WAZIRI MKUU ATEMBELEA MAONESHO YA SIKU YA KIFUA KIKUU DUNIANI KITAIFA SIMIYU

March 24, 2023


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiteremka kutoka kwenye gari lenye maabara inayotumika kupima ugonjwa wa Kifua Kikuu katika maeneo mbalimbali wakati alipotembelea mabanda ya monyesho ya Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, Machi 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa , Mwalimu wa panya wanaonusa na kubaini mate au makohozi yenye vijidudu vya ugonjwa wa Kifua Kikuu, Mariam Chamkwata wa Chuo Kikuu cha Kilimo, Sokoine cha Morogoro, katika maonyesho ya Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani yaliyofanyika kitaifa  kwenye uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu,   Machi 24, 2023. Wa pili kulia ni Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye uwanja a Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu kuwa mgeni rasmi katika  Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, Machi 23, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU AWASILI SHINYANGA AKIWA NJIANI KWENDA SIMIYU

WAZIRI MKUU AWASILI SHINYANGA AKIWA NJIANI KWENDA SIMIYU

March 24, 2023

 


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Ibadakuli Shinyanga akiwa njiani kuelekea Bariadi mkoani  Simiyu ambako atakuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, Machi 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na vionghozi wa Mkoa wa Shinyanga wakati alipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa Ibadakuli mkoani Shinyanga akiwa njiani kwenda Bariadi mkoani Simiyu ambako atakuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani, Machi 24, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

SMAUJATA MANYARA YAANZA KUINOA JAMII VITA YA UKATILI.

March 24, 2023

 Na John Walter-Manyara

Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Manyara imeanza kwa kasi kwa kutoa elimu ya Kujitambua kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari, kujua Ukatili na kuripoti wanapofanyiwa au kuona mtu akifanyiwa Ukatili.

Katibu wa SMAUJATA mkoa wa Manyara ambaye pia ni Mkuu wa Dawati la jinsia Mkoa, Willnes Kimario amewataka wanafunzi kuwafichua wazazi ,walezi na wote wanaofanya ukatili dhidi yao.

Pia amewataka wakawe mabalozi kwa wazazi wao kuwaambia juu ya madhara ya Ukeketaji na Ukatili mwingine kama walivyofundishwa.

Afisa Maendeleo ya jamii Wilaya ya Babati Agatha Patrice amewaasa wanafunzi wasiwe rahisi kukubali lifti wanazopewa barabarani au Chipsi kwani ndo chanzo Cha kufanyiwa Ukatili na kukatisha masomo yao.

Amesema Mtoto wa kike na wa Kiume wote wana haki sawa na wanapaswa kulindwa.

Amesema jamii ikishirikiana vyema na wadau wa kupinga Ukatili pamoja na jeshi la polisi itaongeza nguvu katika kupunguza vitendo hivyo na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Babati Philipo Sulle, amesema upo Ukatili ambao unafanywa pia na Wanafunzi wenyewe kwa wenyewe ukiwemo Ukatili wa kihisia kwa kusemana vibaya na kuwaonya wenye tabia hiyo waache mara Moja.

Ametoa wito kwa wazazi kuongeza usimamizi wa karibu kwa watoto wao ili kuwaepusha na matukio hayo na walimu kuendelea kusisitiza maadili mema yanayofuata tamaduni za Kitanzania.

Mkuu wa shule ya Sekondari Dabil Alfred Sulle, amesema licha ya shule hiyo kutokuwa Mhanga wa Ukatili lakini shule nyingi Za Kata ya Dabil zinatajwa kuwa na Wanafunzi waliokumbana na adha ya Ukatili wa aina mbalimbali.

Mkuu Dawati la Jinsia na Watoto wilaya ya Babati mkaguzi msaidizi wa polisi Daudi Danyesi amewataka wanafunzi na wananchi kwa Ujumla kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi hilo ili wahusika wakamatwe na washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Wanafunzi wameshukuru kwa elimu hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri Kwa jamii.Mkoa wa Manyara kitakwimu katika Ukatili wa kikinsia unatajwa kushika nafasi ya pili huku kwa Ukeketaji ukishika nafasi ya kwanza Kitaifa.

