DIASPORA TUNZENI HESHIMA YA TANZANIA – MAJALIWA

July 31, 2023




 *Awataka walitetee Taifa lao, watangaze fursa zilizopo nyumbani

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanadiaspora wa Tanzania wazingatie sheria za nchi wanazoishi ili waendelee kutunza heshima ya nchi yao.

Ametoa wito huo wakati akizungumza na Watanzania waishio St. Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi.

“Baadhi yenu mko hapa mnatafuta fursa, na wengine wengi wako hapa kwa masomo. Zingatieni sheria za nchi hii, tunzeni heshima ya Tanzania. Teteeni Taifa la Tanzania, zungumzieni fursa zilizopo nyumbani,” alisema Waziri Mkuu

Akisisitiza umuhimu wa kukitangaza Kiswahili, Waziri Mkuu alisema: “Kiswahili kiendelee kutangazwa kwa bidii kwani Kiswahili ni fursa na Kiswahili ni ajira. Tukitangaze Kiswahili na tushike nafasi za kutangaza lugha yetu kwa kasi kwa sababu tuna historia ya muda mrefu na Urusi ambao wamekuwa wakitumia lugha hii,” alisema.

Alisema katika baadhi ya vikao vyake na wawekezaji wa Kirusi, hakupata shida ya mkalimani kwa sababu walikuwa na mtu wao ambaye anatafsiri moja kwa moja kutoka Kirusi kwenda Kiswahili na Kiswahili kwenda Kirusi. “Lakini na sisi ubalozini kwetu tuna Afisa Uchumi ambaye alitusaidia kutafsiri Kiswahili kwenda Kirusi kwenye baadhi ya vikao. Tena aliongea kwa ufasaha zaidi. Tusiache fursa hii itupite,” aliwasisitiza.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwapa picha halisi ya maendeleo na kiuchumi yanayofanyika nchini chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zikiwemo sekta za elimu, afya, miundombinu, utalii, kilimo, maji na akawahakikishia kwamba Tanzania iko salama, wao waweke bidii kwenye masomo yao.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kikao hicho, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk alisema mbali na kazi ya kudumisha mahusiano ya kirafiki na kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi nyingine, Serikali imeendelea kuratibu masuala ya Diaspora.

“Hivi sasa, wizara imekamilisha Mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, ambayo inajumuisha masuala ya Diaspora. Ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa takwimu sahihi za idadi ya Diaspora wetu kote ulimwenguni, tarehe 22 Mei, 2023 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax alizindua rasmi Mfumo wa Kuwasajili Diaspora Kidigitali. Mfumo huo, uliotengenezwa na Wataalam Wazawa utasaidia kurahisisha usajili wa Diaspora wenye asili ya Tanzania pamoja na wanafunzi.”

“Ni dhahiri kuwa Diaspora waliopo katika eneo zima la uwakilishi wa ubalozi wetu hapa Urusi, sasa hawatalazimika tena kusafiri kwenda ubalozini Moscow ili kujisajili. Napenda kutumia fursa hii kuwahamasisha Diaspora wote wajisajili kwa wingi.”

Alisema ana imani kuwa takwimu zitakazopatikana kupitia mfumo huo, zitaiwezesha Serikali kupanga na kuandaa kwa usahihi mahitaji yanayohitajika ili kuwapatia Diaspora huduma wanazozihitaji, ikiwemo huduma za kibenki, Hati za Kusafiria, Vitambulisho vya Taifa na vitambulisho rasmi vya utambuzi wa diaspora wakati wa utekelezaji wa Hadhi Maalum.

“Hadi sasa, mfumo huu umetuwezesha kufahamu kuwa tunao diaspora wenye asili ya Tanzania katika nchi za Vanuatu, Albania, Antigua na Barbuda, Kazakhstan, Azerbaijan pamoja na America Samoa ambazo nchi yetu haina uwakilishi wa Kibalozi,” alisema.

