UFUNGUZI WA MKUTANO WA BUNGE LA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI, UNGUJA

October 11, 2016


Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akifuatana na Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Daniel F.Kigeda(kulia) na Spika wa Baraza l;a Wawakilishi Zanzibar Mhe,Zubeir Ali Maulid (kushoto) baada ya Kuufungua Mkutano wa Pili wa kikao cha tano cha Bunge la tatu la Afrika Mashariki uliofanyika leo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi "B"Unguja.
-------------------------------------

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amelisisitiza Bunge la Jumuiya ya Afika Mashariki (EALA) kuweka mikakati imara katika kukuza sekta ya utalii kwa nchi za Jumuiya hiyo kwani idadi ya watalii wanaoingia kwenye eneo hilo hailingani na vivutio viliopo. 
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani Mjini Zanzibar, wakati akizindua Mkutano wa Pili wa Kikao cha Tano cha Bunge la Tatu la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) unaofanyika Zanzibar. 
Amesema kuwa pamoja na kwamba eneo hilo la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ina vivutio vingi vya utalii, idadi ya watalii wasiozidi milioni 5 wanaoingia katika eneo hilo kutoka nchi za nje ni ndogo ikilinganishwa na watalii Bilioni moja wanaosafiri kwa mwaka duniani kote.

Dk. Shein ameongeza kuwa kiasi hicho cha watalii hakilingani na umaarufu pamoja na vivutio vilivyopo katika eneo hilo la Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na kueleza matumaini yake kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka iwapo juhudi za makusudi zitachukuliwa. 
“Jumla ya watalii waliotembelea Zanzibar mwaka 2014 walikuwa 311,801 ambapo lengo letu ni kufikia watalii 500,000 mwaka 2020”,alisema Dk. Shein. 
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza Miswada inayotarajiwa kujadiliwa katika kikao cha Bunge hilo ikiwa ni pamoja kuweka Sheria kali zitakazopiga marufuku biashara haramu ya kusafirisha binaadamu ambayo ni uhalifu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu.

Akizungumzia kuhusu Mswada wa kudhibiti matumizi ya vifaa vinavyotengenezewa plastiki ikiwemo mifuko, Dk. Shein alisema kuwa Mswada huo umekuja wakati muwafaka na kwamba Zanzibar tokea mwaka 2011 imeshaaza kutekeleza kwa vitendo Sheria ya kupiga marufuku uagiziaji na uzalishaji wa mifuko ya plastiki. 
Alisema kuwa uwamuzi wa kupiga marufuku bidhaa hizo Zanzibar ulichukuliwa baada ya kuona kwamba mifuko hiyo inaharibu mazingira, yakiwemo mazingira ya bahari pamoja na kuathiri sekta muhimu ya utalii. 
Kwa upande wa Mswaada wa Usawa wa Kijinsia na maendeleo, Dk. Shein alisema kuwa anamatumaini kuwa Mswada huo utatoa njia ya kuinua usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo. 
Dk. Shein alitoa pongezi kwa uwamuzi wa Bunge hilo kwa kuamua kuifanya Zanzibar kuwa Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na kueleza kuwa uamuzi huo ni sahihi kutokana na ukweli kwamba Kiswahili sanifu kinazungumzwa Zanzibar na kuahidi kutoa kila ushirikiano uanostahiki kufanikisha shughuli za Kamisheni hiyo. 
Ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake imechukua juhudi za makusudi za kukiimarisha Kiswahili kufikia kiwango cha Kimataifa na tayari imeingizwa kwenye mitaala ya vyuo vikuu kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) hadi kufikia kiwango cha Shahada ya Uzamifu. 
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuishukuru nchi za Jumuiya hiyo kwa namna ilivyojali na kushiriki kikamilifu kuwasaidia wananchi wa Tanzania walioathirika kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 huko Kagera na kueleza kuwa hatua hiyo inathibitisha kuwa mashirikiano baina ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo hayaishii kwenye mikataba laniki imeenda mbali zaidi kwa kujali ubinaadamu. 
Akizungumzia suala zima la changamoto ya ajira ambayo inaikabili nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Shein alisema kuwa nchi hizo hazina budi kuondoka zilipo ambapo mchango wa Pato la Taifa katika nchi hizo linakisiwa kuwa ni asilimia 8.9 ambayo ni kidogo kufikia lengo la asilimia 25 ambayo nchi hizo zimejiwekea kufikia ifikapo mwaka 2032.

Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina hiostoria ya kuwa ni kitovu kikubwa cha biashara ambapo ilitumika na wafanyabiashara pamoja na wavumbuzi waliokuwa wakisafiri katika ukanda wa Afrika Mashariki, hivyo Serikali ya M apinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba inaamini kwamba inaweza kurejesha hali yake hiyo ya zamani ambapo hivi sasa imeamua kuimarisha miundombinu ya bandari, viwanja vya ndege na barabara ili iweze kufikia azima yake hiyo. 
Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein aliwataka Wajumbe wa Bunge hilo kuwa tayari kushirikiana na Serikali katika kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha biashara katika ukanda huo wa Afrika ya Mashariki na Kati. 
Dk. Shein ameongeza kuwa maendeleo ya viwanda pekee ndio yatakayowezesha kuondoa changamoto ya ajira katika eneo hillo. 
Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar  Zubeir Ali Maulid akitoa hutuba yake alipongeza kwa kufanyika mkutano huo na kueleza kuwa kufanyika mkutano huo si tu utaimarisha mashirikiano baina ya Mabunge hayo mawili lakini pia, utatoa fursa zaidi ya pande mbili hizo kujifunza namna ya kuendesha shughili za Bunge kutoka kila upande. 
Mapema Katibu Mkuu wa Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki Daniel Fred Kidega alisisitiza suala la amani na utulivu katika eneo la nchi zinazounda Jumuiya hiyo ili wananchi wake waweze kuendelea na shughuli zao bila ya kuhofia kupoteza maisha yao.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuisifu Zanzibar na kueleza kuwa kuna uwezekano mkubwa kuifanya Zanzibar kuwa eneo muhimu la biashara katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na kueleza kuwa inaweza kuwa ni Dubai ya Afrika.

MAKAMU WA RAIS MAMA SULUHU AWEKA JIWE LA MSINGI WODI ZA WAZAZI HOSPITALI ZA RUFAA MKOA WA DAR ES SALAAM

October 11, 2016
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye hafla ya Uwekaji mawe ya msingi ujenzi wa wodi za wazazi na watoto katika Hospitali za Rufaa za Mkoa wa Dar es Salaam leo Oktoba 11, 2016. Picha zote na Cathbert Kajuna wa Kajunason Blog. Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda akizungumza kwenye hafla ya Uwekaji mawe ya msingi ujenzi wa wodi za wazazi na watoto katika Hospitali za Rufaa za Mkoa wa Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya Uwekaji mawe ya msingi ujenzi wa wodi za wazazi na watoto katika Hospitali za Rufaa za Mkoa wa Dar es Salaam. Pembeni wanaoshuhudia ni Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Makonda.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipewa maelekezo na wadhamini watakaojenga jengo hilo, Amsons Group.
Moja ya Bango la ujenzi wa wodi ya wazazi.

UCHUMI WA ZANZIBAR UNAZIDI KUIMARIKA ASILIMIA 7

October 11, 2016
                                    Mwashungi Tahir na Fatma Makame/Maelezo Zanzibar

Waziri wan chi ofisi ya makamo wa pili ya rais Mohammed Aboud Mohammed amesema uchumi wa Zanzibar     unazidi kuimarika kwa karibu ya asilimia saba na mfumuko wa bei bado upo kwenye tarakimu  moja na  pato la Taifa linazidi kukua.

Ametoa maelezo hayo  ofisini kwake Vuga wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi Serikali ya awamu ya saba kipindi cha pili cha uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein.

Amesema katika awamu hii kwa ujumla harakati za uchumi zinaendelea vizuri na ishara zote za kuimarisha uchumi katika mwaka huu wa fedha zinatoa sura nzuri za mafanikio.

Akizungumzia  suala la Muungano amesema unaendelea kuimarika na  vikao mbali mbali vya watendaji wakuu wa pande mbili wakiwemo  mawaziri vimeshafanyika na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ameshafanya vikao viwili vya kisekta kwa nia ya kutatua changamoto zilizopo.

Waziri Aboud ameelezea kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekamilisha kazi ya kuipandisha hadhi iliyokuwa Idara ya upigaji chapa na mpigaji chapa mkuu wa serikali na kuwa wakala wa serikali wa uchapaji.

Aidha amesema kazi ya kufunga mitambo mipya ya uchapaji imekamilika na mafundi wa kiwanda hicho wanaendelea kupatiwa mafunzo ili kuimudu teknolojia mpya ya mitambo hiyo ili kuongeza ufanisi  na kuongeza upatikanaji wa huduma bora na kwa wakati.

