SIKU YA KUMBUKUMBU YA MASHUJAA ILIYOFANYIKA KIMKOA KATIKA BUSTANI ZA UHURU PARK JIJINI TANGA

July 25, 2013

Na Oscar Assenga,Tanga.
Watanzania wameshauriwa kuacha  tamaa zakupenda  kujilimbikizia mali pamoja na kung’ang’ania madaraka kwani kwa kufanya hivyo kunachangia kasi ya uvunjifu wa amani pamoja na nchi kukosa Baraka za Mungu.

Hayo yameeleza na Askari mstaafu aliyepigana vita ya pili ya dunia Francis Bernado wakati akiongea na waandishi wa habari katika sherehe za kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya mashujaa zilizofanyika kimkoa katika bustani za uhuru park Jijini Tanga na kuhudhuriwa na mkuu wa wilaya ya Tanga,Halima Dendego pamoja na viongozi wengine wa serikali.

Alisema machafuko yalianza kujitokeza kwa sasa ni matokeo ya baadhi ya viongozi kutaka madaraka au kung’ang’ania nafasi Fulani badala ya kuwa na uzalendo wa kuwatumikia wananchi pamoja na taifa kwa ujumla ili kuharakisha maendeleo.

“Tamaa ya kutaka kumiliki vitu vikubwa peke yako ndio inayosababisha nchi kwa sasa kusikia sehemu Fulani kuna machafuko ,watu wamemsahau Mungu na kujifanyia maamuzi bila kufikiri kama anachokifanya kitaleta manufaa gani kwa jamii”alisema Bernado.

Hata hivyo aliiomba serikali kuwa kumbuka askari wastaafu kwa kuwaongezea mafao yao kwani wengi wao wanaishi maisha magumu baada ya kustaafu huku wakiwa wamelitumikia taifa kwa moyo wa upendo na kujituma .

“Naomba serikali ituangalie sisi askari tulioiletea heshima nchi hii kwani kwa sasa inaonekana kama thamani yetu ni ndogo kwa serikali  kutoka na kututelekeza na msaada pekee tunapata kwa familia zetu tu”alisema
Askari huyo mstaafu.
MKUU wa wilaya ya Tanga,Halima Dendego akikabidhiwa ngao na sime na askari wa JWT kwenye sherehe za siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa zilizofanyika Jijini Tanga.
DC Dendego akiweka Sime kwenye mnara wa kijiji cha Miaka 21 ikiwa ni kumbukumbu ya siku ya Mashujaa.
Askari wa Mgambo wakiwa wakijiandaa na gwaride leo.


Askari Mgambo wakiwa wamejipanga tayari kwa ajili ya kukaguliwa na Mkuu wa wilaya ya Tanga,Halima Dendego.


VIONGOZI mbalimbali wakifuatilia maadhimisho hayo wa kwanza mebel kwenye shati la kijani na koti jeusi ni Meya wa Jiji la Tanga,Omari Guledi wanaofuatia kwa nyuma wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Tanga,Abdi Makange,anayefuatia ni Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga,Lucia Mwiru na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga,Kassim Mbuguni.

KOCHA URA AIPIGIA SALUTI COASTAL UNION.

July 25, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.
KOCHA Mkuu wa timu ya URA ya Uganda,Sadik Wassa amesema timu ya Coastal Union ni miongoni mwa timu nzuri hapa nchini ambayo ikiwa na malengo mazuri itatwaa ubingwa wa soka Tanzania kutokana na kusheheni wachezaji wazuri wenye viwango.

Wassa alitoa kauli hiyo juzi mara baada ya kumalizika kwa mechi kati yao na Coastal Union ya Tanga ambapo timu hiyo ilikubali kichapo cha bao 1-0 ambalo liliweka wavuni na Keneth Masumbuko ambaye alimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Uhuru Selemani ambaye aliwatoka mabeki wa URA na kutoa pasi kwa mfungaji huyo kwenye dakika ya 70

Alisema endapo timu hiyo itaendelea kucheza kambumbu kama ilivyokuwa (leo)juzi basi upo uwezekano wa kuja kuwa tishio siku zijazo kwani mpira walioucheza ulikuwa mzuri sana huku akitolea visingizio kuwa kilichomfanya kupoteza mechi hiyo ni kutokana na uchovu wa safari kwa wachezaji wake.

Mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa ulichezwa uwanja wa Mkwakwani mjini hapa na kuhudhuriwa na wapenzi na mashabiki mbalimbali wa soka kutoka wilaya zote za Mkoa wa Tanga.

Mchezo huo ulikuwa na kasi ya vuta ni kuvute ambapo mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyokuwa imeona lango la mwenzake,kipindi cha pili timu zote ziliingia uwanja hapo zikiwa na hari na nguvu ya kutaka kuibuka na ushindi.