Akisoma risala yao, Mwenyekiti wa Diaspora katika Shirikisho la Urusi na Nchi huru za Jumuiya ya Madola (CIS), Pascal Gura alisema jumuiya yao (TADRU- CIS), ina wanachama zaidi ya 200 walioko sehemu tofauti za nchi hiyo.

Alisema kwa sasa wanadiaspora hao wanakabiliwa na changamoto ya mifumo ya kifedha kutokana na vikwazo vya kiuchumi. “Changamoto hii inatokana na Shirikisho la Urusi kuondolewa katika mfumo wa uhamishaji fedha (Swift) ambao unatumiwa na mabenki kupitia kadi za ‘‘Visa na Master card’’.

“Kwa sasa kadi pekee zinazokubali katika baadhi ya mabenki katika Shirikisho la Urusi ni kadi zinazotumia mfumo wa Union Pay. Hivyo, tunaomba benki za Kitanzania zipanue wigo kwa kutoa kadi zenye mfumo wa Union Pay kwa kuwa itaimarisha pia fursa za kibiashara kati ya Tanzania na Urusi,” alisema.

Wanadiaspora hao pia walimkabidhi Waziri Mkuu tuzo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutambua juhudi zake katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Tabia Maulid Mwita, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk, Naibu wa Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ, Ally Suleiman Ameir, Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Balozi Fredrick Kibuta na watendaji wengine wa Serikali.

MWENYEKITI WA CCM TANGA COMREDE RAJABU AKERWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI WENYE THAMANI YA ZAIDI YA BILIONI 3 MKINGA

July 31, 2023

 







NA MASHAKA MHANDO, Mkinga 


MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga Rajabu Abdurahman amekerwa na utekelezaji wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh. Bil 3.155 na amemuagiza Waziri wa Maji na Mkuu wa Mkoa Tanga kuutembelea mradi huo na kuchukua hatua za kinidhamu ikiwa kutabainika ubadhilifu wowote .


Mradi huo unaosimamiwa na wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilayani humo(RUWASA) ambao umeonekana hauna ufanisi wala tija kwa wananchi zaidi elfu kumi wanaokabiliwa na adha ya maji Wilayani humo licha ya serikali kutoa fedha nyingi.


Mwenyekiti huyo alitoa maagizo hayo jana, akiwa Wilayani Mkinga katika mwendekezo wa ziara yake iliyokuwa na lengo la kukiimarisha chama hicho pamoja na kukagua miradi ya maendeleo na kusema watendaji watakaobainika kufanya ubadhirifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo sheria kali zitachukuliwa dhidi yao.


"Lazima tunyooshane mapema hasa kwa wale watumishi wazembe na chama chetu ndio kinachopata taabu wakati wa kampeni sasa sisi tunaanza kuchukua hatua kabla ya kukutana na maswali toka kwa wananchi" alisema Mwenyekiti huyo na kuongeza


 "natoa wito wataalamu wote wa serikali mkoani hapa ni vema mkatumia vizuri fedha zinazoletwa na serikali ili changamoto na kero za wananchi zipate majawabu". 


Aidha alisema kitendo kinachofanywa na Mamlaka hiyo ya Maji Wilayani Mkinga cha kujenga Tank la maji na miundombinu yake  kwa wananchi bila ya kuwa na chanzo cha uhakika wa maji ni uchonganishi wa Rais na wananchi wake kwasababu ujenzi huo ungekwenda sambamba na ukarabati wa bwawa.


"Kinachoonekana hapa mradi wa tank utakamikika halafu maji ya uhakika hakuna, mwisho wa siku Serikali itamlipa mkandarasi pesa nyingi huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma hiyo ilhali wameona tenki likiwa limejengwa," alisema.

 

Alisema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akihangaika mchana na usiku kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo itakayowasaidia wananchi kuondokana na kero mbalimbali jambo la kusikitisha watendaji waliopewa dhamana hiyo hawatekelezi walichoagizwa.