Sambamba na hayo Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais kupitia Tume ya kitaifa ya kuratibu na udhibiti madawa ya kulevya imepania kutoa athari za madawa ya kulevya kwa jamii.

Hivyo Tume hiyo imefanya kikao maalum na maofisa na wapelelezi wa Jeshi la Polisi wa Mikoa na Wilaya  za Unguja kilichoongozwa na mkuu wa Mkoa Mjini Maghribi kuweka mikakati dhidi ya uingizaji na usambazaji wa madawa ya kulevya .

Mh Aboud amesema ofisi yake inashirikiana na Ofisi ya ukaguzi na mdhibiti mkuu wa Serikali kuendesha zoezi la uhakiki wa wafanyakazi wa Ofisi ya Makamo ya Pili ya Rais na Taasisi zake ili kubaini wafanyakazi hewa.

“Katika zoezi hili imebainika kwamba Ofisi yetu hakuna wafanyakazi hewa  kama inavyobainika sehemu nyengine" alisema wazirihuyo.

Aidha amesema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais bado itaendelea kufanya kazi kwa bidii , ufanisi na tija ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa mambo muhimu ya kuzingatiwa hivi sa kwa nchi yetu ni kuimarisha uzalendo na kusimamia matumizi bora ya ardhi kwani watukishirikiano katika masulala hayo tutaweza kudumisha amani na upendo na kupiga hatua zaidi ya maendeleo. 
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed akitoa tarifa ya mafanikio ya Ofisi yake kuhusiana na utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi kwa kipindi cha pili cha uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. 
 Wandishi wa habari wakifuatilia tarifa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alipokuwa na mazungumzo nao  Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alipokuwa akijibu maswali ya wandishi wa habari katika Mkutano wake Ofisini kwake Vuga.Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.

LHRC CHA TOA NENO KUHUSU SIKU YA MTOTO WA KIKE DUNIANI

October 11, 2016
Ndugu wanahabari,

Leo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaungana na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, siku ambayo ilipitishwa na  Umoja wa mataifa mnamo  Oktoba 11, 2011.  Kauli mbiu ya kitaifa kwa mwaka huu ni ‘‘Mimba na ndoa za Utotoni zinaepukika, Chukua hatua kumlinda mtoto wa kike’’. 

Hivyo basi katika kuadhimisha siku hii Kituo kimeangazia mtoto wa kike hapa Tanzania na changamoto anazokumbana nazo. Kwa mujibu wa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, idadi ya watoto wa kike kati ya umri wa miaka 0-17 hapa Tanzania ni  11,263,891 idadi ambayo ni sawa na asilimia 48.8 ya watoto wote chini ya miaka 17, ambapo Tanzania bara  kuna watoto wa kike  elfu 10,943,846 na Tanzania visiwani idadi  yake ni laki 320,045. 

Hivyo basi nusu ya idadi hii ni wanawake na watoto  ikilinganishwa na idadi ya watanzania wote ambao ni milioni 44,928,923 ambapo  kati yao wanawake ni milioni 23,058,933. 
Inasikitisha kuona kuwa mtoto wa kike hapa nchini bado amekuwa akikabiliwa na changamoto nyingi na cha kusikitisha zaidi mtoto huyu anaanza kubaguliwa kuanzia katika ngazi ya familia. 

Katika familia nyingi za kitanzania mtoto wa kike amekuwa akikosa fursa ya kupata Elimu ukilinganisha na mtoto wa kiume na katika mazingira mengine wazazi wamediriki hata kuwaozesha watoto wao wa kike kwa ajili ya kupata fedha ya kusomesha watoto wa kiume. Ukiangalia pia katika suala zima la Elimu ni ukweli usiofichika kuwa idadi ya wasichana wanaoshindwa kumaliza masomo kwa sababu za kupata mimba imekuwa ikiongezeka.

 Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la watoto duniani UNICEF kumekuwa na ongezeko la mimba mashuleni kutoka asilimia 23 hadi 26 yaani takribani watoto wa kike 8000 hapa Tanzania kila mwaka hukatisha masomo kwa ajili ya ujauzito. Vile vile idadi ya watoto wa kike ambao wamekuwa wakimaliza Elimu ya msingi lakini kutokupewa nafasi ya kujiendeleza kielimu hata pale wanapokuwa wamefaulu nayo pia imekuwa ikiongezeka na badala yake mabinti hawa wamekuwa wakilazimika kuingia katika ndoa katika umri mdogo.


