WASIMAMIZI WA KEMIKALI KANDA YA ZIWA WAPIGWA MSASA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

November 15, 2023

 NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA


MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS),imeandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa matumizi salama ya kemikali,wadau wa biashara na matumizi ya kemikali Kanda ya Ziwa ili kulinda afya za watu na mazingira.

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa MMS,Daniel Ndiyo,akifungua mafunzo hayo kwa wasimamizi wa kemikali Kanda ya Ziwa jijini hapa leo,amesema yanakwenda sambamba na Malengo Endelevu (SDG),ili kufikia maisha mazuri endelevu kwa wote ifikapo 2030.

“Ili kufikia lengo namba 3, juu ya afya njema na salama,suala la kuzuia au kupunguza madhara ya kemikali katika afya na mazingira ni lazima lipewe kipaumbele pia, kufikia lengo namba 6 linalohusu maji safi na salama lazima kuzuia au kupunguza utiririshaji wa kemikali na kemikali hatarishi katika vyanzo vya maji ili kulinda afya na mazingira,”amesema.

Ndiyo amesema malengo hayo yatafikiwa endapo wasimamizi hao wa kemikali watakuwa na elimu sahihi ya matumizi salama watakayoyazingatia katika maeneo ya kazi kuhakikisha usalama katika jamii inayozunguka maeneo hayo inafahamu matumizi,madhara na faida za kemikali.

“Matumizi na faida za kemikali ni nyingi,hazina mbadala kwa maisha ya mwanadamu na tunaona zikitumika katika sekta za afya,viwanda,kilimo,maji na madini,hivyo zisipotumika kwa kufuata utaratibu zina hatarisha afya na mazingira na baadhi ni sumu kali kama Sodium Cyanide na kemikali za kuunguza ngozi (Hydrochloric Acid,Sulphiric Acid, Caustic Soda TDI na Toluene,” amesema.

Ndiyo ameeleza licha ya madhara makubwa ya kemikali hizo bado ni muhimu katika uchumi wa mtu mmoja mmoja,zinatumika katika mchakato wa uchenjuaji na upatikanaji wa dhahabu na kutokana na faida na sifa katika uchumi pia kuzingatia madhara yanayoweza kusababishwa na kemikali zinazotumika katika sekta mbalimbali,Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali Na. 3 ya mwaka 2003 na Kanuni zake zilitungwa ili kulinda afya,wanyama na mazingira.

“Sheria na kanuni imeweka masharti mbalimbali kuwezesha kemikali kuingia nchini,kuhifadhiwa,kusafirishwa na kuzitumia bila kuathiri afya na mazingira,moja ya masharti ya msingi ni kutoa elimu kwa makundi ya wafanyakazi na jamii iliyo katika hali hatarishi kulingana na aina ya kemikali,”amesema.

Ndiyo amesema ili jamii iendelee kujenga uchumi wa nchi ikiwa salama ndiyo sababu mamlaka hiyo inawaelimisha wasimamizi matumizi salama ya kemikali watoe elimu sahihi katika kudhibiti madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yasiyo salama katika maeneo yao ya kazi kwa kuzingatia usalama wa nchi.

Mkurugenzi huyo wa Huduma za Udhibiti ameeleza kuwa inawezekana wanauza ama wanatumia bila kufahamu athari ya kemikali,hivyo wasimamizi wakiwa na uelewa mpana wataisaidia kuwaelimisha wateja ni athari zipi zinaweza kutokea wasipozingatia matumizi salama ya kemikali.

“Kanda ya Ziwa ni maalumu kwa shughuli nyingi za uchimbaji na uchenjuaji wa madini hasa dhahabu,hutumika kemikali hatarishi iliyo hatari kwa watu na mazingira ambapo wadau (wasambazaji na watumiaji) zaidi ya 600 wamesajiliwa kulinganisha na wadau 150 miaka mitatu iliyopita,”amesema na kuongeza;

“Elimu hii itakuwa chachu na itawajengea uelewa wa namna ya kuzuia,kujikinga na kujiokoa endapo kutatokea hatari kemikali hizo wakati wa kuzitumia,mtafikisha elimu kwa makundi mengine kulingana na shughuli mnazozisimamia wakiwemo watumishi wa chini yenu pia,mtakuwa mabalozi wa kuwajengea uwezo wananchi karibu na maeneo yenu kutambua kemikali husika,madhara,kujikinga na njia za kusaidia tatizo likitokea”.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Huduma za Udhibiti wamezuia mapipa yaliyotumika kusafirishia kemikali yasiuzwe mtaani bali katika viwanda vya kuzalisha chuma (nondo)na makasha ya plastiki yauzwe katika viwanda vya kurejereza (Recyclig) bidhaa hiyo,watakaokiuka watawajibika kisheria.

