NDAKI AVUNJA UKIMYA KUHUSU ENEO LA CHIBE

April 14, 2022

 



Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akiwaeleza wawakilishi wa wananchi wa vijiji vinavyozunguka lililokuwa eneo la kupumzishia mifugo la Chibe lililopo mkoani Shinyanga sababu za kuwaondoa kwenye eneo hilo muda mfupi baada ya kuwasili hapo leo (14.04.2022).
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema (kulia) akiteta jambo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki muda mfupi kabla ya Mhe. Ndaki kuanza ziara ya ukaguzi wa shughuli mbalimbali zinazohusu  sekta ya Mifugo mkoani humo leo (14.04.2022).Mkaguzi Mkuu wa Nyama kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Bw. Ernest Nigo (wa pili kutoka kushoto) akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) namna moja ya mitambo ya kusindika nyama iliyopo kwenye Machinjio ya Manispaa hiyo inavyofanya kazi  muda mfupi baada ya Mhe. Ndaki kufika Machinjioni hapo leo (14.04.2022). Kushoto ni Meneja wa Shamba la Mifugo la Mabuki lililopo mkoani Mwanza, Bi. Lynn Andey.Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akitoa maelekezo ya namna ya kutumia lililokuwa eneo la kupumzishia Mifugo la Chibe lililopo Mkoani Shinyanga  kwa msimamizi wa eneo hilo ambaye pia ni Meneja wa Shamba la Mifugo la Mabuki lililopo Mwanza Bi. Lynn Andey (kulia)  leo (14.04.2022).

 
Sasa kutumika kuzalishia na kunenepeshea mifugo

Baada ya sintofahamu ya muda mrefu  kuhusu hatma ya matumizi ya zaidi ya ekari 5000 za eneo  lililokuwa likitumika kupumzishia mifugo “holding ground”  la Chibe lililopo mkoani Shinyanga  , Hatimaye Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameamuru wananchi  wote wanaofanya shughuli mbalimbali za kibinadamu kwenye eneo  hilo kuondoka ifikapo Agosti 30  mwaka huu.

Mhe. Ndaki ameyasema hayo leo (14.04.2022) mara baada ya kufika na kukagua eneo hilo ambapo amewataka wananchi wanaolitumia  kwa shughuli za kilimo kuhakikisha wameondoka mara baada ya mavuno ya mazao yao ambayo kwa wakazi wa mkoa wa Shinyanga huwa ni  kati ya mwezi Aprili hadi Agosti.

“Kwanza ni lazima mfahamu kuwa hili ni eneo la Serikali na mnaishi humo kimakosa na naona tayari mmelima aina mbalimbali za mazao tena bora mngeishia kulima tu, mmeamua kujenga na makazi kabisa, sasa serikali tunataka kulitumia na kwa kuwa hatutaki muone kama mmenyang’anywa mazao yenu ninawapa mpaka mwezi wa 8 muwe mmeshavuna na kuondoa mazao yenu” Amesema Mhe. Ndaki.

Aidha Mhe. Ndaki amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga kufanya operesheni ya kuwaondoa  watu wote ambao watakuwa hawajaondoka kwenye eneo hilo baada ya muda uliowekwa ili Serikali kupitia Wizara yake iweze kuanza kulitumia  kwa ajili ya kuzalisha na kunenepeshea ng’ombe na mbuzi wa nyama watakaouzwa kwenye viwanda  vilivyopo hapa nchini.

“Tunataka kuendelea kuongeza mauzo yetu nje ya nchi hivyo mbali na Serikali kulitumia eneo hili kwa ajili ya kuongeza tija kwenye mifugo yetu hivyo tutawakaribisha pia wafanyabiashara binafsi na vikundi vya ushirika kuleta mifugo yao hapa kwa ajili ya kuiongezea thamani na kuiuza kwenye viwanda vyetu ambavyo vipo kama vitano hivi lakini vyote vinafanya kazi chini ya uwezo wake kwa kukosa malighafi” Ameongeza Ndaki.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi na  wananchi wa vijiji vinavyozunguka  eneo hilo,Mwenyekiti wa Kijiji cha Chibe ambacho ni moja ya vijiji vinavyotumia shamba hilo Bw.  Masalu Malale amekiri wao kuvamia  eneo hilo ambapo alibainisha kuwa yeye na wananchi wake wataondoka kwa hiyari ndani ya muda waliopewa kwa sababu uwepo wao hapo ulitokana na eneo hilo kutotumiwa na Serikali  kwa shughuli yoyote ya kiuchumi.

“Kwenye kijiji changu kuna kaya kama 10 ndani eneo hili na baada ya kutambua kuwa tupo kwenye eneo la Serikali tulikubaliana kuwa pindi ikitaka kutumia eneo hili tutaondoka bila tatizo lolote” Alisema Masalu.

Mbali na  kufika kwenye eneo hilo, Mhe. Ndaki alipata fursa ya kutembelea machinjio ya Manispaa ya Shinyanga ambapo baada ya kukagua namna shughuli zinavyofanyika kwenye machinjio hiyo aliuagiza uongozi wa Manispaa hiyo kuwahamasisha wafugaji waliopo Mkoani Shinyanga kwenda kuchinja mifugo yao kwenye machinjio hiyo ili kuiongezea uwezo wake wa kufanya kazi badala ya hivi sasa ambapo  jumla ya mifugo 36 pekee inachinjwa kwa siku badala ya mifugo 500 ambayo ingekidhi uwezo uliosimikwa wa machinjio hiyo.

“Tutashirikiana kutafuta wawekezaji watakaokuwa na uhakika wa kupata ng’ombe na mbuzi wa kutosha na masoko ya mifugo hiyo japo mmeniambia mmeshaanza mazungumzo na mtu mwenye nia ya kuwekeza hapa ila naomba muwe makini sana kwa sababu pale Machinjio ya Dodoma tulipata mwekezaji ambaye ametuletea ugomvi mkubwa sana kiasi cha kuifanya machinjio yetu kutofanya kazi yake kwa ufanisi” Amesema Ndaki.

Mapema kabla ya kuanza ziara yake Mhe. Ndaki alifika kumsalimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema ambapo alipokea taarifa ya mkoa huo inayohusu  utekelezaji wa shughuli mbalimbali za sekta za Mifugo na Uvuvi.

MWISHO


MELI ZA MAGARI KUTUA BANDARI YA TANGA KUANZIA MWEZI MEI

April 14, 2022

 



Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Mrisha Masoud akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya wadau wa Bandari ya Tanga walipotembelea bandarini baada ya kumalizika kwa kikao chao na mamlaka hiyo.


Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Mrisha Masoud akizungumza wakati wa wadau wa Bandari ya Tanga kilichofanyika kwenye Hotel ya Tanga Beach kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa masoko na Uhusiano Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania Makao Makuu Nikodemas Mushi


Kaimu Mkurugenzi wa masoko na Uhusiano Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania Makao Makuu Nikodemas Mushi akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ziara na kikao cha wadau wa Bandari ya Tanga

AFISA Mfawidhi wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC )Mkoani Tanga Captain Christopher Shalua akizungumza jambo wakati wa kikao cha wadau wa Bandari

Wadau wa kikao hicho wakifuatilia matukio mbalimbali

NA OSCAR ASSENGA,TANGA.

BANDARI ya Tanga inatarajiwa kuanza kupokea Meli za Magari ifikapo Mwezi Mei mwaka huu ambayo yatakuwa yakipelekwa kuhifadhiwa eneo la Mwambani Jijini Tanga .

Hatua hiyo inatajwa kwamba itafungua fursa mpya za kiuchumi kwenye Bandari ambayo kwa sasa inafanyiwa maboresho makubwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma zake.

Hayo yalisemwa na Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Mrisha Masoud wakati wa ziara ya wadau wa Bandari ya Tanga walipotembelea bandarini baada ya kumalizika kwa kikao chao na mamlaka hiyo.

Meneja Mrisha alisema eneo la mwambani lina ukubwa wa hekta 176 sasa kama walivyosema wanatarajia kuhudumia shehena kubwa kutoka 750,000 mpaka kufikia Milioni 3000,000 hivyo mzigo utakuwa ni mwingi.

Alisema kutokana na hilo wamependelea eneo hilo watalitumia kufanya shughuli za nyengine ikiwemo kupakilia mizigo kwenye makontena na kuweka kontena tupu na shughuli zinazoambatana na shughuli za kibandari

Hata hivyo aliwaeleza wadau hao kuhusu maboresho ya Bandari ya Tanga ikiwemo jinsi mradi wa maboresho ulivyo mpaka sasa awamu zote tatu ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni kuongeza kina kutoka mita tatu mpaka mita 13 kwenye mlango bahari,sehemu ya kujeuzia meli na vifaa ambapo iligharimu Bilioni 172.3.

Alisema pia wameona maboresho ya base mbili zenye urefu mita 450 zilizogharimu Bilioni 256.8 na wameona ahadi iliyolewa na mkandarasi ambapo mpaka mwezi Mei watakabidhiwa kipande cha mita 150 na itakapofika octoba wakabidhi mita zote 450.

Hata hivyo alisema kwamba hoja ambazo zimewasilishwa na wadau kwenye kkao hivho wamezichukua na kwenda kuzifanyia kazi na wao wametusikiliza kuwaeleza namna maboresho makubwa yaliyofanyika na kuhaidi kuitumia kwa ajili ya kupitisha shehena zao.

Awali akzingumza mara baada ya ziara ya wadau hao kwenye Bandari hiyo kushuhudia maboresho makubwa yaliyofanyika Kaimu Mkurugenzi wa masoko na Uhusiano Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania Makao Makuu Nikodemas Mushi alisema mkutano huo ulikuwa na nia ya kukutana na wadau wanaohudumiwa na Bandari ya Tanga ambayo inayohudumia mikoa ya kanda ya kaskazini ikiwemo nchi Jirani Rwanda.

Alisema kupitia mkutano huo wanaamini watafungua ukurasa mpaya wa kiboshara na lengo lao ni kuondoa nafasi ya maswali na hoja na changamoto mbalimbali ambazo hazijaweza kutoka upande mmoja kwenda mwengine.

Kaimu Mkurugenzi huyo wa Masoko na Uhusiano alisema wadau wametoa maoni huku akieleza kwamba Meneja wa Tanga na timu yake wamesikia na wamejipanga tayari kuanza kuzifanyia kazimara moja,.

Alisema na suala ambalo linawahusu makao makuu watalibeba na kulipeleka huku ili yaweze kufanyiwa maamuzi na huo ni mkakati wa kimasoko

Mwisho.