Ndugu wanahabari,
Hali hii ya Watoto wakike kutokupata fursa ya elimu husababisha ongezeko kubwa la watoto wa kike wanaosafirishwa kutoka vijijini na kuletwa mijini kwa minajili ya kuja kuendelezwa kielimu na matokeo yake mabinti hawa wamejikuta katika wakati mgumu kwa kufanyishwa kazi za ndani bila malipo stahiki na wakifanyiwa vitendo vingi vya kikatili na vya kuwadhililisha. 

Hali hii imepelekea mabinti wengine kutoroka kutoka kwa waajiri wao na kuanza kuishi mtaani na hivyo kurubuniwa na kujiingiza katika biashara za ngono na wengine hata madawa ya kulevya.

Tumeendelea pia kushuhudia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kingono kama ubakaji na ulawiti kwa Watoto wa kike na cha kusikitisha zaidi vitendo hivi vimekuwa vikifanywa na Ndugu wa karibu sana wa Watoto hawa wakiwemo wazazi, walezi, majirani na hata walimu huko mashuleni. matukio haya yamekuwa hayafikishwi Katika vyombo vya Sheria kwani mengi huzungumzwa kifamilia na kuwaacha watuhumiwa wakiendelea na maisha yao.

Ndugu wanahabari,
Tanzania pia ni nchi moja wapo yenye idadi kubwa ya ndoa za utotoni kwa takribani  ya asilimia 35 watoto wa kike hapa nchini huozeshwa nchini ya umri wa miaka 18 na hivyo kukatishwa ndoto zao za kujiendeleza kielemu na hata ustawi mzima wa maisha yao.

Inasikitisha zaidi kuona pia pamoja na juhudi mbalimbali za utetezi na ushawishi wa wanaharakati katika kupinga vitendo hivi viovu na mila kandamizi bado Ukeketaji umekuwa ni tatizo kubwa sana hapa nchini. Kwa mujibu wa takwimu za Viashiria vya Idadi ya watu na afya 2010, asilimia 14.6% ya wanawake Tanzania wamekeketwa na wengi wao ni watoto wa kike. 

Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa mbinu mpya zimekuwa zikibuniwa ikiwemo  kukeketa watoto mara wanapozaliwa. 

Vilevile, kwa mujibu wa taarifa ya haki za Binadamu ya mwaka 2015 inayotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kila mwaka ongezeko la matukio ya Ukatili kwa watoto ikiwemo watoto wa kike kupewa adhabu kali ambazo hazilingani na makosa waliyoyafanya, mfano unakuta mtoto anachomwa mikono moto kwa kosa la kuunguza mboga.

Kwa kifupi watoto wa kike wanapata athari mbalimbali ikiwemo;
1.      Kuendelea kudidimiza nafasi ya mwanamke katika Jamii na taifa zima kwa ujumla na kuendeleza mfumo dume kwani ukatili mwingi huanzia katika ngazi ya familia

2.      Kutokuendelezwa kielimu kwa mtoto wa kike na hii hupelekea kuendelea kuwa na idadi kubwa ya Wanawake ambao hawana Elimu na hivyo kuendelea kuwa tegemezi kwa wanaume na pia kushindwa kujikwamua kiuchumi.

3.      Idadi kubwa ya athari za kiafya zinazowapata watoto wa kike kwa ajili ya kujifungua katika umri mdogo ambayo husababisha wengine kupoteza maisha, kupatwa na fistula na maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na magonjwa mengine ya zinaa.

4.      Malezi duni ya watoto kwa kuwa watoto hawa wanakuwa bado ni wadogo kuweza kukabiliana na jukumu kubwa la malezi na matunzo ya familia.

5.      Kuendelea kuongezeka kwa Ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwani watoto hawa mara nyingi huolewa na watu waliowazidi umri sana na hivyo kutokuwa na maamuzi yoyote katika nyumba.

Hivyo basi tunapendekeza yafuatayo:

1.      Katika ngazi ya familia wazazi na walezi kuthamini na kuwajali watoto bila ubaguzi wa jinsi zao. Watoto wote wapewe fursa sawa kielimu na kujiendeleza kimaisha. Wazazi kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili hasa Ukatili unaoanzia majumbani,sambamba na hilo kutoa taarifa za matukio ya Ukatili wanayofanyiwa watoto na sio kutatua matatizo haya katika ngazi ya familia ilihali haki ya mtoto inapotezwa.

