Umoja wa Ulaya watoa Bilioni 22 kusaidia mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula

Umoja wa Ulaya watoa Bilioni 22 kusaidia mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula

February 16, 2017
Katika kusaidia Tanzania kuwa moja ya nchi ambazo wananchi wake wana lishe salama, Umoja wa Ulaya (EU) umechangia Euro milioni 9.5 (Tsh. 22 Bilioni) kwa ajili ya kusaidia kutekelezwa kwa mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula unaotekelezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wenye thamani ya Euro milioni 24.5 (Tsh. 57.7 bilioni) unaotarajiwa kufanyika katika mikoa ya kanda ya kati. Akizungumza kuhusu msaada huo, Mkuu wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De Geer alisema EU imeamua kusaidia jamii ya Tanzania kupata lishe bora kwani wao wanaamini kuwa pasipo lishe bora mambo mengi ambayo yanahusu maendeleo ya taifa hayawezi kufanyika kwa kasi ambayo yanatakiwa kwenda nayo lakini pia mpango wa kusaidia lishe salama ni moja ya mambo ambayo EU imepanga kusaidia.
Mkuu wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De Geer akizungumza kuhusu mchango wa Euro milioni 9.5 (Tsh. 22 Bilioni) kwa ajili ya kusaidia kutekelezwa kwa mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP). (Picha zote na Rabi Hume)
“Kupitia mradi huu EU pamoja na WFP ziko katika nafasi nzuri ya kubaini na kuunga mkono uhusiano katika kilimo, afya, usalama wa chakula na lishe ambao hapo kabla haukuwa umeelezwa kwa kina na kufuatiliwa kikamilifu, matumaini yetu ni kuwa viongozi na wananchi kwa pamoja wataungana kufanikisha mradi huu,” alisema Van De Geer. Nae Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Michael Dunford aliishukuru EU kwa kutoa msaada ambao utawezesha jamii ya Tanzania katika mikoa wa Dodoma na Singida kusaidiwa kupata lishe salama ikiwa ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs).
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Michael Dunford akizungumza kuhusu mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula.
“Tunashukuru kwa mchango huu kutoka Umoja wa Ulaya kwani umeiwezesha WFP kuendelea na programu hii bunifu inayolenga kukidhi mahitaji ya watu walio hatarini zaidi na hasa watoto katika kipindi cha ukuaji wao” alisema Dunford. Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya alisema mradi huo utafanyika kwa mikoa miwili ya Dodoma na Singida ambapo takwimu za kudumaa kitaifa ni aslimia 34 na Dodoma ni asilimia 34 na Singida ni 36.5 na utafanyika kwa miaka mitano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya akielezea jinsi mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula utakavyofanyika nchini, takwimu za kudumaa na mikoa ambayo utafanyika.
Aidha Dk. Ulisubisya alisema uwekezaji huo wa WFP utahusisha kuwapa chakula, kutoa elimu jinsi ya kuzalisha vyakula vya aina mbalimbali, kuwawezesha kuwa na wanyama, jinsi ya kuwa na mazao ya kuuza na walengwa wakubwa ni kina mama wajawazito na watoto.
Mkuu wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Roeland Van De Geer na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Michael Dunford wakisaini makubaliano ya Umoja wa Ulaya (EU) kutoa mchango wa Euro milioni 9.5 (Tsh. 22 Bilioni) kwa ajili ya kusaidia kutekelezwa kwa mradi wa Lishe na Usalama wa Chakula.

MPINA AKITOZA FAINI YA SHILINGI MILIONI 25 KIWANDA CHA CHEMICOTEX CHA MBEZI JOGOO JIJINI DAR ES SALAAM KWA UCHAFUZI WA MAZINGIRA

February 16, 2017


Kulia Bwana Navneft Meneja katika Kiwanda cha Chemicotex, alieleza jambo kwa wajumbe wa msafara wa Naibu Waziri Mpina katika ziara ya kushtukiza kiwandani hapo leo.

Naibu Waziri Mpina akitolea Msisitizo adhabu ya uchafuzi wa mazingira aliyoitoa katika kiwanda cha Chemicotex Jijini Dar esSalaam alipofanya ziara ya kushtukiza leo.



NA EVELYN MKOKOI – DAR ES SALAAM
Kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina, amekitoza faini ya shilingi Milioni 25, kiwanda kinachotengeneza biadhaa mbali mbali za matumizi ya manyumbani kama vile mafuta ya kujipaka mwili na dawa za meno cha chemicotex, mkilichopo Mbeji Jogoo jijini Dar es Salaam Kwa uchafuzi wa mazingira.

