NIC Yatunukiwa Cheti Cha Superbrand Kwa Mafanikio Sekta Ya Bima Nchini Tanzania.

August 14, 2023

 Katika jitihada za kutambua ufanis na utoaji wa huduma bora katika sekta ya bima nchini, Shirika la Bima la Taifa, NIC, imepokea cheti cha ubora kutoka kwa taasisi ya Superbrands kuwa kinara katika sekta hiyo ikiwa ni baada ya kufanyika kwa utafiti na tathmini ya kina ya huduma zake. Heshima ya kipekee ni uthibitisho kujizatiti imara kwa NIC katika weledi, ubunifu, na utoaji wa bidhaa na huduma za bima za ubora wa hali ya juu kuwahudumia Watanzania nchini kote.


Kutambuliwa kwa NIC na Superbrand kunaonesha namna kampuni ilivyojikita katika kuboresha viwangu vya juu vya ubora, kuwajali wateja, na kuzingatia weledi. Tukio hili si mafanikio tu kwa NIC, bali inaonyesha jitihada za makusudi na mchango wa pamoja unaonyeshwa na wafanyakazi, washirika, na wadau wote.

Shirika la bima la Taifa, NIC, kwa muda mrefu linajiendesha kama kinara katika soko la huduma za hisa nchini, likihudumia mahitaji ya wateja kwa kuwapatia huduma tofauti za bima ambazo zinalinda Maisha, mali, na biashara zao. Cheti hiki cha kutambuliwa na Superbrands, kinaiweka NIC kwenye nafasi ya kuwa shirika linaloaminiwa na mtoaji wa huduma endelevu za bima, na kuonyesha kujizatiti kwakwe kuhakikisha usalama katika masuala ya kifedha na kuwapatia utulivu wa akili kwa wateja wake.

Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dkt. Elirehema Doriye ameonyesha furaha yake kwa mafanikio ya kutambuliwa na cheti hiki cha heshima kwa kusema kuwa, “ni heshima kubwa kupokea cheti cha utambulisho kutoka kwa taasisi ya Superbrand. Kutambuliwa huku ni uthibitisho wa kazi kubwa tunayoifanya Pamoja na kujitolea kwa kila mfanyakazi wa NIC, na inatuongezea chachu zaidi ya kuendelea kuboresha viwango vya huduma katika ya bima Tanzania.”

Kujitolea kwa NIC katika shughuli zake kwa kuzingatia weledi ni wa namna ya kipekee. Shirika limejizatiti kuendelea kuleta maendeleo chanya kwa jamii na kuchangia kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya Tanzania. Kutambuliwa na Superbrand kumekuja wakati sahihi na kuongeza ari zaid ya NIC kuendeleza ubora wa viwango vya hali ya juu, kutumia ubunifu na teknolojia ili kuwapatia wateja huduma wanazohitaji na kusaidia sekta nzima kusonga mbele zaidi.

Wakati NIC ikisonga mbele, pia inaipokea heshima ya cheti hiki cha ubora kama changamoto ya kuwa bora zaidi na kuendelea kutoa huduma za kipekee, kuborasha ubunifu, na kuchangia maendelea chanya kwa ukuaji na ustawi wa Tanzania.


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa, NIC, Dkt. Elirehema Doriye (kulia) akiwa anapokea cheti cha kutambuliwa kwa huduma na bidhaa bora kutoka kwa Mkurugenzi wa Ukanda wa Afrika Mashariki Miradi ya Superbrands Bwana Jawad Jaffer (kushoto) wakati wa hafla wa utoaji wav yeti iliyofanyika katika hoteli ya Hyatt Regency the Kilimanjaro jijini Dar es Salaam. Ni mara ya kwanza NIC kutambuliwa na taasisi ya Superbrands kama kinara katika utoaji wa huduma na bidhaa za bima kwa sekta hiyo nchini.






SERIKALI INAENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA-MAJALIWA

August 14, 2023

 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii nchini zikiwemo za afya, hivyo amewataka wananchi waendelee kuipa ushirikiano.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Agosti 14, 2023) wakati akizungumza na wananchi baada kuweka jiwe la msingi Hospitali ya Wilaya ya Newala akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara. Amesema kuwa Serikali imedhamiria kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Newala asimamie ipasavyo upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa sababu Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia huduma hiyo.

Waziri Mkuu amesema Serikali kila mwezi inapeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa hivyo hatarajii wananchi wanaokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wanakosa dawa. Amewasisitiza wapeleke dawa kulingana na magonjwa yanayopatikana katika wilaya hiyo.

