KAMATI YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YATEMBELEA MGODI WA BARRICK NORTH MARA,YAVUTIWA NA UTENDAJI WAKE

February 21, 2024

 

Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiangalia utunzaji wa mazingira walipofanya ziara ya kikazi katika mgodi wa Barrick North Mara.


-Yaamuru vitendo vya uvamizi wa Mgodi huo vikomeshwe mara moja

***
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea Mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo wilayani Tarime na kutoa ushauri wa kuboresha sekta ya madini ili iweze kuwanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.

Pia imepongeza kampuni hiyo kwa kufanya uwekezaji mkubwa wenye tija na ufanikishaji wa miradi ya kijamii kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) sambamba na kuendeleza mahusiano na wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayozunguka mgodi.

Ziara ya Kamati hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wake, Mh. David Mathayo David.

Awali wajumbe wa Kamati hiyo walipata maelezo kuhusu shughuli za uendeshaji wa mgodi huo kabla ya kutembelea sehemu mbalimbali, ikiwemo eneo la majitaka, kinu cha kuchenjua dhahabu na baadhi ya miradi ya kijamii iliyotekelezwa kutokana na fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) katika vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara.

Baadhi ya miradi hiyo ni Shule ya sekondari Matongo, mradi mkubwa wa maji wa Nyangoto na ule wa kilimo biashara unaoendeshwa na vijana katika kijiji cha Matongo.

Akiongea kwa niaba ya kamati baada ya kumaliza ziara hiyo, Dk.David Mathayo alisema “Kwa muda mfupi mmebadilisha mazingira ya mgodi huu. Mnatunza mazingira vizuri, wabunge wamefurahi - na kwa niaba yao ninawapongeza, endeleeni kuwa watunzaji wazuri wa mazingira kwa usalama wa wananchi wetu.”

Pia Kamati hiyo iliipongeza Barrick kwa kuendelea kuwa mfano mzuri katika ulipaji wa kodi mbalimbali serikalini, pamoja na utoaji wa mabilioni ya fedha za kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

“Kwenye kampuni kubwa za kibiashara ninyi [Barrick] mnaongoza kwa kulipa kodi na kutoa gawio kwa Serikali,” Mathayo alisema katika sehemu ya hotuba yake ya kuhitimisha ziara hiyo.

Kamati hiyo pia ilieleza kuridhishwa na jinsi Kampuni ya Barrick Gold inavyotekeleza Sheria ya ‘Local Content’ na hivyo kuwezesha Watanzania wengi wakiwemo wazawa wanaoishi jirani na migodi yake kunufaika na uwekezaji wake kupitia biashara na ajira, miongoni mwa mambo mengine.

Nao baadhi ya Wabunge wa kamati hiyo walipongeza Barrick kwa kuendelea kuleta mapinduzi kupitia uwekezaji mkubwa wa sekta ya madini nchini na walishauri mgodi uangalie uwezekano wa kuwasaidia wachimbaji wadogo ili wajikwamue kiuchumi kwa kuwapatia baadhi ya maeneo wachimbaji hao.

Akiongea wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Mh. Steven Kiruswa ,alitoa wito kwa wadau waliopo kwenye sekta ya madini kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa na Serikali ikiwemo kanuni inayohusiana na mgawanyo wa fedha za Uwajibikaji kwa jamii (CSR) na ushirikishwaji wa wazawa wa Tanzania katika shughuli za Mnyororo wa madini (Local content).

"Pamoja na changamoto tulizozisikia kutoka kwa viongozi wa wananchi wa eneo hili linalozunguka mgodi, natoa pongezi kwa kampuni ya Barrick kwa uendeshaji migodi yake nchini kwa weredi, uwazi na kuchangia pato la Taifa kupitia kodi, sambamba na kuleta maendeleo kwa wananchi kupitia miradi inayotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR).

Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Melkiory Ngido, aliwashukuru wajumbe wa kamati hiyo kwa kutembelea mgodi huo na kuahidi kuwa maoni na ushauri uliotolewa na wajumbe yatafanyiwa kazi “Barrick siku zote tutahakikisha tunaendesha shughuli zetu kwa uwazi na kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na Serikali”,alisisitiza.

