TBN
Joachim E. Mushi
0756469470
WAMA FOUNDATION YAKANUSHA TAARIFA ZA RAIA MWEMA"

WAMA FOUNDATION YAKANUSHA TAARIFA ZA RAIA MWEMA"

December 02, 2016


WANAWAKE NA MAENDELEO FOUNDATION
D A R ES SALAAM | IJUMAA |DESEMBA 2, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katika gazeti la Raia Mwema toleo No 486 la Tarehe 30 Novemba, 2016 kumeandikwa habari yenye kichwa kilichosomeka “Mali za Salma Kikwete kuuzwa kwa mnada?”.  Katika habari hiyo kumetolewa madai ati kwamba taasisi ya WAMA inayoongozwa na Mheshimiwa Mama Salma Kikwete inao mzigo mkubwa bandarini ambao haujalipiwa ushuru na kodi. Na kwa sababu hiyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania imepanga kuuza mali hizo.
Kwa niaba ya Taasisi ya WAMA napenda kutoa masikitiko yetu kwamba habari hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote. Kwa maoni yetu gazeti hilo lina dhamira mbaya dhidi ya Taasisi ya WAMA na Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Mama Salma Kikwete. Nia yao ni kupaka matope na kuchafua majina na sifa ya taasisi yetu na kiongozi wake.
Ukweli kuhusu jambo hili ni kwamba, WAMA ilitumiwa maboksi Kumi na Moja (11) ya vitabu vikiwa ni zawadi (grant) kutoka Nakayama Foundation ya Japani ambayo ndiyo iliyofadhili ujenzi wa Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo Nyamisati, Kibiti. Maboksi hayo yaliyotumwa kupitia BL 243016002211 yaliwasili bandarini tarehe 27/06/2016. Yalitolewa tarehe 10/8/2016 baada ya WAMA kulipia kodi zote na ushuru wote unaotahili tarehe 26/07/2016.
Vitabu hivyo vimekwishapelekwa shuleni na wanafunzi wanavitumia. Hakuna mzigo wowote wa Taasisi ya WAMA uliopo bandarini unaosubiri kutolewa wala kuuzwa na TRA. Hivyo basi, gazeti hilo kuandika kuwepo kwa mzigo mkubwa wa WAMA bandarini ni jambo la kughushi ambalo limefanywa kwa dhamira mbaya na kwa sababu wanazozijua wao.
Tumelitaka gazeti la Raia Mwema limuombe radhi Mwenyekiti wa WAMA Mheshimiwa Mama Salma Kikwete na kuiomba radhi WAMA Foundation kwa kuandika taarifa za uongo. Gazeti hilo limechafua sifa ya Mwenyekiti wa WAMA na WAMA Foundation kiasi ambacho wanao wajibu wa kuomba radhi na kusafisha majina na heshima zetu mbele ya jamii.
Ikiwa hawatatekeleza haya ndani ya kipindi cha siku Saba, yaani kabla ya tarehe 07 Desemba, 2016, tutalazimika kuchukua hatua zipasazo za kisheria.

Daudi Nasib,
Katibu Mtendaji,
Dar es Salaam,
Tel: +255 22 2781287
info@wamafoundation.or.tz

MAKAMU WA RAIS MAMA SAMIA AENDESHA HARAMBEE YA SH.BILIONI 1 KUSAIDIA MFUKO WA UKIMWI NCHINI

December 02, 2016
 Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati akizundua Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa Udhibiti Ukimwi (ATF)  Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam jana.

WILAYA YA KAKONKO MKOANI KIGOMA HATARINI KUPOROMOKA KIUCHUMI KWA KUKOSA FURSA ZA KIUCHUMI WILAYANI KAKONKO

December 02, 2016



Na Rhoda Ezekiel Globu ya Jamii-Kigoma.

WILAYA ya Kakonko Mkoa wa Kigoma imeelezwa kuendelea kuporomoka kiuchumi kutokana na mzunguko mdogo wa fursa za kibiashara kupelekwa wilaya ya jiran na watumishi wa idara  inayohudumia  wakimbizi katika kambi ya mtendeli kuishi Wilayani Kibondo, hali inayo pelekea shughuli zao zote kufanyika Wilayani humo.

Kufuatia hali hiyo mkuu wa Wilaya Kanali Hosea Ndagala  alitoa  wito kwa watumishi  hao kutoa fursa za kiuchumi kwa wafanya biashara wa Wilaya ya Kakonko wakati wa ujenzi wa nyumba za kudumu za wakimbizi, lengo likiwa ni kuongeza mzunguko  wa kibiashara kwa Wananchi wanao izunguka kambi hiyo na kuacha tabia ya kutoa tenda zote za ujenzi kwa wafanya biashara wa Wilaya ya Kibondo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Wilayani humo, Ndagala alisema watumishi wengi wa Kambi ya mtendeli wamekuwa wakifanya biashara na wafanya biashara wa Kibondo,wakati kambi hiyo inahudumia wakimbizi katika Wilaya ya Kakonko hali inayo pelekea uchumi wa wananchi wa Kakonko waliotegemea kuupata kupitia kambi hiyo kuanzishwa kukosekana na kuhamia wilya nyingine ya Kibondo.