Awali, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt… Matiko George alisema Serikali imetoa shilingi bilioni 2.85 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo jengo la maabara, wagonjwa wa dharura, huduma ya mama na mtoto, mionzi, utawala, wodi za wanawake, wanaume na watoto.

Alisema faida za mradi huo ni pamoja na punguzia gharama kwa wananchi ambao walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika halmashauri za jirani za Newala Mji, Masasi na Hospitali ya Rufaa ya Ndanda.

“Hospitali hii itakuwa na uwezo wa kufanya huduma za upasuaji kwa akina mama watakaokuwa wanapata changamoto ya kujifungua kwa njia ya kawaida. Pia huduma za za afya za kinywa na macho nazo zitatolewa hospitalini hapa.”

Pia, Dkt George amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na kupeleka vifaa tiba vya kisasa katika hospitali za wilaya pamoja na vituo vya afya jambo linalowaongezea ari ya kufanya kazi kwa bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha, kuimarisha na kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya nchini. Vifaa tiba vilivyoko katika jengo la kutolea huduma za dharura kwenye hospitali hii vinalingana na vile vinavyotumika katika hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili.”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Newala Matiko Stephen, wakati alipokagua na kuweka jiwe la msingi la Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Newala, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Mtwara Agosti 14, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa ukumbi wa mikutano ya shule ya sekondari Nambunga, iliyopo wilayani Newala, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Mtwara Agosti 14, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikata utepe kuzindua ukumbi wa mikutano ya shule ya sekondari Nambunga, iliyopo wilayani Newala, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Mtwara Agosti 14, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua ujenzi wa jingo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Mji wilayani Newala, akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Mtwara Agosti 14, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



WANAFUNZI WAHIMIZWA KUPENDA MASOMO YA SAYANSI

August 14, 2023

 

Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Maulilio Kipanyula akikabidhi majarida ya OYLA Africa kwa wawakilishi wa wanafunzi wa shule zilizopokea msaada wa majarida hayo kutoka kampuni ya Baobab Shalom Limited katika hafla fupi iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Msalato Jijini Dodoma tarehe 14 Agosti 2023.
…..

Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Maulilio Kipanyula amewahimiza wanafunzi wa kitanzania kupenda masomo ya sayansi na teknolojia kutokana na mchango wake katika kuleta maendeleo ya nchi.

Prof. Kipanyula amesema Sayansi na Teknolojia imeleta mapinduzi makubwa kitaifa na kimataifa na hasa katika sekta za elimu, habari, biashara na huduma mbali mbali za kijamii.

Ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita imeweka kipaumbele katika sekta ya elimu ambapo imewekeza kwa kiwango kikubwa ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa vya kujifunzia na kufundishia hivyo kuwahamasisha wanafunzi kujifunza kwa bidii na kuwa wabunifu.

Alikuwa akizungumza katika hafla fupi ya kugawa majarida 700 yanayofahamika kama OYLA Africa ambayo yametolewa na kampuni ya Baobab Shalom Limited ya jijini Dar es Salaam kufuatia Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yaliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye na Mkurugenzi wa Baobab Shalom Limited Bw. Yev Semikov katika ofisi za TEA jjijini Dodoma tarehe 14 Agosti 2023.

Bw. Semikov amesema lengo la Majarida hayo ni kuwezesha wanafunzi wanaoyatumia kuwa wabunifu na wadadisi kwa lengo la kuboresha mazingira na maisha yao kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye ameshukuru kampuni ya Baobab Shalom Limited kwa kutoa msaada huo wa majarida kupitia Mfuko wa Elimu unaosimamiwa na TEA na kuongeza kuwa TEA iko tayari wakati wote kushirikiana na wadau wa elimu na kuwahakikishia kuwa misaada ya elimu inayopita kwenye Mfuko wa Elimu wa Taifa inasimamiwa kikamilifu na kutumika kama ilivyokusudiwa.


Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Maulilio Kipanyula akikabidhi majarida ya OYLA Africa kwa wawakilishi wa wanafunzi wa shule zilizopokea msaada wa majarida hayo kutoka kampuni ya Baobab Shalom Limited katika hafla fupi iliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Msalato Jijini Dodoma tarehe 14 Agosti 2023.

Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Baobab Shalom Limited Bw. Yev Semikov (wa pili kushoto) wakisaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kwa ajili ya kugawa majarida 700 ya OYLA Africa yanayohimiza wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hisabati katika hafla fupi iliyofanyika jjijini Dodoma tarehe 14 Agosti 2023.
Mkurugenzi Mkuu wa TEA Bi. Bahati Geuzye (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Baobab Shalom Limited Bw. Yev Semikov (wa pili kushoto mstari wa mbele) baada ya kusaini Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kwa ajili ya kugawa majarida 700 yanayohimiza wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hisabati katika hafla fupi iliyofanyika jjijini Dodoma tarehe 14 Agosti 2023.


Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Maulilio Kipanyula ( wa pili kulia mstari wa mbele) akipokea jarida la OYLA Africa kutoka kwa Mkurugenzi wa Baobab Shalom Limited Bw. Yev Semikov (wa pili kushoto). Majarida hayo yanalenga kuhimiza wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hisabati.


Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Msalato ya jijini Dodoma walioshiriki hafla ya kupokea Majarida ya OYLA Africa kwa ajili ya kuhimiza wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hisabati yaliyotolewa na Kampuni ya Baobab Shalom Limited ya jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wanafunzi katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi wakiwa wameshika magazeti ya OYLA Africa yaliyotolewa Kampuni ya Baobab Shalom Limited ya jijini Dar es Salaam.

AFYA CHECK KWA KUSHIRIKIANA NA OFISI YA MBUNGE WA JIMBO LA TANGA KUZINDUA KAMBI MAAALUMU YA MATIBABU BURE TANGA

August 14, 2023
MBUNGE wa Jimbo la Tanga (CCM) Ummy Mwalimu ambaye pia ni Waziri wa Afya akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari mapema leo
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Japhet Simeo akizungumza wakati wa mkutano huo

Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shiloo akizungumza




TAASISI ya  Afya Check kwa kushirikiana na ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga wanatarajia kuzindua kambi maalum ya kupima afya  bure kwa wananchi wa Jiji la Tanga  kwa siku tano ikiwa ni mpango wa kuihamasisha  jamii kuwa na desturi ya kupima afya zao mara kwa mara ili pale wanapogundulika kuwa na matatizo mbalimbali waweze kupata matibabu ya haraka.


Akizungumza na waandishi wa Habari leo Waziri wa Afya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amesema kambi hiyo itafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia Augost 21 ambapo wananchi 5000 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi katika magonjwa ya Kisukari,  shinikizo la damu, Saratani ya tezi dume,saratani ya mlango wa kizazi.

Waziri Ummy amesema magonjwa yatayopimwa ni yale yanayoambukiza na yasiyoambukizwa na endapo mtu atakutwa na ugonjwa atapatiwa tiba bure na kwa wale ambao watakuwa na magonjwa yatakayohitaji  upasuaji watapatiwa tiba watakapokuja madaktari bingwa huku akiipongeza banki ya CRDB ambao ndio wadhamini wakuu wa kambi hiyo. 

"Takwimu inaonesha wapo watu laki mbili ambao hawajajitambua afya zao katika upimaji wa vvu, tunawashauri na kuwahamasisha watu kupima na kama watu wote ambao wana maambukizi wangekuwa wanafuata masharti ya kumeza dawa tunaweza kuutokomeza kabisa" amesema.

"Niwapongeze sana sana wadau wetu wakubwa CRDB, benki yetu kwa kujitolea na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan,  katika kufadhili huduma zinazowasaidia wananchi" amebainisha.

"Sasa, nitoe wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Tanga kujitokeza, wilaya zote kujitokeza kuja kupima katika viwanja vya shule ya sekondari ya Usagara, lengo ni watu 5000 lakini hata tukipata zaidi itakuwa vizuri" amesisitiza.

Awali akizungumza Mratibu mkuu wa Afya check Isack Maro amesema lengo la kuweka kambi mkoani hapa ni kutaka kuwajengea wananchi tabia ya kupima afya kwa hiyari mara kwa mara na hii ni mara baada ya kumaliza mkoani Dar es salaam ambapo zaidi ya wananchi 9324 walifanyiwa vipimo.

"Kitakwimu watanzania tunatumia gharama kubwa sana kujitibu na mara nyingi ni kwa sababu tumechelewa kugundua tatizo sasa kampeni hizi zilianzishwa kuhakikisha kwamba watanzania  wanajenga tabia ya kuoenda kupima afya zao mara kwa mara na hii inaonyesha kuyokana na matukio tunayoyaona  kutokana na hizi kambi ambazo tumezifanya kwa muda mrefu"

"Kwa  sasa hivi ndio tumetoka kumaliza vipimo kwa wakazi wa mkoa wa Dar es salaam na wilaya zake zote na tukafanikiwa kuwapatia huduma za afya za bure wananchi takriban 9324 walifanikiwa kupatiwa  huduma zote za kibingwa pamoja na hufuma za kawaida  bila kusahau wakapatiwa dawa na vipimo"

