WAZIRI KAIRUKI AELEZEA VIPAUMBELE VYAKE

October 10, 2017
Greyson Mwase na Asteria Muhozya.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ameeleza vipaumbele  vyake katika Wizara kuwa ni pamoja na  udhibiti wa utoroshaji wa madini nchini, maslahi kwa wafanyakazi huku akiwataka watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu.

Kairuki ameyasema hayo mapema leo tarehe 10 Oktoba, 2017 jijini Dar es Salaam  alipozungumza na  watumishi wa Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake, waliopo Dar es Salaam na Makao Makuu  ya Wizara Dodoma. Lengo La kikao hicho lilikuwa ni kufahamiana na kupanga mikakati  ya kushirikiana ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa Uchumi wa nchi.

Taasisi zilizoshiriki katika kikao hicho ni pamoja na  Wakala wa Jiolojia  Tanzania (GST), Shirika la Madini la  Taifa (STAMICO), Chuo cha Madini Dodoma (MRI) pamoja na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini na Mpango wa Kuongeza Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (TEITI).

Amesema kuwa Sekta ya Madini  inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwataka wataalam wa madini kubuni mbinu za ukusanyaji wa maduhuli pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye uchimbaji madini.

Katika hatua nyingine aliwataka wataalam hao kubuni mikakati  ya kuzuia utoroshaji wa madini nchini ili nchi ipate mapato stahiki.Amewataka watumishi kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na kuwa wabunifu ili  sekta hiyo iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Naye Naibu  Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewakumbusha  watumishi kuzingatia Dira na Dhima ya Wizara  ikiwemo kufanya kazi kwa tija ili hatimaye  sekta ya madini iweze kuchangia katika uchumi wa nchi kwa kuwa mchango wa sekta husika bado ni kidogo.
 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki  (kushoto) akitoa maelekezo kwa watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake (hawapo pichani) Kulia ni Naibu  Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
 Kaimu Katibu Mkuu wa iliyokuwa  Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (kushoto mbele) pamoja na watendaji wengine wa Wizara wakifuatilia maelekezo  yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki. (hayupo pichani).
 Sehemu ya  watendaji wa Wizara ya Madini wakifuatilia maelekezo  yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki
 Naibu  Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia)  akifafanua jambo katika kikao hicho. Kushoto ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.
 Kamishna wa Madini Nchini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (kulia mbele) akieleza majukumu ya Wizara ya Madini kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki na Naibu  Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hawapo pichani) 
 Sehemu ya watumishi wa Wizara ya Madini, Makao Makuu Dodoma wakifuatilia maelekezo kutoka kwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (hayupo pichani) kwa njia ya video conference.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kushoto) na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo(kulia) wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa iliyokuwa  Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (hayupo pichani)

NISHATI YA UMEME NI KIUNGO MUHIMU KUCHOCHEA UWEKEZAJI WA VIWANDA”-DKT MWINUKA

October 10, 2017
NISHATI ya  umeme imeelezwa kuwa ni kiungo muhimu katika kuchochea uwekezaji wa viwanda hapa nchini ambao utasaidia kuinua kwa kasi uchumi ikiwemo maendeleo kwa watanzania.

Hayo yalibainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Dkt Tito Mwinuka hivi karibuni wakati akizungumza katika baraza kuu la 47 la wafanyakazi wa Tanesco  mjini hapa ambapo alisema kwa kutambua umuhimu huo wataihakikishia serikali malengo yao ya viwanda yanatimia.

Alisema kutokana na hali hiyo wataendelea kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana katika maeneo mbalimbali hapa nchini bila kuwepo kwa vikwazo vya namna yoyote ile ili azma hiyo iweza kutimia kwa vitendo na hivyo kuchochea kasi ya uchumi.

“Kama mnavyojua serikali ya awamu ya tano imeazimia kukuza uchumi nchi kufikia ule wa kati wa viwanda hivyo kufikia azma hiyo nishati ya umeme ni kiungo muhimu katika kuchochea uwekezaji wa viwanda ambao utasaidia harakati za maendeleo “Alisema

“Hivyo napenda kuihakikishia serikali kwamba tunatambua wajibu tulio nao katika kutimiza malengo hayo kwa kuongeza uwajibikaji na ufanisi kazini ambao ndio utakuwa dira ya kufikia mafanikio “Alisema.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema tokea kuanzishwa kwa baraza hilo limekuwa ni sehemu muhimu kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali kwa maslahi ya wafanyakazi ambao wamewaamini kuwawakilisha.

