Release No. 027
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 17, 2014
WATANO WALALAMIKIWA KAMATI YA MAADILI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewalalamikia wana familia watano wa mpira wa miguu kwa Kamati ya Maadili kuhusiana na udanganyifu katika mtihani wa utimamu wa mwili wa waamuzi na usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi.
Riziki Majala na Army Sentimea ambao ni wakufunzi wa waamuzi, na Oden Mbaga na Samwel Mpenzu ambao ni waamuzi wanadaiwa kughushi nyaraka kuhalalisha mtihani huo kinyume cha taratibu.
Naye Sabri Mtulla analalamikiwa na TFF kwa madai ya kuidanganya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwa hakukuwa na pingamizi lolote juu ya usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi huku akijua wazi kuwa jambo hilo si kweli.
Kwa mujibu wa kanuni, malalamiko hayo yamefikishwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itachunguza ili kujiridhisha kama yana msingi au la. Ikibaini kuna kesi ndipo walalamikiwa watafika mbele ya kamati hiyo.
TWIGA STARS, ZAMBIA KUCHEZA MACHI 2
Mechi ya pili ya raundi ya kwanza kuwania Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Zambia (Shepolopolo) itachezwa Machi 2 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
Twiga Stars tayari imeingia kambini kujiandaa kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni. Twiga Stars chini ya Kocha Rogasian Kaijage inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Karume ambao ni wa nyasi za bandia kama ulivyo ule wa Azam Complex.
Shepolopolo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.
Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuiondoa Shepolopolo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Zimbabwe. Zimbabwe ilishinda mechi ya kwanza ugenini.
Wachezaji wa Twiga Stars waliopo kambini ni Amina Ali, Anastazia Katunzi, Asha Rashid, Donisia Minja, Esther Chabruma, Etoe Mlenzi, Everine Sekikubo, Fatuma Issa, Fatuma Makusanya, Fatuma Mustafa, Fatuma Mwisendi, Fatuma Omari, Flora Kayanda, Happiness Mwaipaja, Maimuna Mkane, Mwajuma Abdallah, Mwapewa Mtumwa, Pulkeria Charaji, Sherida Boniface, Sophia Mwasikili, Therese Yona, Vumilia Maarifa na Zena Said.