2.      Wito kwa Jamii kuwajibika katika kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili. Kuthamini nafasi ya kila mtoto na kuona mtoto wa mwenzako ni wa kwako; pia kutoa taarifa ya matukio ya Ukatili katika maeneo wanayoishi na sio kufumbia macho na kuwaficha waovu.

3.      Serikali kuhakikisha kuwa sheria zilizopo zinasimamiwa na zinatekelezwa pale zinapovunjwa kwa kuweka mifumo iliyowazi na rahisi ya kupata na kufuatilia haki. Vile vile kubadilisha sheria ambazo bado zimekuwa ni kandamizi kwa mtoto wa kike ikiwemo Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoafiki mtoto wa kike kuolewa katika umri wa miaka 15. Serikali itekeleze agizo lilitolewa na Mahakama Kuu Julai 8 2016 la kubadili kifungu na 13 cha sheria ya ndoa 1971 juu ya ndoa za utotoni

4.      Serikali kwa kupitia taasisi zake kama polisi na mahakama kuhakikisha kuwa Mashauri yanapolekwa Mahakamani yanasikilizwa bila vikwazo na kutolewa maamuzi kwa wakati stahiki maana ‘justice delayed is justice denied’ - ‘kuchelewesha haki ni kunyima haki’.

5.      Wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa ya matukio ya Ukatili wanayofanyiwa watoto ili wale wanaofanya vitendo hivi waaibishwe na waadhibiwe kwa mujibu wa sheria; tunavitaka vyombo vya Habari visiishie tu kuripoti matukio haya pindi yanapofanyika bali hata kuendelea kufuatilia mashauri yaliyopo mahakamani ili kusaidia mashauri haya yafanyiwe kazi kwa wakati.

6.      Pamoja na hilo tunaviomba vyombo vya habari kuwa makini jinsi wanavyoripotia matukio haya ya Ukatili kwa watoto kwani utoaji wa taarifa hizi wakati mwingine umekuwa pia ukiendelea kuwavunjia haki watoto hawa kwa kutozingatia sheria inayotaka utoaji wa taarifa za watoto kutunza majina halisi ya watoto na hata sura zao.

7.      Na mwisho kabisa tunaomba viongozi wetu katika ngazi zote za kijamii na hata kitaifa kuibeba ajenda ya haki za watoto na hususani haki za watoto wa kike kama ajenda ya kitaifa ili kuhakikisha wanalindwa dhidi ya vitendo viovu na wana mazingira salama ya kukua na kuwa watu wema na mustakabali mzuri wa maisha yao ya sasa na ya baadae.

Tunawashukuru sana.

Wasalaam, Kituo cha Sheria na Haki za Binada

Dr. Helen Kijo-Bisimba Mkurugenzi Mtendaji


MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA KIKE DUNIANI, BARAZA LA WOTOTO MKOANI MWANZA LATAKA MTOTO WA KIKE KUPEWA FURSA SAWA KATIKA JAMII.

October 11, 2016
Mwenyekiti wa Baraza la Watoto mkoani Mwanza, Paulina Mashauri, akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani ambayo Jijini Mwanza yamefanyika hii leo Oktoba 11, katika Uwanja wa Furahisha na kuwashirikisha watoto kutoka shule na taasisi mbalimbali.
Na BMG
Haleluya Benjamin ambaye ni Katibu wa baraza la Watoto mkoani Mwanza, akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani ambayo Jijini Mwanza yamefanyika hii leo Oktoba 11, katika Uwanja wa Furahisha na kuwashirikisha watoto kutoka shule na taasisi mbalimbali.
Mwanafunzi James John kutoka shule ya msingi Kitangiri A Jijini Mwanza akizumzia Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani ambayo Jijini Mwanza yamefanyika hii leo Oktoba 11, katika Uwanja wa Furahisha ambapo amesema haungi mkono baadhi ya vitendo wanavyofanyiwa watoto wa kike ikiwemo unyanyasaji kama vile ubakaji, mimba na ndoa za utotoni.
Msimamizi wa Watoto Baraza la Watoto mkoani Mwanza, Karus Masinde, akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani ambayo Jijini Mwanza yamefanyika hii leo Oktoba 11, katika Uwanja wa Furahisha na kuwashirikisha watoto kutoka shule na taasisi mbalimbali.
Mmoja wa vijana walioshiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani ambayo Jijini Mwanza yamefanyika hii leo Oktoba 11, katika Uwanja wa Furahisha na kuwashirikisha watoto kutoka shule na taasisi mbalimbali.
Wanafunzi wasichana wakiigiza michezo na maigizo mbalimbali
Wanafunzi wasichana wakiigiza michezo na maigizo mbalimbali
Kulikuwa na matukio mbalimbali ikiwemo wanafunzi kuonesha uwezo wao wa kujibu maswali
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi akitoa ufafanuzi wa jambo
Na George Binagi-GB Pazzo
Baraza la Watoto mkoani Mwanza limeitaka jamii kutoa fursa sawa ya malezi bora kwa watoto wa kike kama ilivyo kwa watoto wa kiume katika masuala mbalimbali ikiwemo fursa ya kupata elimu.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Paulina Mashauri, ameyasema hayo kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani ambayo Jijini Mwanza yamefanyika katika Uwanja wa Furahisha na kuwashirikisha watoto kutoka shule na taasisi mbalimbali.

