DC KISARE ASISITIZA TRA KUENDELEA NA MWENDO WA KUKUSANYA KODI BILA VITISHO

September 22, 2023

 

Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mh. Kisare Makori Akiongea na Timu ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu waliofika katika Wilaya yake kwaajili yakutoa elimu ya Kodi kwa  Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kilimanjaro.Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mh. Kisare Makori Akiongea na Timu ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu waliofika katika ofisi zake kwa ajili ya kujitambulisha kabla ya kuanza kwa kwa zoezi la kutoa Elimu ya Kodi ya Mlango kwa mlango kwa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kilimanjaro


Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kisare Makori amesema kuwa anakumbuka kauli ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo amewataka maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi bila vitisho na hilo linajidhihirisha kwa kusema kuwa siku hizi TRA ni rafiki sana na wafanyabiashara na hilo ni jambo jema na lenye kudumisha uzalendo wa ulipaji kodi wa hiari.

Ameyasema hayo mwanzoni mwa wiki katika ofisi yake iyopo Moshi wakati alipotembelewa na maafisa kutoka TRA Makao makuu walipofika katika ofisi yake kwa ajili ya kujitambulisha kabla ya kuanza ya zoezi la Elimu ya kodi Mlango kwa Mlango kwa wafanyabiashara wa Moshi sambamba na kusikiliza changamoto zao ili waweze kuzifanyia kazi.

Makori amesema kuwa anafurahia kuwepo kwa elimu ambayo itawafikia wafanyabiashara moja kwa moja katika maeneo yao ya biashara na kuwataka wafanyabiashara hao kushirikiana na maafisa wa TRA ili kufikia lengo lilokusudiwa.

“Natoa pongezi kwa hatua waliyofikia Maafisa wa TRA ya kukusanya kodi bila Mitulinga kama maagizo ya Mh. Rais yalivosema kwaajili ya faida ya Nchi yetu na maendeleo ya Taifa letu, pia kama tujuavyo Serikali haina biashara yoyote isipokua kodi, hivyo utoaji wa elimu ni hatua kubwa sana na itaongeza “sovereignty” na uwezo wakulipakodi utaongezeka.”

Nae kiongozi wa zoezi hilo, Afisa Mkuu Elimu kwa Walipakodi na Mawasiliano Lydia Shio kutoka TRA Makao Makuu amesema uwepo wa maafisa ni kutoa elimu ya kodi na kusikiliza changamoto zao ambazo hata wao wanashindwa kuzileta katika ofisi zao hivyo wameamua kuwafata katika maeneo yao ili kujua uhalisia wa biashara zao na kuwakumbusha malipo ya kodi kwa hiari.

“Tumekuja kwa lengo la kutoa elimu kwa Walipakodi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Kilimanjaro tukianzia na Wilaya ya Moshi Mjini ili kuwakumbusha walipakodi waweze kujua wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati kwaajili ya kuongeza pato la Taifa, wafanyabiashara wengi wamesema kua huko nyuma walikua wakiwaona maafisa kutoka TRA wanawakimbia na hawajui wanakimbia kwa kosa gani ila kwa sasa hawana haja ya kukimbia maana tukifika wanatusikiliza na kufanya kilichotuleta na wao wanauliza maswali na kuwasilisha changamoto zao kwa ufafanuzi Zaidi ili aweze kulipakodi inavotakiwa”

Mmoja wa wafanyabiashara wa mtumba katika eneo la soko kuu la Memorial Betty Urono ameeleza kuwa yeye anatumia machine ya risiti na inamsaidia sana na angependa kuwaona wafanyabiashara wenzake wanatumia pia ili kulipakodi kwa usahihi na kujenga taifa letu na maendeleo ya nchi.

“mimi natumia machine ya risiti EFD ni nzuri na inasaidia sana katika kutunza kumbukumbu zetu ni nzuri katika bishara yangu, mimi natoa risiti na nawaomba wengine pia watoe risiti kwa faida yao na ya Nchi yetu pia.”

Mkoa wa Kilimanjaro umekua ni moja wapo ya mkoa wenye historia nzuri katika ulipaji na ukusanyaji kodi na kufikia malengo na muendelezo wa gurudumu la kuongeza pato la Taifa na maendeleo kiujumla hii ni kutokana na ushirikiano unaopatikana kutoka kwa wafanyabiashara na taasisi ya TRA ya Mkoa wa Kilimanjaro katika kutimiza malengo ya Serikali yetu katika kuendeleza maendeleo ya Mkoa na Nchi kiujumla.