Awali akitoa maelezo kuhusiana na shughuli za kampuni, Melkiory Ngido ,alisema Barrick kupitia migodi yake ya North Mara na Bulyanhulu imewekeza hapa Tanzania shilingi zaidi ya trilioni sita, na kwamba kati ya kiasi hicho, Serikali imepokea trilioni tatu ambazo zimelipwa kwa mifumo wa kodi na gawio tangu mwaka 2019 ilipokabidhiwa na kuanza kuendesha migodi hiyo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Kuhusu mgodi wa North Mara, Ngido alisema: “Huu mgodi ulitakiwa kuisha [kufika kikomo] mwaka 2026 lakini kwa juhudi za uwekezaji na za kitaalamu utaenda hadi miaka 15 ijayo - utafika hadi mwaka 2039.”

Ngido, alisema Barrick kupitia mpango wake ujulikanao kama The Barrick-Twiga Future Forward Education Programme, imetoa Dola za Kimarekani milioni 30 sawa na shilingi takriban bilioni 70 kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya shule za sekondari za juu upande wa mabweni na madawati, miongoni mwa mambo mengine katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mradi huu upo chini ya TAMISEMI na sisi kama Twiga na Barrick tunafurahi kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan, ili watoto wote waende A level (high school) na wasome katika mazingira rafiki,” alisema, Ngido.

Kamati hiyo ya Bunge pia ilielezwa kuwa asilimia 96 ya wafanyakazi takriban 3,000 wa Mgodi wa North Mara ni Watanzania, na kwamba juhudi za kuongeza idadi ya wafanyakazi wanawake zinaendelea.

Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeiagiza Serikali ya mkoa kumaliza tatizo la uvamizi katika mgodi wa North Mara unaofanywa na makundi ya watu (intruders) mara kwa mara kwa lengo la kuiba mawe yenye dhahabu.

“Uwekezaji huu ulindwe, hivi mpaka watu wanabeba mapanga na kuvamia mgodi, vyombo vyetu [vya ulinzi na usalama] vinakuwa wapi, vyombo visaidie kutatua tatizo hili (uvamizi mgodini) kwa sababu tunajirudisha nyuma wenyewe na tunaharibu taswira ya nchi yetu kwa wawekezaji,” alionya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mathayo.

Kwa upande mwingine, Kamati hiyo imeagiza Serikali ngazi ya wilaya na mkoa kumaliza malalamiko ya wananchi kuhusu mchakato unaotumika katika uthaminishaji wa ardhi inayohitajika kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za mgodi wa North Mara.

Baadhi ya viongozi waliofuatana na Kamati hiyo katika ziara hiyo ni Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Madiwani na Wenyeviti wa vijiji kutoka Kata tano zenye vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi wa Noth Mara.


Migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu inaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiangalia utunzaji wa mazingira walipofanya ziara ya kikazi katika mgodi wa Barrick North Mara
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakikagua mradi wa kilimo biashara ulioanzishwa na mgodi wa Barrick North Mara kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo katika kijiji cha Matongo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo David akizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika mgodi wa Barrick North Mara . kushoto ni Naibu Waziri wa Madini,Mh.Stephen Kiruswa na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda.
Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Melkiory Ngido (wa pili kushoto) akitoa ufafanuzi katika kikao hicho na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea mgodi wa Barrick North Mara ,kushoto ni Meneja wa mgodi wa North Mara,Apolinary Lyambiko,kulia ni Meneja wa Mahusiano ya Jamii wa mgodi huo Francis Uhandi.
Diwani wa kata ya Nyamwaka, Mwita Marwa Magige akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini katika mgodi wa Barrick North Mara 
Baadhi ya wabunge kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakifuatilia maelezo kutoka kwa watendaji wa Barrick wakati walipotembelea mgodi wa North Mara

DKT. MPANGO AIAGIZA WIZARA YA VIWANDA KUTATUA CHANGAMOTO YA SOKO LA MATUNDA TANGA

February 21, 2024

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Philip Mpango ameigiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Tanga kuchukua hatua za mapema katika kukabiliana na changamoto ya soko la matunda yanayozalishwa mkoani humo.


Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kabuku Wilaya ya Handeni akiwa ziarani mkoani Tanga leo tarehe 21 Februari 2024.

Ameuagiza uongozi wa mkoa wa Tanga kufanya tathimini na kutambua kiasi cha matunda yanayozalishwa katika eneo hilo.

Aidha Makamu wa Rais amemuagiza Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara kukutana na wamiliki wakubwa wa viwanda vya kuchakata matunda (Bakhresa na Jambo Product) ili waweze kutumia matunda yanayozalishwa Wilaya ya Handeni na Tanga kwa ujumla katika bidhaa zao.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kabuku na Watanzania kwa ujumla kuongeza jitihada katika utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema athari za uharibifu wa mazingira zimepelekea ongezeko la joto kupita kiasi, ongezeko la mvua ambayo imepelekea uharibifu wa miundombinu na mlipuko wa magonjwa.

Amesema ni muhimu watanzania kutambua uhifadhi ya mazingira ni jukumu la kila mmoja kwa kuacha kukata miti ovyo, kuacha kuchoma misitu pamoja na kupanda miti na kuitunza.

Makamu wa Rais amewasisitiza wananchi wa Kabuku kuhakikisha wanazingatia elimu kwa watoto ili kuwa na kizazi bora na chenye maarifa kwa manufaa ya Taifa.

Pia amewaasa wananchi wa eneo hilo kuzingatia lishe kwa kuwa ndio msingi wa afya bora ya mwili na akili.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Wizara imepokea shilingi bilioni 25 kwaajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji eneo la Segera hadi Kabuku mkoani Tanga kwa lengo la kukabiliana na adha ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.

Waziri Aweso amesema mradi huo unatarajia kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2025 ambapo tayari mkandarasi anaendelea na kazi.

Aidha Waziri Aweso ametoa wito kwa mkandarasi kuhakikisha anafanya kazi na kukamilisha kwa wakati pamoja na kuwashirikisha wananchi na viongozi wa eneo husika wakati wote wa ujenzi wa mradi huo.

Aidha ameahidi kwamba Wizara ya Maji itahakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa TAMISEMI Deogratius Ndejembi amesema tayari Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) imepokea shilingi bilioni 30 ambazo zitaanza kushughulikia changamoto mbalimbali za barabara hapa nchini.

Ameongeza kwamba kwa upande wa Wilaya ya Handeni, Serikali tayari imetenga fedha kwaajili ya ujenzi wa barabara ya Sindeni – Kwedikazo ya kilometa 37.7 kwa kiwango cha lami.

Amesema katika Wilaya hiyo TARURA itaanza mchakato mara moja wa kuhakikisha barabara zilizoharibiwa na mvua zinatengenezwa ili ziweze kupitika vema.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Kabuku Wilaya ya Handeni wakati akiwa ziarani mkoani Tanga tarehe 21 Februari 2024.

BILIONI 988 KUTUMIKA KUBORESHA MIUNDOMBINU DAR ES SALAAM

BILIONI 988 KUTUMIKA KUBORESHA MIUNDOMBINU DAR ES SALAAM

February 21, 2024

 

Bilioni 988/ kutumika kuboresha miundombinu Dar es Salaam

Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imesaini mkataba wa mradi wa kuboresha miundombinu katika jiji la Dar es salaam (DMDP)awamu ya pili utakao gharimu bilioni 988.83.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo jijini Dar es salaam Waziri wa fedha Mwigulu Nchema amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha miundombinu katika jiji inaimarika.

Amesema mkataba huo wa DMDP II unaashiria dhamira ya serikali ya kuimarisha miundombinu na kukuza ustawi wa kiuchumi kwa wakazi wa jiji hilo.