Naye,Mkuu wa Kitengo cha Sheria Maabara ya Mkemia Mkuu, Gilbert Ndeoruo,amesema makasha ya kemikali ynayouzwa holela mtaani yakitumika vibaya wahusika watawajibika kisheria ingawa mengine yapo si ya kemikali zikiwemo za majumbani zinatumika bil shida na zipo taratibu za kufuata.

“Wanaokiuka sheria tunazosimamia,kwanza tunawaelimisha na sheria imetupa nguvu kifungu cha 61 (e),mdau anapokiri tunatoa adhabu (faini) na wanaokataa tunawapeleka mahakamani itoe adhabu ambayo ni sh. milioni 2 hadi 5 kulingana na kosa.Rai yetu wadau wazingatiye sheria bila shuruti,huduma zimesogezwa karibu kanda zote,tunatoa huduma kidijitali kupata leseni na vibali kwa wakati,hakuna mtu kutoa visingizio,”amesema

Kwa upande wa baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Elizabert Chagu wa Buckreef Geita Gold Mine,amesema watumiaji na wauzaji wadogo wa kemikali hawana uelewa wa madhara ya kemikali na kushauri walete watumishi wao wapate elimu waongeze udhibiti.

Kinyogoli Juma wa Prochem Trading Ltd amesema mafunzo hayo yana manufaa makubwa kwa wasimamizi wa kemikali,wamepata uelewa mpana kuwa zisitumike vibaya,hivyo watazingatia sheria za kemikali na matumizi salama na sahihi kuepuka madhara ya kiafya.



SERIKALI YAUPONGEZA MFUKO WA PEPFAR UKITIMIZA MIAKA 20 YA KURUDISHA MATUMAINI YA WENYE VVU NCHINI.

November 15, 2023

 *Zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 6 zatumika


*Mwaka 2022 pekee ikitumia Dola 450 milioni kupambana na maambukizi ya ukimwi nchini


Na Zuhura Rashidi, Iringa


SERIKALI ya Tanzania imeupongeza Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR), kwa jitihada zake katika kuleta matumaini mapya katika mikoa iliyoelemewa na mzigo mkubwa wa maambukizi ya ugonjwa wa HIV na Kifua Kikuu.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi. Halima Dendegu wakati wa ziara ya wawakilishi wa mfuko wa PEPFAR, Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), mashirika yanayotekeleza miradi ya ukimwi pamoja na waandishi wa habari mkoani humo wakitembelea miradi na vituo vinavyotoa huduma za ukimwi ikiwa ni sehemu ya matukio kuadhimisha miaka 20 tokea kuanzishwa kwa mfuko huo.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema Iringa ni mmoja wa mikoa iliyoathiriwa sana na maambuki ya VVU lakini kwa msaada wa PEPFAR chini ya Shirika la USAID imewawezesha kuwa na vituo vya huduma na tiba (CTC) 261 kutoka vinane vilivyokuwepo awali, huku 136 vikiendeshwa na USAID vilivyosaidia kuleta mabadiliko chanya katika utoaji elimu na huduma bora kwa kutumia vifaa vilivyoboreshwa na wahudumu wa afya wenye elimu na ujuzi katika utoaji wa huduma bora za afya.

“Tafadhali pokeeni pongezi za dhati kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani, tunashukuru sana kwa misaada tunayoipokea kwani tunatarajia kushuka kwa maambukizi mapya kwa magonjwa ya ukimwi, kifua kikuu huku tukiendelea kupunguza unyanyapaa kwa wenye VVU.

Awali akizungumza mafanikio miradi ya PEPFAR inayosimamiwa na USAID, Mkurugenzi Mkazi wa shirika hilo nchini, Bwana Craig Hart alisema tokea mwaka 2003 serikali ya Marekali imetoa zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 6 ikiwa ni pamoja na Dola 450 Milioni kwa mwaka 2022 pekee katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi chini Tanzania.

“Mwaka 2003 ni watanzania 1000 tu waliokuwa wakipokea dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV), leo wakati tukiadhimisha miaka 20 ya PEPFAR zaidi ya watanzania milioni 1.5 wananufaika na mpango huu wa tiba wa kuokoa maisha yao ikiwa ni asilimia 98 ya watu wanaoishi ya VVU.