Alisema hadi sasa mkoa wa Tanga umepokea kiasi cha sh 356,830,194,471 huku pia ikiwa inatarajia mradi mkubwa wa maji ya miji 28 Tanga zikiwa wilaya za Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani ambao utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 181 kwa wilaya hizo.


Meneja wa RUWASA Wilayani Mkinga Thomas Kaijage, alisema bwawa hilo linachangamoto na linahitaji kufanyiwa ukarabati ili liweze kutunza maji ya kutosha yatakayoweza kuhudumia Wananchi hao na kuongeza kuwa wanategemea kupata fedha kwa bajeti ya mwaka 2023/2024.


Kaijage alisema kwa mujibu wa mkataba wa utekelezaji wa mradi huo kazi ya ukarabati wa bwawa hilo zitafanywa na wakala wa uchimbaji wa mabwawa na visima (DDCA) baada ya usanifu kukamilika.


Aidha alisema mradi huo unaojengwa Wilayani humo unakwenda sambamba na ujenzi wa Tank la maji litakaloweza kuhifadhi mita za ujazo 300,vituo 28 vya kuchotea maji,Ofisi ya Chombo Cha watoa huduma ngazi ya jamii(CBWSO),Machujio ya Maji(treatment Plant),uchimbaji na ulazaji wa mabomba na ufukuaji wa mitaro mita 48,000 na ukarabati wa Nyumba ya Pampu(pump house).


Mbunge wa wilaya ya Mkinga Dastan Kitandula alisema Rais ameridhia kata ya Gombero kuboreshewa miundombinu ya usambazaji wa maji na ujenzi wa tank ili kuweza kuwahudumia wananchi wanaokabiliwa na adha ya Maji kwa kipindi kirefu.


Aidha alisema upo mradi wa maboresho ya Bwawa la Gombero ambalo ndio chanzo kikuu cha maji utakaogharimu Shs Bil 4,na mradi mkubwa utakaotoa maji mto Zigi kuelekea Horohoro ambao utagharimu zaidi ya Shs Bil 34 na kuifanya Wilaya hiyo kuondokana na adha hiyo ya maji.


Ziara ya Mwenyekiti huyo itadumu kwa takriban siku 20 ambapo atatembelea Wilaya za Mkinga,Muheza,Korogwe Mji na Korogwe Vijijini na Wilayani Lushoto kama alivyoahidi kuzitembelea Wilaya zote za Mkoa Tanga mara baada ya kuchaguliwa na kushika wadhifa huo.

USIMAMIZI MBOVU WA MIRADI YA MAENDELEO MKINGA WAMSIKITISHA MWENYEKITI WA CCM MKOA WA TANGA

July 31, 2023






 NA MASHAKA MHANDO Mkinga


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga Ustadh Rajab Abrahaman Abdalah amesikitishwa na usimamizi mbovu wa miradi ya maendeleo unaofanywa na halmashauri ya wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.


Mwenyekiti alizungumza hayo jana wakati akikagua kwa nyakati tofauti, ujenzi wa zahanati za vijiji vya Mzingi-Mwagogo iliopo kata ya Parungu-Kasera, zahanati ya kijiji cha Temboni kilichopo kata ya Maramba na shule ya msingi Mwandusi- Mtundani iliopo kata ya Manza.


Akikagua ujenzi wa zahanati ya Mzingi-Mwagogo, ambayo imepakwa rangi kabla ya ujenzi wake kukamilika ikiwa imetumia hadi sasa shilingi milioni 67, alisema miradi hiyo kumekosekana nguvu ya usimamizi na kufanyika matumizi mabaya ya fedha.


Alisema ilani ya CCM inaelekeza kila kijiji kiwe na zahanati lakini viongozi hao kwa miaka kumi wameshindwa kuwaondolea wananchi kero ilidumu miaka mingi na kusababisha akina mama wajawazito kujifungulia njiani wakifuata huduma Vijiji vya jirani.


