February 21, 2014

NANI KUKALIA USUKANI WA LIGI KUU LEO, YANGA AU MBEYA CITY?????

 Na Reporter wa Sufianimafoto, Dar
TIMU ya Mbeya City wakifungwa na Coastal na Yanga wakiibuka na ushindi dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa LEO katika mechi ya Ligi Kuu Bara, watakuwa wametoa mwanya kwa wanajangwani hao kukalia usukani wa ligi hiyo.
Katika mfulilizo wa ligi hiyo, Mbeya City watacheza na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Yanga wakiwa katika Dimba la Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwakaribisha Ruvu Shooting.
Ushindi kwa Yanga utawawezesha kuongoza katika msimamo wa ligi hiyo kwa saa 24 kabla ya Azam FC keshokutwa kucheza na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na kutegemea matokeo ya mchezo huo.
Azam FC kwa sasa wanaongoza msimamo huo kutokana na kufikisha jumla ya pointi 36, wakifuatiwa na Yanga na Mbeya City ambao kila mmoja ana pointi 35 wakiwa na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Yanga wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kuifunga timu hiyo bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, ambayo kwa sasa inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 25.
February 21, 2014

MATOKEO KIDATO CHA NNE HADHARA

Naibu Katibu mkuu NECTA, Dkt. Charles Msonde
MATOKEO ya Kidato cha nne kwa 2013 yametangazwa huku watahiniwa 235,227 wakifaulu mtihani huo ikiwa ni sawa na asilimia 58.25 ya waliofanya mtihani huo. Jumla ya wanafunzi 404,083 walifanya mtihani huo huku waliofaulu kwa daraja la I-III wakiwa wanafunzi 74,324 sawa na asilimia 21.09 ya waliotahiniwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) leo jijini Dar es Salaam, shule 10 za sekondari zilizofanya vizuri (zilizoongoza) ni pamoja na St. Francis Girls, Marian Boys, Feza Girls, Precious Blood, Canossa, Marian Girls, Abbey, Anwarite Girls, Rosmini na Don Bosco Seminary.
Akitangaza matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari, Kaimu katibu mkuu wa NECTA, Dk. Charles Msonde, alisema katika matokeo ya mwaka 2013, shule kumi za sekondari zilizofanya vibaya zaidi ni pamoja na Singisa Sekondari, Sekondari ya Hurui, Sekondari ya Barabarani, Sekondari ya Nandanga, Sekondari ya Vihokoli, Sekondari ya Chongoleani, Sekondari ya Likawage, Sekondari ya Gwandi, Sekondari ya Rungwa na Sekondari ya Uchindile.

RAIS MALINZI AAHIDIWA USHIRIKIANO CAF

February 21, 2014
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemwahidi ushirikiano Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.

Ahadi hiyo imetolewa leo (Februari 21 mwaka huu) makao makuu ya CAF jijini Cairo na Rais wa shirikisho hilo Issa Hayatou alipokutana na Rais Malinzi aliyekwenda kujitambulisha huko.

Utambulisho wa Rais Malinzi kwa Rais Hayatou uliongozwa na mtangulizi wake Leodegar Tenga ambaye aliiongoza TFF kwa vipindi viwili kuanzia 2004 hadi 2013.

Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), alimweleza Rais Hayatou kuwa uchaguzi wa TFF ulikuwa mzuri.
February 21, 2014
KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Mvomero, imedaiwa kumvua Uongozi Katibu wa Wilaya wa Chama hicho hicho wilayani humo, Mrisho Ramadhani, kwa madai ya kukisaliti Chama.


Habari toka ndani ya kikao cha siri kilichoketi Ofisi ya Wilaya zinadai, Kamati ilimvua ukatibu Mrisho kutokana na kufanya maamuzi ya kukiunganisha Chadema na Vyama vingine bila ridhaa ya Chama, na kumdharilisha Diwani wake, Luka Mwakambaya.

Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina Mtoa habari wetu alisema, Mrisho amebakiwa na Ukatibu Mwenezi wa Wilaya, amabapo suala lake limepelekwa kwenye Mkutano Mkuu akajadiliwe na kutolewa maamuzi.
February 21, 2014

MWANAHARAKATI ATAKA SERIKALI KUSITISHA MCHAKATO WA KATIBA

Raisa  Said, Tanga
 
Katika hatua inayotishia mchakato wa upatikanaji katiba mpya, mwanaharakati mmoja wa Tanga amefungua shauri linaloitaka serikali kusitisha mchakato  hadi hapo itakapofanyia marekebisho ya masuala ambayo amedai kuwa yanakiuka katiba ya sasa, utawala bora, uwazi, demokrasia na haki ya kijamii.

Mwanaharakati huyo, Dr. Muzamil Kalokola, ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Kuhifadhi Mawazo ya Mwalimu Nyerere alifungua shauri hilo juzi katika Mahakama Kuu jijini Tanga dhidi ya  Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba Kama mdaiwa wa Kwanza, Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kama mdaiwa wa Pili na Mwanasheria wa Serikali kama mdaiwa wa tatu.

