Madereva 20 kuchukua kesho mbio za magari Tanga.

July 06, 2013
Oscar Assenga,Tanga.
MADEREVA maarufu  20 wa mbio za magari wa  mkoa wa Tanga  wakiwamo wanawake wawili kesho Jumapili watachuana vikali katika michuano ya “Chillly Will 77 Sprint Rally “.

Mwenyekiti wa Chama cha Mbio za Magari Mkoa wa Tanga,Hussein Moor(Makoroboi) alisema  kuwa mgeni rasmi katika michuano hiyo atakuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga,Halima Dendego.

Alisema michuano hiyo itaanza kayofanyikia Pongwe nje kidogo ya mji wa Tanga  katika eneo la viwanda.

Aliwataja washiriki wa michuano hiyo kuwa ni pamoja na Ally
Kiraka,Twalib Hatib,Said Baghoza,Tonny Kurban,Utu Nirmal,Akida Saad,Ally Asgar Papuu,Shani Abbas,Nail Nail Haria Alli Hamud,Hashim Ramzani na Faizn Ramzani.

Meneja Uhusiano  wa kinywaji cha Chilly Willy,Meshack Nzowa alisema kuwa wameamua kudhamini mashindano hayo ili kutoa burudani kwa wakazi wa Jiji la Tanga lakini pia kuhamasisha vijana kushiriki mbio za magari.

                    MWISHO

"Mtonga FC Mabingwa wa Gambo Cup"

July 06, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.
TIMU ya Mtonga FC jana ilifanikiwa kuchukua Ubingwa wa Kombe la Gambo Cup na kukabidhiwa Kombe la Mashindano, Ngombe,Jezi seti 1 na mpira miwili baada ya kuwafunga mabingwa wa soka wilaya ya Korogwe,Korogwe United mabao 2-1,katika mechi ya fainali iliyochezwa uwanja wa Chuo cha Ualimu wilayani hapa.

Mashindano hayo yalianzishwa na Mkuu wa wilaya ya Korogwe,Mrisho Gambo na kufadhiliwa na Benki ya NMB yenye lengo la kukuza na kuibua vipaji vya wachezaji wachanga wilayani humo na yalishirisha timu 85 kutoka tarafa nne ambapo yaligharimu kiasi cha sh.milioni 21.4.



Kabla ya kuanza mpambano huo kulikuwa na burudani kutoka kwa wasanii chipukizi wa bongofleva huku dokta Nyau akitoa burudani kwa wadau wa soka waliojitokeza kushuhudia mechi hiyo ambayo ilikuwa na upinzani mkubwa kutokana na historia ya timu hizo.

Mtonga Fc ndio kuweza kupata bao la ambalo lilifungwa na Seleman Msagama katika dakika ya 19 baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Miraji Mtoi na kupiga shuti kali ambalo lilimshinda mlinda mlango wa Korogwe United Feruzi Ponda na kutinga wavuni.

Baada ya bao hilo kuingia Korogwe United waliweza kujipanga  huku wakipeleka mashambulizi langoni mwa Mtonga Fc na kuweza kufanikiwa kuwasadhisha bao hilo dakika ya 33 kupitia Dullah Shauri aliyetumia uzembe wa mabeki kupachika wavuni bao hilo.

Bao hilo liliweza kuzidisha hasira kwa timu ya Mtonga Fc ambapo waliweza kujipanga mithili ya mbogo aliyejeruhiwa hali iliyozaa matunda katika dakika ya 43 kwa kupata bao lililofungwa na Chale Dafa baada ya kuunganisha krosi iliyopigwa na Mohamed Bunu.




Mshindi wa pili ambaye ni timu ya Korogwe United walikabidhiwa Mbuzi wawili,jezi seti 1 na mpira mmoja,mshindi wa tatu ilichukuliwa na Bungu Kibaoni ambao wakipata Mbuzi mmoja,jezi seti moja na mpira mmoja huku mshindi wa nne mpaka wa nane wakipewa jezi seti moja na mpira mmoja na mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Chiku Gallawa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadhi hizo,Gallawa aliwapongeza benki ya NMB kwa kufadhili mashindano hayo ambayo yalileta mwamko mkubwa kwa vijana kupenda soka wilayani humo na kuwataka umoja waliouonyesha katika michuano waupeleke mpaka kwenye shughuli za maendeleo.



Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi,Mratibu wa Mashindano hayo Zaina Hassani alisema mashindano hayo yalikuwa ya aina yake katika wilaya hiyo ambayo yaliweza kushirikisha timu nyingi na hajawahi kutokea na kumpongeza mkuu huyo wa wilaya na kutaka wadau wengine waige mfano huo na kudhamini ligi nyengine wilayani humo.

Mwisho.