Naye Haleluya Benjamin ambaye ni Katibu wa baraza hilo amesema bado watoto wa kike wanakabiriwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa fursa ya kupata elimu, mimba na ndoa za utotoni hivyo ni vyema jamii ikaungana pamoja katika kutokomeza changamoto hizo.

Msimamizi wa Watoto Baraza la Watoto mkoani Mwanza, Karus Masinde, ameiomba jamii na serikali kwa ujumla kutoa kipaumbele kwa watoto wa kike katika masuala mbalimbali ikiwemo ya kupata elimu pamoja na fursa za kiuongozi.

Kitaifa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yamefanyika mkoani Shinyanga yakiambatana na kauli mbiu isemayo, Msichana Kushika hatam, ikiwa na lengo la kuihamasisha jamii kutoa fursa kwa mtoto wa kike katika masuala mbalimbali katika jamii ikiwemo kupata elimu na uongozi.

MAADHIMISHO YA SIKU YA SACCOS DUNIANI YAFANYIKA JIJINI DAR ES SALAAM

October 11, 2016

 Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Saccos Duniani, Stellah Mtayabarwa (kushoto), akimwelekeza jambo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Florens Turuka (kulia), alipotembelea banda la Saccos la Mamlaka ya Bandari (PTA), katika ufunguzi wa maadhimisho hayo uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam leo.
 Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT), Benard Kalinga (katikati), akihutubia wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Florens Turuka na kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo, Stellah Mtayabarwa.
 Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Habibu Mhezi (kulia), akizungumza kwenye mkutano huo. Kushoto ni Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Mrakibu wa Polisi (SP), Scholastica Luhamba.


 Mjasiriamali Zamda Sasillo (kushoto), akiwa na wateja walitembelea banda lake katika maadhimisho hayo. Kutoka kulia ni  Magdalena Samkumbi, Lubanzo Kalufya na Ashura Shoka.
 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Florens Turuka (kulia), akizungumza na Ofisa Uendeshaji Mkuu, Mfuko wa Pembejeo, Pili Mogasa.
 Ofisa Masoko wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, akitoa maelezo kwa  Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Florens Turuka (kulia), kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na mfuko huo.
 Ofisa Masoko wa Benki ya Posta Tanzania, Ezekiel Fumbo (kushoto), akimuelekeza Dk. Turuka kazi mbalimbali zinazofanywa na benki hiyo.
 Viongozi Meza kuu wakipiga makofi wakati wakipokea maandamano ya maadhimisho hayo.
 Wadau wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
 Wasanii wa Kikundi cha Utamaduni cha Sanaa cha Magereza kikitoa burudani kwenye hafla hiyo.
 Wasanii wa Kikundi cha Utamaduni cha Sanaa cha Magereza kikionesha umahiri wa kucheza ngoma aina ya chaso inayochezwa na wenyeji kutoka Pemba.
Hapa ni mserebuko wa ngoma ya chaso ya wenyeji wa Pemba.

Na Dotto Mwaibale

SERIKALI imesema itaendelea kushirikiana na vyama vya akiba na mikopo ili kujenga mazingira bora ya kuinua uchumi nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Florens Turuka wakati wa ufunguzi wa Siku ya Saccos duniani uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo.

"Vyama vya akiba na mikopo ni wadau wakubwa wa serikali kwani vinasaidia sana katika kiinua uchumi wa nchi hivyo hatuna budi kuendelea kushirikiana" alisema Dk.Turuka.