Ukanda wa Tarafa ya Bashnet ndo unaotajwa kuongoza kwa vitendo vya Ukatili huku kesi zikimalizwa kinyumbani.

SMAUJATA Manyara wametoa elimu hiyo katika Shule tano za wilaya ya Babati Dabil Sekondari, shule ya Msingi Mandi, Shule ya Msingi Barmot, Shule ya Msingi Sabilo na Shule ya Msingi Lomhong.

Kiongozi mwingine aliyekuwa kwenye jopo la watoa elimu ni Katibu msaidizi SMAUJATA Mkoa wa Manyara Rest George Chuhila




BODI YA USHAURI TFS YATEMBELEA HIFADHI YA MAZINGIRA ASILIA AMANI

March 24, 2023

 BODI ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wametembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani iliyopo Muheza mkoani Tanga lengo likiwa ni kukagua uboreshaji wa miundombinu na huduma za kiutalii ambapo imelidhishwa na hatua iliyofikiwa pamoja na uwekezaji uliofanyika.

Wakati wa ziara hiyo wajumbe wa bodi walilidhishwa na uwekezaji mkubwa uliofanyika wa miundombinu na mazingira ya hifadhi uliofanywa na fedha za Uviko 19 lakini pia bajeti binafsi kuboresha maeneo yaliosalia.

Akizungumza mara baada ya kukagua miradi na vivutio vya utalii vya hifadhi hiyo, mjumbe wa Bodi Wakili Msomi Piensia Christopher Kiure aliupongeza uongozi wa TFS kwa uwekezaji mkubwa waliofanya kwenye hifadhi hiyo na kuutaka kuongeza ubunifu katika kuitangaza hifadhi hiyo.

Amesema uwekezaji mkubwa umeshafanyika na sasa ni wakati wa kuhakikisha kunakuwepo na mikakati thabiti ya kujitangaza huku akiwataka maafisa utalii kuwa wabunifu na kusimamia utekelezaji wa malengo kwa hali yoyote.

“Uwekezaji uliofanyika hapa ni mkubwa sana, hifadhi ina vivutio vingi na miundombinu imeimarika ongezeni nguvu ya kuitangaza, maafisa utalii, wengi wenu ni vijana onyesheni mnatosha, kuweni wabunifu, toeni mawazo na muwe tayari kuyasimamia, na sio lazima lazima uwe na fedha kuanza hili,” anasema Wakili Msomi Kiure.

Aidha, Wakili Msomi Kiure aliutaka uongozi kuingia mikataba (MOU) na nchi zinazofanya vizuri kwenye utalii ikolojia ili kuwe na utaratibu wa kubadirishana wataalamu lengo likiwa ni kubadirishana ujuzi.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi CPA. Bahati Lucas Masila aliupongeza uongozi wa TFS kwa kuhifadhi na kuhakikisha miundombinu ya utalii hifadhini hapo inaboreshwa na kuahidi kutumia sehemu ya likizo yake kudhuru na familia yake kupumzika kwa kile alichosema kuvutiwa na hali ya utulivu.

Someni Mteleka ni Mkuu wa Kitengo cha Utalii TFS anasema katika kuhakikisha uwekezaji uliofanyika unakuwa wenye tija, pamoja na mambo mengine tayari wameandaa video za lugha nne tofauti (Kichina, Kijerumani, Kingereza na Kiswahili) lengo likiwa ni kuwafikia watalii wengi zaidi huku wakifungua njia ya Amani kwenda Hifadhi ya Nilo iliyopo Lushoto.

Naye Naibu Kamishana Msaidizi TFS na Mhasibu Mkuu Peter Mwakosya anasema katika mwaka huu wa fedha, Wakala imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha zaidi hifadhi zake ili kuwavutia watalii wengi zaidi na hivyo kuchangia katika kufikia idadi ya watalii 5,000,000 hadi ifikapo 2025 iliyowekwa na Serikali huku mapato yakiongezeka. Tulizo Kilaga anaripoti.







