WACHEZAJI KIKAPU TANGA WAOMBA MSAADA WA KUIPELEKA TIMU MBEYA.

November 15, 2013
Mkoa wa Tanga, mabingwa watetezi wa michuano ya taifa ya kikapu (Taifa Cup) kwa mwaka jana, bado hawajathibitisha ushiriki wao katika michuano ya mwaka huu kutokana na ukata wa fedha. 

Habari zinasema mpaka sasa timu yao inafanya mazoezi bila matumaini ya kuelekea mjini Mbeya itakapofanyika michuano hiyo kwa mwaka huu mwishoni mwa mwezi wa 11.

“Michuano hii ya kikapu taifa kwa mwaka jana ilifanyika mkoani hapa (Tanga), hivyo ikawa rahisi kwetu kuweka kambi na kupata mahitaji mengine, ndiyo maana tukaibuka mabingwa, lakini mwaka huu hali katika kambi si nzuri kwani bajeti inatubana mpaka sasa hatujui mustakabali wetu,” afisa  wa timu hiyo alisema.

Kwa mujibu wa barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa chama cha mpira wa kikapu mkoa wa Tanga (TRBA), Carlistus Zakaria timu hiyo inahitaji kiasi cha Sh mil 11, ili kuweza kusafiri mpaka Mbeya. Vilevile kiasi hicho cha fedha kitaweza kuhudumia kambia kwa malazi na chakula pamoja na vifaa vya michezo kwa muda wote watakaokuwa Mbeya.

“Timu yetu ina wachezaji 24 Wavulana na Wasichana pamoja na viongozi wanane hivyo kufanya idadi ya watu 32, tunahitaji kiasi cha Sh mil 3.5 za nauli kuenda na kurudi, Sh mil 5.2 za chakula kwa siku zote tutakazokuwa Mbeya pamoja na Sh mil 8.8 za vifaa vya michezo na fedha za dharura,” ilisema sehemu ya barua hiyo.

Aidha kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari ambacho kimetaka hifadhi ya jina lake mpaka sasa Mkoa wa Tanga, haujaonyesha nia ya kuwasaidia mbali ya kuwapelekea barua kutoka Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), ambayo inaweka wazi kila kitu juu ya ushiriki wetu.

“Kinachotutia uchungu juu ya kupuuzwa huku ni kuwa, mwaka jana tulipouletea heshima Mkoa wetu kila mtu alitusifia, lakini hawakujua kama vizuri vyataka gharama.

Sasa ili tuendelee kuuletea vikombe mkoa wetu tunawaomba wadau wa mchezo huu watusaidie tufike Mbeya.

“Tumeamua hatuhitaji fedha, hata wakitokea watu wakitudhamini usafiri, wengine wakatupa vifaa na wengine wakatuhakikishia chakula hatuna matatizo.

Kikubwa tunahitaji kushiriki michuano hii kwa hali na mali, tukishindwa kushiriki itakuwa aibu kubwa kwa mkoa wetu,” kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, kwa mujibu wa barua ya TBF, iliyotolewa Aprili mwaka huu na kutiwa saini na Katibu Mkuu Msaidizi wa shirikisho hilo Michael Maluwe, imeweka wazi kuwa Serikali ya Mkoa inawajibika moja kwa moja kuhakikisha timu hizo zinashiriki michuano ya Taifa Cup.

“Ni wajibu wa kila mkoa kuhakikisha unawajibika katika maandalizi na kuipeleka timu ya mkoa kwenye kituo cha mashindano,” imesema sehemu ya barua hiyo na kuongeza kuwa. “Mambo muhimu ya kuzingatia ni gharama za nauli kwa timu, gharama za malazi na chakula vilevile usafiri wa ndani, posho na ada ya ushiriki ambayo ni Sh 100,000.”

Aidha timu ya kikapu ya Tanga imeweka wazi kuwa mtu binafsi, kampuni ama taasisi ambayo itaguswa na matatizo ya kambi hiyo, ambayo inapigana kuhakikisha inatetea ubingwa wake ilioupata mwaka jana wanafungua milango kupokea msaada wowote utakaowawezesha kuishi mjini Mbeya kuanzia Novemba 30 mpaka Disemba 8 mwaka huu itakapokamilika michuano hiyo.

Wamebainisha kuwa wapo tayari kutangaza biashara ya mfadhili yeyote atakayewasaidia ama mtu aliyeguswa anaweza kuwatumia fedha katika akaunti ya benki namba 4172506984 NMB Bank (badaraka Branch).