Dk. Turuka aliwataka viongozi wa vyama hivyo kumaliza changamoto zao wao wenyewe na wanachama wao pale zinapotokea badala ya kukimbilia serikalini.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT), Benard Kalinga alisema vyama hivyo vimepata mafanikio makubwa kwani wamefanikiwa kuanzisha Saccos 4,000 ambazo zipo hadi vijijini na kuwa na wanachama milioni 1.5 nchini.

"Sheria namba sita ya vyama vya ushirika ya mwaka 2013 imeanza kutumika baada ya kupata idhini ya Rais mwezi Oktoba 2013 lakini ni dhahiri kuwa kumekuwa na malalamiko mengi juu ya baadhi ya maeneo yaliyoko kwenye sheria hiyo" alisema Kalinga.


Alisema licha ya kupata mafanikio hayo changamoto kubwa waliyonayo ni ushirikishwaji wa kuandaa sheria inayoongoza vyama vya ushirika nchini.


DC STAKI ASIMAMIA ZOEZI LA KUCHOMA SHAMBA LILILOLIMWA MIRUNGI

October 11, 2016

 Wakazi wa Kijiji cha Kisesa Kata ya Vudee wakishuhudia zoezi la uteketezaji wa shambala Mirungi
Mkulima wa zao la Mirungi Johnson Charles Kangara akiwa ameshika mafuta ya taa tayari kwa ajili ya kuteketeza shamba lake la Mirungi

 Shamba la Mirungi likiteketea baada ya agizo la Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe Rosemary Staki
 Dc Staki akiwasisitiza wananchi kutojihusisha na kilimo cha zao la Mirungi

Na Mathias Canal, Kilimanjaro

Mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu Uongozi wa Wilaya ya Same ulitangaza vita dhidi ya wakulima wa Bangi, na Mirungi huku akitangaza kuwa kifungo cha miaka 30 kitawahusu wakulima wote wanaojishughulisha na kilimo hicho haramu kwani Bangi na Mirungi ni hatari kwa afya za watumiaji na kuisababishia serikali hasara kwa kutopokea Kodi.

Kiama hicho kilitangazwa na Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe Rosemary Staki Senyamule wakati akikabidhiwa mradi wa Ruvu muungano uliojumuisha zahanati sita, Nyumba mbili za waganga, matanki saba ya kuvuna maji na madarasa 54, ofisi 16 za walimu, vyumba na vyoo vya chuo cha ufundi makanya uliofadhiliwa na shirika la World Vision Tanzania.

Dc Staki alisema kuwa kwa asilimia kubwa serikali imekuwa ikiwadhibu wanaoingiza Mirungi na Bangi sokoni huku ikiwasahau kuwachukulia hatua wale wote wanalima zao hilo.

Hivi karibu katika kijiji cha kisesa kata ya Vudee Wilayani humo ilibainika kuwa kuna wakulima wa Mirungi ambao wanajihusisha na zao hilo kwa muda mrefu pasina serikali kuwabaini na kuwa sugu kwa kilimo hicho hatimaye kukiona kama kilimo cha halali.

Dc Staki alipotangaza kiama cha kukabiliana na wale wote wanaojihusisha na kilimo hicho aliahidi kuwatafuta wakulima hao na hatimaye kuwachukulia hatua za kisheria na kuhakikisha kuwa Wilaya ya same inakuwa safi pasina kuwa na Mirungi.

Hata hivyo katika ziara yake ya kazi Mhe Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Staki alipozuru kijiji cha kisesa kata ya Vudee alifanikiwa kumuweka chini ya ulinzi mkulima wa zao la Mirungi Johnson Charles Kangara na hatimaye kumuelekeza kuwasha kiberiti yeye mwenyewe katika shamba zima na kuchoma zao hilo.

Dc Staki ameahidi kuhakikisha Wilaya ya Same inasifika kwa kilimo cha mazao mengine rafiki katika jamii ya Biashara na chakula na kuteketeza mazao yote haramu.

TANZANIA IMEANZA KUFANYA UTAFITI WA MBEGU YA MAHINDI MEUPE KWA KUTUMIA GMO

October 11, 2016
 Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. Hassan Mshinda, akizindua utafiti huo katika Kituo cha Utafiti cha Makutupora mkoani Dodoma juzi.
 Watafiti kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi wakiwa tayari kwa upandaji wa mbegu hizo katika Kituo cha Utafiti cha Makutopora mkoani Dodoma.
 Mratibu wa Jukwaa la Bioteknolojia Tanzania (OFAB), Philbert Nyinondi, akishiriki kupanda mbegu hizo.
 Mkurugenzi wa Sayansi Hai wa Costech, Dk.Flora Tibazarwa akishiriki katika zoezi hilo la upandaji mbegu hizo.


