RC SHIGELLA MGENI RASMI TANGA CITY MARATHON JUMAMOSI WIKI HII MJINI TANGA

March 30, 2018


Mratibu wa Mashindano ya Riadha ya Tanga City Marathon, Juma Mwajasho kulia akitetea jambo na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya kuelekea mashindano hayo Jumamosi wiki hiikushoto ni Meneja wa Mkwabi Super Market ya Jijini Tanga ambao niwaandaaji wakuu wa mbio hizo,Kawkab Hussein na Katibu wa Chama cha Riadha Mkoani Tanga (RT) Hassan Mwagomba
Katibu wa Chama cha Riadhaa Mkoa wa Tanga (RT) Hassan Mwagomba akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uwepo wawashiriki kutoka Visiwa vya Shelisheli, Unguja na Pemba ambao watapat afursa ya kuonyesha umahiri wao kulia ni Meneja wa Mkwabi Super Marketya Jijini Tanga ambao ni waandaaji wakuu wa mbio hizo,Kawkab Hussein,

Meneja wa Mkwabi Super Market ya Jijini Tanga ambao ni waandaaji wakuu wa mbio hizo, Kawkab
Hussein akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano huu kuhusiana na zawadi zitakazotolewa msimu huu

Sehemu ya medali zitakazotolewa kwenye mashindano hayo

MKUU wa mkoa wa Tanga, Martine Shigella ametarajiwa kushuhudia mashindano ya riadha ya Tanga City Marathon msimu wa piliyanayotazamiwa kufanyika Jumamosi wiki hii mjini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mratibu wa Mashindano hayo, Juma Mwajasho alisema maandalizi yamekamilika kwa asilimia kubwa huku baadhi ya washiriki wakithibitisha kushiriki.

Alisema katika mashindano hayo msimu huu watazamia washiriki zaidi ya600 ambapo washindi watakabidhiwa zawadi mbalimbali zikiwemo medali ambazo zimeandaliwa na wadhamini wa mashindano hayo.

Aidha alisema mashindano hayo yatashirikisha wakimbaji kwenye umbali wa kilomita 21,10 na 5 ambapo wataanzia mbio hizo kwenye eneo la Mkwabi Super Market kuzunguka maeneo mbalimbali Jijini Tanga na kuishia eneo hilo.

“Lakini kwa mara ya kwanza washiriki wote watakaoshiriki mashindano hayo watapewa medali na mgeni rasmi kwenye mashindano hayo.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Riadhaa Mkoa wa Tanga (RT) Hassan Mwagomba alisema mashindano hayo pia yatashirikisha washiriki kutoka Visiwa vya Shelisheli, Unguja na Pemba ambao watapata fursa yakuonyesha umahiri wao.

Alisema njia zitakazopitia mashindano hayo zimeboreshwa zaidi kiusalama kwa wakimbiaji ili kuweza kuepukana na adhari zinazoweza kujitokeza wakati yakiendelea.

Naye kwa upande wake,Meneja wa Mkwabi Super Market ya Jijini Tanga ambao ni waandaaji wakuu wa mbio hizo,Kawkab Hussein alisema msimu huo wameboresha mashindano hayo kwa kutoa zawadi kwa mshindi wa kwanza hadi wa kumi.

Alizitaja zawadi zinazotolewa kuwa ni mshindi wa kwanza km 21 atapata700,000 wa pili 500,000, huku mshindi wa tatu akipata 300,000 huku wengine kuanzia wa nne hadi wa kumi watapata kifuta jasho cha 50,000.

Hata hivyo alisema katika kilomita 10 mshindi wa kwanza atapata 250,000, wa pili 150,000 na wa tatu 100,000 huku washindi wa kuanzia nafasi ya nne mpaka 10 watapewa 30,000 pia kutakuwa na vituo maalumu kwaajili ya kutoa huduma ya maji kwa wakimbiaji.

WATALII WENGI WAZIDI KUTEMBELEA TANZANIA - WAZIRI KIGWANGALLA

March 30, 2018


Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akipokelwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudensi Milanzi mjini Dodoma jana ambapo alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa 25 wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo.
.............................................................................

Tanzania imefanikiwa kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,284,279 mwaka 2016 hadi kufikia 1,327,143 mwaka 2017 hali iliyopelekea kuongezeka kwa mapato ya Serikali.

