CHADEMA TANGA YAPONGEZA UAMUZI WA KUVULIWA UONGOZI KATIBU MSAIDIZI

November 29, 2013
Na Oscar Assenga, Tanga
SIKU Chache baada ya Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Taifa (Chadema) kuamua kumvua uongozi ndani ya chama hicho aliyekuwa katibu Msaidizi Zitto Kabwe chama hicho mkoani hapa kimeipongeza hatua hiyo kwa kusema italeta umakini mkubwa kwa viongozi waliobaki.



Uamuzi huo ulitolewa kwa mujibu ibara ya 7.7.16 kifungu (V) ambayo inaeleza kuwa kamati hiyo ina mamlaka ya kumwachisha ujumbe wa kamati kuu mjumbe mteule ambaye ataenda kinyume cha katiba, kanuni na maadili au kushindwa kukidhi matakwa ya kuteuliwa kwake.

WAFUGAJI KILINDI WACHOSHWA NA MATUKIO YA KIKATILI YA MIFUGO YAO

November 29, 2013
Na Elizabeth Kilindi,Kilindi.

MVUTANO   unaoashiria mapigano na mauaji kwa mara nyingine tena unafukuta baina ya wakulima na wafugaji  Wilayani Kilindi Mkoani Tanga baada ya wafugaji kuchoshwa na  matukio ya  kikatili ya mifugo yao kuuawa  kwa kuwekewa  sumu kwenye malisho na  kufia porini.


Tukio hilo la kusikitisha lilitokea  juzi katika kitongoji cha Kipaluke, Kijiji cha Kigwama, Kata ya Msanja Tarafa ya Mswaki Wilayani Kilindi  ambako ng'ombe nane  walifia porini  kati ya 14 waliyodaiwa  kula majani yenye sumu.



PANGANI YAZINDUA UTARATIBU WA UTOAJI VIBALI SHUGHULI ZA UFUGAJI MDOGO

November 29, 2013
Na Burhan Yakub,Pangani.
Wilaya ya Pangani imezindua rasmi cha kitabu cha utaratibu wa
utoaji wa vibali vya shughuli za ufugaji mdogo wa viumbebahari ambao utawawezesha wakazi wa mwambao wa pwani kufanya shughuli za uzalishaji mali bila kuathiri mazingira.

Kitabu hicho  kilichozinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Hafsa Mtasiwa hivi karibuni kikiwa kimeandaliwa na mradi ujulikanao “Pwani Project”kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho,Mkurugenzi wa mradi wa Pwani,Baraka Kalangahe alisema yaliyoandikwa ni hali halisi ya sasa ya ufugaji mdogo wa viumbebahari na matatizo yanayoikabili tasnia ya maendeleo ya ufugaji mdogo wa viumbe bahari katika Wilaya ya Pangani.

Mengine yaliyoandikwa ni taarifa muhimu za maeneo yanayofaa kwa ufugaji mdogo wa viumbebahari katika Wilaya ya Pangani, maeneo yanayofaa kwa vijiji vya Buyuni, Mkwaja, Mikocheni, Sange,Kipumbwi, Mikinguni,Stahabu,Ushongo Bweni , Mkwajuni,  Pangani Magharibi, Mwembeni,Msaraza na   Kigurusimba.

Mkurugenzi huo pia alisema Kitabu hicho kinatoa mwongozo wa utoaji wa vibali, ufuatiliaji na udhibiti.

Akizungumza baada ya kuzindua kitabu hicho,Mkuu wa Wilaya alisema mradi huu utasaidia kuongeza thamani ya bahari nakuonya kuwa mtendaji atakayesababisha kuzorota katika eneo lake atamuwajibisha.

WAZIRI KIGODA MGENI RASMI TAMASHA LA HANDENI KWETU

November 29, 2013
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Viwanda Biashara na Masoko ambaye pia ndio mbunge wa Handeni, Dkt Abdallah Kigoda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Utamaduni, lililopangwa kufanyika Katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni mkoani Tanga, Desemba 14 mwaka huu.

Tamasha hilo linafanyika kwa mara ya kwanza wilayani hapa, huku likitarajiwa kuwa la aina yake kutokana na maandalizi yanayoendelea kushika kasi, ambapo kwenye uwanja huo, Tamasha hilo litaanza saa 2 asubuhi hadi saa 12 za jioni.

Akizungumza jana mjini Handeni, Mratibu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema maandalizi yamezidi kushika kasi kwa kuangalia mazoezi ya vikundi kadhaa vitakavyotoa burudani katika tukio hilo.

“Tunashukuru Mungu kuona mambo yanazidi kuwa mazuri kwa kuhakikisha kuwa Desemba 14 mwaka huu tunafanya tamasha lenye mguso na kila mmoja wetu kufaidishwa.

“Huu ni wakati wa kila mtu kujipanga ili aje kushiriki kwa namna moja ama nyingine, ukizingatia kuwa juhudi hizi zote zipo kwa ajili ya kujenga ushirikiano kwa watu wote,” alisema Mbwana.