“Hatua hii itawezesha serikali ya Tanzania kupata mkopo kutoka benki ya Dunia wenye thamani ya dolla za kimarekani milioni 361.1 sawa na shilingi bilioni 988.093 kutekeleza mradi DMDP kwa awamu ya pili”amesema.

Amesema mradi huo wa DMDP II ni muendelezo wa utekelezaji wa mpango wa tatu wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano 2021/22 mpaka 2025/26,lakini pia ni utekelezaji wa irani ya uchaguzi ya CCM na ajenda ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa(TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa amesema watahakikisha fedha hizo zinaenda zilipokusudiwa kwani ni dhamira ya Rais kuona jiji la Dar es salaam linakuwa jiji la kibiashara.

Amesema fedha hizo zitaenda kujenga miundombinu ya barabara,ujenzi wa madampo makubwa ya takataka,masoko 18,vituo vya mabasi 9 pamoja na mifereji ya maji ya mvua ili kuzuia mafuriko pindi mvua kubwa zinaponyeesha.

“Tunakwenda kufanya usimamizi wa hizi fedha ili zilafanye lililokusudiwa na kazi ianze mara moja lakini pia tutafanya ushawishwi kwa Rais ili kurudisha hadhi ya jiji la Dar es salaam”Amesema.

Naye,Mkurugenzi mkaazi wa benki ya Dunia nchini Nathan Belete amesema wataendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika kuinua uchumi wa nchi kwani kwa zaidi ya miaka 15 wameweza kufanya mambo mengi ya maendeleo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa wabunge wa Dar es salaam Dkt Faustine Ndugulile amesema hawatakubali upotevu wa fedha hizo wala kazi zilizokusudiwa kufanywa chini ya kiwango hivyo ametoa rai kuanza kwa mchakato wa kazi hizo mapema ili ifikapo mwezi April wakandarasi waangie kazini.

“Asilimia 10 ya watanzania nyumbani kwao ni Dar es salaam lakini pia asiliamia 70 ya uchumi wa nchi unatokea hapa hivyo kipaumbele lazima kiwe barabara kwani hakuna mashamba hapa”Amesema Ndugulile.

TAFITI ZINAZOHUSU CHAKULA NA LISHE KUFANYIWA UCHUNGUZI WA KIMAABARA

TAFITI ZINAZOHUSU CHAKULA NA LISHE KUFANYIWA UCHUNGUZI WA KIMAABARA

February 21, 2024





Tafiti zinazohusu chakula na lishe kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara

Serikali kupitia Wizara ya Afya imepanga kuweka sharti kwa kufanya uchunguzi wa kimaabara kwenye tafiti zozote nchini zinazohusisha masuala ya chakula na lishe katika Maabara ya Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC).

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema hayo jana Februari 20, 2024 wakati wa ziara yake ya kukagua na kuona kazi zinazofanywa na Taasisi ya Chakula na Lishe kwa upande wa Maabara iliyopo Mikocheni Jijini Dar Es Salaam.

“Tunampango wa kufanya uchunguzi wa kimaabara kwa mtu yeyote au shirika lolote linalofanya tafiti zinazohusu masuala ya chakula na lishe, lazima zithibitishwe na ushahidi wa kisayansi baada ya sampuli kuchukuliwa na kuletwa katika maabara hii, isiwe tu ni tafiti za kwenye makaratasi.” Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema maabara hiyo ya chakula na lishe ni moja ya maabara kubwa na zinazoaminika katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika ambapo amefurahishwa na kazi wanazofanya ikiwa ni pamoja na kuja na ushahidi wa kisayansi.


“Lakini pia kuna utafiti ambao wameufanya na kushauri kwamba wataalamu wa Afya wanashauri na kuelekeza watoto wa umri chini ya miezi Sita wasipewe chakula kingine chochote zaidi ya maziwa na mama”. Amesema Waziri Ummy.


Maabara hiyo imegawanyika katika sehem Tatu ambayo ni maabara ya chakula (food chemistry) ambayo inafanya uchunguzi wa viinilishe (macro and micro nutrients), maabara inayofanya uchunguzi wa viashiria vya viini lishe mwilini (micronuient biomarkers), na maabara inayofanya uchunguzi wa hali ya lishe (body composition) ikiwa ni pamoja na kugundua kama chakula kimeharibika.