WAZIRI MAKAMBA ASEMA HADI KUFIKIA DESEMBA VIJIJI 3000 KATI YA 12,600 NCHINI VITAUNGANISHWA NA UMEME WA REA

August 14, 2023


 NA MASHAKA MHANDO, Bumbuli


WAZIRI wa Nishati January Makamba, amesema hadi kufikia Desemba mwaka huu, vijiji 3,000 kati ya vijiji 12,600 vilivyopo hapa nchini ambavyo havina umeme wa REA, vitaunganishwa na huduma hiyo.


Sanjari na suala la umeme, Makamba ambaye ni mbunge wa jimbo la Bumbuli, amewataka wana-CCM mkoani Tanga kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Rajabu Abdallah MNEC, kutokana na kazi anazozifanya tangu achaguliwe mwaka jana.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji wa Bumbuli, Waziri Makamba alisema Mwenyekiti huyo amekuwa wa kipekee kutokana na kwamba tangu achaguliwe umoja miongoni mwa wana-CCM umeimarika.


"Tumuunge mkono Mwenyekiti wetu kazi anazozifanya hazina kifani tangu achaguliwe amesukuma maendeleo ya mkoa wetu, lakini pia ameleta umoja kwa wana-CCM, fitina na majungu yamepungua," alisema Makamba.


Akizungumza changamoto mbalimbali zilizopo katika jimbo hilo, Makamba alisema halmashauri ya Bumbuli sasa angalau imekuwa na mzunguko wa fedha tofauti na awali ilipoanzishwa.


Alisema halmashauri inataka kujenga stendi mpya ya kisasa lakini changamoto iliyokuwepo ni ukosefu wa eneo la kujenga mradi huo mkubwa kutokana na kukosa eneo la kujengea stendi hiyo.


Akijibu swali kutoka kwa mpiga kura wake ambaye alisema katika kitongoji chake hakina umeme na hajui mbunge huyo ni lini atawapatia nishati hiyo, Waziri Makamba alisema kwa Tanzania kuna vijiji 3,000 na vitongoji 36,000 bado havijapata nishati ya umeme.


Alisema katika jimbo lake vijiji vyote vimepata umeme tofauti na maeneo mengine ambayo hata hivyo alisema kwamba wakandarasi wapo katika maeneo hayo wakiendelea na kazi za kuweka umme huo.


"Tunawaomba wananchi muwe na subira tunatarajia hadi kufika Desemba vijiji vyote vitakuwa vimewekewa umeme, mnajua mikoa kama Katavi na Rukwa bado hawajaunganishwa na  umeme wa gridi ya Taifa.


Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga, Abdallah akizungumza na wananchi wa jimbo la Bumbuli alisisitiza kutaka wananchi wamuunge mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na kuutendea haki mkoa huo kwa kuleta fedha nyingi katika miradi mbalimbali.

CCM TANGA YASITISHA UJENZI WA SHULE SHIKIZI KUTOKANA NA KUJENGWA KATIKA CHANZO CHA MAJI

August 14, 2023









CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga, kimesitisha ujezi wa shule shikizi inayojengwa katika  kijiji cha Mahezangulu, katika halmashauri ya Bumbuli, kutokana na shule hiyo kujengwa katika chanzo cha maji.


Akitoa maelekezo ya kusitishwa kwa ujenzi wa madarasa mawili ya shule hiyo inayojengwa katika kitongojo cha Kweusolo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abdallah alisema wananchi lazima waheshimu vyanzo vya maji na utunzaji wa mazingira.


Awali Mwenyekiti wa kijiji cha Mahezangulu, Seif Sekidele alisema kutokana na uhitaji wa shule shikizi kwa watoto wa kitongoji hicho walionelea wajenge shule katika eneo hilo licha ya kuwa ni eneo la chanzo cha maji kutokana na uhitaji mkubwa wa shule.


"Mheshimiwa Mwenyekiti kijiji chetu kina shule mbili za msingi lakini ukiingia shule ya Mahezangulu darasa lenye watoto 50 basi 32 wanatoka katika kitongoji hicho," alisema Mwenyekiti huyo wa kijiji.


Meneja wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani Lushoto Erwin Sizinga, alisema serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 243 kwa ajili ya mradi wa maji wa kijiji hicho na eneo lililojengwa shule ni la chanzo cha maji cha mradi huo.