Wadhamini katika tamasha hilo ni pamoja na gazeti la Mwananchi, Clouds Media Group, ni Phed Trans, Clouds Media Group, Grace Products, Screen Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles & Construction Ltd, Katomu Solar Specialist, PLAN B SOLUTIONS (T) LTD, Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group duka la mavazi la Chichi Local Ware, Smart Mind & Arters chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog, Pamoja Pure Blog na Taifa Letu.com.

WACHEZAJI KIZIMBANI UNITED WATOA YA MOYONI.

November 29, 2013
Na Masanja Mabula -Pemba .

Hatimaye wachezaji na mashabiki wa Klabu ya Kizimbani United wametoa ya moyoni na kusema kuwa sababu zilizopelekea timu hiyo kufanya vibaya kwenye michuano ya ligi kuu Zanzibar ni kuwepo na upendeleo wakati wa upangaji wa timu .

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi , wamesema kuwa tatizo la upangaji wa timu limekuwa ni kikwazo cha kuweza kufanya vizuri ambapo baadhi ya wachezaji wamekuwa wakipangwa kutokana na kuwa na uhusiano wa Kocha pamoja na viongozi wa timu .

Wamesema kuwa licha ya baadhi yao kuwa na viwango  lakini wamekuwa wakikalia benchi , kwa sababu ya kutokuwa na usuhuba na viongozi pamoja na kocha jambo ambalo limeiweka pabaya timu hiyo .

"Unajua kama huna usuhuba na viongozi pamoja na Kocha ,basi utakalia benchi mpaka uchoke , hata kama unakiwango kama Messi na  hii ndiyo iliyopelekea timu kufanya vibaya kwenye michuano ya ligi kuu ya Zanzibar " alieleza mmoja wa wachezaji jina tunalo .

Aidha nao mashabiki wa timu hiyo wamesema kuwa kitendo cha kuchezesha wachezaji wasio na uwezo kunaweza kuleta athari kwa klabu ikiwa ni pamoja na kushuka daraja .

Meneja wa Klabu hiyo Juma Saleh amekanusha taarifa hizo na kusema kuwa mchezaji anaweza kujihakikishia namba kutokana na juhudi yake mazoezini na kwamba suala la upendeleo halipo ndani ya klabu hiyo .

"Kocha anaangalia juhudi ya mtu mazoezini , na bidii ya mchezaji ndiyo inayomfanya mchezaji ajihakikishie namba kwenye kikosi , lakini suala la viongozi kuwa na wachezaji wao halipo ndani ya klabu yetu " alifahamisha meneja .

 Naye Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya klabu hiyo Juma Mzee amesema kuwa wachezaji wanaolalamika kutochezeshwa hawana elimu na hawajifahamu nini wanatakiwa wafanye , kwani lengo la viongozi ni kuona kuwa timuinafanya vyema na  inasonga mbele .

"Tatizo la wachezaji wetu hawana elimu pamoja na nidhamu ya mchezo , hili ndio chanzo cha baadhi yao kulalamika kwamba hawapewi nafasi ya kucheza , mimi najua wachezaji wote wamechezeshwa kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo  " alifahamisha .

Timu ya soka ya Kizimbani United kwa sasa inaendelea na mazoezi ikiwinda na michuano ya super 8 baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Zanzibar na kuambulia alama 8 katika mechi kumi na moja ilizocheza .

NGWASUMA:KUPAGAWISHA UKUMBI WA KINGSTONE MOROGORO DESEMBA 6

November 29, 2013


Na Raisa Said,Tanga.
BENDI ya Mziki wa Dansi ya nchini FM Academia “Wazee wa Ngwasuma”inatarajiwa kufanya onyesho kali la Mlipuko wa Burudani mkoani Morogoro  Desemba 6 mwaka huu katika ukumbi wa Kingstone Night Club.

Onyesho hilo linatarajiwa kuanza majira ya saa tatu usiku ambalo litakuwa la aina yake kutokana na aina ya wanamuziki wa bendi hiyo iliyojizolewa umaarufu mkubwa hapa nchini.

Akizungumzia onyesho hilo,Meneja wa Ukumbi wa huo,Juma Abajalo alisema maandalizi yake yanaendelea vizuri ambapo wasanii wa bendi hiyo watawasili mkoa wa Morogoro siku moja lengo likiwa ni kuhakikisha wanakata kiu ya wapenzi wa mziki wa dansi mkoani humo.

Abajalo alisema onyesho hilo linatarajiwa kuwa la aina yake ambapo aliwataka wakazi wa mkoa wa Morogoro kujitokeza kushuhudia burundani ambazo zitapakana siku hiyo ambapo wasanii hao watapata nafasi ya kulitawala jukwaa mahiri litakalokuwa kwenye ukumbi huo maarufu mkoani hapa.

“Ninachoweza kusema maandalizi ya kuelekea onyesho hilo yamekamilika kwa asilimia kubwa hivyo tunawaomba wapenda burudani mkoani hapa kukaa mkao wa kula “Alisema Abajalo.

Abajalo alisema ukumbi huo wa Kingstone Night Club onyesho hilo linafanyika baada ya ukarabati mkubwa uliofanywa na wamiliki wake lengo likiwa ni kuwapa mambo mazuri wapenzi wa burudani mkoani humo.