Benki ya CRDB kuendelea kurahisisha ukusanyaji mapato Hospitali ya KCMC

September 22, 2023

 


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Benki ya CRDB na Hospitali ya Kanda ya KCMC iliyopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, zimeingia makubaliano ya kuendelea kuifanya Benki ya CRDB kuwa mtoaji wa huduma za fedha hasa ukusanyaji mapato hospitalini hapo.

Azma ya Benki ya CRDB siku zote ni kuhakikisha inatoa huduma bora na shindani zinazokidhi mahitaji ya wateja wake ikiamini kuwa huduma bora, za kisasa, jumuishi na rahisi za fedha ni muhimu kwa maendeleo ya taifa. Hivyo, Benki ya CRDB imewekeza rasilimali zake katika ubunifu wa huduma na bidhaa zake, ikiwamo kuanzisha na kuboresha kiendelevu mfumo wa upokeaji na ufanyaji malipo kwa njia za kieletroniki unaotumika kwenye taasisi tofauti ikiwemo hii ya Hospitali ya KCMC.

Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema Hospitali ya KCMC ni moja ya taasisi za mwanzo kuingia ubia na Benki ya CRDB kutumia mfumo huu wa malipo, mwaka 2014. Ubia huu ulienda sambamba na uzinduzi wa kadi maalum ya malipo ya Hospitali ya KCMC iliyopewa jina “TemboCard KCMC.”

Katika mwaka wa kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo hospitalini hapo, zaidi ya shilingi bilioni 4.1 zilikusanywa na mpaka mwaka 2022, makusanyo hayo yameongezeka mara mbili na kufika shilingi bilioni 8.7 kwa mwaka.

“Tangu tulipoingia mkataba na Hospitali ya KCMC kuanza kuutumia mfumo wetu mpaka mwaka jana, tumeiwezesha Hospitali ya KCMC kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 52.8. Hiki ni kiasi kikubwa kukusanywa ndani ya miaka minane na makusanyo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka,” amesema Raballa.

Raballa amesema katika kuimarisha ushirikiano na hospitali na pia ili kusogeza karibu zaidi huduma kwa wateja wake mwaka 2020 Benki ya CRDB ilifungua tawi hospitaini hapo. Tawi hilo linawafaa pia wafanyakazi wa hospitali, wanafunzi wanaojifunza hospitalini hapa, wagonjwa, wafanyabiashra na wananchi kwa ujumla wanaoishi au kupita maeneo ya hospitali.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya KCMC, Profesa Gileard Masenga amesema kabla hawajaanza kutumia mfumo wa Benki ya CRDB, walikuwa wanakusanya mapato kidogo na kuna nyakati walilipwa hata kwa fedha bandia .

“Kama mnavyofahamu uendeshaji wa hospitali ni wa gharama kubwa, hivyo usimamizi wa mapato ni kati ya vipaumbele muhimu vya hospitali yoyote. Ndio maana leo tupo tena hapa kuuhuisha mkataba wetu ili kuendelea kuwa na ufanisi mkubwa katika ukusanyaji wa mapato yetu,” amesema Profesa Masenga.

Awali, mkurugenzi huyo amesema wahasibu walilazimika kukaa na fedha nyingi kwenye ofisi zao jambo lililokuwa linawaweka kwenye hatari ya kuvamiwa hivyo kupoteza mapato ya hospitali ndio maana mwaka 2004 ilikuwa rahisi kwa menejimenti ya hospitali kushawishika kuingia makubaliano na Benki ya CRDB kutumia teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato na kwamba mfumo huu umeondoa makosa ya kibinadamu kwa kiasi kikubwa hivyo kuongeza makusanyo.

Profesa Masenga pia amesema uhusiano wa Benki ya CRDB na Hospitali ya KCMC hauishii kwenye huduma za benki pekee kwani wao ni miongoni mwa wanufaika wa uwekezaji unaofanywa kwa jamii na Benki ya CRDB.

Profesa Masenga amesema Benki ya CRDB imewajengea eneo la mapumziko kwa wagonjwa na wasaidizi wao, na mara kadhaa imewasaidia vifaatiba na kompyuta ili kuboresha utoaji wa huduma hospitalini.