Kipindi cha pili Coastal Union walifanya mabadiliko yaliyoweza kuzaa matunda kwa kuwatoa Daniel Lyanga ambaye nafasi yake ilichukuliwa Selamani Kassim Selembe kwenye dakika ya 54 kuingia kwa mchezaji huyo kuliongeza nguvu ya mashambulizi na kuweza kufanikiwa kucheza nusu uwanja.

Wachezaji wengine walioingia kipindi cha pili na kuongeza kasi ya mashambulizi yaliyofanikiwa kudhaa matunda ni Abdi Banda aliyechukua nafasi ya Othumani Tamim dakika 55 huku dakika moja baadae akatoka Hamadi Juma na kuingia Mbwana Kibacha mabadiliko hayoa yaliweza kuleta mafanikio makubwa hasa kwenye kikosi hicho ambacho kinajiandaa na Ligi kuu Tanzania bara.

Wakionekana kucheza kwa kujipanga na kujituma ,Coastal Union waliweza kufanya mashambulio ya mara kwa mara langoni mwa URA huku wachezaji wake wakipiga mashuti yaliyokuwa yakiupanguliwa na mlinda mlando wa URA Bwete Brian.

Kutokana na mashambulio hayo Coastal Union waliweza nao kujipanga na kuweza kuthibiti vizuri safu yao ya ulinzi kwa kuwa makini na wachezaji wa URA hali ambayo iliwapa wakati mgumu kufika langoni mwa Coastal Union ambapo katika dakika ya 83 Coastal Union walifanya mabadiliko ya kumtoa Keneth Masumbuko na kumuingiza Pius Kisambale.

Huku URA walifanya mabadiko kwenye dakika ya 84 wakimtoaWalulya Derrick na kumuingiza Lugya Ronald  ambapo licha ya kucheza vema lakini walishindwa kubadilisha matokeo kwenye mechi hiyo ambayo ilikuwa na upinzani mkubwa kwa timu zote mbili.

Wachezaji walioweza kuwakonga nyoyo vilivyo mashabiki wa Coastal Union ya Tanga ni Uhuru Selemani ambaye alikuwa mwiba kwa wachezaji wa Uganda huku mashabiki wa soka waliojitokeza kwenye mechi hiyo wakimshangilia vilivyo kila alipokuwa akigusa mpira,huku wachezaji wengine akiwemo Juma Nyoso,Haruna Moshi "Boban"nao pia waliweza kutii kiu ya mashabiki kwa kucheza vema kwenye nafasi yake.

Kikosi cha Coastal Union leo kiliwakilishwa na mlinda mlango Shaban Kado,Hamad Juma,Othuman Tamim,Markus Ndehele,Juma Said "Nyoso"Jerry Santos,Uhuru Seleman,Crispian Odula,Daniel Lyanga,Haruna Moshi Boban na Keneth Masumbuko.

Kwa upande wa URA waliwakilishwa na Bwete Brian,Walulya Derrick,Sekijo Samweli,Munaaba Allan,Docca Musa,Agaba Oscar,Nkugwe Elkamack,Feri Ally,Ngama Emanuel,Lutimba Yayo,Kasibante James,Mugabi Yasin,Ganya Willy na Lugya  Ronald.

Mwisho.

TAIFA STARS YATUA UGANDA KUIVAA THE CRANES

July 25, 2013
Na Boniface Wambura,Uganda.
Taifa Stars imewasili salama hapa Kampala tayari kwa mechi ya marudiano ya mchujo dhidi ya Uganda (The Cranes) kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Stars ambayo iliwasili ikitokea jijini Mwanza ilipokuwa imepiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakwenda Afrika Kusini mwakani imefikia hoteli ya Mt. Zion iliyoko eneo la Kisseka katikati ya Jiji la Kampala.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Kim Poulsen ameridhishwa na kiwango cha hoteli hiyo, kwani ndiyo ambayo timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ilifikia Novemba mwaka jana ilipokuja Kampala kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Stars ambayo ilitiwa chachu na Rais Jakaya Kikwete alipokutana nayo Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati ikiondoka kuja Kampala, na kuitakia kila la kheri itafanya mazoezi yake ya mwisho kesho (Julai 26 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kujiandaa kwa mechi ya Jumamosi.

Kocha Kim amesema ingawa mechi hiyo ni ngumu, lakini kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwani wachezaji wako wako vizuri na ari kwa ajili ya mechi iko juu.

Wachezaji wote wako katika hali nzuri, isipokuwa Khamis Mcha aliyekuwa na maumivu ya goti, lakini kwa mujibu wa madaktari wa timu anaendelea vizuri kwani tayari wanampa mazoezi mepesi.

Kikosi cha kamili cha Stars ilichoko hapa kinaundwa na makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.

Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.

Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari siku ya Jumatatu (Julai 29 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
+256 793910742
Kampala