Erick Mashauri aelezea jinsi VAT inavyoathiri biashara utalii, aiomba serikali kupitia tena ongezeko hilo

Erick Mashauri aelezea jinsi VAT inavyoathiri biashara utalii, aiomba serikali kupitia tena ongezeko hilo

September 25, 2016

Kufuatia serikali kupitisha muswada wa ongezeko la VAT kwa watalii ambao wanakuja nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali, MO Blog imepata nafasi ya kufanya mahojiano na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri ili kujua ni kwa kiasi gani ongezeko hilo limeathiri biashara kwa makampuni yanayopeleka watalii mbugani na kwa sekta ya utalii kwa ujumla.

Mashauri alisema kuwa ongezeko la VAT kwa watalii limeathiri kwa kiasi kikubwa biashara zao kwani serikali ilifanya maamuzi ya haraka bila kuangalia athari ambazo zingejitokeza baada ya kupitisha muswada na haikuwashirikisha wao kama wadau wa karibu ambao wanafanya biashara ya kuwahudumia watalii wawapo nchini.

"Ongezeko la VAT ambalo serikali ilifanya limevuruga biashara ya utalii, ilisahau kama wageni hawa huwa wanafanya booking mwezi mmoja kabla ya safari, tukashangaa serikali inapeleka muswada haraka haraka bungeni na kuupitisha bila kuangali athari ambazo zitajitokeza,

"Baada ya kuongeza VAT ilibidi makampuni ya utalii yarudishe pesa kwa watalii na wengine wametaka kupelekana hata mahakamani kwani tayari wameshaingia mikataba alafu anakuja unaanza kumwambia tena inabidi alipie VAT, jambo ambalo nchi kama Kenya tayari wameitoa kwani waliona jinsi inavyoathiri utalii lakini hapa kwetu ndiyo tunaileta," alisema Mashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri akizungumza kuhusu ongezeko la VAT limevyoathiri biashara ya utalii kwa makampuni yanayowahudumia watalii wawapo nchini. (Picha zote zimepigwa na Rabi Hume, MO BLOG)

Mashauri alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kupitia tena muswada huo na kuangali jinsi gani ongezeko la VAT linakavyoathiri biashara ya utalii nchini na ikiwezekana iitoe ili watalii wengi waje nchini na serikali iweze kupata pesa nyingi tofauti na sasa ambapo imeongeza VAT ambayo inachangia watalii kupungua.

"Serikali inasema bora waje watalii wachache lakini wanaolipa VAT, wakija watalii wa VIP au wa kawaida wote wanatoa pesa sawa na kwanza watalii wa VIP ambao wanawataka wao hata hoteli wanazotumia wakiwa hifadhi kama Serengeti sio za watanzania, zinamilikiwa na watu wa nje,

"Nafikiri serikali ipitie tena VAT na tozo inayofanywa na TANAPA kwani zote ni pesa za serikali, iangalie jinsi gani gharama hizo zinatuathiri, hakuna haja ya kuweka gharama kubwa hawa watu hawaondoki na hizo hifadhi, waweke gharama za kawaida ili watalii waje wengi zaidi," alisema Mashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri ameiomba serikali kupitia tena muswada wa VAT ili ikiwezekana itolewe kwani ongezeko hilo linaweza kusababisha idadi ya watalii wanaokuja nchini kupungua kwa kiasi kikubwa.

Aidha Mashauri aliishauri serikali kufanya mabadiliko ya matangazo ambayo imekuwa ikiyatumia kujitangaza kimataifa ya kutumia viwanja vya michezo kuwa njia hiyo haiwezi kusaidia kwa kiasi kikubwa kama inavyotarajia na badala yake itumie vyombo vya usafiri.

"Wanaokwenda mpirani wengi hawapendi utalii, njia rahisi ni kuingia mikataba na makampuni ya mabasi na treni, wakitangaza wale hapa tutawakimbia watalii, wanaingia mikataba mara moja na tangazo linakaa mwaka mzima, hebu fikiria mfano Uingereza kuna mabasi zaidi ya 300, kama tangazo kila siku likionwa na watu milioni moja tu kwa mwaka tutapata watalii wengi," alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri akielezea jinsi watalii wanavyonyang'anywa vinyago wanavyo nunua nchini na kuiomba serikali iliangalie jambo hilo na kuwaruhusu watalii kuondoka na vinyago hivyo kwani wao ndiyo wateja wakubwa wa biashara hiyo.

Pia Mashauri aliiomba serikali kuweka utaratibu wa watalii ambao wanakuja nchini kuruhusiwa kuondoka na vinyago ambavyo wamekuwa wakinunua nchini kwani hizo ndizo zawadi ambazo wanaweza kuzipata nchini na kuwapelekea ndugu zao katika nchi ambazo wametoka.