MZUMBE YAFUNGUA DAWATI LA JINSIA KAMPAS KUU YA MOROGORO.

MZUMBE YAFUNGUA DAWATI LA JINSIA KAMPAS KUU YA MOROGORO.

March 24, 2023

 


 
NA FARIDA MANGUBE,  MOROGORO.

Wajumbe wa Dawati la jinsia Chuo kikuu Mzumbe kampasi kuu ya Morogoro wametakiwa kutunza siri na kutoa msaada unaostahili kwa walioathiriwa na Vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kujenga jamii iliyo bora.

Akizungumza wakati akifungua Dawati la jinsia chuo kikuu Mzumbe kampas kuu ya Morogoro kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Rebecca Nasemwa ambae amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo wa Morogoro Fatma Mwasa alisema kumekuwa na ongezeko la matukio yanayohusiana na unyanyasaji wa kijinsia na mashambulio ya aibu yanayohusisha wanafamilia na jamii kwa ujumla, hivyo kuzinduliwa kwa Dawati hilo maalumu liwe chachu ya kutokomeza ukatili wa jinsia chuoni hapo.

Alisema kuanzishwa kwa Dawati hilo ni moja ya hatua kubwa za kutimiza malengo ya serikali ya kupunguza na kumaliza kabisa ukatili wa kijinsia kwenye jamii hususani vyuoni.

“Mtu akinyanyaswa hata uwezo wake wa kufikiri unapungua maana atatumia muda mrefu kufikiria jinsi ya kujinasua badala ya kutumia muda huo kufikiria jambo lingine kwa ajili ya ustawi wa jamii.” Alisema Rebecca.

Aidha alikitaka chuo kikuu Mzumbe kupitia Dawati hilo kufanya tafiti na kuibua mambo ya ukatili yanayoendele kwenye vijiji vinavyozunguka Chuo hicho kwajili ya kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini.

Pia aliupongeza uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kujenga jengo maalumu kwa ajili ya Dawati la jisnia.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judith Nguli aliwataka wanafunzi, walimu pamoja na watumishi wote ya Chuo Kikuu Mzumbe kutoa taarifa bila ya uwaga za unyanyasaji wa kijinsia kwenye Dawati hilo lililofunguliwa.

Naye Kaim Makamu Mkuu wa Chuo kikuu Mzumbe Prof.William Mwegoha alisema Dawati hilo litafanya kazi kwa kuzingatia muungozo wa Serikali.

Pia alitaja njia zitakazotumika kupata taarifa za unyanyasaji wa kijinsia ni pamoja na mlengwa kufika moja kwa moja kwenye ofisi za Dawati la jinsia, kupiga simu kupitia namba ya wazi ambayo mtu yeyote anaweza kupiga na kutoa taarifa zake na kutumia sanduku la maoni.

Kwa upande wao wanafunzi waliipongeza Serikali kupitua Chuo Kikuu Mzumbe kwa kufungua Dawati la jinsia chuoni hapo kwani litasaidia kupunguza unyanyasaji wa kijisnia unaofanywa na baadhi ya watu wasio na maadili.

Walisema ukatili na unyanyasaji wa kijinsia umekuwa ukisababisha wanafunzi wengi kutofikia malengo yao na wengine kuacha kabisa masomo.

MEJA JENERALI MBUGE MIKOA IANZISHE TIMU YA WATAALAM YA KUKABILIANA NA MAAFA

March 24, 2023


Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge akifungua Kikao kazi cha Kuweka Mkakati wa Kuanzisha Timu ya Wataalam ya Kukabiliana na Maafa Mkoa wa Dodoma (Dodoma Mult Agency Emergency Response Team – DoMAERT) kilichofanyika Jijini Dodoma.


Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Wataalam ya Usimamizi wa Maafa kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wakifuatilia kikao hicho.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Wataalam ya Usimamizi wa Maafa kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wakifuatilia kikao hicho.
Mkurugenzi Msaidizi Idara  ya Menejimenti ya Maafa (Utafiti) Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi akiwasilisha Sera, Sheria na Mfumo wa Usimamizi wa Maafa wakati wa kikao kazi cha Kuweka Mkakati wa Kuanzisha Timu ya Wataalam  ya Kukabilianana Maafa  Mkoa wa Dodoma (Dodoma Mult Agency Emergency Response Team – DoMAERT) kilichofanyika  Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa (Utafiti) Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Charles Msangi akiwasilisha Sera, Sheria na Mfumo wa Usimamizi wa Maafa wakati wa kikao kazi cha Kuweka Mkakati wa Kuanzisha Timu ya Wataalam ya Kukabilianana Maafa Mkoa wa Dodoma (Dodoma Mult Agency Emergency Response Team – DoMAERT) kilichofanyika Jijini Dodoma.

Mtaalam Mshauri kutoka DarMAERT Dkt. Christopher Mnzava (aliyesimama) akiwasilisha Muundo wa Timu Mtambuka ya Wataalam ya kukabiliana na Maafa pamoja na Taratibu, Majukumu ya Kiutendaji wakati wa kukabiliana na Maafa katika kikao hicho.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge (wa tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja  na baadhi ya Wajumbe wa  Kamati ya Wataalam ya Usimamizi wa Maafa baada ya  Kikao kazi cha Kuweka Mkakati wa Kuanzisha Timu ya Wataalam  ya Kukabiliana na Maafa  Mkoa wa Dodoma (Dodoma Mult Agency Emergency Response Team – DoMAERT) kilichofanyika  Jijini Dodoma.


Na Mwandishi wetu- Dodoma

Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge  amewataka Wataalam  kuanzisha Timu Mtambuka ya Wataalam ya Kukabiliana wa Maafa kila Mkoa ambayo itarahisisha  mawasiliano ndani ya Mkoa wakati wa kukabiliana na dhahrura.

Meja Jenerali Mbuge ameyasema hayo wakati akifungua Kikao Kazi cha Kuweka Mkakati wa Kuanzisha Timu ya Wataalam ya Kukabilianana Maafa  Mkoa wa Dodoma (Dodoma Mult Agency Emergency Response Team – DoMAERT) kilichofanyika  Jijini Dodoma.

Amesema uwepo wa timu hiyo pia itasaidia kuunganisha nguvu kwa wadau waliopo ndani ya Mkoa na kuweza kutumia rasilimali zilizopo kuhakikisha maafa yanakabiliwa na wananchi kuwa katika mazingira salama.

“Nchi yetu imekuwa ikipata maafa mara kwa mara ambayo uratibu wake unahitaji kila Mkoa kuwa na Timu Mtambuka ya Wataalam ya Kukabiliana wa Maafa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi ya Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na kanuni zake hivyo uundwaji wa timu hizo ni muhimu kwa usalama wa wananchi na mali zao,” Amesema Meja Jenerali Mbuge.

Pia Mkurugenzi huyo  amewasisitiza  washiriki kupitia kikao kazi hicho kuhakikisha kila mmoja  kwa nafasi yake anafahamu jukumu lake na  kulitekeleza kikamilifu pamoja na  tayari kwa ajili ya kukabiliana na maafa ndani ya Mkoa.

Katika hatua nyingine ameeleza Meja Jenerali Mbuge kwamba Idara ya Menejimeti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu  imeendelea kuchukua hatua za kupunguza madhara kwa kuhakikisha usimamizi na uratibu wa maafa na huduma za dharura zinatolewa kwa wakati kwa kuzingatia mipango, miongozo na mikakati ya kitaifa na kisekta.

“Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 inaratibu na kusimamia masuala ya maafa nchini,”Amebainisha Mkurugenzi huyo.

Aidha Mkurugenzi huyo akawahimiza wananchi kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha malengo ya mapambano dhidi ya maafa yanafaikiwa kama iliyokusudiwa.