“Misaada yetu kwa watu wa Tanzania ni uwekezaji wa baadae, kwani kufikia mwaka 2050 robo ya watu wote duniani wataishi Afrika, nchini Tanzania theluthi mbili ya idadi ya watu wakiwa ni vijana chini ya umri wa miaka 25, hivyo kufanya uwekezaji katika kizazi kijacho kuwa ni jambo muhimu mno na lisiloepukika”, anasema Bwana Hart.

Naye Mratibu wa Mfuko wa PEPFAR nchini Bi. Jessica Greene alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa kugusia maeneo manne ambayo mfuko huo umekuwa ukiyapa kipaumbele akiyataja kama; tiba, utoaji huduma bora, vituo vya afya na dawa za kupunguza makali ya VVU.

“Tumeungana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha vipaumbele hivi vinafanikiwa na tutandelea kuhakikisha watu wenye VVU wanapata huduma boza za matunzo na tiba”, alisema Bi. Jessica.

Baadhi ya miradi inayofadhiliwa na PEPFAR chini ya usimamizi wa USAID ni USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini unaolenga utoaji huduma jumuishi za matunzo, matibabu na kuzuia maambukizi ya VVU na kifua kikuu na kuboresha mazingira wezeshi ya utoaji wa huduma bora za afya katika mikoa sita ya kusini mwa Tanzania, huku mradi wa USAID Kizazi Hodari Kusini unaoangalia utoaji wa huduma jumuishi za watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi pamoja na walezi wao ili kuboresha afya, ustawi na ulinzi wa watoto yatima pamoja na vijana katika mikoa 11, miradi hii ikiendesha na Shirika la Deloitte.

Mradi mwingine ni ‘Epic’ unaotekelezwa na Shirika la FHI360 uKjjikita katika kufikia na kuendeleza udhibiti wa janga la VVU huku ukijihusisha katika kutoa msaada wa kitaalamu na huduma za moja kwa moja katika kuondoa vikwazo kufikia malengo ya 95-95-95 ukilenga makundi maalumu wakiwemo wasichana, wamama vijana, wanaume na wanawake walio katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU.

Aidha mradi wa ‘Hebu Tuyajenge’ ukishirikisha watu wanaoishi na VVU, unalenga katika kuongeza matumizi ya huduma za upimaji VVU, tiba na uzazi wa mpango mongoni mwa vijana balehe na wenye VVU ukitekelezwa na Baraza la Taifa la Watu wanaoishi na VVU Tanzania (NACOPHA).

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi. Halima Dendego, akipokea cheti cha shukurani kwa kutambua  mchango wake katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na unyanyapaa kwa wenye VVU katika Mkoa wa Iringa, kutoka kwa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la maendeleo ya Kimataifa (USAID), Bwana Craig Hart, wakati wa ziara ya waandishi wa habari mkoani humo leo ikiwa ni sehemu ya matukio kuadhimisha miaka 20 ya Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR). Ziara hiyo, ililenga kuangalia mafanikio ya miradi inayohudumia wenye VVU na kusimamiwa na mashirika ya Deloitte, Nacopha na FHI360. 
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la maendeleo ya Kimataifa (USAID), Bwana Craig Hart, akikabidhi cheti cha shukurani kwa Mkurugenzi wa mradi wa USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini Dk. Marina Njelekela, kwa kutambua mchango wa shirika hilo, likiwa ni moja ya Mashirika yanayofadhiliwa na Shirika la USAID katika kutoa huduma bora kwa wenye VVU. Hii ni sehemu ya matukio ya kuadhimisha miaka 20 ya mfuko wa PEPFAR Mkoani Iringa leo. Wa kwanza kushoto ni muwakilishi wa PEPFAR  nchini, Bi. Jessica Greene na Mkurugenzi Msaidizi wa USAID kitengo cha afya nchini, Bi. Anna Hofmann.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya   Kimataifa (USAID), Bwana Craig Hart, akikabidhi cheti cha shukurani kwa Mkurugenzi wa Mradi wa USAID Kizazi Hodari Kanda ya Kusini, Bi. Dorothy Matoyo (kulia) kwa kutambua mchango wa shirika hilo, likiwa ni moja ya Mashirika yanayofadhiliwa na Shirika la USAID katika kutoa huduma bora kwa wenye VVU. Hii ni sehemu ya matukio ya kuadhimisha miaka 20 ya mfuko wa PEPFAR Mkoani Iringa leo. Wa kwanza kushoto ni mwakilishi wa PEPFAR  nchini, Bi. Jessica Greene na Mkurugenzi Msaidizi USAID kitengo cha afya nchini, Bi. Anna Hofmann.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la maendeleo ya Kimataifa (USAID), Bwana. Craig Hart, akikabidhi cheti cha shukurani kwa Mkurugenzi wa Shirika la FHI360, Bwana Bernard Ogwang,  kwa kutambua mchango wa shirika hilo, likiwa ni moja ya Mashirika yanayofadhiliwa na Shirika la USAID katika kutoa huduma bora kwa wenye VVU. Hii ni sehemu ya matukio ya kuadhimisha miaka 20 ya mfuko wa PEPFAR Mkoani Iringa leo