Mwisho, Waziri Ummy ametoa wito kwa Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi, kupunguza matumizi ya sukari na chumvi ili kuepuka kupata magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwa yamekuwa yakiongezeka kila siku.


CCM YAUPONGEZA UBALOZI WA UINGEREZA KUHAMIA DODOMA

February 21, 2024

 Chama Cha Mapinduzi kimeumepongeza Ubalozi wa Uingereza nchini kwa kuitikia wito wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuzitaka ofisi za ubalozi mbalimbali zilizopo Tanzania kuhamia Dodoma.


Pongezi hizo, zimetolewa leo, tarehe 21/2/2024, jijini Dodoma na Katibu wa NEC wa Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Ndg. Rabia Abdalla Hamid, wakati akizungumza na ujumbe wa Maafisa wa Ubalozi wa Uingereza, katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM, Dodoma.

Ujumbe wa Maafisa wa Ubalozi wa Uingereza, ukiongozwa na Mkuu wa Ofisi ya Dodoma, Bi. Godfrida Magubo, mapema leo, umetembelea Ofisi za Makao Makuu ya CCM, Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha na kuitambulisha Ofisi ya Ubalozi huo, iliyopo Dodoma, ambayo ilifunguliwa Januari 2024.

‘’Chama Cha Mapinduzi kinawashukuru na kuwapongeza sana kwa kuunga mkono juhudi za kuhamia Makao Makuu ya Nchi hapa Dodoma,’’ Rabia alisema akiwapongeza.

Aidha, ameutaka Ubalozi wa Uingereza wawe mabalozi wa kuhamasisha ofisi zingine za ubalozi mbalimbali nchini kuhamia Dodoma.

Ndg. Rabia ameongeza kusema, ‘’ Chama na Serikali tumehamia Dodoma moja kwa moja, na hatukusudii kurudi nyuma, hivyo natoa wito kwa ofisi zingine za ubalozi wa nchi mbalimbali kuhamia Dodoma kama ninyi mlivyofanya’’.

Katibu wa NEC Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa na ujumbe wa Maafisa wa Ubalozi wa Uingereza wamezungumza na kujadiliana mambo mbalimbali ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Uingereza.





CCM WAMPA KONGOLE RAIS SAMIA KWA KUIMARISHA DEMOKRASIA

February 21, 2024

 NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan,kwa juhudi zake za kuimarisha diplomasia inayoongeza fursa za kiuchumi zinazoleta tija na mafanikio kwa pande zote za Muungano.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,wakati akitoa tathimini na uchambuzi wa fursa na mafanikio ya Tanzania Kimataifa kupitia mahojiano yaliyofanyika katika Kituo cha Radio ya Bahari FM,kilichopo Migombani Zanzibar.

Mbeto,alifafanua kuwa Rais Dkt.Samia,ameendelea kuipaisha Tanzania kiuchumi ili ifike katika kilele cha maendeleo endelevu sambamba na kupata hadhi ya nchi iliyoendelea kiuchumi Barani Afrika.

Alisema Chama Cha Mapinduzi kwa upande wa Zanzibar kinapongeza kwa dhati juhudi,maarifa,ubunifu na uchapakazi wa Rais wa Dkt.Samia na kwamba utendaji huo uliotuka ndio kibali cha Wananchi kumpa ridhaa ya kushinda kwa kishindo Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Katika maelezo yake Katibu huyo wa NEC,aliwasihi Wananchi bila kujali tofauti za kisiasa,kidini na kikabila kumuunga mkono kwa kila hatua anayopiga katika kutafuta fursa mbalimbali kupitia ziara,makongamano na mikutano ya kimataifa.

Katibu huyo mwenezi alisema kupitia ziara zake amekuwa akitangaza fursa za Utalii kupitia dhana za Royal Tour na Uchumi wa Buluu zinazofafanua kwa kina rasilimali zilizopo nchini zikiwemo mbuga za wanyama,Bahari,mito,maziwa,vivutio vya mambo ya kale ili raia wa kigeni waje kwa wingi nchini kwa ajili ya Uwekezaji na utalii.