"Kila aliyepewa dhamana na serikali lazima atimize wajibu wake, msipofanya haya mnakifanya Chama Cha Mapinduzi kipate wakati mgumu inapofika uchaguzi wakati fedha zinaletwa lakini viongozi wanashindwa kuzisimamia, kiukweli chama hakijaridhika na kimesikitishwa na uzembe wa viongozi kushindwa kusimamia fedha hizi," alisema Mwenyekiti.


Mwenyekiti alisema uwamuzi uliotumika kupaka rangi jengo hilo haukuwa sahihi kwasababu huwezi kupaka mafuta kabla ya kuoga ambapo wangetumia fedha hizo kununua milango na madirisha jengo hilo lingeweza kutumika kwa muda mfupi na kuwasaidia wananchi hao.


Halkadhalika pia alikuta matumizi mabaya ya fedha kwenye zahanati ya Matemboni ambayo hadi sasa tayari imetumia kiasi cha shilingi milioni 62 wakibakisha milioni 3 ambazo haziwezi kumaliza ujenzi huo ambao hadi sasa wanajenga zahanati hiyo kwa miaka kumi sasa.


Pia alipofika katika ujenzi wa madarasa matatu ya shule ya msingi Mwandusi-Mtundani alikuta madarasa mawili yamejengwa chini ya kiwango licha ya serikali kuleta fedha nyingi.


Mwenyekiti alisema haikubaliki majengo hayo kujengwa chini ya kiwango ilhali viongozi wapo wanashindwa kusimamia fedha hizo wakati Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akileta fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya huduma za jamii.


Kufuatia hatua Mwenyekiti huyo alitoa maelekezo maelekezo kwa mkuu wa wilaya ya Mkinga Kanali (Mstaafu) Maulid Sulumbu afuatilie miradi hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati ili kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu.


Lakini pia amemtaka mkuu huyo wa wilaya kuhakikisha watu waliochezea fedha katika miradi hiyo wanachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine na Mwenyekiti aliahidi kurudi tena wilayani humo kuona kama miradi hiyo imekamilika na kuanza kazi.


Mbunge wa jimbo hilo Dastan Kitandula alimpa Mwenyekiti huyo salamu za Rais Dkt Samia kwamba wameridhika na kazi anazozifanya hasa kuwaletea fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo suala la maji.


Wananchi mbalimbali waliozungumza na blog hii, wameonesha kurodhishwa na ziara ya Mwenyekiti kupitia na kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa ilani ya CCM.


"Hatujawahi kuwa na Mwenyekiti anayekuja wilayani na kulala huko kwa siku nne, kiukweli kura zetu hazikupotea bure, tunaye Mwenyekiti mwenye uwezo na utashi wa kusimamia kazi za chama.


Mwisho

DC JOKATE AKABIDHI NYUMBA 8 KWA WATOTO WANAOISHI MAZINGIRA HATARISHI

July 31, 2023

 Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, Jokate Mwegelo amekabidhi nyumba nane kwa Watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi zenye thamani ya zaidi ya Tsh. milioni 50.


Nyumba hizo zimejengwa kwa  ufadhili wa pamoja kati ya Kanisa la Anglican Msambiazi pamoja na  KKKT Emao Old Korogwe ikiwa na lengo la kuwanufaisha watoto hao kutoka katika wimbi la umasikini.

DC Jokate amesema “Rai yangu kwa hawa waliopatiwa nyumba hizi nane wasije wakatumia nyumba hizi kwa kuziuza au kupangisha kwanza ifahamike nyumba hizi ni za hawa Watoto kwahiyo Wazazi wanakaa kama Walezi tu wa kuwasaidia kuzishika lakini kwenye zile hati za makabidhiano majina yaliopo ni ya Watoto husika “

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa nyumba hizo Mratibu wa Kituo cha Watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi Anglican Msimbazi Mery Msendekwa amesema kuwa  Kanisa la KKKT EMAO limejenga nyumba nne na Anglican Msambiazi limejenga nyumba nne huku zote zikiwa na thamani ya Tsh. milioni 50.4

Mchungaji na Mlezi wa kituo cha Anglican Msimbazi Canon Jackson Matunga amesema lengo ni kuwawezesha Watoto hao kuishi mazingira mazuri na nyumba hizo ni mali za Watoto na endapo Mtoto atanyanyaswa kupitia nyumba hizo Kanisa litasimama na kuhakikisha watoto hao wanapata haki zao.