ROSTAM AZIZ NDIYE BABA WA MATAJIRI WOTE TANZANIA, MENGI WA PILI AFRIKA NZIMA KATIKA WAMILIKI WA VYOMBO VYA HABARI

November 15, 2013

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam 

TANZANIA imeongoza katika orodha ya tatu ya matajiri wapya wakubwa Afrika iliyotolewa na jarida la Forbes, mfanyabishara Rostam Aziz aliyeacha siasa kwa shinikizo la chama chake, CCM ili kubaki kwenye biashara pekee akitajwa kuwa tajiri zaidi nchini.

Rostam aliyejiuzulu Ubunge wa Igunga mwaka 2011, jarida la Forbes limesema ana utajiri wa thamani ya dola za Kimarekani Bilioni 1. 
Mtanzania tajiri zaidi; Rostam Aziz ana zaidi ya dola Bilioni 1

Rasilimali zake kubwa ni pamoja asilimia 35 ya hisa katika kampuni ya Vodacom Tanzania, kampuni kubwa ya simu za mkononi Tanzania, ikiwa na wateja zaidi ya milioni 9.5; kampuni ya madini ya Caspian Mining, pamoja na biashara anazofanya kwa kushirikiana na  na bilionea wa Hong Kong, Li Ka-shing. Azizi pia amewekeza Dubai na Oman.

Mtanzania mwingine, Reginald Mengi ni tajiri mkubwa wa pili Afrika katika uwekezaji kwenye sekta ya Habari, baada ya Koos Bekker wa Afrika Kusini. Binafsi, Mengi anamiliki kampuni ya IPP yenye magazeti 11, Televisheni tatu na vituo 10 vya Redio. 

Rasilimali nyingine za Mengi ni migodi ya dhahabu, kampuni kadha za madini na kampuni ya soda ya Coca-Cola. Ana utajiri wa jumla ya dola za Kimarekani Milioni 550 kwa mujibu wa tathmini za FORBES.

Mtu mpya katika orodha ya matajiri 50 wa Forbes 50 ni Mualgeria, Issad Rebrab, ambaye ameingia na tajiri wa thamani ya dola Milioni 3.2. Rebrab ni muanzilishi wa Cevital, kampuni ya familia inayotengeneza sukari, mafuta ya kupikia na jibini. Cevital pia inamiliki viwanda vya uzalishaji bidhaa za kusambaza.

Bilionea wa Kenya na Afrika Mashariki, Vimal Shah ameingia kwenye orodha hiyo na utajiri wake wa dola Bilioni 1.6. Shah, baba yake na kaka yake kwa pamoja wanamiliki kampuni ya mafuta ya kupikia Bidco. 

Pato la mwaka la kampuni hiyo ni dola Mlioni 500. Bidco pia inatengeneza unga wa chakula na sabuni za manukato katika nchi 14 Afrika. Pia ni muwekezaji wa Tatu City, kampuni mpya yenye thamani ya dola Bilioni 3  ya Satellite itakayokuwa na maskani yake, Nairobi.

Mmorocco, Aziz Akhannouch ana utajiri wa dola Bilioni 1.4 kutokana na kumiliki kwake kampuni ya Akwa Group, iliyoanzishwa na baba yake ambayo kwa sasa inamiliki kampuni za Afriquia Gas na Maghreb Oxygene pamoja na vyombo vya habari, uwekezaji wa ardhi na hoteli. Akhannouch kwa sasa ni Waziri wa Kilimo na Uvuvi wa Morocco. Mkewe, Salwa Idrissi, anamiliki majengo ya kifahari.

Aspen Pharmacare, walioshiriki kuanzisha Gus Attridge ya Afrika Kusini wameingia kwenye orodha hiyo kwa utajiri wao wa dola Milioni 525.

Mtanzania, Mohammed ‘Mo’ Dewji anaingia katika orodha hiyo kwa utajiri wake wenye thamani ya dola milioni 500. Ni Mtendaji Mkuu wa kampuni ya METL, iliyoasisiwa na baba yake, Gulam Dewji. 

Baada ya kumaliza masomo ya biashara katika chuo Kikuu cha Georgetown, Marekani alirejea nyumbani kuendeleza biashara za baba yake na pia kwa sasa ni mwanasiasa, Mbunge wa jimbo la Singida Mjini.
KAYA CHACHE SINGIDA ZAJIUNGA NA CHF

KAYA CHACHE SINGIDA ZAJIUNGA NA CHF

November 15, 2013


E83A4423
Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Katala Beach hoteli mjini Singida.
E83A4411
Mjumbe wa bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Lyidia Choma (kulia) akitoa taarifa yake kwenye siku ya wadau wa Mfuko huo na ule wa Afya ya Jamii (CHF).Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Katala Beach Hotel mjini Singida. Kushoto (aliyeshika mike) ni Meneja wa NHIF mkoa wa Singida, Agnes Chaki.
E83A4406
Mkurugenzi wa takwimu na uhai wa mfuko wa NHIF makao makuu, Michael Mhando akitoa nasaha zake kwenye mkutano wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Katala Beach Hotel mjini Singida. Kushoto ni mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone, Wa kwanza kulia ni kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Mussa Kamala, Mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi na katibu tawala mkoa wa Singida,Liana Hassan.
E83A4435
Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone, (wa pili kulia) akifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa kwenye mkutano wa siku ya wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii. Wa kwanza kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bi. Lyidia Choma.Wa tatu kulia ni Katibu Tawala mkoa wa Singida, Liana Hassan na,Mkuu wa Wilaya ya Singida,Queen Mlozi na kaimu Mganga Mkuu mkoa wa Singida,Dk.Mussa Kimala.
Na Nathaniel Limu
Zaidi ya asilimia 73 ya kaya za mkoa wa Singida, hazijajiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF), hali inayochangia wanafamilia watibiwe bila utaratibu maalum.
Hayo yamesemwa na mkuu wa moa wa Singida, Dk. Parseko Kone, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa mkutano wa siku ya wadau wa Mfuko wa Taifa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii (NHIF) wa mkoa wa SIngida.
Akifafanua, amesema kati ya kaya 259,251 za mkoa wa Singida, ni kaya 45,575 tu, ndizo zilizojiunga na mfuko wa afya ya jamii kati ya mwaka 1998 na Septemba 30 mwaka huu. Hii ni sawa na asilimia 17.6 tu.
“Hata hivyo,wilaya ya Iramba imekuwa ikifanya vizuri katika uandikishaji wa wananchi, kwani takwimu zinaonyesha hadi Septemba 30 mwaka huu, wamekwisha andikisha asilimia 50.3 ya kaya zilizolengwa. Hali hii inaonyesha kuwa viongozi bado hatujatimiza wajibu wetu wa kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko huu”, amesema Dk.Kone.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa, amesema pia inawezekana watoa huduma wamekuwa ni chanzo cha kuwakatisha tama wananchi waliojiunga na hivyo, kuwafanya wananchi wengine wasite kujiunga na Mfuko huu.
“Kwa kuwa wadau wote tumekutana hapa leo, ni nafasi yetu kuangalia nini sababu ya kuzorota kwa utaratibu huu ambao katika baadhi ya halmashauri hapa nchini, umeimarika zaidi",amesema Dk.Kone.
Awali mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Lyidia Choma, alisema Mfuko huo umeidhinisha shilingi bilioni 10, ili zitolewe kwa watoa huduma kuwawezesha kupata vifaa tiba na kukarabati maeneo yao ya kutolea huduma.
“Utaratibu huu ni mikopo ya bei nafuu ambayo hairejeshwi kwa fedha taslimu, isipokuwa kwa kukatwa katika madai ambayo mtoa huduma anawasilisha kwa Mfuko”,amefafanua.
Alifafanua kuwa kwa mkopo wa vifaa tiba, mkopo hurudishwa kwa makato ya asilimia 10 ambayo hulipwa ndani ya miezi 24 na mikopo ya ukarabati wa maeneo ya kutolea huduma, ni miezi 36.
Kauli mbiu ya mwaka huu, ni Afya Bora kwa wote sasa kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