Ndagala alisema halmashauri ya Wilaya ya Kakonko ni halmashauri ambayo uchumi wake bado upo chini,unahitaji kuinuliwa hivyo akawaomba wafanyakazi wa kambi ya Mtendeli pamoja na shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR kutoa vipaumbele kwa  Wananchi wa Wilaya ya Kakonko ili kuinua uchumi wa Wilaya hiyo kwa kuwapatia ajira za ujenzi na ununuzi wa vifaa vya ujenzi kwa wafanya biashara wa Kakonko.

Hata hivyo Mkuu huyo aliwaomba watumishi wote  wa Kambi hiyo na mashirika yanayo hudumka wakimbizi kurudi kuishi Kakonko kwakuwa sababu iliyo kuwa ikiwapelekea waishi Kibondo ya kukosekana kwa Nyumba  za kupanga Wilayani humo limekwisha Wananchi wamejitahidi kujenga nyumba zenue ubora ambazo wanaweza kupanga na kufanya kazi zao za kuhudumia wakimbizi wakiwa wilayani humo.

"Tenda nyingi za ujenzi wa Nyumba za kudumu za Wakimbizi zimekuwa zikitolewa kwa wafanya biashara wa kibondo jambo ambalo sio zuri ukizingatia Wilaya yetu inakambi yenye wakimbizi wengi shughuli zao za Kijamii zinategemea wilaya yetu ni lazima Wananchi wetu na Wilaya kwa ujumla tunufaike na ujio wa wakimbizi sio wilaya yetu inaadhirikana Wilaya nyingine inanufaika",alisema Ndagala

Aidha mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kakonko ,Juma Maganga  alisema Mpaka sasa Kambi ya Mtendeli ina jumla ya wakimbizi 50,000 ambapo kambi hiyo imejaa na inatarajiwa kuanzishwa kambi nyingine kufuatia hali hiyo Wilaya yetu inawahudumia wote hao na wanategemea huduma nyingine kama vile ukataji wa kuni uchotaji wa maji kutoka kwa Wanakijiji wanao xunguka kambi,endapo fursa za kiuchumi zinapo pelekwa kibondo haileti picha nzuri kwa wanNchi wetu.

alisema kwa sasa ni fursa mojawapo kwa wilaya  ya kakonko kunufaika na ujio wa wakimbizi  kupitia mradi wa uanzishwaji wa majengo ya kudumu kwa wafanya biashara kupata tenda za kuhudumia vifaa vya ujenzi,vyakula kwa Mafundi na wakimbizi mara watakapo kurejea  nchini kwao baada ya kuridhika uwepo wa amani.

Pia tungependa watumishi wote warudi Kakonko kambi haiwezi kuwa katika Wilaya yetu na watumishi wanaishi Wilaya nyingine jambo hilo sio zuri linaweza kupelekea uharibifu Mkubwa ukizingatia wakombizi hao baadhi hutoroka nyakati za usiku  na kufanya vitendo vya kiuhalifu kwa Wananchi wanao izunguka kambi.

Kwa upande wake Mkuu wa kambi ya Mtendeli Inocent Mwaka alisema Suala hilo atalifanyia kazi atazungumza na wahusika iliwaweze kufanya mambo hayo yaliyo pendekezwa na Mkuu wa Wilaya kwa kuwashawishi kuwahamishia watumishi wote wa kambi katika Wilaya ya kakonko na kutoa fursa kwa Wananchi wa Kakonko kunufaika na ujio wa wakimbizi hao.

Chanzo:MichuziBlog.

ULEGA AENDELEA NA ZIARA YA KUWASHUKURU WANANCHI JIMBONI KWAKE

December 02, 2016


Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kibuyuni Kata Panzuo, alipokuwa katika ziara yake ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua, pia kusikiliza kero zao, hususani ile ya Mifugo kuharibu vyanzo vya maji pamoja na mazao yao.
Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mkuruwili, alipokuwa katika ziara yake ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua, pia kusikiliza kero zao.
Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya Mbulali FC inayo shiriki kombe la Ulega.
Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa timu ya Nyatanga FC.





CHAMA CHA AFYA YA JAMII TANZANIA (TPHA) CHAPATA VIONGOZI WAPYA

December 02, 2016
 Mwenyekiti Mteule wa Chama cha Afya ya Jamii Tanzania (TPHA), Shaibu Mashombo (wa nne kushoto), akiwa na viongozi wenzake wateule waliochaguliwa katika mkutano mkuu wa chama hicho 2016 jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Dismas Vyagusa, Violeth Shirima, Dk. Godfrey Swai, Dk.Nderineia Swai, Dk. Feliciana Mmasi,  Dk. Mwanahamisi Hassan na Dk.Elihuruma Nangawe ambaye alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho aliyemaliza muda wake.
Mwenyekiti wa Chama cha Afya ya Jamii Tanzania (TPHA), aliyemaliza muda wake Dk.Elihuruma Mangawe (katikati), akiongoza kikao cha mkutano mkuu wa chama hicho. Kushoto ni Katibu Mkuu wa TPHA, Fabian Magoma na kulia ni Ofisa Utawala wa chama hicho, Erick Goodluck.
 Mwenyekiti Mteule wa Chama cha Afya ya Jamii Tanzania (TPHA), Shaibu Mashombo (kulia) akiwaelekeza jambo wajumbe kabla ya kufanyika kwa uchaguzi uliompa nafasi hiyo.
Wajumbe wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Wajumbe wa mkutano huo.
Usikivu katika mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.


Na Dotto Mwaibale

CHAMA cha Afya ya Jamii (TPHA) kimepata viongozi wapya ambapo kimemchagua Dk. Shaibu Mashombo kuwa Mwenyekiti.

Mashombo alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 35 na kumbwaga Feliciana Mmassy aliyepata kura 10 na kura moja ikiharibika.

Katika nafasi ya Mhariri Mkuu Dk.Godfrey Swai aliibuka kidedea dhidi ya Ndeniria Swai aliyepata kura 15 na kura tisa zilikataa ambapo katika nafasi ya Katibu Mwenezi wagombea walikuwa wawili Elizabeth Nchimbi aliyepata kura 15 na Ndeniria Swai ambaye aliibuka mshindi kwa kupata kura 29 huku kukiwa hakuna kura iliyopotea.

Katika nafasi ya Mtunza Fedha licha ya kuwepo na ushindani makali aliyeibuka mshindi ni Mwanahamisi Hassan ambaye alipata kura kura 20 dhidi ya mgombea mwenzake Violeth Shirima aliyepata kura 24.

Nafasi ya Katibu wa Mipango ilikwenda kwa Dk. Mwanahamisi Hassan aliyepata kura 38 dhidi ya Othman Shem aliyeambulia kura tano huku Feliciana Mmasi na Dismas Vyagusa wakishinda nafasi ya wajumbe wa kamati ya utendaji.



IGA yatoa mafunzo ya Usimamizi wa Miradi ya Jotoardhi

December 02, 2016


                                            Na Johary Kachwamba - TGDC

Wataalamu kutoka Chama cha Kimataifa cha Jotoardhi (International Geothermal Association-IGA) wametoa mafunzo ya usimamizi wa miradi ya jotoardhi kwa wataalamu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC).

Mafunzo haya yanafadhiliwa na Shirika la Msaada wa Usimamizi wa Nishati chini ya Benki ya Dunia (ESMAP) katika jitihada za kuijengea uwezo TGDC ili iweze kusimamia miradi ya jotoardhi ambayo bado ni teknolojia ngeni nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Meneja Mkuu TGDC, Mhandisi Kato Kabaka alitoa shukrani kwa ESMAP na kusema “ni fursa muhimu kwetu kama kampuni katika maandalizi ya kuendeleza nishati ya jotoardhi inayolenga kusaidia taifa kufikia malengo yaliyo katika dira ya 2025”.
Mtaalamu wa Nishati kutoka Shirika la Msaada wa Usimamizi wa Nishati chini ya Benki ya Dunia (ESMAP) Dkt. Thrainn Fridrikson aliwapongeza TGDC kwa jitihada walizofikia na kuahidi kuendeleza ushirikiano na TGDC pamoja na IGA wakati wote wa mchakato wa kuwajengea uwezo wataalamu wa jotoardhi nchini.

Mhandisi Uchorongaji, Amani Christopher kutoka TGDC alishukuru wakufunzi na wafadhili kwa niaba ya TGDC “mafunzo haya yana tija sana kwetu hasa waandisi tuliotoka katika mufunzo ya vitendo nchini Kenya kwa kuwa sasa tunaweza kuowanisha utekelezaji na usimamizi wa miradi ya jotoardhi, hasa kipengele cha uchorongaji” alisema Amani.

Mafuzo hayo yalihusu usimamizi katika manunuzi, taratibu za kisheria, uchorongaji na fedha za kugharamia miradi.
Kaimu Meneja Mkuu Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Kato Kabaka akizungumza na wataalamu wa nishati ya jotoardhi kutoka TGDC, Shirika la Msaada wa Usimamizi wa Nishati chini ya Benki ya Dunia (ESMAP) na Chama cha Kimataifa cha Jotoardhi (IGA) wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wataalamu wa jotoardhi nchini.
Mtaalamu kutoka Chama cha Kimataifa cha Jotoardhi (IGA) Mhandisi Cristian Scanzoni akiwasilisha mada kuhusu usimamizi wa uchorongaji visima vya jotoardhi wakati wa miradi. Mafunzo hayo maalum yalifadhiliwa na ESMAP na yalilenga kuwajengea uwezo wataalamu wa Jotoardhi Tanzania.
Wataalamu wa nishati ya jotoardhi kutoka Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Shirika la Msaada wa Usimamizi wa Nishati chini ya Benki ya Dunia (ESMAP) na Chama cha Kimataifa cha Jotoardhi (IGA) katika majadiliano wakati wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo  yaliyafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki ya Dunia Tanzania.