Mkurugenzi TSB alipongeza Jiji la Tanga kuzindua kitalu cha Mkonge

October 21, 2022


 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe Hashim Mgandilwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Sipora Liana kwa kuzindua zoezi la ugawaji wa mbegu za Mkonge bure kwa wananchi.

 

Mapema wiki hii, Jiji la Tanga lilitoa bure miche takribani 358,000 kwa wakulima wa Mkonge walioko Kwenye kata sita za halmashauri hiyo.

 

“Natoa pongezi nyingi sana kwa Mhe Mgandilwa na Mama Liana kwa kuzindua zoezi la ugawaji wa mbegu za Mkonge bure kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa ambaye aliagiza kuwa kila Halmashauri ya Wilaya, Manispaa na Jiji katika Mikoa inayofaa kwa Kilimo cha Mkonge kuanzisha kitalu cha mbegu za Mkonge kisichopungua ekari 10 na kugawa mbegu bure kwa wananchi.

 

“Hii ni fursa nzuri kwa wakulima wa Mkonge katika Jiji la Tanga, Bodi ya Mkonge inawaahidi ushirikiano wa kila hali wasisite kuwasiliana nasi pindi wanapohitaji ushauri wa kitaalamu na mambo mengine yanayohusu sekta ya Mkonge milango iko wazi,” amesema Mkurugenzi Kambona.

 

Akizindua zoezi hilo la kugawa miche ya Mkonge kwa wakulima hao, DC Mgandilwa alisema lengo ni kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na kufikia lengo la serikali la kuzalisha tani 120,000 ifikapo mwaka 2025.

 

“Nawaomba miche hiyo mkaipande kwenye mashamba yenu na si kuiacha ikaharibikia mashambani hapo mtakuwa hamjaitendea haki serikali ambayo imetumia rasilimali kuendeleza miche hiyo,” alisema DC Mgandilwa

 

Pamoja na mambo mengine, baadhi ya wakulima waliopatiwa miche hiyo, wameishukuru serikali kwa kuwapatia zao mbadala la biashara ambalo litawakwamua kiuchumi tofauti na sasa ambapo walikuwa wanategemea mihogo kama zao kuu la biashara ambalo kwa sasa halifanyi vizuri hivyo kuja kwa mkonge fursa mpya ya kujikomboa kiuchumi kutokana na faida zake.