Kutokana na makubaliana haya, sio hospitali pekee itakayonufaika na mfumo huu bali pia wale wote wanaohudumiwa hospitalini hapa. Malipo sasa yatakuwa yanafanyika kutumia ‘control number’ . Hivyo yeyote anayehudumiwa Hospitali ya KCMC hata hitaji kufanya malipo kwa fedha taslimu, hivyo kuweza kufanya malipo kielektroniki.

Mhudumiwa ataweza kulipa kwa kutumia kadi za benki ikiwemo za Visa na MasterCard, pia ataweza kutumia SimBanking, internet banking na pia CRDB wakala. Malipo haya ya kisasa yanamwezesha mfanya malipo yoyote kulipia huduma ya kwake au ya mtu mwingine moja kwa moja hospitalini, akiwa popote alipo, ndani au nje ya nchi ilimradi awe na control number, ulipo tupo!








TMDA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE KATIKA KIPINDI CHA MIONGO MIWILI

TMDA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE KATIKA KIPINDI CHA MIONGO MIWILI

September 22, 2023

 Na Mwandishi Wetu


MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba ( TMDA) imesema imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yake kwa kuhakikisha jamii inalindwa afya zao na inakuwa salama kutokana matumizi ya dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa nyinginezo zinazohusiana na afya.

Akizungumza leo wakati wa Kikao kazi cha Wahariri na Waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Adan Fimbo amesema katika kipindi cha miongo miwili katika usimamizi wa bidhaa za dawa, vifaa tibana na vitendanishi wanajivunia mafanikio makubwa katika kutoa huduma.

Ametaja baadhi ya mafanikio yaliyokiwa katika kipindi cha miaka 20, ni kuanzishwa kwa Mamlaka ya udhibiti, Kukamilisha ujenzi wa upanuzi wa Maabara ya Dar es Salaam, Kubuni, kuanzisha na kutekeleza mradi wa Duka la Dawa Muhimu (DLDM / ADDO)

Pia kuzindua na kuanzisha Ofisi ya Kanda ya Ziwa, jijini Mwanza (sasa Kanda ya Ziwa Mashariki), kukamilisha ujenzi wa Ofisi ya Makao Makuu ya iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa - TFDA (sasa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu TMDA na Kanda ya Mashariki)

Ametaja mafanikio mengine ni kuzindua rasmi jengo la Ofisi ya Makao Makuu ya iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa - TFDA (sasa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu TMDA na Kanda ya Mashariki), kuanzisha, kukidhi na kutekeleza mifumo ya utendaji kazi ya kimataifa ya ISO 1901:2018

Pia kupata tuzo ya kuwa taasisi ya kwanza yenye mifumo bora ya utendaji kazi Serikalini (Best Managed Institution in Tanzania), Maabara ya TMDA kuwa na umahiri unaotambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO Prequlified Laboratory) na Kituo cha umahiri wa usajili dawa barani Afrika

Ametaja pia Maabara ya mafunzo ya umahiri kwa Mamlaka za Udhibiti Dawa barani Afrika, Kuanzisha mifumo ya kielekroniki ya utoaji huduma kwa wateja,Kutoa huduma za udhibiti kwa njia ya kielektroniki (automation of regulatory services)

Fimbo ametaja kuimarika kwa makusanyo hivyo kuchangia asilimia 15 ya mapato yake katika gawio la Serikali na kuwa na ziada ya asilimia 70 kama inavyoekekezwa na Hazina

Mengine ni Kukamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi ya TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki Mwanza na kuanza kutumi, Kuanzisha mazingira wezeshi na rafiki ya ufanyaji biashar nchini kwa bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA

Pia Kufikia Ngazi ya tatu ya Shirika la Afya Duniani - WHO(WHO Maturity L-3) kwa kuwa na mifumo bora ya udhibiti dawa barani Afrika hivyo kuwa taasisi ya kwanza ya udhibiti na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia ngazi hiyo

Aidha Maabara ya TMDA kupata hadhi ya juu ya ngazi ya nne umahiri wa Shirika la Afya D\uniani, Kubadili jina kutoka TFDA kuwa TMDA, Kukamilisha ujenzi wa jengo la Ofisi ya TMDA Kanda ya Kati Dodoma na kuanza kutumika

Pia Mamlaka kupewa jukumu la udhibiti wa bidhaa za tumbaku,kuanzisha mfumo wa kufuatilia utoaji taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa njia ya simu

Mafanikio mengine ni Mamlaka kupata Hati safi kwa miaka 20 mfululizo kutokana na ukaguzi wa hesabu za taasisi kwa ukaguzi unaofanywa na ofisi ya CAG na kutimiza miaka 20 ya taasisi katika kulinda afya ya jamii kwa ufanisi.

