Utoaji wa Chakula Mashuleni utasaidia kuongeza kiwango cha Taaluma kwa wanafunzi

Utoaji wa Chakula Mashuleni utasaidia kuongeza kiwango cha Taaluma kwa wanafunzi

April 30, 2013

Na Oscar Assenga, Mkinga.
IMEELEZWA kuwa utoaji wa chakula mashuleni utasaidia kupunguza utoro na kufanya mahudhurio ya wanafunzi kuwa mazuri ikiwemo kupanda kiwango cha taaluma kwani watoto watakuwa na nguvu ya kusoma na kuelewa watakachokuwa wakifundishwa.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa chakula kwa wanafunzi iliyofanyika Duga Maforoni na Maramba ambapo alisema anaamini ulaji wa chakula mashuleni utakuwa endelevu na kuwataka wazazi na viongozi kushirikiana na walimu ili kufanikisha suala hilo.
Mgaza alisema katika kufanikisha zoezi hilo la utoaji wa chakula wazazi na wadau wachangie kwa kiasi ambacho kitakuwa kikihitajika kwa kila mtoto kwani watakapopata chakula mashuleni itasaidia pia kuimarisha afya ya watoto wao.

Aidha Mgaza aliwashauri wazazi wilayani humo kujitahidi kuwapeleka watoto wao shuleni ili kuweza kuepuka gharama ambazo zitaweza kuwakuta baade kwani zitakuwa kubwa kuliko wanavyokuwa wakifiria.

Hata hiyo mkuu huyo wa wilaya alisisitiza suala la uvaaji vya viatu mashuleni ambapo alisema tatizo la watoto kukosa viatu linapaswa kuangaliwa na wazazi kwa kuhakikisha kila mtoto wake anavaa viatu ili kuweza kuwaepusha na magonjwa ambayo huenda wakayakuta wakati wakiwa beya.

Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Elimu wilayani humo, Juma Mhina alisema wanaamini zoezi la uhamasishaji lishe shuleni kwa kushirikiana na wenyeviti wa vijiji na wazazi litaweza kupata mafanikio makubwa.
Mhina alisema wanaamini mpaka ifikapo mwezi wa saba mwaka huu shule zote zilizopo wilayani humo zitakuwa zinapata chakula cha mchana mashuleni ambapo alisema lengo la kampeni hiyo ni kuwawezasha wanafunzi kusoma kwa bidii na kuweza kuelewa wanachofundishwa.

      Mwisho.

 

Coastal Union yaipania Yanga.

April 30, 2013

Na Oscar Assenga, Tanga.

UONGOZI wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga umesema umepania kuibuka na ushindi kwenye mechi yao na Yanga ambayo inayotarajiwa kuchezwa  Mei mosi mwaka huu katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana,Mwenyekiti wa timu hiyo,Hemed Aurora “Mpiganaji”alisema wanaamini kuwa mechi hiyo wapinzani wao wataingia uwanjani hapo wakiwa wamebeteka kutokana na kuwa tayari walishatangazwa kuwa mabingwa hivyo watacheza bila umakini mkubwa.

Aurora alisema  licha ya haya wao watacheza kwa tahadhari kubwa ikiwemo kufa na kupona ili kuweza kupata matokeo mazuri na sio kufungwa ili kuweza kutimiza malengo yao walijiwekea ya kumaliza ligi wakiwa katika nafasi tano za juu kwenye msimamo.

Alisema licha ya majeruhi kuonekana kuiletea wakati mgumu timu hiyo lakini wao watatumia wachezaji waliopo kwenye mechi zilizo salia pamoja na kuangalia namna nzuri wachezaji ambao watawasajili msimu unaokuja wasije wakawa kama msimu huu kutokana na wachezaji wengi kuwa na majeruhi.

Aidha alieleza mikakati yao ni kuhakikisha mechi zao mbili zilizosalia wanapambana vilivyo ili kuweza kupata pointi sita muhimu ambazo zitaweza kuwasaidia kukaa kwenye nafasi za juu.

  “Tunakwenda kucheza na Yanga kwa hamasa kubwa ya kushinda kwani Yanga tiyari wameshachukua ubingwa na nadhani hawatacheza kwa hari hivyo watatumia nafasi hiyo kuibamiza timu hiyo “Alisema Aurora.

Aidha aliwataka mashabiki wa soka mkoani hapa kujitokeza kwa wingi ili kuweza kuiunga mkono timu hiyo hasa kwenye mechi hiyo kwani kujitokeza kwao itasaidia kuipa hamasa timu hiyo kushinda au kupata matokeo mazuri.

Mwisho.









 



TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA NCHINI TFF LEO

TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA NCHINI TFF LEO

April 30, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI Aprili 30, 2013

 LIGI KUU YAINGIA RAUNDI YA 25
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea katika raundi yake ya 25 kesho (Mei Mosi) kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam, Turiani, Morogoro na Mlandizi.

Licha ya kuwa tayari Yanga imetawazwa kuwa mabingwa wa VPL msimu huu (2012/2013), mechi dhidi ya Coastal Union itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni moja kati ya zitakazovuta macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu nchini.

Mechi hiyo namba 172 itachezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara wakati mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam. Kamishna wa mechi hiyo ni David Lugenge kutoka Iringa.

Viingilio katik mechi hiyo itakayoanza saa 10.15 jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mchezo.

Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa African Lyon katika mechi namba 170 itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000 uko tayari kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons. Nayo Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani kuikabili Oljoro JKT kutoka Arusha.

Mwisho

MTANZANIA APEWA ITC KUCHEZA MSUMBIJI

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Yusuf Kunasa kucheza nchini Msumbiji.

 Shirikisho la Mpira wa Miguu cha Msumbiji (FMF) lilituma maombi TFF kumuombea hati hiyo Kunasa anayekwenda kujiunga na timu ya Estrela Vermelha da Beira inayocheza Ligi Kuu nchini humo.

Kunasa ambaye msimu huu hakuwa na timu (free agent) amejiunga na timu hiyo akiwa mchezaji wa ridhaa (amateur). Zaidi ya wachezaji kumi kutoka Tanzania hivi sasa wanacheza katika klabu mbalimbali nchini Msumbiji.

 Mwisho.
 
MECHI YA SIMBA, POLISI MOROGORO YAINGIZA MIL 18/-

Mechi namba 163 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa juzi (Aprili 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Simba kuibuka ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Morogoro imeingiza sh. 18,014,000.

Watazamaji 3,145 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 3,564,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 2,747,898.31.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 2,841 na kuingiza sh. 14,205,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 36 na kuingiza sh. 720,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 1,812,331.75, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 1,087,399.05, Kamati ya Ligi sh. 1,087,399.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 543,699.53 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 422,877.41.

 Boniface Wambura

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)