SALHA ISRAEL ATEMBELEA KAMBI YA TANZANIA TOP MODEL 2013

November 15, 2013


 Salha israel mrembo alieng'ara miaka ya 2011 katika mashindano ya urembo nchini,akiongea na washiriki wa Tanzania Top Model 2013 namna ya kujiamini wakiwa katika jukwaa na kujibu maswali endapo watakabiliana na vyombo vya habari.
Washiriki wakimsikiliza kwa makini Salha Israel wakati akiongea nao.
 Washiriki wakiwa katika picha ya paoja na Salha israel.
  Mrembo Salha Israel atembelea kambi ya washiriki wa sindano la Tanzania Top model iliopo katika hoteli ya Jb Belmont iliyopo maeneo ya posta kwa lengo la kuwapa mbinu mbalimbali za kufanya vizuri jukwaani kwani shindano hilo lina upinzani mkali kwa washiriki wenyewe kwa wenyewe.
  Salha alitoa mbinu mbalimbali za kujiamini kwa mwanamitindo awapo jukwaani pamoja na mbinu za kujibu maswali kiusahihi kwa wanahabari ambapo imezoeleka kwa washiriki wengi hushindwa kujibu maswali kiusahihi kitu ambacho hupunguza ari ya shindano.
  Fainali za mashindano haya zitafanyika desemba 7,pia washiriki watapigiwa kura na wananchi ambapo namba maalumu itaolewa hivi punde kumpigia mshiriki umpendae ili kumuongezea alama amabazo zitamwezesha mshiriki wako ashinde.

DIWANI AMKINGIA KIFUA MTENDAJI WA KIJIJI.

November 15, 2013
Na Oscar Assenga,Mkinga.
DIWANI wa Kata ya Gombero wilayani Mkinga mkoani Tanga,Mohamed Bamba amewataka wananchi wa Kijiji cha Kichangani kuwa watulivu ikiwemo kushiriki katika shughuli za kimaendeleo wakati mchakato wa kurejeshwa fedha za serikali ya kijiji hicho 515,000 zilizopotea ukifanyika.

Bamba alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano mkuu wa kijiji hicho
ambapo pamoja na mambo mengine ulikuwa ni kusoma mapato na matumizi kwa wananchi hao.

Wakiwa kikao hapo wananchi walihoji upotevu wa fedha hizo za serikali
ya kijiji hicho ambazo zilipotea kutokana na matumizi mabaya kwa kumtuhumu mtendaji wa kijiji hicho Hamisi Juma kuhusika na tuhuma hizo kwa kumtaka kuzirejesha haraka iwezekanavyo kabla ya kuchukuliwa hatua.

Akizungumza katika mkutano huo,mkazi wa kijiji hicho mchungaji Daudi
Malulu alisema suala la kiongozi huyo wa kijiji kufanya ubadhirifu wa fedha hizo ndani ya serikali utaweza kuwagawa wananchi ikiwemo kukwamisha maendeleo ya wananchi hivyo kuwataka viongozi hao kuwajibika kwa kuzilipa fedha hizo.
  “Ninaweza kusema suala hili sio la kufumbiwa macho tunaziomba
mamlaka husika kulivalia njuga ili kuweza kupatikana ufumbuzi wake kwani hali hiyo ikiendelea hivyo itapelekea kukwamisha miradi ya maendeleo “Alisema Malulu.

Naye mkazi wa kijiji hicho,Mzee Abdallah Mohamed Nzibo alitaka hatua
zichukuliwa dhidi ya mtendaji huyo kutokana na ubadhirifu za fedha za serikali ya kijiji hicho ili kuweza kuwa fundisho kwa watendaji wengine wenye tabia kama hizo.
 
Baada ya tuhuma hizo,Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Hamisi Juma
alisema suala la ubadhirifu wa fedha hizo alipokea na kuhaiadi
kulifanyia kazi ili waweze kupata majibu yake kwenye mkutano mkuu wa kijiji hicho utakaofanyika mwezi desemba mwaka huu.

Hata hivyo diwani Bamba alitolea ufafanuzi kuhusu tuhuma za mtendaji
  huyo za upotezo wa fedha hizo kwa kusema suala la sh.208000 zinajulikana na wapi zilipotea na watafuatilia ili ziweza kupatikana haraka iwezekanavyo.

Bamba alisema suala la 314000 wananchi pamoja na serikali ya kijiji
watakaa ili kuweza kufahamu fedha hizo zimepotea kwa nani ili ziweza kupatikana ili ulipwaji wake ufanyike haraka.

Hata hivyo diwani huyo alisisitiza upotevu wa fedha halali ambazo

zimepotea katika serikali ya kijiji hicho ni sh.208000 ambazo
watahakikisha wanafanya jitihada za kubaini muhusika wake ili
atakapobainika hatua kali za kisheria zidi yake ziweze kuchukuliwa.

Aliongeza kuwa fedha nyengine ambazo wameelezwa na wananchi wao
watahakikisha wanaziangalia kwa umakini katika mahesabu kwa sababu huenda zikawa zimekosewa.