Faini hiyo inayotakiwa kulipwa baada ya wiki mbili inatokana na ukiukwaji mkubwa wa sheria ya mazingira unaofanywa na kiwanda hicho kilichopo katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ya kutiririsha maji taka na maji machafu katika mfereji wa maji ya mvua.

Naibu Waziri Mpina ameshangazwa na uthubutu wa uchafuzi wa mazingira unaofanywa na kiwanda hicho, pamoja na jitihada za serikali kupitia Ofisi yake na NEMC za kuthibiti uharibifu wa mazingira kwa kutoa adhabu mbali mbali kwa waharibifu.

“Ujio wangu katika kiwanda hiki unatokana na malalamiko ya wananchi ya kututiririshiwa maji machafu katika makazi yao na maeneo ya biashara,  hakuna atakaesalimika kwa kosa la kutokutunza mazingira na afya za watu, alisistiza Mpina”.

“Mpo Barabarani mnachafua mazingira Hadharani bila haibu, mmedharau jitihada za serikali hii ya awamu ya tano na kuona kama ni nguvu za soda, adhabu hii ilipwe kama ilivyo elekezwa hatuta kuwa na uvumilivu kwa muwekezaji yeyote atakaechafua mazingira. Alisema”.

Kwa Upande wake Mwanasheria kutoka NEMC Bw. Heche Mananche aliongeza kwa kusema kuwa Mmiliki wa kiwanda endapo hatakuwa tayari kulipa faini hiyo anaweza kupelekwa mahakamani.

Wakati Huo Huo, Naibu Waziri Mpina Amezindua Mfereji wa kutirirsha maji katika kiwanda cha Cement cha wazo, baada ya kujiridhirisha na utekelezaji wa maagizo yake kiwandani hapo katika moja ya ziara zake mwaka jana, ambapo ilibainika kuwa kiwanda hicho kimekuwa ni kero kwa wananchi majirani kwa kutiririsha maji na kusababisha mafuriko hasa katika kipindi cha mvua.

Kwa upande wake mkazi wa eneo la wazo bwana David kahaga aliupengeza uongozi wa kiwanda hicho kwa ujenzi wa mtaro huo na kusema kuwa umetatua changamoto katika shule ya msingi jirani na kiwanda hicho ambayo ilikuwa ikikumbwa na mafuriko mara kwa mara hasa katika kipindi cha mvua, lakini bado wakazi hao wana hofu na usalama wao baada ya ujenzi wa mtaro huo  na kuwa bado wanakabiliana na changamoto kubwa ya vumbi itokanayo na uchimbaji wa malighafi za uzalishaji katika kiwanda hicho.




TIMU YA NGAYA YA COMORO YAWASILI NCHINI KUMENYANA NA YANGA JUMAMOSI UWANJA WA TAIFA

February 16, 2017

 Wachezaji wa Timu ya Ngaya ya nchini Comoro wakiwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam leo mchana kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Yanga utakaofanyika kesho kutwa Uwanja wa Taifa. Katika mchezo wa awali uliofanyika Comoro Yanga ilishinda bao 5-1.


 Picha ya pamoja na viongozi wao baada ya kuwasili.
Mmoja wa viongozi wa timu hiyo (kushoto), akitoa maelekezo kabla ya kuondoka uwanjani hapo. (Picha na blog ya habari za jamii.com)
Wachezaji wa timu hiyo wakiingia kwenye gari kuelekea hotelini walikofikia.

Na Dotto Mwaibale

KIKOSI cha Timu ya Ngaya kutoka nchini Comoro kimewasili nchini kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Yanga katika dimba litakalofanyika kesho kutwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Timu hiyo imewasili leo saa saba na nusu mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), huku ikiwa imeongozana na baadhi ya viongozi wake.

Mara baada ya kuwasili timu hiyo ilipokelewa na wananchi wa nchi hiyo wanaoishi hapa nchini  hata hivyo viongozi wa timu hiyo hawakuwa tayari kuzungumza chochote na wanahabari badala yake walipiga picha ya pamoja na wachezaji na kisha kupanda kwenye magari na kuondoka.

Katika mchezo wa awali uliofanyika nchini humo Yanga iliibuka kwa ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya timu hiyo.


Katibu Mkuu wa Yanga Charles Mkwasa alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na kuwa waamuzi wake wanatarajiwa kufika kesho.