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la maendeleo ya Kimataifa USAID Craig Hart, akikabidhi cheti cha shukurani kwa Mkurugenzi wa mradi wa Rise project, Maende Makokha, kwa kutambua mchango wa shirika hilo, likiwa ni moja ya Mashirika yanayofadhiliwa na Shirika la USAID katika kutoa huduma bora kwa wenye VVU. Hii ni sehemu ya matukio ya kuadhimisha miaka 20 ya mfuko wa PEPFAR Mkoani Iringa leo. Kushoto ni mwakilishi wa PEPFAR  nchini, Jessica Greene na  Mkurugenzi Msaidizi USAID Kitengo cha Afya nchini, Bi. Anna Hofmann.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Bwana Craig Hart, akikabidhi cheti cha shukurani kwa Mkurugenzi wa Shirika wa Nacopha, Bwana Deogratius Rutatwa, kwa kutambua mchango wa shirika hilo, likiwa ni moja ya Mashirika yanayofadhiliwa na Shirika la USAID katika kutoa huduma bora kwa wenye VVU. Hii ni sehemu ya matukio ya kuadhimisha miaka 20 ya mfuko wa PEPFAR Mkoani Iringa.

Mratibu wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi ( PEPFAR) nchini, Bi. Jessica Greene  akizungumza katika hafla hiyo.

 Mkurugenzi Mkazi  wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Bw Craig Hart (katikati) , akipozi kwa picha ya kumbukumbu mjini Iringa leo, na baadhi ya wawakilishi kutoka mfuko wa PEPFAR, USAID na Mashirika yanayoratibu miradi ya Ukimwi inayofadhiliwa na PEPFAR kwa usimamizi wa USAID. 


MAELFU MBEYA WAJITOKEZA KUPIMA AFYA KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA KISUKARI DUNIANI

November 15, 2023

 Tarehe 14 Novemba kila mwaka, duniani kote huadhimishwa Siku ya Kisukari Duniani. Maadhimisho haya yanafanyika kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu kisukari, kuhamasisha watu kuchukua hatua za kuzuia na kudhibiti ugonjwa huo, na kushirikiana katika kupambana na changamoto zinazowakabili watu wanaoishi na kisukari.


Katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani yalikuwa ya kipekee na yenye tija ambapo hospitali kupitia timu ya wataalamu wa afya imetoa elimu na ushauri kuhusu kisukari, chunguzi wa afya bila malipo pamoja na uchangiaji damu salama kwa jamii.

Akiongea wakati wa zoezi hilo Dkt. Alumbwage Nyagawa mratibu wa zoezi hilo amesema lengo kubwa ni kusogeza huduma kwa wananchi na kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kupima afya zao pamoja na kupatiwa elimu, uchangiaji damu sambamba na huduma za upimaji wa magonjwa mbalimbalimbali yasiyo ambukiza.

“..sisi kama hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya tumekuja kusogeza huduma kwa wananchi ili kuwawezesha kupima afya, kutoa elimu, pamoja na wao kuweza kuchangia damu.” – Dkt.Alumbwage Nyagawa

Aidha. Dkt. Alumbwage Nyagawa ametoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara kwa kuwa wengi hufikiri wana afya njema wawapo majumbani
Jambo ambalo si kweli kwani wengi wao baada ya vipimo mahali hapa wamekutwa na changamoto mbambali.

“..kwasababu watu wengi wanakaa majumbani wanajiona wapo sawa lakini kwa uhalisia wanakuwa na changamoto za kiafya.” - Dkt.Alumbwage Nyagawa

Epafra Isaya ni mwananchi mwenye uziwi aliyejitokeza kapata huduma ya upimaji wa afya amesema amefurahishwa na huduma nzuri alizopata mahali hapo kwa kuwa amepata nafasi ya kupima shinikizo la damu, ugonjwa wa kisukari, hivyo amefurahishwa na huduma hizo kwa kuwa wao viziwi wamekuwa wakipata wakati mgumu sana kupata elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza.

“..nimefurahi kwasababu sisi viziwi mara nyingi hatuna uelewa wa magonjwa haya yasiyoambukiza. “

Nae Jeofrey Simime ameishukuru Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusema jambo hili linatija kwa jamii kwa kuwa mtu unaweza ukawa unaishi ukidhani uko salama lakini kumbe una changamoto za kiafya.

“..naishukuru Serikali yetu ya Awamu ya 6 kwa kutuletea huduma hii ya vipimo kwa wananchi ili kufanya uchunguzi wa afya zao kwa kuwa jambo hili linatija kwa jamii, mtu unaweza ukawa unaishi ukidhani uko salama kumbe unamagonjwa,.” - Jeofrey Simime.





HALI YA UPATIKANAJI WA CHAKULA NCHINI YASAIDIA KUPUNGUZA UMASIKINI

November 15, 2023

 Na. Josephine Majura na Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam


Tanzania imekuwa kwenye kiwango kizuri cha upatikanaji wa chakula kutokana na kuwepo kwa takwimu sahihi za hali ya Maisha katika kaya, hali iliyopolekea kiwango cha umasikini wa chakula kushuka nchini.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akifungua Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 15 ya Mradi wa Utafiti wa Kupima Hali ya Maisha zinazojumuisha Tafiti za Kilimo Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (Living Standards Measurement Study-Intergrated Survey on Agriculture (LSMS-ISA), katika Hoteli ya Delta, jijini Dar es Salaam.

Amesema Programu hiyo ya utafiti iliyoanza 2008 ambayo ilifadhiliwa na Benki ya Dunia imeweka alama sio tu katika uzalishaji wa takwimu muhimu za hali ya maisha katika kaya bali pia takwimu zilizozalishwa zimekuwa nyenzo muhimu za kutathmini sera na programu zinazotekelezwa na Serikali, taasisi binafsi na wadau wa maendeleo.


“Kiwango cha umasikini kwa sasa kimepungua hasa umasikini wa upatikanaji wa chakula, chakula kipo kwa wingi cha kutosha ambapo sisi watanzania leo tunalisha mpaka nchi jirani” amesema Chande


Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt Albina Chuwa, amesema miaka 15 ya mradi huo umeleta mafanikio makubwa nchini na barani Afrika kwa ujumla.


“Wakati utafiti unaanza 2008 katika Bara la Afrika nchi nyingi zilikua zinafanya utafiti kwa kutumia karatasi lakini sasa teknolojia imekuwa na sasa utafiti unafanywa kwa kutumia vishkwambi” amesema Dkt. Chuwa.


Naye, Meneja Miradi kutoka Benki ya Dunia, Bw. Gero Carletto, ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika programu hiyo na juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kupunguza umasikini wa chakula.


“ Kumekuwa na maendeleo makubwa sio tu katika kupunguza umaskini bali pia katika viashiria vingine vingi. Jopo la kitaifa la utafiti, limekuwa makini katika kuelewa vyema mienendo ya umaskini”. Bw. Carletto


Naye, Kamisaa wa Sensa, Mhe. Anna Makinda, amewataka watafiti kurudisha tafiti hizo kwa wananchi kwa maana wao ndio wahusika wakuu.


Amesema utafiti huu umefanikiwa kwa sababu umeweza kumfikia mtu mmoja mmoja na kuelezea ukweli kuhusu maisha yake jambo ambalo si rahisi.


“Hawa wataalam wa takwimu tunasema sasa wakati umefika utafiti wao uenze kuwatumikia hawa wananchi lakini pia utasaidia utendaji wa serikali katika kuwahudumia wananchi wake” amesema Makinda.


Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na watalamu wa uchumi, sera na watafiti kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo matokeo ya baadhi ya tafiti zilizofanyika chini ya mradi huo zinawasilishwa.


Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akifungua Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 15 ya Mradi wa Utafiti wa Kupima Hali ya Maisha zinazojumuisha Tafiti za Kilimo Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, uliofanyika katika Hoteli ya Delta jijini Dar es salaam. Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na watalamu wa uchumi, sera na watafiti kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo matokeo ya baadhi ya tafiti zilizofanyika chini ya mradi huo zinawasilishwa.


Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa, akizungumza wakati akimkaribisha Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), kufungua Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 15 ya Mradi wa Utafiti wa Kupima Hali ya Maisha zinazojumuisha Tafiti za Kilimo Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, uliofanyika katika Hoteli ya Delta jijini Dar es salaam. Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na watalamu wa uchumi, sera na watafiti kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo matokeo ya baadhi ya tafiti zilizofanyika chini ya mradi huo zinawasilishwa.


Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Mhe. Anna Makinda, akizungumza jambo wakati wa Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 15 ya Mradi wa Utafiti wa Kupima Hali ya Maisha zinazojumuisha Tafiti za Kilimo Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, unaofanyika katika Hoteli ya Delta jijini Dar es salaam. Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na watalamu wa uchumi, sera na watafiti kutoka nchi mbalimbali za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo matokeo ya baadhi ya tafiti zilizofanyika chini ya mradi huo zinawasilishwa.

 

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) (wa sita kushoto), Meneja Miradi kutoka Benki ya Dunia, Bw. Gero Carletto (wa tano kulia), Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa (wa tano kushoto), Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Mhe. Anna Makinda (wa sita kulia) na Mtakwimu Mkuu wa Serikali – Zanzibar, Bw. Salum Kassim Ali, wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi kutoka Benki ya Dunia na Serikali, baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 15 ya Mradi wa Utafiti wa Kupima Hali ya Maisha zinazojumuisha Tafiti za Kilimo Katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambao umefunguliwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), katika Hoteli ya Delta jijini Dar es salaam.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)

RAIS WA ROMANIA KUFANYA ZIARA YA KITAIFA NCHINI

November 15, 2023

 



NSSF YATOA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII KATIKA MKUTANO MKUU WA SABA WA JUKWAA LA WAHARIRI

November 15, 2023

 

WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, akizungumza kwenye mkutano wa 7 wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Mkoani Lindi.




Na MWANDISHI WETU, LINDI

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeshiriki na kutoa elimu ya hifadhi ya jamii katika Mkutano Mkuu wa Saba wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika Mkoani Lindi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Robert Kadege Meneja wa Huduma kwa Wateja, alisema miongoni mwa elimu iliyotolewa ni pamoja na elimu kuhusu majukumu ya waajiri, faida na mafao ya wanachama, pamoja na elimu ihusianayo na kazi za Mfuko kwa ujumla.

Bw. Kadege ambaye ni Meneja wa Huduma na Wateja alisema Mfuko unaendelea kuwakumbusha waajiri wote wa sekta binafsi kuwasilisha michango yao pamoja na ya wanachama wao kwa wakati kwani ni takwa la sheria.

Alisema katika kuhakikisha waajiri wanalipa michango kwa wakati, Mfuko umeweka mifumo mbalimbali ukiwemo wa Employer Portal ambapo mfumo huo unamuwezesha mwajiri kuwasilisha michango popote alipo bila ya kulazimika kufika ofisini.

Naye, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Bi. Lulu Mengele, alisema kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya habari Mfuko ulionelea ni vyema ushiriki katika mkutano huo kwa lengo la kutoa elimu ya hifadhi ya jamii kwa wahariri ambao ni wadau muhimu.

“Kama tunavyojua mwaka 2018, Serikali ilifanya maboresho makubwa katika sekta ya hifadhi ya jamii yaliyopelekea NSSF kuwa Mfuko pekee unaohudumia wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kwa hiyo NSSF tumeona hii ni fursa ambayo tumeipata kupitia jukwaa la wahariri. Bi. Lulu aliendelea kwa kusema vyombo vya habari ni daraja la moja kwa moja kati ya Mfuko na wanachama wakiwemo wananchi.

"Tunatambua mchango mkubwa wa wahariri na vyombo vya habari kwa ujumla katika kupeleka taarifa sahihi kwa jamii, wahariri wakipatiwa taarifa sahihi na wao wataweza kuhabarisha kwa usahihi zaidi", alisema Bi. Lulu.

NSSF ilitumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi ambao hawajajiunga na Mfuko kutembelea ofisi mbalimbali za NSSF ili waweze kujiunga na kuanza kuchangia kwa ajili ya kujiwekea akiba zao

Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Lindi, Juma Namuna, amesema Mfuko katika Mkoa huo unaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ambayo ni kutoa elimu na kuandikisha wanachama wapya, kukusanya michango na kulipa kwa wakati.




Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (kulia),akimkabidhi cheti cha shukrani Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Bi. Lulu Mengele
Picha pamoja