Akizungumza wakati wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii uliofanyika mjini Dodoma, Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema Wizara yake itaendelea kuvutia watalii wengi zaidi ili kukuza utalii na kuongeza pato la Taifa.

“Mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani Bilioni 2.1 mwaka 2016 hadi Dola za Kimarekani Bilioni 2.2 mwaka 2017” alisema Dk. Kigwangalla.

Akifafanua Dkt. Kigwangala amesema lengo la Serikali ni kuona mafanikio haya yanazidi kuimarika, hivyo kila mtumishi katika Wizara hiyo lazima atimize wajibu wake ipasavyo katika kutimiza lengo la Wizara hiyo ambalo ni kuhifadhi na kusimamia maliasili, malikale na kuendeleza utalii.

Aliongeza kuwa ili kufanikisha majukumu ya Wizara hiyo ipasavyo ni muhimu kuwa na bajeti ambayo itawezesha kushughulikia changamoto za migogoro ya mipaka katika maeneo ya hifadhi, kufanya mapitio ya Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali, upungufu wa watumishi, uhaba wa vitendea kazi, kutoa elimu ya maadili na kusimamia watumishi.

Alisema Wizara yake itaendelea na mapambano dhidi ya ujangili, biashara haramu ya nyara, magogo na kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria kwa watumishi wote watakaogundulika kukiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kushiriki katika vitendo hivyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudensi Milanzi amesema kuwa Wizara hiyo itazingatia ushauri utakaotolewa na Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ili kuongeza tija katika kutatua changamoto zinazojitokeza.

“Wizara itaendelea kupambana dhidi ya ujangili, biashara haramu ya nyara na magogo na kuwachukulia hatua kali watumishi wote watakaogundulika kukiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kushiriki katika vitendo hivyo “ Alisisitiza Meja Jenerali Milanzi.

Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 iliendelea na utaratibu wa kuendeleza watumishi katika mafunzo ya aina mbalimbali kama ifuatavyo:-Jumla ya watumishi wanne (4) wanahudhuria mafunzo ya muda mrefu nje na ndani. Aidha, mtumishi mmoja(1) yupo nje ya nchi.

Watumishi wengine kumi na moja (11) walihudhuria mafunzo ya muda mfupi. Mafunzo haya yalihusu watumishi wa kada mbalimbali.

Jumla ya watumishi saba (7) wamehudhuria mafunzo ya ujasiliamali unaohusiana na maandalizi ya kustaafu. Aidha, Wizara bado inaendelea na utaratibu wa kuwaandaa watumishi wote wanaokaribia kustaafu kuhakikisha wanapata mafunzo hayo.

Akifunga mkutano huo wa siku moja Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Japhet Hasunga aliwataka watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa ili kufikia lengo lililokusudiwa la uhifadhi wa maliasili, malikale na kuendeleza Utalii.

Waziri wa Mali Asili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla akihutubia Wafanyakazi wa Wizara hiyo wakati wa Mkutano wa 25 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika mjini Dodoma jana.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Maj. Gen. Gaudensi Milanzi akizungumza na Wafanyakazi wa Wizara hiyo wakati wa mkutano huo.


Baadhi ya wajumbe wa mkutano huo wa baraza wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi, Mhe. Dk. Hamisi Kigwangalla.


Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. HamisI KigwangalLa (katikati) akiimba wimbo wa mshikamano pamoja na Katibu Mkuu Wizara hiyo, Maj. Gen. Gaudensi Milanzi pamoja na viongozi wengine wa Shirikisho la Wafanyakazi.


Baadhi ya ya Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi wa Wizara ya Maliasili na Utalii Wakiimba wimbo wa mshikamano wa wafanyakazi wakati wa mkutano huo uliofanyika mjini Dodoma.


Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akisalimiana na Katibu Mteule wa Tughe Tawi la Wizara ya Maliasili na Utalii, William Mwita muda alipowasili kufunga mkutano huo wa baraza. Katikati anayemtambulisha kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi.


Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara wizara hiyo, Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi muda mfupi kabla ya kufunga mkutano huo wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.


Naibu Waziri wa Malisili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na watumishi wa wizara hiyo wakatika akifunga mkutano huo wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.



Baadhi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Wizara hiyo walioshiriki baraza hilo.

Baadhi ya watumishi wa Wizara na wajumbe wa baraza hilo.