HAKUNA UHABA WA DAMU SALAMA UNAOITESA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA TANGA -BOMBO

July 31, 2023


Na Mwandishi Wetu, TANGA.

UONGOZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo umesema hakuna uhaba wa damu kama ilivyoandikwa na mmoja ya gazeti kwamba unaitesa kutokana na uwepo wa jitihada mbalimbali 

Jitihada hizo ni pamoja na kutumia taasisi mbalimbali za kiserikali na kidini kuhamasishaji wa kuchangia kwa hiari jambo ambalo limekuwa likifanyika kwa nyakati tofauti tofauti na limekuwa na mwamko mzuri wa wananchi kuchangia

Pia katika taarifa hiyo iliyotoka kwenye chombo hicho cha habari ilionekana kuwa na mapungufu kwa kukosa mikakati iliyoelezewa wakati wa halfa hiyo.

Akizungumza leo na waandishi wa Habari Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo-Dkt Naima Yusuf alisema kwamba uhaba upo lakini hospitali imeweka mchakato wa upatikanaji wa damu kwa wakati kupitia uchangishaji katika halfa mbalimbali.

 Alisema sio kwamba uhaba wa damu unaitesa hapana bali kuna mpango ambao upo kwa upatikanaji wa damu kwa mwaka na bado wanasisitiza wananchi kujitokeza kuja kuchangia kwa hiari.

 “Sio kwamba uhaba wa damu unaitesa Hospitali ya Rufaa ya Bombo Lakini pia wagonjwa wanapohitaji damu wanapata kwa wakati”Alisema

Awali akizungumza Mkuu wa Idara ya Maabara katika Hospitali hiyo Sinde Mtobu alisema kwamba wastani wa matumizi kwa mwezi ni chupa za damu 500 mpaka 600 na wanakusanya kwa wananchi chupa 300 mpaka 400.

Katika kukabiliana na uhaba huo wakati mwengine kituo cha damu salama kutoka Kanda ya Kaskazini wanapopewa taarifa wanakuwa tayari kusaidia kwa ajili ya kutosheleza mahitaji kwa wakati husika.

 Alisema hivyo wanapungukiwa chupa 200 na sio kila mwezi kuna wakati mwengine wanakuwa na damu nzuri inatosheleza hivyo ni wastani tu huku jitihada ya Taasisi na wadau kwa kuzunguka kwenye Taasisi za Umma kuchangisha damu kwenye shule za Sekondari za Umma na Serikali.

Aidha alisema wananchi wanafika kuchangia damu kwenye kituo chao cha bombo ikiwemo baadhi ya jamii ndugu zikiwemo taasisi za dini,Jai  na Bilali Muslim ambazo wanashirikiana na viongozi wa kisiasa kutafuta njia ya kuweza kuwasaidia kupata damu muda wote.

“Taasisi zipo nyingi Tanga kila taasisi yenye watu kila mwaka mara moja inaweza kutuunga mkono kuchangia damu kwa kutoa kalenda yao nasi tutashirikiana nao kuhakikisha tunakwenda kuendesha zoezi la kuchangia damu”Alisema Mtobu.

Hata hivyo alisema kwamba wanawashukuru Tanga Uwasa kwa kuchangia damu ikiwemo Kanisa la Wasabato na KKKT huku akiendelea kuisa taasisi nyengine kwa niaba ya hospitali zikiwa na matukio mengine zitusaidie ili waweze kuendelea kuwahudumia wagonjwa.