Mshauri wa Mradi wa WEMA, Dk. Alois Kullaya  (kushoto) na Meneja mradi huo Mr  Silvester  wakishiriki kwenye upandaji wa mbegu hizo.


 Watafiti wakichoma masalia ya vifungashio vya mbegu za mahindi kama sheria ya GMO inavyoelekeza baada ya zoezi hilo.

Na Dotto Mwaibale

KWA mara ya kwanza Tanzania  imeanza kufanya utafiti wa mbegu ya mahindi meupe kwa kutumia teknolojia ya uhandisi jeni (GMO) ambao utachukua takriban miaka mitatu ili kupata matokeo ya mbegu nzuri itakayostahimili mabadiliko ya hali ya hewa ambayo imekuwa changamoto kubwa kwa wakulima.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dk. Hassan Mshinda alisema kuanza kwa utafiti huo ni hatua nzuri kwa nchi katika kuinua kilimo nchini.

Alisema utafiti huo ambao unafanyika katika nchi tano za Afrika, kwa hapa nchini unafanyika katika kituo cha Makutopora mkoani Dodoma na kuwa nchi hizo  nyingine ni Kenya, Uganda, Africa ya Kusini na Msumbiji. 

Mtafiti na Mshauri wa mradi wa mahindi yanayostahimili ukame ( WEMA) Dk. Alois Kullaya, alisema Tanzania ilikuwa ikifanya tafiti katika hatua ya maabara, na sasa kwa mara ya kwanza wapanda kwenye mazingira halisia. " Ni kweli tarehe tano ya mwezi huu, tulipanda mahindi meupe katika hatua ya utafiti kwenye mazingira. Tunataka tujiridhishe na uwezo wa mahindi hayo katika kustahimili ukame". Matokeo ya utafiti huu, utatoa nafasi kwetu kama watafiti na viongozi wetu kufanya maamuzi yenye tija kwa taifa badala ya kuwa watazamaji na kushambikia marumbano tusiyofahamu chanzo chake" alisema Kullaya.

Mtafiti Kiongozi wa masuala ya bioteknolojia kutoka Costech Dk. Nicholas Nyange aliishukuru serikali kwa kuruhusu watafiti wake kuweza kufanya majaribio ya uhandisi jeni hapa nchi. Hii ni hatua nzuri katika nchi yoyote inayoamini katika maendeleo ya sayansi na teknolojia. 
"Tumekuwa tukitishiwa kama watoto  Usiguse GMO utakufa, wakati nchi nyingine wanazalisha nakufanya biashara. Tunafanya biashara kubwa na India, China, Marekani na Afrika ya Kusini, na hawa wote wanatumia teknolojia ya uhandisi jeni". 

 "Tufanye utafiti, tuone kama tutakufa kweli au tutatoka kimasomaso"  aliongeza Nyange kwa tabasamu. 

Itakumbukwa kuwa Mradi wa WEMA hadi sasa  umezalisha mbegu 11 za mahindi kwa njia za kawaida. Na baadhi ya mbegu hizo zimeingia sokoni mwaka huu kwa bei ya kawaida. Hivyo, uzalishaji wa Mahindi ya GMO itakuwa ni hatua mbele katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi. 




UMUHIMU WA HIFADHI YA MAZINGIRA ASILIA AMANI, KIVUTIO CHA UTALII NA CHANZO MUHIMU CHA MAJI YANAYOTUMIKA JIJINI TANGA

October 11, 2016
 Geti la kuingilia katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani iliyopo katika Wilaya ya Muheza na Korogwe Mkoani Tanga.
Kinyonga aina ya pembe tatu (three hornes chameleon) ambao hupatikana katika hifadhi ya Mazingira Asilia Amani tu.
 Moja ya vyura aina ya Usumbara (Leptopelis vermiculatus) ambao wanaopatikana katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani pekee.
Sehemu ya maporomoko ya maji katika hifadhi ya Msitu wa asili ya amani iliyopo Wilayani Muheza Mkoani Tanga ambayo imekuwa kivutio kwa watalii wanaotembelea eneo hilo.

Moja ya vyanzo vya maji katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani.