Na
Oscar Assenga, Lushoto.
MKUU wa wilaya ya Lushoto, Alhaji Majid Mwanga
amesema fitna ya michezo zikiwekwa pembeni mpira ukichezwa hakuna timu yoyote
mkoani Tanga itakayoweza kuifikia timu ya Lushoto Shooting ya Lushoto.
Mwanga alitoa kauli hiyo juzi wakati wa halfa ya
kuipongeza timu ya Lushoto Shooting kwa kufanikiwa kumaliza vema mzunguko wa
kwanza wa ligi ya mkoa.
Alisema licha ya timu hiyo kumaliza ligi hiyo wakati
katika nafasi nzuri lakini bado haijamfurahisha hivyo kuwataka viongozi kuhakikisha
wanaiandaa vema kwa ajili ya duru la pili pamoja na kuchukua ubingwa wa ligi
hiyo.
Aidha aliwataka viongozi wa timu hiyo kuwa wabunifu
kwa kubuni miradi ambayo inaweza kuwasaidia katika timu yao kuliko kuendelea
kuwategemea wafadhili ambao huenda wakati mwengine wasiwasaidie.
Akizungumzia suala la nidhamu,DC Mwanga alisema
hategemei kusikia nidhamu kwenye timu za wilaya hiyo hazipo wakati zikiwa zinashiriki
katika mashindano mbalimbali ikiwemo kuacha kuingia uwanjani na vitu
visivyostahili.
Alisema kazi kubwa ya wilaya hiyo ni kuhakikisha
wachezaji hao wanauzwa kwa gharama yoyote ili waweze kuleta mafanikio na
watakuwa tayari kuwauza mahali popote duniani kutokana na viwango vyao.
Awali akizungumza ,Katibu wa chama cha soka Mkoa wa
Tanga,Beatrice Mgaya aliwataka wachezaji wa timu hiyo kuzingatia nidhamu pamoja
na kujiandaa vya kutosha ili kuweza kutimiza azma yao ambayo yamejiwekea na
kuhaidi kuisapoti timu hiyo.
Katika halfa hiyo pia wadau wa michezo wilayani humo
waliweza kufanya harambee ya kuichangia timu hiyo ambapo jumla ya sh.milioni
3,480,000 zilipatikana ambapo kati ya hizo fedha taslimu zilikuwa ni 150,000 na ahadi
zilikuwa ni 3,330,000.
Naye Katibu wa timu ya Lushoto Shooting,Frank
Shemptemba alisema timu hiyo inakabiliwa
na changamoto mbalimbali ikiwemo kuwa na vifaa za kufanyia mazoezi ambayo
havikizi mahitaji ya wachezaji na mara nyingi wachezaji hujitafutia wenyewe
hali ambayo inasababisha kuwa na vifaa
ambavyo sio bora.
Shemptemba alisema pamoja na timu hiyo kufanya
vizuri kwenye mzunguko wa kwanza lakini pia waliwashukuru wadau mbalimbali akiwemo
mkuu wa wilaya Lushoto na Korogwe ,Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini,Steven
Ngonyani “Maji Marefu”Shabani Boznia,Julius Kimako kwa jitihada zao kuisapoti
timu hiyo.
Mwisho.
“Wizara itenge bajeti za kutosha kwenye Halmashauri”
Na Oscar Assenga, Lushoto.
WIZARA ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo imeshauriwa
kutenga bajeti ya kutosha katika Mashindano ya Shimisemita ambayo hushirikisha
timu kutoka halmashauri mbalimbali hapa nchini ili kuzipa ufanisi na ushindani
timu zinazoshiriki.
Ushauri huo ulitolewa jana na Afisa Michezo wa
wilaya ya Lushoto,Stephen Shemdoe wakati akizungumza na gazeti hili na kuongoeza
kuwa licha ya kufanya hivyo lakini pia alishauri kuwa uwepo utaratibu wa
kushirikisha kila idara ili kuleta hamasa zaidi kwa idara kufanya maandalizi.
Shemdoe alisema suala lengine ni kuhakikisha usafiri
kwa timu ambazo zinashiriki mashindano hayo zinawafikia walengo kwa wakati ili
kurahisisha ushiriki wao kwani zinapochelewa huwaondolea hamasa washiriki hali
ambayo huzifanya timu kushindwa kufanya vizuri licha ya kujiandaa.
Aidha alisema tiyari timu za halmashauri hiyo ambazo
zitashiriki mashindano hayo mwaka huu zimekwisha kuanza mazoezi tokea jana na
wanatarajia kucheza mechi mbalimbali za majaribio.
Shemdoe alisema ili mashindano hayo msimu huu yaweza
kuwa na msisimuko na ushindani waamuzi ambao wanachezesha mashindano hayo wawe
wale ambao wanatambulika na chama cha waamuzi nchini FRAT na wenye kujua
kutafsiri vema sheria kumi na saba za mpira wa miguu.
Afisa Michezo huyo alisema timu ambazo zilianza
kujiandaa ni za mchezo wa mpira wa miguu na mpira wa pete ambazo mwishoni mwa
wiki zinatarajiwa kucheza mechi za kujipima nguvu na timu za halmashauri ya
Korogwe.
Mwisho.