Mdai huyo anataka Mahakama itoe  amri kumzuia Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba kutoendelea na mchakato huo hadi hapo shauri hilo litakaposikilizwa.

Pia ameitaka mahakama kutoa amri na  kutamka kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekiuka katiba ya sasa kwa kutoa uwezo ambao juu ya uwezo wao wa kikatiba hususan masuala ambayo yanayohusiana na orodha iliyoko katika Nyongeza ya pili ya Katiba hiyo.
February 21, 2014


TANGA TUPO IMARA KUIKABILI KILIMANJARO.
Na Oscar Assenga,Tanga.
Timu ya Mkoa wa Tanga ipo kwenye mazoezi makali ikijiwinda na mchezo wake na timu ya Kilimanjaro kwenye mechi ya mashindano ya mikoa itakayoanza Jumapili kwenye dimba la CCM Mkwakwani mkoani hapa.

Akizungumza na mtandao wa Tanga Raha,Meneja wa timu hiyo,Martin Kibua alisema maandalizi ya mechi hiyo yanaendelea vizuri kwa timu hiyo kuwa imara ili kuweza kuwakabili wapinzani wao hao.

Kibua alisema anaimani kubwa na kikosi hicho kitafanya vizuri hasa kutokana na kambi ambayo waliiweka wiki moja mkoani hapa wakijiandaa na mchezo huo.

Kikosi cha timu ya mkoa wa Tanga kinaundwa na wachezaji 20ambao wamedhamiria kuipa ushindi timu hiyo kwenye mchezo huo.

  “tunaimani kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mpambano huo kwani dhamira yetu kubwa ni kupata matokeo mazuri hasa tukiwe kwen ye dimba letu la hapa nyumbani “Alisema Kibua.

Viingilio kwenye mechi hiyo vinatarajiwa kuwa ni sh.2000 ili kuweza kuwapa fuksa mashabiki mbalimbali wa soka kujitokeza kushuhudia mchezo huo.

February 21, 2014
UCHAGUZI WA KAMATI YA UTENDAJI YA TASWA

Uchaguzi wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) utafanyika Machi 2, 2014 jijini Dar es Salaam.



Kwa mujibu wa taarifa zilizoifikia Tanga Raha blog kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi huo,Boniface Wambura zimeelewa kuwa fomu kwa ajili ya waombaji uongozi zinaanza kutolewa Jumatatu (Februari 24 mwaka huu) kwenye ofisi za Idara ya Habari. Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Alhamisi (Februari 27 mwaka huu) saa 9 alasiri.



Ada kwa wagombea wa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mhazini na Mhazini Msaidizi ni sh. 50,000 kwa fomu. Nafasi za wajumbe wa Kamati ya Utendaji fomu zinapatikana kwa sh. 20,000.



Kamati ya Uchaguzi inawahimiza wanachama wa TASWA kujitokeza kwa wingi kugombea, lakini vilevile waisome vizuri Katiba ya chama chao.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI LEO FEBRUARY 21, 2014

February 21, 2014
Release No. 028
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 21, 2014

TWIGA STARS, ZAMBIA SASA KUCHEZA FEB 28
Mechi ya pili ya raundi ya kwanza kuwania Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Tanzania (Twiga Stars) na Zambia (Shepolopolo) sasa itachezwa Februari 28 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Twiga Stars tayari ipo kambini kujiandaa kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni. Twiga Stars chini ya Kocha Rogasian Kaijage inafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Karume ambao ni wa nyasi za bandia kama ulivyo ule wa Azam Complex.

Shepolopolo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Februari 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nkoloma jijini Lusaka.

Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuiondoa Shepolopolo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Zimbabwe. Zimbabwe ilishinda mechi ya kwanza ugenini.
February 21, 2014
SALAMU ZA UKARIBISHO ZA MKURUGENZI MTENDAJI WA TAWODE, BI. FATUMA HAMZA  KATIKA UFUNGUZI WA MAFUNZO YA UONGOZI NA UTAWALA BORA KWA WAHESHIMIWA MADIWANI WANAWAKE KUTOKA HALMASHAURI ZA MKOA WA  TANGA, TAR 11-13 FEBRUARY 2014.


Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Naibu Waziri , Ofisi ya Makamu wa Raisi, Mazingira,  Ummy Ally Mwalimu, Wakuu wa Wilaya, Waheshimiwa Madiwani wanawake  kutoka Halmashauri Mbalimbali, Watendaji wa serikali, Ndugu wawezeshaji, Waandishi wa Habari na Ndugu washiriki,  namshukuru mungu kwa kutuamsha na kukutana pamoja siku ya leo.
Habari za asubuhi na karibuni sana katika Mafunzo ya Uongozi na Utawala Bora (kwa ajili ya Maendeleo ya Wanawake na watoto) kwa waheshimiwa madiwani wanawake kutoka Wilaya nane za Mkoa wa Tanga ambazo ni Mkinga, Muheza, Korogwe,  Lushoto, Handeni, Kilindi, Pangani na Tanga.