Akifafanua pamoja na mafanikio tajwa, Mamlaka inaendelea kuboresha huduma zake kwa kuzingatia maoni ya wateja. mathalan, kwa Mujibu wa utafiti uuliofanywa na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University of Dar es Salaam Business School) wa Desemba 2020 kuhusu wateja kuridhika na huduma zitolewazo na Mamlaka.

Amesema katika halmashauri 28 kwenye mikoa 14 ya Tanzania, ulibaini kuwa asilimia 47 tu ya wananchi ndiyo wanaifahamu TMDA. Ni dhahiri kwamba matokeo haya yanaakisi mabadiliko ya jina la taasisi yaliyofanyika mwaka 2019.

"Hata hivyo, Mamlaka inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kuongeza uelewa wa wananchi kuifahamu Mamlaka.Kwa kuwa upo umuhimu mkubwa wa wadau wote wa TMDA kuifahamu Mamlaka na majukumu yake...

"Wahariri na Waandishi wa Habari wana wajibu mkubwa katika kuhakikisha kuwa Mamlaka inajulikana kwa jamii na Sheria tajwa inasimamiwa kiufanisi, TMDA imekuwa na utaratibu wa kukutana na wadau wake kwa lengo la kuwaelimisha juu ya kazi zake sanjari na majukumu ya kila mdau katika kutekeleza Sheria husika."

Kuhusu suala la uelimishaji jamii limepewa kipaumbele kikubwa na TMDA na ndiyo sababu tumewaita hapa Wahariri walioko mbele yako kwa lengo la kuwashirikisha mafanikio yaliyofikiwa na TMDA ili kujadiliana kwa pamoja namna ya kushirikiana zaidi katika kuhakikisha kuwa soko la Tanzania lina bidhaa zilizo bora, salama na fanisi ili kumlinda mlaji.

Amesema kimsingi, kazi hii sio rahisi na inahitaji ushirikiano wa karibu kati yetu sisi TMDA, waandishi wa habari na wananchi wote kwa ujumla wao.

Ameongeza ni matumaini yao kupitia tasnia ya habari, wataweza kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwapa elimu endelevu ili waweze kufanya maamuzi sahihi wakati wa kuchagua, kununua na kutumia bidhaa zinazodhibitiwa na TMDA kutoka katika soko.

Kuhusu Kikao kazi hicho amesema mada mbalimbali zimewasilishwa katika kikao hiki ambapo ni matarajio yao kuwa baada ya semina hiyo, washiriki waweze kuelewa vyema nini Mamalaka imetekeleza na katika kuhakikisha sheria na majukumu ya TMDA yanatekelezwa katika kulinda afya ya jamii.

Aidha, kupitia hoja zitakazoibuliwa baada ya mada husika kutolewa, tutaainisha kwa pamoja maeneo ya ushirikiano katika kuielimisha zaidi jamii kupitia vyombo vya habari kuhusu masuala yahusuyo udhibiti wa bidhaa za dawa vifaa tiba na vitendanishi kutokana na ukweli usimamizi wa Sheria hautakuwa na mafanikio kama hatutakuwepo na ushirikishwaji wa wadau wetu hususan vyombo vya habari.

"Ni imani yetu kuwa Wahariri na Waandishi hawa wakirudi kwenye maeneo yao ya kazi wataweza kueneza ujumbe watakaopata leo kwa watu wengi zaidi na hivyo kuwezesha jamii kupata elimu, kujilinda na kutumia dawa, vifaa tiba na vitendanishi vilivyosajiliwa au kupitishwa na TMDA."
Mkurugenzi Mkuu wa TMDA Adam Fimbo akizungumza wakati wa Kikao kazi cha Wahariri na Waandishi wa habari kilichofanyika jijini Dar es Salaam

 Baadhi ya Wahariri wa Habari na watendaji wa TMDA wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, albert Chalamila alipokuwa akizungumza katika kikao kazi hicho.

Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Gaudencia Simwanza akitoa neno la ukaribisho kwa Wahariri wa Habari waliohudhuria katika kikao kazi hicho.

  Baadhi ya Wahariri wa Habari na Watendaji wa TMDA katika kikao kazi hicho. 

Picha ya Pamoja. Kaimu Meneja Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Martha Malle, akitoa mada katika kikao kazi hicho kuhusu Sheria na Kanuni mbalimbali za udhibiti, za Mamlaka hiyo.