“Baraza hili limesaidia shirika kujua changamoto na kero
zinazowakabili mahala pa kazi na kwa pamoja ufumbuzi wake na
changamoto hizo zimepatiwa ufumbuzi kwa faida ya wafanyakazi na shirika kwa ujumla “Alisema.

Alisema serikali ya awamu ya tano imeazimia kukuza uchumi nchi kufikia ule wa kati wa viwanda hivyo ili kufikia azma hiyo nishati ya umeme nikiungo muhimu katika kuchochea uwekezaji wa viwanda ambao utasaidia harakati za maendeleo.

CHADEMA MANISPAA YA IRINGA WAPATA PIGO TENA

October 10, 2017
 Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi  CCM manispaa ya Iringa Said Rubeya akizungumza na wanachama wa chama hicho wakati wa kuwapokea wanachama wapya kutoka chama cha demokrasia na maendeleo manispaa ya Iringa akiwa sambamba na viongozi wa chama katika ofisi za CCM wilaya  pale sabasaba.
 Edwin bashir ni katibu wa chama cha mapinduzi manispaa ya Iringa akiwa na Baraka Kimata aliyekuwa katibu mwenezi na Diwani wa kata ya Kitwiru ambaye amejiunga rasmi na CCM pamoja Raymond kimata aliyekuwa kiongozi wa redbrigad manispaa ya Iringa na katibu mwenezi wa kata ya kitwiru naye kajiunga na CCM
Baraka Kimata aliyekuwa katibu mwenezi na Diwani wa kata ya Kitwiru ambaye amejiunga rasmi na CCM akionyesha kadi ya mpya ya chama cha mapinduzi CCM
Mbunge wa viti maalumu mkoa wa iringa kupitia chama cha mapinduzi CCM Ritta Kabati akizungumza jambo wakati wa kuwapokea wanachama hao wapya.


Na Fredy Mgunda,Iringa.

 Chama cha mapinduzi (CCM) manispaa ya Iringa kimeendelea kujiimalisha kwa kuvuna wanachama watano kutoka chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) manispaa ya Iringa wakiwa na mikakati ya kuja kulikomboa jimbo la Iringa mjini ambalo lipo chini ya chama cha CHADEMA.

Akizungumza wakati wa kuwapokea wanachama hao kutoka kata ya kitwiru mwenyekiti wa CCM manispaa ya Iringa Said Rubeya aliwapongeza wanachama kwa kutambua kazi inayofanywa na chama cha mapinduzi chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano DR John Pombe Magufuli.

“Mimi nimefurahi sana nyie kurudi nyumbani maana mtakuwa na msaada mkubwa sana katika kukijenga chama hapa manispaa ya Iringa ili tuweze kulikomboa jimbo hili katika uchaguzi ujao nah ii ndio mikakati yetu”alisema Rubeya

WAZIRI MPINA AANZA KAZI WIZARA MPYA YA MIFUGO NA UVUVI

October 10, 2017


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina akiweka sahini katika kitabu cha wageni cha Wizara hiyo mara maaba ya kuripoti.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega Akimsikiliza Waziri wa Wizara hiyo Mpya Mhe. Luhaga Joelson Mpina hayupo katika picha mara baada ya Mawaziri hao kuripoti katika Wizara hiyo katika Ofisi za Dar es Salaam.


Katika picha sehemu ya baadhi ya watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakifurahia jambo mara baada ya kuwapokea Mawaziri waliopewa dhamana ya wizara hiyo mpya, hawapo katika picha.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina akiongea na baadhi ya watumishi wa Wizara hiyo hawapo katika picha, katika Ofisi a Dar es Salaam mara baada ya kuripoti, katikati ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdalah Ulega kulia  ni Dkt. Yohana Budeba katibu Mkuu wa Wizara hiyo upande wa Uvuvi.