CRDB Bank kupeleka wateja wake 24 kushuhudia fainali za kombe la Dunia, Urusi

April 18, 2018


Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja, Tully Esther Mwambapa akionyesha vipeperushi vya kampeni mpya ya Benki hiyo kwa wateja wake, ijulikanayo kama #TwenzetuRussia, itakayowawezesha watumiajiwa kadi za malipo za TemboCard Visa za Benki hiyo kujishindia safari ya kwenda kuangalia mechi za michuano ya kombe la Dunia, zitakazofanyika nchini Urusi kuanzia mwezi Juni mwaka huu.
Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja, Tully Esther Mwambapa akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati akitangaza kampeni mpya ya Benki hiyo kwa wateja wake, ijulikanayo kama #TwenzetuRussia, itakayowawezesha watumiajiwa kadi za malipo za TemboCard Visa za Benki hiyo kujishindia safari ya kwenda kuangalia mechi za michuano ya kombe la Dunia, zitakazofanyika nchini Urusi kuanzia mwezi Juni mwaka huu.

Benki ya CRDB leo imetangaza kuanza rasmi kwa kampeni ijulikanayo kama “Furahia kandanda murua nchini Urusi” #TwenzetuRussia, itakayowawezesha watumiaji wa kadi za malipo za TemboCard Visa za Benki hiyo kujishindia safari ya kwenda kuangalia mechi za michuano ya kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Urusi, kuanzia mwezi Juni mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa Benki hiyo Bi. Tully Esther Mwambapa, alisema kuwa Benki ya CRDB imeanzisha kampeni kwa kushirikiana na kampuni ya Visa International ili kutoa fursa kwa wateja wake kwenda kushuhudia fainali hizo, ambazo huvutia hisia za watu wengi dunuani kote.

“Wateja wetu wenye TemboCardVisa, TemboCardVisa-Electron, TemboCard Visa-Gold, TemboCardVisa- Platinum na TemboCardVisa-Infinite, wakati wa kampeni hii watatakiwa kulipia bidhaa au huduma wanazonunua kwa kutumia TemboCardVisa zao kupitia mashine za malipo (POS) zilizopo sehemu mbalimbali kama kwenye migahawa, maduka, mahospitali, vituo vya mafuta na kwingineko, ili waweze kujishindia zawadi hii kubwa” alisema.

Bi.Mwambapa aliendelea kusema kuwa “iii mteja aweze kushinda, anatakiwa kufanya miamala mingi zaidi kila wiki na kadri mteja anavyolipia zaidi kwa kutumia TemboCardVisa yake, ndivyo anavyojiongezea nafasi kubwa zaidi ya kushinda.

Washindi wa wawili watakaokuwa wamefanya miamala mingi zaidi kila wiki watajishindia safari ya kwenda Urusi ambayo itagharamiwa kila kitu na Benki ya CRDB, ambapo jumla ya tiketi 24 zitatolewa” alisema Bi. Tully Mwambapa.

Bi.Mwambapa aliendelea kusema kuwa pamoja na washindi wawili wa kwanza kujishindia safari hiyo, Benki pia kila wiki itatangaza washindi wengine 10 kupitia vyombo mbalimbali vya habari ambao watajishindia zawadi kemkem ikiwemo luninga zitakazokuwa zimeunganishwa na kulipiwa kinga’muzi cha DSTV, jezi za timu za mataifa mbalimbali, mipira, kofia, fulana na na zawadi zingine nyingi.

Othman Michuzi Editorial Director & Chief Photographer CELL: +255 713 775869 /+255 789 103610 WEB: issamichuzi.blogspot.com mtaakwamtaa.co.tz michuzijr.blogspot.com EMAIL: othmanmichuzi@gmail.com Dar Es Salaam. Tanzania. East Africa.

MPRU YAPATA BOSI MPYA

April 18, 2018


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina(aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati Ndogo ya Kutathmini Utendaji wa Sekta ya Uvuvi katika Ziwa Victoria baada ya kukabidhi taarifa hiyo mjini Dodoma hivi karibuni.Waliokaa kuanzia kushoto Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Bonaventure Baya Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi, Dk Yohana Budeba, aliyesimama kuanzia kushoto John Komakoma Kaimu Meneja wa MPRU.
Na John Mapepele, Dodoma

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina amemteua John David Komakoma kukaimu nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu nchini (MPRU) baada ya kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa awali Dkt. Milali Machumu kutokana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kubaini dosari katika usimamizi wa Kitengo hicho.

Pia Waziri Mpina amevunja Bodi ya Wadhamini ya MPRU iliyokuwa chini ya Uenyekiti wa Profesa John Machiwa ambayo ilikuwa na Wajumbe nane.

Mpina alisema ameamua kuvunja bodi na kumsimamisha Mtendaji huyo kwa mamlaka aliyonayo kulingana na Sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Na 29 ya mwaka 1994.

Aidha Mpina amemwagiza Katibu Mkuu wa Uvuvi kuunda Kamati ya kuchunguza utendaji wa kazi wa Mtendaji wa awali.

Akizungumza mara baada ya uteuzi huo Komakoma ambaye ni mtaalam wa Bailojia ya Baharini amesema atahakikisha kuwa maeneo yote ya bahari yaliyotengwa yanahifadhiwa kikamilifu ili kuleta Mchango mkubwa katika taifa letu.

“Nina imani kwamba maeneo haya ni muhimu sana kwa uhifadhi wa raslimali za bahari na utalii endelevu hivyo hatuna budi kuyasimamia kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo” alisisitiza Komakoma.

Kitengo cha Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu kiliundwa na sheria ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu  Mwaka 1994 ambapo baadhi ya majukumu yake makuu yameanishwa katika sehemu ya VI kifungu cha 10 ambayo ni pamoja na kulinda na kuhifadhi maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa bioanuai pamoja na mifumo ya ikolojia ya baharini na mwambao wa pwani.

Kuhamasisha wananchi kutumia kwa busara raslimali ambazo hazitumiki kabisa au hazitumiki kikamilifu kwa sasa, kusimamia maeneo ya bahari na mwambao wa pwani ili kuwezesha matumizi endelevu ya raslimali na ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa.

Kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi wanashirikishwa katika nyanja zote za upangaji,uendelezaji na usimamizi wa raslimali.

Hadi sasa kuna Hifadhi za Bahari tatu na Maeneo Tengefu 15 hapa nchini katika mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Mtwara.

Kabla ya uteuzi huu Komakoma alikuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi katika Kitengo cha Udhibiti Ubora, Usalama, Viwango na Masoko ya Mazao ya Uvuvi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi.