Wizara ya Nisahati na Madini yatoa ufafanuzi mradi wa umeme wa Kinyerezi II

January 14, 2016
Mkuu wa Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, wakati alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu mradi wa umeme wa Kinyerezi Awamu ya Pili, akielezea kuhusu habari zilizoandikwa kimakosa katika moja ya magazeti ya kila siku nchini jijini leo. Kulia ni Ofisa Habari Mwandamizi wa Idara ya Habari-Maelezo, Magreth Kinabo. (Picha na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)


Na Nyakongo Manyama- MAELEZO
14/01/2016
WIZARA ya Nishati na Madini  imekanusha habari iliyopotosha umma kuhusu   mradi wa umeme wa Kinyerezi II kuwa bado haujaanza na gharama zilizoandikwa si za kweli.

Wizara hiyo imekanusha habari hiyo, iliyoandikwa katika gazeti la Mtanzania la leo Januari 14, mwaka huu toleo namba8063,  lenye kichwa cha habari “ Harufu ya Jibu Mradi wa Umeme.”

Habari hiyo  ambayo ilieleza kwamba mradi huo ulizinduliwa na Rais Mstaafu wa  Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Dkt.Jakaya Kikwete uligharimu Sh. trilioni 1.6 na kwamba fedha za ujenzi wa mradi huo zimetokana ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Japan,ambapo Serikali ya Tanzania itakuwa na hisa ya asilimia 40 na kampuni ya SUMITOMO ya Japan asilimia 60. 

 Aidha habari hiyo ilidai kuwa Serikali inachangia fedha za ndani kwa asilimia 12 na zilizobaki zikiwa na mkopo kutoka benki ya Japan na kwamba gharama za mradi huo ziko juu ikilinganishwa miradi mingine akitolea mfano Kampuni ya TALLAWARA Power Station ya nchini Australia anayodai ilitaka kujenga mradi huo kwa dola za Marekani milioni 350.

Hayo yamesemwa leo na  Mkuu wa Mawasiliano Serikali  wa wizara hiyo,  Badra  Masoud alipokuwa akizungumza  na waandishi wa habari kuhusu habari hiyo katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam. 

“Serikali  ya Tanzania  iliingia makubaliano na Serikali ya Japan  ya mkopo wa masharti nafuu  wa dola za Marekani  milioni 292  kwa ajili ya kutekeleza mradi wa  kuzalisha umeme wa Megawati 240 utakaojengwa na kampuni ya SUMITOMO kama mkandarasi wa “EPC contractor” na sio kama mbia wa Serikali yaTanzania kama ilivyodaiwa.

“Mradi huo unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia TANESCO  na hakuna mwekezaji mwingine katika mradi huo.Hivyo si kweli kwamba Serikali ya Tanzania na kampuni ya SUMITOMO zinawekeza kwa ubia wa asilimia 40 (kwa Serikali ya Tanzania) na asilimia 60 kwa SUMITOMO. Kwa maana hiyo, hatutauziwa umeme utakaozalishwa na mradi huu kwani ni mali yetu na hakuna gharama yoyote ya ziada kama alivyodai mwandishi wa habari hiyo,” alisema Badra.

Aidha Badra alisema mwandishi huyo alidai kwamba mradi huo ulizinduliwa na Rais wa  Serikali ya Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete, wakati ni  kwamba mradi huo haujazinduliwa bado na sasa upo katika maandalizi ya kuwekwa katika jiwe la  msingi.

 Akizungumzia kuhusu gharama za mradi huo, alieleza kuwa unatekelezwa kwa dola za Marekani milioni 344 sawa na Sh. bilioni 740 zikiwa ni mkopo wa masharti nafuu wa asilimia 85 sawa  na dola za Marekani 292 na mchango wa Serikali ya Tanzania kwa asilimia 15 sawa na dola za Marekani milioni 52 na sio asilimia 12 kama ilivyodaiwa na mwandishi huyo. 
“Mwandishi wa habari hii amejaribu kufananisha uwekezaji huu na uwekezaji wa TALLAWARA Power Station ya Australia na kudai kwamba gharama yake ingekuwa ndogo kuliko gharama ya mradi huu. 

Taarifa hii haina ukweli wowote kwa sababu gharama ya dola milioni 344 zinazotarajiwa kutumika mkatika mradi huu iko chini kuliko dola milioni 350anazodai mwandishi kwamba zingetumiwa na kampuni TALLAWARA.

“Aidha, kampuni ya TALLAWARA haijawahi kuomba au kuonesha nia ya kuwekeza katika mradi wowote wa kufua mradi wa umeme nchini. Pia ni muhimu ifahamike kwamba makubaliano ya mkopo huu yalikuwa yanakwenda sambasamba na utekelezaji wa mradi wenyewe (EPC with Financing).  
   
Badra aliongeza kwamba pamoja na kwamba gharama za uwekezaji wa mradi huo wa kwanza wa aina ya “Combined Cycle” nchini zinawiana na gharama za miradi mingine ya aina hiyo duniani, gharama za uwekezaji zinaweza kutofautiana kutegemeana na mazingira ya nchi na nchi, teknolojia iliyotumika na aina ya mitambo.

Hivyo sio suala la kulinganisha gharama ya mradi mmoja na mwingine.

Wizara hiyo imeshauri waandishi wa habari kufuata miiko na maadili ya uandishi wa habari kwa kuandika habari  zenye ukweli na sahihi na zilizozingatia pande zote mbili kwa kuwa ipo na tayari kujibu maswali ya waandishi wakati wowote.
 VODACOM MZUNGUKO WA 14

VODACOM MZUNGUKO WA 14

January 14, 2016
Baada ya kusimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania mzunguko wa kumi na nne (14) unatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa michezo 8 kuchezwa katika viwanja mbalimbali, huku timu 16 zikichuana kusaka pointi 3 muhimu.

Jumamosi uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, Maafande wa JKT Ruvu watawakaribisha Maafande wa Mgambo Shooting, Toto Africans watawakaribisha Tanzania Prisosns uwanja wa CCM Kirumba, huku Stand United wakicheza dhidi ya Kagera Sugar uwanja wa Kamabarage mjini Shinyanga.

Uwanja wa Tafa jijini Dar es salaam, Simba SC watawakaribisha wakata miwa wa Mtibwa Sugar saa 10 jioni, Mbeya City watakua wenyeji wa Mwadui FC uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Coastal Union dhidi ya Majimaji uwanja wa Mkwakwani, huku mchezo kati ya Azam FC dhidi ya African Sports ukianza saa 1 usiku.

Jumapili ligi hiyo itaendelea kwa mchezo mmoja uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, ambapo Young African watawakaribisha Ndanda FC kutoka Mtwara.
STARTIMES RAUNDI YA 11 KUENDELEA WIKIENDI

STARTIMES RAUNDI YA 11 KUENDELEA WIKIENDI

January 14, 2016
Ligi Daraja la Kwanza (StarTimes League) inaendelea wikiendi hii kwa michezo 12 kuchezwa katika viwanja mbalimbali, huku timu 3 za juu kutoka katika kila kundi zikipata nafasi ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao moja moja.
Kundi A, Jumamosi Mji Mkuu watawakabili Africa Lyon uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, KMC dhidi ya Kiluvya uwanja wa Mabatini Mlandizi, Polisi Dodoma watacheza dhidi ya Friends Rangers uwanja wa  Mgambo Mpwapwa, huku Jumapili Polisi Dar wakiwakaribisha Ashanti uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Kundi B, Njombe Mji watakua wenyeji wa Kimondo uwanja wa Amani Njombe, Lipuli FC dhidi ya Kurugenzi uwanja wa Wambi – Mafinga, uwanaj wa Majimaji mjini Songea JKT Mlale watakua wenyeji wa Polisi Morogoro, huku Jumapili kukichezwa mchezo mmoja Ruvu Shooting dhidi ya Burkinafaso uwanja wa Mabatini, Mlandizi.

Kundi C, Rhino Rangers watawakaribisha JKT Kanembwa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, Panone FC dhidi ya Geita Gold uwanja wa Ushirika mjini Moshi, uwanja wa Karume Musoma, wenyeji Polisi Mara watacheza dhidi ya Polisi Tabora, huku siku ya Jumapili Mbao FC wakiwakaribisha JKT Oljoro uwanja wa CCM Kirumba.
JKT MLALE YAFUZU HATUA YA 16 BORA

JKT MLALE YAFUZU HATUA YA 16 BORA

January 14, 2016
Michezo ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) mzunguko wa tatu imeendelea kwa mchezo mmoja kuchezwa mjini Songea, ambapo timu ya JKT Mlale imeiondosha Majimaji kwa mabao 2-1.

Michuano hiyo ambayo Bingwa wake ataiwakilisha Tanzania kwenye kombe la Shirikisho Afrika 2017 (CC), imekua ya kuvutia na hasa kwa timu za madaraja ya chini kuziondosha timu za mdaraja ya juu.

JKT Mlale imekua timu ya kwanza kutoka daraja la kwanza kufuzu kwa hatua ya 16 bora, ambapo sasa inasubiria washindi wengine 15 kutoka katika michezo itakayochezwa wikiendi ya Januari 23-17, 2015.

Mpaka sasa kuna timu za saba za daraja la Pili zinawania kufuzu kwa hatua ya nne, timu hizo ni Abajalo  (Dasm), Madini (Arusha), Mvunvuma (Kigoma),

Pamba (Mwanza), Wenda (Mbeya), Mshikamano (Dsm), na Singida United (Singida), huku za daraja la kwanza timu 8 zikisaka nafasi ya kuingia hatua ya 16.

Timu za daraja la kwanza ni Ashanti United (Dsm), Burkinafaso (Morogoro), Friends Rangers (Dsm), Geita Gold (Geita), Lipuli (Iringa), Njombe (Njombe), Panone (Kilimanjaro) na Rhino Rangers (Tabora).

MKE WA MAKAMU WA RAIS MSTAAFU MAMA ASHA BILAL AHITIMU STASHAHADA YA UZAMILI KATIKA MENEJIMENTI YA KIMATAIFA

January 14, 2016

 Mke wa Makamu wa Rais mstaafu Mama Asha Bilal, (katikati) akiwa na wahitimu wenzake walipokuwa wakitunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Kimataifa wakati wa Mahafali yao yaliyofanyika Chuo cha Diplomasia Kurasini jijini Dar es Salaam, jana Januari 13, 2016. 

Mke wa Makamu wa Rais mstaafu Mama Asha Bilal, (wa tano kutoka kulia) akiwa na wahitimu wenzake walipokuwa wakitunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Kimataifa wakati wa Mahafali yao yaliyofanyika Chuo cha Diplomasia Kurasini jijini Dar es Salaam, jana Januari 13, 2016. 
 Mke wa Makamu wa Rais mstaafu Mama Asha Bilal, (katikati) akiwa na wahitimu wenzake Janeth Nyoni (kushoto) na Hadija Hashim, baada ya kutunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Kimataifa wakati wa Mahafali yao yaliyofanyika Chuo cha Diplomasia Kurasini jijini Dar es Salaam, jana Januari 13, 2016.
Mke wa Makamu wa Rais mstaafu Mama Asha Bilal, (wa pili kulia) akiwa na baadhi ya wageni waalikwa wakati wa sherehe ya maafali yake yaliyofanyika Chuo cha Diplomasia Kurasini jijini Dar es Salaam, jana Januari 13, 2016. Mama Asha na wenzake walitunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Kimataifa. 
 Mke wa Makamu wa Rais mstaafu Mama Asha Bilal, (wa kwanza kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni waalikwa baada ya kutunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Kimataifa wakati wa Mahafali yao yaliyofanyika Chuo cha Diplomasia Kurasini jijini Dar es Salaam, jana Januari 13, 2016. 
 Mke wa Makamu wa Rais mstaafu Mama Asha Bilal, (kushoto) akiwa na Meneja Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Lulu Mengele, baada ya kutunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Kimataifa wakati wa Mahafali yao yaliyofanyika Chuo cha Diplomasia Kurasini jijini Dar es Salaam, jana Januari 13, 2016. Kulia ni mke wa Balozi wa Tanzania nchini Geneva, Rose Mero.
 Mke wa Makamu wa Rais mstaafu Mama Asha Bilal, (katikati) akiwa na baadhi ya wahitimu wenzake wa Chuo cha Diplomasia Kurasini jijini Dar es Salaam, jana Januari 13, 2016, baada ya kutunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Kimataifa kwenye Mahafali yaliyofanyika Chuoni hapo.
Baadhi ya Wahitimu wa Chuo hicho wakiwa katika mahafali hayo wakisubiri kutunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Kimataifa, jana Januari 13, 2016. 
Picha na Mafoto Media/Muhidin Sufiani

WATEJA WA TIGO PESA WAANZA KUVUNA GAWIO LA ROBO MWAKA

January 14, 2016
Mkuu wa Fedha na Tahadhari wa Huduma ya Fedha kwa njia ya mtandao wa Kampuni ya simu ya Tigo, Obedi Laiser (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu gawio la mwaka huu  kwa watumiaji wa Tigo Pesa ambalo watumiaji hao wameanza kulipata kuanzia jana. Kulia ni Meneja wa Mawasiliano wa Tigo, John Wanyancha.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Meneja wa Mawasiliano wa Tigo, John Wanyancha (kulia), akizungumza katika mkutano huo.


Na Dotto Mwaibale

Kampuni inayongoza katika kuleta maisha ya kidijitali kwa jamii, Tigo, imetangaza tena malipo ya robo mwaka ya shilingi bilioni 4.4 (dola milioni 2.1) kwa watumiaji wake wa huduma ya Tigo Pesa wapatao milioni 4.6. 

“Gawio hili la faida linalipwa kwa watumiaji wote wa Tigo Pesa wakiwemo wateja binafsi, mawakala wa rejareja na washirika wetu wa kibiashara, kila mmoja kutokana na thamani  ya fedha aliyojiwekea katika akaunti yake ya Tigo Pesa,” alisema Mkuu wa Fedha na Tahadhari wa Huduma ya Fedha kwa njia ya mtandao, Obedi Laiser.

 Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Laiser alisema  kuwa hii itakuwa ni mara ya kwanza Tigo kuwalipa gawio la faida watumiaji wa Tigo Pesa kwa mwaka wa 2016  akibainisha kuwa malipo hayo ni faida inayopatikana kutokana na amana ya mfuko wa Tigo Pesa uliyowekezwa katika benki za kibiashara hapa nchini. 

“Tunayo furaha kubwa kutangaza gawio hili la faida kwa mara ya saba mfululizo tangu tulivyoanza kufanya hivi mwaka 2014. Bila shaka hii inaonyesha ni jinsi gani Tigo inajizatiti kuwaletea watanzania maisha bora ya malipo kwa njia ya mtandao,” amesema Laiser.

Tigo ilikuwa kampuni ya kwanza duniani kutoa gawio kwa wateja wake mwaka 2014 

“Tunaamini gawio hili la kwanza la faida ya Tigo Pesa kwa mwaka 2016 litakuwa ni kivutio kikubwa kwa mamilioni ya watumiaji wa Tigo Pesa katika kufanikisha mahitaji  yao mbalimbali ya kifedha ya mwanzo wa mwaka,” amesema Laiser.

Malipo haya kwa watumiaji wa Tigo Pesa hutolewa kwa mujibu wa mwongozo wa Benki Kuu uliotolewa mnamo Februari mwaka 2014. Mpaka sasa Tigo imelipa jumla ya bilioni 35.5 kwa wateja wake tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu mwaka juzi na kampuni hiyo. 


ZOEZI LA KUWASAKA WAHAMIAJI HARAMU LAPAMBA MOTO MKOANI MBEYA

January 14, 2016
Afisa Uhamiaji  Mkoa wa Mbeya Ndugu Asumsyo Achacha akizungumza ofisni kwekwe juu ya zoezi linaloendelea la kuwasaka wahamiaji haramu mkoani humo.
Na jamiimojablogu,Mbeya
Zoezi la kuwasaka wahamiaji haramu na wageni wanaofanya kazi bila kibali limeendelea kufanikiwa mkoani Mbeya ambapo jumla ya wageni 20 wamekamatwa mkoani humo kutokana na makosa mbalimbali likiwemo la kuingia nchini kinyume cha sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwakwe Afisa uhamiaji Mkoa wa mbeya Ndugu Asumsyo Achacha amesema hatua hiyo imefanyika ikiwa ni kutekeleza majukumu yao ya kila siku sanjali na kutekeleza agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani Dkt Charles Kitwanga alilotoa hivi karibuni.
Aidha amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa sheria mpya  ya kuratibu ajira za wageni ,Sherii Na.1 ya mwaka 2015 ambayo inawataka wageni wote walioajiliwa hapa nchini kuwa na vibali vya kazi na hati za ukaazi nchini.
Afisa uhamiaji huyo amewataja raia hao waliokamatwa katika msako huo ni pamoja wakenya watatu (3)wamalawi 14 pamoja na wakongo watatu (3).
Aidha amesema kuwa mwaka 2015 jumla ya wahamiaji haramu 478 kutoka mataifa mbalimbali walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali  ikiwemo kufikishwa mahakamani pamoja na kufukuzwa nchini.
Amesema mbali na changamoto zilizojitokeza ikiwemo upungufu wa vitendea kazi ,fedha pamoja na rasilimali  bado shughuli za uhamiaji mkoani humo ziliendelea kufanyika kama kawaida na kwa ufanisi mkubwa.
Pia Afisa Uhamiaji huyo amebainisha kuwa zoezi hilo ni endelevu hivyo ofisi yake itahakikisha kila mtu aliyevunja sheria anakamatwa hivyo ametoa wito kwa waajiri kuacha tabia ya kuwapa ajira wafanyakazi wa kigeni wasio na vibali vya kazi na ukaazi kwani msako huo utaendelea katika viwanda ,migodi mashuleni na mahotelini.
Mwisho.