MKUU WA KITUO CHA POLISI CHA KILINDI EDWARD LUSEKELO APIGWA RISASI

October 25, 2013
Na Oscar Assenga,Kilindi.
Askari wa Jeshi la Mgambo wa Kijiji cha Lwande Wilayani
hapa,Salum Mgonje amekufa kwa kushambuliwa na mapanga na kundi la watu waliokuwa wakipinga kitendo cha mwenzao kulipishwa ushuru wa manunuzi ya zao la hiliki wa Serikali ya Kijiji.

Mashambulizi hayo baadaye yalizusha mapigano baina ya kundi la watu waliokuwa wakimsaidia mfanyabiashara huyo na askari wa jeshi la polisi walipokwenda jioni kuwakamata waliohusika na mauaji ya mgambo.

Katika mapigano hayo,Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kilindi Edward Lusekelo ambaye aliongoza askari waliokwenda kuwakamata waliohusika na mauaji ya Mgambo alijeruhiwa kwa kupigwa risasi ya bunduki aina ya ShortGun.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamnada wa Polisi wa Mkoa wa Tanga,Constantine Massawe ni kuwa askari wa mgambo aliuawa juzi mchana katika kijiji cha Lwande wakati mkuu wa kituo alijeruhiwa saa 2.30 jioni kijijini hapo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi,Selemani Liwowa alisema chanzo cha mapigano hayo mfanyabiashara huyo kutoka Kijiji cha Lulago Kata ya Lwande kwenda Kijiji cha Lwande kununua hiliki ambapo baada ya kukaidi kulipa ushuru mgambo alilazimika kumtia msukosuko ili aweze kulipa kama ilivyo sheria ya kijiji.

“Ndipo zikatokea purukushani baina mgambo na wafanyabiashara ambapo baadaye walimshambulia kwa mapanga na kisha kumuua”alisema Liwowa.

Alisema taarifa za mauaji ya mgambo zilizpofika kituo cha Polisi
ilimlazimu mkuu wa kituo kuongoza kikosi kilichokwenda kijiji cha
Lwande kwa ajili ya kuwasaka waliohusika ndipo walipotokea
likajitokeza kundi la watu wenye silaha wakaanza kuendesha mapigano na askari wa jeshi la Polisi.

Akithibitisha habari hizi,Kamanda Massawe alisema tayari watu wanne wanashikiliwa kuhusiana na tukio hili huku mkuu wa kituo cha Polisi akiwa amekimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo kwa ajili matibabu.

Alisema mkuu huyo wa kituo amejeruhiwa mbavuni na mkononi ambapo inaonekana alifyatuliwa zaidi ya risasi tatu ambapo wengine waliojeruhiwa ni afisa mtendaji wa kata ya Lwande na askari mwingine wa Mgambo.