"Kuna tatizo kubwa la watalii kunyang'anywa vinyago wakifika uwanja wa ndege, hivi wanadhani hawa watalii zawadi gani wanaweza kuipata nchini tofauti na vinyago maana vingine ata kwao vipo, lakini watalii wakifika uwanja wa ndege wafanyakazi wa pale wanavichukua eti hawana kibali cha kuondoka navyo,

"Watalii wanakuwa wanaona nchi yetu hakuna mfumo wa kufanya kazi pamoja maana anayeuza vinyago amepewa leseni ya kuuza na mteja wa hivyo vinyago ni nani kama sio watalii, nadhani iliangalie jambo hilo kwakweli limekuwa likiwakera sana watalii pindi wanapokuwa wanarejea nchi walizotokea," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri akizungumza na waandishi wa habari ambao walimtembelea ofisini kwake mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kuhusu Erick Mashauri amekuwa mmoja wa washindi wa tuzo za Top 100 kupitia kampuni yake ya Travel Partner ikishika nafasi ya 30 kati ya kampuni 100, amekuwa akifanya biashara ya kupeleka watalii katika hifadhi mbalimbali tangu mwaka 2007 na kupitia kampuni yake ametoa ajira rasmi kwa watanzania wasiopungua 90.

Na Rabi Hume, MO BLOG

NANI MKALI WA KUSUKA DAR??? SUKA SUKA YAPIGA HODI KAA CHONJO KAMA WEWE NI MSUSI

September 25, 2016

#SukaSuka ni jukwaa la Times FM ambalo linavumbua wakali wa kusuka Mtaa Kwa Mtaa kila wiki mara 3. Kwa miezi miwili tumekua tukiingia kitaani kusaka wakali ambao wanaweza kusuka mitindo yote kwa speed zaidi ya mwendo kasi. Washindi wanatapa zawadi papo hapo kutoka #DarlingHair kuwanao karibu ili kuwasaidia mbinu na njia za kijasiriamali waweze kufanikiwa katika fani yao ya ususi.
Bila Msusi Dada zetu wasingeringa hapa mjini. Bila Msusi mabrothermen wasingedata kwa watoto wa hapa town! Piga Salute kwa Wasusi Wote.
Kama we ni msusi mkali uwe mwanamke, mwanaume tunakuja kitaani kwako soon kama kawa. jiandae kwa zawadi kibao na kutoboa katika ususi #SukaSuka2016 #SukaSukaNaTimesFM
Akinadada wakikusuka mitindo yote kwa speed zaidi ya mwendokasi.

MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA ANAYO MAMLAKA YA KISHERIA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO NA HOJA ZILIZOWASILISHWA KWAKE NA BAADHI YA WANACHAMA NA VIONGOZI WA CUF

September 25, 2016


UTANGULIZI

Kuna baadhi ya watu wanadai kuwa, Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya chama cha siasa, hivyo msimamo wake juu ya mgogoro wa uongozi wa chama cha CUF ni batili. Napenda kutumia fursa hii kuwafahamisha kuwa, Msajili wa hana mamlaka ya kuingilia uamuzi halali uliofanywa na kikao halali cha chama cha siasa, Lakini, kama uamuzi ni batili na kikao ni batili au uamuzi ni halali umefanywa na kikao batili au uamuzi batili umefanywa na kikao halali, msajili hawezi kuutambua, kwani Sheria ya Vyama vya Siasa inampa Msajili wa Vyama vya Siasa wajibu wa kusimamia utekelezaji wa baadhi ya maamuzi ya chama cha siasa ikiwamo suala la upatikanaji wa viongozi wa kitaifa wa chama cha siasa kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama husika. Ni vyeme ieleweke wazi kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Usajili wa Vyama vya Siasa uamuzi wa kufanya mabadiliko yoyote kwa viongozi wa kitaifa wa chama cha siasa ni lazima upelekwe kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ili atambue mabadiliko hayo.

Hivyo, kuhusu mgogoro wa uongozi katika chama cha CUF uliojitokeza kufuatatia kujiudhuru kwa Profesa Lipumba ni kwamba, malalamiko na hoja zilizowasilishwa kwa Msajiili wa Vyama vya Siasa na baadhi ya viongozi wa CUF ikiwamo Profesa Lipumba zilikuwa za aina tatu, ambazo ni zifuatazo:-

1. Kupinga utaratibu uliotumika kuendesha Mkutano Mkuu wa Taifa wa tarehe 21 Agosti, 2016;
2. Kujiuzulu na kutengua kujiuzulu uenyekiti wa taifa wa CUF; na
3. Kupinga uhalali wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi cha tarehe 28 Agosti, 2016 kilichofanyika Zanzibar na maamuzi yake.