" Najua wapo baadhi ya watu wachache wanakosoa na kubeza juhudi hizi za Rais Dkt.Samia,wakidai anafanya ziara nyingi nchi za nje lakini tukumbuke kuwa ziara hizo sio za kifamilia bali anaenda kutafuta fursa za kiuchumi na kuimarisha mahusiano mema ya kidiplomasia yakiambatana kuingia na mikataba mikubwa yenye tija kwa nchi.

Alisema bajeti Kuu ya Tanzania kwa mara ya kwanza imefikia kiasi cha zaidi ya Trioni 41 ambapo asilimia 35 imeelekezwa katika miradi ya maendeleo inayowanufaisha Wananchi.

Mbeto,akizungumzia ziara za Rais Dkt.Samia,Makao Makuu ya dhehebu la dini ya Kikiristo Vatican,amesema imejenga mahusiano makubwa na kudhihirisha kuwa kiongozi huyo hana ubaguzi anajali imani za dini za wananchi wote.

Alieleza kuwa pamoja na hayo ziara hiyo ya kukutana na Papa Francisko wamekubaliana kuongeza miundombinu ya kijamii na kiuchumi ikiwemo ujenzi wa skuli,vyuo vikuu,hoteli kubwa za kitalii na viwanda vitakavyowanufaisha wananchi wote.

Pia ziara nyingine ya nchini Norway imeendelea kufungua fursa mpya za kiuchumi zikiwemo Uwekezaji katika Sekta za uvuvi pamoja na kuingia mikataba ya kushirikiana katika teknolojia ya masuala ya Gesi na Mafuta nchini.

Mafanikio hayo yanatokana na utekelezaji wa makubaliano na Wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ibara ya 132 (a)-(e) imeelekeza katika kipindi Cha miaka mitano ijayo,CCM itahakikisha kuwa mahusiano ya nchi kikanda na kimataifa yanaendelea kuimarishwa lengo Kuu ni kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha Amani,uhuru na maslahi ya Taifa katika nyanja za kimataifa.
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis.

DC SIMANJIRO AWATAKA VIONGOZI KUIFUATA JAMII

February 21, 2024

 


Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera amewataka viongozi wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, kufanya mikutano vitongojini ili kubaini, kero, migogoro na changamoto za jamii ili wazitatue.

Dk Serera akizungumza na wakazi wa kitongoji cha Getini mji mdogo wa Mirerani, amesema viongozi wa mamlaka ya mji mdogo wanapaswa kushiriki kwenye mikutano ya vitongoji ili kusikiliza kero za watu.

"Hatuwezi kutatua mgogoro, kero na changamoto za jamii kwa kukaa ofisini hivyo viongozi wa mamlaka fanyeni mikutano ili mtatue matatizo yao," amesema Dk Serera.

Amesema viongozi wasipofika chini na kufahamu matatizo ya watu hawataweza kuyatatua hivyo wabadilike kwa kufanya hivyo.

Hata hivyo, ofisa mtendaji wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Isack Mgaya amesema wataweka utaratibu wa kufanya mikutano hiyo ili kutekeleza agizo hilo.

"Awali mara moja moja tulikuwa na utaratibu wa kufika kwenye mikutano ya kitongoji inayoandaliwa katika vitongoji kila baada ya miezi mitatu," amesema Mgaya.

Diwani wa kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi ameishukuru serikali kwa kutenga fedha za ujenzi wa kituo cha afya kitakachosogeza huduma za afya kwa ukaribu.

"Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea kituo cha afya ili kuepusha wanawake wajawazito na watoto kufuata huduma za afya umbali mrefu," amesema Mnyawi.

Mkazi wa kitongoji cha Msikitini, Adam Komba ameiomba serikali kutafuta namna ya kuyadhibiti maji ya bwawa la kidawashi kwani yanasababisha mafuriko.

"Maji ya mto Nduruma yamedhibitiwa na bonde la mto Pangani kwa kuchimba mtaro mkubwa unaopitisha mkondo wa maji yake hadi mto Kikuletwa ila hayo mengine ndiyo yanasababisha mafuriko," amesema Komba

MASESA AWAASA MADEREVA KUPUNGUZA MWENDOKASI WAWAPO NDANI YA HIFADHI YA MIKUMI

February 21, 2024

 Na Richard Mrusha Mikumi.


WATUMIAJI wa Vyombo vya moto wametakiwa kupunguza mwendokasi zaidi pindi wanapopita kwenye Hifadhi ya taifa ya mikumi ili kuepuka kugonga wanyama na kusababisha hasara kubwa ya kukosa fedha kutokana na utalii unaofanyika kwenye Hifadhi hiyo.

Hayo yamesemwa februari 19,2024 na kamishna mkuu Msaidizi wa hifadhi ya Taifa Mikumi Kamanda ,Augustine Masesa wakati akizungumza na waandishi wa Habari kwenye ofisi za Makao makuu ya Hifadhi hiyo zilizopo mikumi mkoani Morogoro.

Kamanda Masesa Amesema pamekuwepo na changamoto kubwa ya wanyama kugongwa kutokana na mwendo kasi wa magari yanayokatisha kwenye Hifadhi hiyo licha kuwataka kutembea mwendo mdogo lakini wanakwenda mwendokasi kwa kufanya hivyo inasababisha madhara ya mara Kwa mara Kwa wanyama wetu

"Kama shirika ama Hifadhi Sasa tunafikiria kufunga kamera (CCTV) katika Hifadhi hii ya mikumi ili kudhibiti na kubaini wanaokwenda Kwa spidi kubwa kwani tunaamini kufanya hivi kutaokoa wanyama wetu kuwa salama zaidi."Amesema

Pia katika hatua nyingine Kamanda Masesa ametoa rai Kwa watanzania na hasa kupitia nyakati za sikukuu mbalimbali na likizo kujitokeza na kutembelea Hifadhi ya taifa ya mikumi ili kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo hususani wanyama kama Simba , tembo,Swala,chui,viboko,mamba ikiwa sehemu ya Kukuza utalii wetu

Amesema hakuna mahala kwingine unaweza kuona wanyama hao Kwa ukaribu zaidi ya Hifadhi ya taifa ya mikumi hivyo nivema tukajenga tabia ya kutembelea na si kuwaachia wageni tu japo katika siku za hivi karibuni pamekuwepo na ongezo la watalii wa ndani kutembelea Hifadhi hiyo.

Pia akizungumzia royal tour ambayo ilizinduliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwanza Amesema wanamshukuru sana kiongozi huyo mkuu wa nchi kwani imeleta chachu na matunda yake yanaonekana kwani watalii wameongezeka ukilinganisha na huko nyuma .

Masesa Amesema watalii wengi ambao wanakuja kutembelea Hifadhi ya taifa Mikumi wanatoka Zanzibar Asubuhi na Ndege na kufika Hifadhi ya mikumi baada ya kutalii jioni wanarudi kulala Zanzibar hali ambayo kama Hifadhi inawapa hamasa Sasa ya kukaribisha wawekezaji ili kujenga hoteli kubwa za nyota tano ili watalii waweze kulala hifadhini pindi wanapokuja kutalii.

Aidha Amesema wanaendelea kuimarisha miundombinu na zaidi ujenzi wa kiwanja cha ndege ili Kuruhu ndege kubwa kutua na kuongeza idadi kubwa ya watalii lakini Kwa kifupi royal tour imelipa na mambo yanakwenda vizuri .

"Kikubwa watanzania waendelea kuja kutembelea vivutio vyetu na Kwa musimu huu wa sikuku ya pasaka basi watumie fursa hii kuja na watapata huduma zote ndani ya Hifadhi ikiwemo sehemu za maradhi, chakula , lakini Kuna utalii wa michezo na kubwa zaidi na chautofauti wataona wanyama Kwa karibu zaidi."Amesema