"Wenzetu wa bonde la mto Pangani walitwambia chanzo cha maji katika kijiji hiki kina maji ya kutosha isipokuwa wananchi wasilime katika chanzo hiki ili chanzo kiwe cha uhakika na endelevu," alisema Sezinga.

Mbunge wa jimbo la Bumbuli na Waziri wa Nishati, January Makamba, alisema alikataa kuwasaidia kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo na kumweleza Mwenyekiti wa kijiji hicho kama mbunge yupo tayari kutoa fedha ili wapate eneo jingine kwa ajili ya kujenga shule nyingine badala ya hiyo.


Diwani wa kata ya Mahezangulu Rashid Abdallah 'Chid boy' alitaka serikali ikubali shule hiyo iendelee kujengwa katika eneo hilo na wataalamu watafute chanzo kingine cha maji ili watoto wa kitongoji hicho wapunguziwe umbali wa kwenda katika shule ya msingi Mahezangulu. 


Diwani alikubali kauli ya Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Mahezangulu kwamba hakuna eneo jingine litakaloweza kujengwa shule zaidi ya eneo hilo ambalo ni la serikali ambalo zamani lilikuwa linepandwa miti na sasa ipo miti miwili tu na wananchi wanalima mahindi.

"Natoa maelekezo hapa pasiendelezwe paachwe, kuleta fedha kuindeleza shule hii ni kuendelea kuharibu chanzo cha maji bora tupate lawama kutoka kwa wananchi lakini tukilende hiki chanzo cha maji," alisema Mwenyekiti wa CCM mkoa.

Alimwagiza mkuu wa wilaya ya Lushoto Kalist Lazaro kuhakikisha wananchi hawalimi katika eneo hilo ili kuziokoa fedha za serikali zilizoletwa kwa ajili ya mradi wa maji, zisipotee bure.

Alisema CCM katika ilani yake ilisema kwamba hadi mwaka 2025 wananchi katika maeneo ya Vijiji watapata maji kwa asilimia 85 hivyo kuruhusu ujenzi huo kutasababisha ahadi hiyo isikamilike kwasababu ya watu kushindwa kutunza mazingira.

Mwenyekiti wa CCM mkoa ameendelea ziara zake za kutembelea wilaya za mkoa wa Tanga kuona uhai wa chama na utekelezaji wa ilani ya chama ya mwaka 2020-2025.

Mwisho

MBUNGE KATOA MATREKTA BURE LIMENI VIJANA MUINUKE KIUCHUMI - DAFFA

August 14, 2023









Katibu wa Mbunge jimbo la Ulanga mkoani Morogoro Thomas Daffa amewataka vijana wa wilaya hiyo kutumia vyema fursa ya kilimo aliyoitoa Mbunge wa jimbo hilo Mhe Salim Alaudin Hasham ili wainuke kiuchumi.

Daffa amesema ni wakati wa vijana sasa kutumia kilimo kama njia ya kubadilisha maisha yao kiuchumi kwani kwasasa kilimo kimekuwa ni Njia ya mafanikio katika maeneo mengi duniani.

Pia Daffa amesema kwa Fursa ambayo Mbunge wa jimbo hilo ameitoa kwa vijana kuwa atawalimia mashamba yao bure kwa kutumia trekta zake binafsi ni vyema sasa kwa vijana kuacha kukaa vijiweni na kupiga soga badala yake waingie shambani kwani Taifa linawategemea sana.

Siku za hivi karibuni Mbunge Salim Hasham alisema atatoa trekta zake kuwalimia vijana bure mashamba yao hivyo kila kijana anayetaka kulimishiwa basi afike kwenye ofisi yake ili aweze kupatiwa msaada huo kwa lengo la kuhakikisha vijana wanajiajiri na kupunguza tatizo la ajira wilayani humo.

Aidha Daffa amewasisitiza vijana kuacha kutumika kuvuruga amani ya nchi ambayo imetunzwa na waasisi wetu na badala yake ni muda wa kufanya vitu vyenye tija kwa jamii na Taifa letu kwa ujumla.

Daffa pia ameongoza harambee ya ujenzi wa ofisi ya  Chama cha Mapinduzi kata ya kichangani na kuweza kukusanya kiasi cha Mil 3,222,000/= ambayo itaanzisha ujenzi huo ili mpaka kufikia mwezi disemba basi kata hio iweze kupata ofisi ya chama.

Jimbo la Ulanga Lina jumla ya kata 21 na vijiji 159 hivyo chama cha Mapinduzi kinafanya hivyo kujiimarisha kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka  2024 na ule uchaguzi mkuu 2025.