Malalamiko na hoja zote tajwa hapo juu zinahusu hatma ya baadhi ya viongozi wa kitaifa wa chama cha CUF. Viongozi hao ni wafuatao:-

TANROADS NA TBA ZAAGIZWA KUFANYA TATHMINI KWENYE MIUNDOMBINU YA BARABARA NA MAJENGO YA SERIKALI

September 25, 2016

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga  ameuagiza  uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), na Wakala wa Majengo Nchini (TBA), mkoa wa Kagera kufanya tathmini ya kina kwenye miundombinu ya barabara, madaraja na majengo ya Serikali yalioathirika na tetemeko la ardhi.


Eng. Nyamhanga ametoa agizo hilo Mkoani Kagera mara baada ya kukagua athari za tetemeko la ardhi katika barabara za Bukoba- Mtukula, Kyaka-Bugene na jengo la Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Tanzania na Uganda  ambapo amesema ni muhimu kufanya utafiti wa kitaalam katika miundombinu hiyo kabla ya hatua za ukarabati kuanza.

Amesema kufanyika kwa utafiti huo utasaidia kubaini athari nyingine zilizojificha ambazo zimetokana na tetemeko hilo.
“Undeni kikosi kazi cha wataalam maramoja waweze kuchunguza ili kujua sehemu mbalimbali zilizoathirika ili tuweze kuzitengeneza mapema iwezekanvyo”, amesema Eng. Nyamhanga.

Katika hatua nyingine Eng. Nyamhanga amemuagiza Mkandarasi wa Kampuni ya M/S China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) inayojenga barabara ya Kyaka-Bugeni (KM 59.1) kumaliza kipande cha Kilomita mbili katika barabara hiyo ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.

Amesema kuwa kukamilika kwa kipande hicho kutaimarisha hali ya usafiri wa wananchi katika wilaya za Bukoba na Karagwe na hivyo kuhuisha shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera.
Eng. Nyamhanga yupo mkoani Kagera kukagua athari za uharibifu wa miundombinu kufuatia tetemeko la ardhi lililopiga mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza Septemba 10 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu takribani 17, majeruhi zaidi ya 100, uharibifu wa nyumba takribani 800 na miundombinu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga (kushoto) akikagua sehemu ya barabara ya Bukoba-Mtukula ambayo imepata athari kutokana na tetemeko la ardhi lilitokea Mkoani Kagera hivi karibuni. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Kagera Eng. Andrea Kasamwa.

BARABARA ZA ARUSHA KUKAMILIKA MWAKANI

September 25, 2016

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka mkandarasi M/S Hanil Jiangsu J/V anayejenga barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa KM 14.1 na barabara ya mchepuo (Arusha bypass) yenye urefu wa KM 42.4 kuhakikisha barabara hizo zinakamilika ifikapo mwezi Machi na Oktoba mwakani.


Profesa Mbarawa amesema hayo mara baada ya kukagua ujenzi barabara hizo na kujiridhisha na hatua iliyofikiwa kwa barabara zote.

“Meneja hakikisha ujenzi wa barabara hizi unakwenda sambamba na ujenzi wa sehemu ya barabara inayoelekea Ikulu ya mjini Arusha ili kuiunganisha vizuri barabara hiyo kwa kiwango cha lami”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akielekea kukagua kingo za Daraja la Themi linalojengwa katika barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa KM 14.1 jijini Arusha.

Amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Arusha Bw. Gabriel Daqarro kushirikiana na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoani humo kuhakikisha maji yanayopita kwenye madaraja yaliyopanuliwa kufuatia ujenzi unaoendela hayasababishi mafuriko kwenye makazi ya wananchi.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha Eng. Johnny Kalupale amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara mkoani Arusha utakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

“Tumejipanga kuhakikisha barabara ya Sakina-Tengeru na ile ya mchepuo zote zitakamilika kama ilivyopangwa ili kupunguza msongamano hali itakayovutia ongezeko la watalii na hivyo kukuza uchumi wa mkoa wa Arusha”, amesema Eng. Kalupale. Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua uwanja wa ndege wa Arusha na kusisitiza kuwa nia ya Serikali ni kuupanua uwanja huo ambao ni wa nne kwa uingizaji wa mapato nchini ili kuondoa msongamano uliopo sasa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Mkazi Shin Pil Soo wakati akikagua Daraja la Nduruma lenye urefu wa mita 60 linalojengwa katika barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa KM 14.1 jijini Arusha.