SAO HILL HUZALISHA MICHE MILIONI 5 YA MITI KILA MWAKA

March 19, 2024

 

Mhifadhi mkuu wa shamba la miti Sao Hill PCO Tebby Yoram alisema kuwa miche hiyo huoteshwa kwa ajili ya kupandwa katika shamba hilo na mingine kugaiwa wananchi,wadau na taasisi mbalimbali.
Baadhi ya miti ikivunwa katika shamba la miti Sao Hill wilaya ya Mufindi mkoani Iringa
Mhifadhi mkuu wa shamba la miti Sao Hill PCO Tebby Yoram alisema kuwa miche hiyo huoteshwa kwa ajili ya kupandwa katika shamba hilo na mingine kugaiwa wananchi,wadau na taasisi mbalimbali.






Na Fredy Mgunda, Iringa.



SHAMBA la miti Sao Hill lililopo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa huotesha miche milioni 5 ya miti kila mwaka katika bustani tatu zilizopo katika shamba hilo.




Akizungumza na waandishi wa habari Mhifadhi mkuu wa shamba la miti Sao Hill PCO Tebby Yoram alisema kuwa miche hiyo huoteshwa kwa ajili ya kupandwa katika shamba hilo na mingine kugaiwa wananchi,wadau na taasisi mbalimbali.




PCO Yoram alisema kuwa lengo la kubwa la kugawa miche hiyo ni kuendeleza uhifadhi wa misitu kwa wananchi na taasisi hizo kuendelea kupanda miti kwa wingi katika mashamba na kushiriki katika kuhifadhi shamba hilo.




Alisema kuwa kuelekea kilele cha siku ya upandaji miti kitaifa itakayofanyika katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro na uongozi wa shamba hilo umejipanga kupanda miti kwenye vyanzo vya maji vilivyopo katika shamba hilo.




PCO Yoram alisema kuwa wanapanda miti kwenye vyanzo vya maji kwa lengo la kuendelea kutunza vyanzo vya maji na shamba la miti Sao Hill hupanda hekta 2500 hadi hekta 300 kila mwaka.




Aidha PCO Yoram alisema kuwa licha ya kupanda miti mingi lakini shamba hilo huvunwa Laki 6 hadi 7 ujazo wa uvunaji wa mazao ya miti katika shamba hilo kwa kuvinufaisha viwanda 400 ambavyo hutumia malighafi za misitu.

DKT. BITEKO ASHIRIKI SHEREHE YA KUWEKWA WAKFU NA KUSIMIKWA ASKOFU MPYA JIMBO KATOLIKI LA MAFINGA

March 19, 2024

 --Asema Rais Samia anaendelea kutoa ushirikiano kwa madhehebu ya Dini

--Asisitiza utunzaji wa mazingira
--Ampongeza Dkt. Samia kwa kuendesha nchi kwa utulivu na kasi ya maendeleo
--Atoa neno kuhusu Uchaguzi Serikali za Mitaa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemwakilisha Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe ya kuwekwa Wakfu na Kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo jipya Katoliki la Mafinga, Mhashamu Vincent Cosmas Mwagala na kueleza kuwa Dkt. Samia anaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano kwa Kanisa Katoliki na madhahebu mengine ya Dini ili kuwaletea maendeleo Watanzania.

Amesema, nia ya Rais, Dkt. Samia ni kuona wananchi wanapata huduma bora katika nyanja mbalimbali ikiwemo Zahanati, Barabara, Maji, Shule na umeme wa uhakika hivyo ili kutekeleza suala hilo kwa ufanisi Serikali inashirikiana na Taasisi binafsi ikiwemo madhehebu ya Dini katika kuwapelekea maendeleo wananchi.

Akizungumza na Wananchi waliohudhuria sherehe hiyo katika Halmashauri ya Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa, Dkt. Biteko amesisitiza kuhusu utunzaji wa mazingira na kutoa angalizo kuwa yeyote anayeharibu mazingira aonekane kama adui na achukuliwe hatua kwani athari za kutokutunza mazingira ni kubwa, akitolea mfano kuwepo kwa mgawo wa umeme kutokana na kutokuwa na maji ya kutosha kuzalisha umeme.

“Leo tumejenga mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere, mradi ule ni mkubwa sana, lile si bwawa tu bali ni ziwa kwani urefu wake ni kilometa 100 na upana wake ni kilometa 25, uwepo wake unahitaji maji ya kutosha na ikizingatiwa kuwa gharama kubwa zimetumika kujenga mradi huo zaidi ya shilingi Trilioni Sita, ni lazima tulinde mazingira ili kupata faida mbalimbali ikiwemo maji ya kutosha kuzalisha umeme.” Amesema Dkt. Biteko

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa tarehe 19 Machi, 2024, Rais, Dkt. Samia ametimiza miaka mitatu akiwa madarakani ambapo amedhihirisha kwa vitendo kuwa ni kiongozi bora ambaye ameendelea kuiweka nchi katika hali ya utulivu.

Ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia ameendelea kutekeleza miradi mbalimbali aliyoikuta mara baada ya kuapishwa ikiwemo barabara, reli, umeme na ameendelea kubuni miradi mipya na kuiendeleza kwa kasi kubwa.

Dkt. Biteko ametoa wito kwa viongozi wa Dini na Watanzania kumuombe Rais Samia ili aendelee kuongoza nchi kwa ufanisi akiwa na afya njema na pia kuiombea nchi ili iendelee kuwa ni mahali salama pa kuishi.

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Watanzania kuchagua viongozi wanaokerwa na shida za wananchi na wanaozitatua na kwamba wasichague viongozi kwa kigezo cha ukabila, dini au mahali walipotoka bali msingi uwe ni maendeleo na utanzania.

Kwa upande wake, Askofu Mpya wa Jimbo la Mafinga, Mhashamu Vincent Mwagala amesema Kanisa Katoliki litaendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika masuala ya ya ustawi wa jamii ili amani iendelee kutamalaki na kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Pia amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuhudhuria sherehe hiyo na kuwasilisha ujumbe wenye matashi mema kutoka kwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile na Spika Mstaafu, Mama Anna Makinda.





JESHI LA POLISI KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI MKOA WA TANGA WATOA NENO KUHUSU MAFUNZO YANAYOTOLEWA KWA MADEREVA BODABODA

March 19, 2024

 Na Mwandishi Wetu,Tanga


JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Tanga kimeelezea kwa kina kuhusu mafunzo ya usalama barabarani yanayotolewa na Shirika la Amend kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini yanavyosaidia kutoa elimu ya matumizi salama ya barabara kwa madereva bodaboda wa Mkoa huo.

Akizungumza jijini Tanga,Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani William Mwamasika amesema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa madereva bodaboda wa Mkoa huo na wanaushukuru Ubalozi wa Uswisi pamoja na Amend Tanzania kwa kuona umuhimu wa madereva bodaboda kupatiwa mafunzo hayo.

"Jeshi la Polisi Kitengo cha usalama barabarani Mkoa wa Tanga tunawashukuru Ubalozi wa Uswisi nchini kwa udhamini wa mafunzo haya na kuona kuna haja ya kuongeza nguvu kwenye utoaji elimu ya usalama barabarani hasa katika kundi hili ambalo linaonekana kuwa hatarini  zaidi."

Pamoja na shukrani hizo, mkakati uliopo kwa sasa ni kuhakikisha mafunzo ya usalama barabarani kwa madereva bodaboda yanayotolewa katika Wilaya zote za Mkoa wa Tanga kwani kwa sasa yanafanyika katika Jiji la Tanga na tayari madereva bodaboda zaidi ya 200 wamefikiwa na lengo ni kuwafikia madereva 500.

Hivyo katika kufanikisha kampeni hiyo Kamanda Mwamasika amesema  watakaa kikoa cha pamoja kuona ni maeneo yapi yafikiwe ili kuhakikisha vijana hao wa kundi la bodaboda wanapata mafunzo yatakayowawezesha kujilinda wao wenyewe na kulinda abiria wao lakini waachwe kuwa visababishi vya ajali barabarani.

Kwa upande wake Ofisa Miradi wa Amend Tanzania Ramadhan Nyanza ametumia nafasi hiyo kuwaomba vijana wanaojihusisha na bodaboda kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo yanayotolewa bure kwani tayari Ubalozi wa Uswisi wameshafadhili.

"Tunatoa mafunzo haya bure kwa hiyo vijana wajitokeze kwa wingi,watumie mafunzo haya na nafasi hii kupata elimu.Tunafahamu wao ni madereva lakini kuwa dereva bila kutii sheria za usalama barabarani inamaana unakuwa mtu ambaye unaendesha chombo cha moto kwa kudhamiria kusababisha ajali,"amesema Nyanza.

Aidha amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa madereva bodaboda katika Wilaya zote Mkoa wa Tanga na lengo la kwenda katika Wilaya zote ni kuifikia jamii.Hivyo wanaomba bodaboda wajitokeze kwa wingi katika mafunzo hayo.

 Pia amesema katika mradi huo mbali ya kutoa mafunzo hayo, wanatarajia kufanya uboreshaji wa miundombinu salama katika Shule ya Msingi Azimio na Makorora ikiwa ni muendelezo wa miradi wanayoifanya ndani ya Jiji la Tanga ,lengo likiwa kuendelea kuwalinda wanafunzi wanapokuja na kuondoka shuleni.

Pia amesema wanaandaa kanuni za maadili ambazo wanashirikiana na Jeshi la Polisi na kwamba watayajumuisha rasmi katika elimu ya usalama barabarani na kanuni hizo zitakuwa zinalenga kusaidia kupunguza ajali lakini kuwalinda aabiria

SEKTA YA AFYA NEEMA TUPU MIAKA 3 YA RAIS DKT SAMIA

March 19, 2024

Na Mwandishi Wetu, Dar

Wizara ya Afya imempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluh Hassan katika kipindi cha miaka mitatu ambapo Sekta ya afya imepatiwa kiasi cha shilingi Trilion 6.722 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele mbalimbali ili kuimarisha huduma za afya nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema wamepokea zaidi ya shilingi bilioni 20 kwenda Bohari ya Dawa MSD ili kuongeza  upatikanaji wa dawa kwenye Hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya nchini ambapo hadi kufikia Desemba 2023 zaidi ya asilimia 84 zimepelekwa kutoka asilimia 58 mwezi Desemba, 2022 na kupelekea kupungua kwa malalamiko katika hospital za umma nchini.


Ameongeza kuwa kupitia fedha hizo wizara ya afya imetekeleza kwa mafanikio makubwa majukumu yake, ikijikita zaidi kwenye maeneo ya Ujenzi wa  miundombinu ya kutolea huduma za  afya nchini, kuimarisha upatikanaji wa dawa na bidhaa nyingine za Afya.


"Ndani kipindi cha Miaka mitatau Serikali kupitia Wizara ya Afya inaeendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya, Upatikanaji wa Huduma za Ubingwa na ubingwa Bobezi nchini,  kuimarisha huduma za Uchunguzi wa magonjwa ikiwemo huduma za Mionzi, kuimarisha Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, kudhibiti maambukizi ya HIV/UKIMWI,  kifua kIkuu, malaria na magonjwa ya mlipuko, Ajira kwa watumishi na ufadhili wa wanafunzi katika ngazi na fani mbalimbali pamoja na kupitishwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote." amesema Waziri Ummy.


Amesema kuwa,  uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan  katika kuimarisha huduma ubingwa na ubingwa bobezi umewezesha wananchi wengi kupata huduma hizi ndani ya nchi kwa gharama nafuu badala ya kuzitafuta nje ya nchi.


Hata hivyo, amesema uwekezaji huu umeweza kuvutia wagonjwa mbalimbali kutoka nje ya nchi  na hivyo kuifanya Tanzania kuwa Kituo cha Tiba Utalii kwa ukanda wa nchi za afrika mashariki na kusini mwa Afrika.


Ameongeza kuwa kwa kipindi hicho cha miaka mitatu vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka  kutoka vituo 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 9,610 Machi 2024 ikiwa  ni sawa na ongezeko la vituo 1,061.


"Serikali ya awamu ya sita imejenga na kufanya maboresho ya miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo mapya, ukarabati na kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya katika mikoa mipya mitano, maboresho hayo yamegharimu jumla ya Shilingi Trilioni 1.02."amesema Waziri Ummy na kuongeza kuwa,


kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majengo mapya, ukarabati na kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya katika mikoa mipya mitano. Maboresho hayo yamegharimu jumla ya Shilingi Trilioni 1.02." amesema Waziri Ummy na kuongeza kuwa,


"Upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi umehakikisha kila mwananchi anapata mahitaji yote muhimu ya msingi ya kimatibabu pale anapoenda kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya."


Sambamba na hayo amesema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hasssan katika kuimarisha ubora wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kupitia Viashiria vikuu vinavyotumika kupima mwenendo wa ubora wa huduma kwa Nchi Wanachama wa Shirika la Afya Duniani imejidhihirisha wazi kuwa Tanzania imefanya vizuri katika kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika kipindi cha miaka mitatu.


Amesema kuwa, Serikali inaendelea kuajiri wataalam katika Sekta ya  Afya ambapo jumla ya wataalam 35,450 wa kada mbalimbali wameajiriwa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 hivyo kufanya, jumla ya ajira za mikataba kwa watumishi wa Afya 2,836 kupitia miradi mbalimbali ya Serikali zilitolewa.


’HATUJARIDHIKA NA UREJESHEJA FEDHA ZA MIKOPO YA KKK’’

March 19, 2024



Na Munir Shemweta, CHALINZE

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imesema kuwa, haijaridhishwa na urejeshaji mikopo ya fedha za mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi (KKK) unaofanyika kwenye halmashauri mbalimbali nchini.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 18 Machi 2024 na Kamati hiyo wakati ilipotembelea na kukagua utekelezaji mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika eneo la Msolwa katika halmashauri ya wilaya ya Chalinze mkoa wa Pwani.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe, Timotheo Mzava ameeleza kuwa, mbali na Kamati yake kuridhishwa na mradi wa KKK kwa ujumla lakini hawajaridhishwa na namna mikopo hiyo inavyorejeshwa na halmashauri.

Akitolea mfano wa Halmashauri ya Chalinze katika mkoa wa Pwani, Mhe, Mzava amesema pamoja na halmashauri hiyo kukopeshwa kiasi cha shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya mradi wa KKK lakini imeshindwa kurejesha fedha kwa wakati.

 ‘’Kama Kamati bado hatujaridhishwa kabisa namna ya kasi ya urejeshaji fedha hizi na wito na msisitizo wetu zifanyike kila aina ya jitihada kuhakikisha fedha zinarudi ili zikasaidie maeneo mengine yenye uhitaji ili dhamira ya Rais ya kutoa fedha hizo iweze kufikiwa’’ alisema Mzava

Kwa mujibu wa Mhe, Mzava, hadi Machi 2024 kwa ujumla wizara imepokea marejesho ya shilingi bilioni 22.7 kati ya shilingi bilioni 50 sawa na asilimia 45 kutoka kwenye halmashauri na taasisi mbalimbali zilizonufaika na mkopo huo.

Amesema, fedha zinazotolewea kama mkopo usio na riba kwa halmashauri zikirejeshwa zitasaidia kukopesha halmashauri nyingine na hivyo kuisaidia kutatua changamoto za sekta ya ardhi nchini na kuboresha katika maeneo mengine.

Hata hivyo, ametaka kufanyika jitihada mbalimbali ili kusaidia katika urejeshaji mikopo hiyo na kuweza kuzisaidia halmashauri nyingine ili ziweze kuondoa changamoto za sekta ya ardhi nchini.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amebainisha kuwa, mpaka sasa halmashaurii zilizorejesha kiasi chote cha fedha ya mkopo ni 12 huku zile zilizorejesha sehemu ya fedha zikiwa ni 43.

Mhe, Pinda amesema, Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) ni program ya miaka kumi inayotekelezwa na wizara yake kwa kushirikiana na halmashauri mbalimbali nchini.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa Programu hiyo ulianza mwaka 2018/2019 na unatarajiwa kukamilika 2028/2029. Lengo la Programu ya KKK ni Kupanga miji na kuhakikisha makazi holela yanaondolewa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Programu hiyo inatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ambazo ni mamlaka za upangaji na sekta binafsi ambapo program hiyo inagharimiewa na serikali kupitia fedha za ndani za bajeti ya maendeleo.

Serikali ilitoa mtaji wa shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya utekelezaji wa program ya KKK kwa utaratibu wa kuzikopesha halmashauri na taasisi ambapo wizara kwa kushirikiana na wizara ya fedha na Ofisi ya Rais TAMISEMI ziliweka utaratibu kwa kuweka vigezo vya kutoa mkopo huo bila riba kwa ajili ya utekelezaji wa program.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe, Timotheo Mzava akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon mara baada ya Kamati yake kuwasili mkoa wa Pwani kukagua utekelezaji Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika halmashauri ya Chalinze mkoa wa Pwani tarehe 18 Machi 2024. Katikati ni Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Geophrey Pinda.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akisalimiana na Mbunge wa Jimbo la Chalinze na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe, Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii katika halmashauri ya wilaya ya Chalinze Machi 18, 2024.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe, Timotheo Mzava na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Geophrey Pinda wakimsikiliza Afisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Deo Msilu (wa pili kulia) kuhusu mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi unaotekelezwa katika eneo la Msolwa Halmashauri ya Chalinze Machi 18, 2024.
Afisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Deo Msilu akisisitiza jambo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokwenda kukagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika eneo la Msolwa Chalinze Machi 18, 2024.
Afisa Ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze Deo Msilu (Kulia) akielezea matumizi ya kifaa cha upimaji mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokwenda kukagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi katika eneo la Msolwa Chalinze Machi 18, 2024.
Mbunge wa jimbo la Chalinze na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe, Ridhiwani Kikwete akimkabidhi Hati Milki ya Ardhi mmoja wa wananchi wa Chalinze wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokwenda kukagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi eneo la Chalinze machi 18, 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
SEKRETARIETI YA MAADILI NENDENI MKASIKILIZE MALALAMIKO YA WANANCHI-WAZIRI SIMBACHAWENE

SEKRETARIETI YA MAADILI NENDENI MKASIKILIZE MALALAMIKO YA WANANCHI-WAZIRI SIMBACHAWENE

March 19, 2024

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiongea na maafisa uchunguzi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kikao kazi cha wachunguzi Kilichofanyika katika ukumbi wa Ngorongoro jijini Arusha tarehe 18 Machi 2024.


Kamishna wa Maadili, Jaji (Mst.) Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi akiongea na maafisa uchunguzi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kikao kazi cha wachunguzi Kilichofanyika katika ukumbi wa Ngorongoro jijini Arusha tarehe 18 Machi 2024.



..........

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb) ametoa wito kwa watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Umma kutoka ofisini kwenda kwa wananchi kusikiliza malalamiko yao na kuyatafutia ufumbuzi badala ya kukaa ofisini kusubiri wananchi wachache wanaolalamikia viongozi.

“Sekretarieti ya Maadili nendeni mkawasilikize wananchi, yapo mambo wanayapigia kelele sana kuhusu tabia na mwenendo wa viongozi wao. Kelele zao zinaposikika tokeni mkawasikilize, hii itasaidia kutatua kero zao na mtawasaidia pia viongozi kujirudi na kufuata misingi ya maadii,” alisema.

”Tusichelewe sana kushughulikia malalamiko yanayotolewa na wananchi hadhalani.”

Mhe. Simbachawene alisema hayo jijini Arusha tarehe 18 Machi, 2024 wakatiakifungua kikao kazi cha Wachunguzi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadii ya Viongozi wa Umma.

“Misingi hii lazima tuilinde na hili ndilo jukumu letu. Misingi hii isipozingatiwa, wananchi wanakosa huduma na malengo ya nchi hayatafikiwa,” alisema.



Kwa mujibu wa Mhe. Waziri, lazima watumishi wa Sekretarieti ya Maadili watoe elimu kuhusu misingi ya maadli na kusikiliza changamoto zao.

Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene alisema jukumu la kusimamia maadili linahitaji mtumishi anayetumia mbinu, busara na weledi wa hali ya juu kutokana na kuwahusu viongozi wakubwa na ni la kikatiba.

“Maadili ni zaidi ya sheria, lazima msimamie maadili ya viongozi wote kuanzia ngazi ya chini. Twende mbali tuanzie ngazi ya chini huko serikali za mitaa kusimamia maadili. Tusihangaike na viongozi wanaojaza fomu za Tamko tu kwasababu lazima kiongozi yeyote lazima awe mwadilifu,” alisema na kuongeza kuwa, “maadili katika jamii zetu ni jambo la msingi na lilikuwepo hata wakati wa ujima.”

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi alieleza kuwa Taasisi imeona umuhimu wa wachunguzi wote kuwa na kikao cha pamoja kujadili mustakabali wa majukumu yao.

“Hii ni mara yetu ya kwanza tangu Taasisi ilipoanzishwa mwaka 1996 kuwa na kikao kama hiki kwa lengo la kuwakutanisha wachunguzi wote ndani ya Taasisi kujadili kwa kina mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wa kazi na mafanikio kwa mujibu wa matakwa ya Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,” alisema.

Kwa mujibu wa kifungu cha 19(2) cha Sheria ya Maadili ya Viongizo wa Umma Na. 13 ya 1995, majukumu ya Sekretarieti ya Maadili ni kupokea malalamiko ya ukiukwaji wa maadili, kufanya uchunguzi, kupokea matamko, kufanya uhakiki na kutoa elimu ya maadili.

Majukumu mengine ni kufanya utafiti wa hali ya uadilifu nchini, kutoa ushauri katika mambo ya uadilifu na kubuni mikakti ya ukuzaji maadili.

Mhe. Sivangilwa alizitaja mada zitakazo wasilishwa kuwa ni; Utendaji katika Ofisi za Kanda, Viambata vya Makosa ya Maadili, Utaratibu wa zoezi la Uhakiki, Mikakati ya utendaji kazi pamoja na Changamoto na utatuzi wake katika kushughulikia malalamiko na uchunguzi.
KOICA KUONGEZA NGUVU UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO

KOICA KUONGEZA NGUVU UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO

March 19, 2024

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, akimkabidhi zawadi yenye picha ya Mlima Kilimanjaro, Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) anayeshughulikia mambo ya kimkakati, Mhe. Dong Ho Kim, baada ya kumaliza kikao kilichojadili ushirikiano na utekelezaji wa miradi ikiwemo ya miundombinu, elimu na afya, kilichofanyika jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba akizungumza kuhusu miradi ya maendeleo wakati wa kikao na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) anayeshughulikia Mambo ya Kimkakati Mhe. Dong Ho Kim, jijini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA), anayeshughulikia mambo ya kimkakati, Mhe. Dong Ho Kim, akizungumza wakati wa kikao na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba ambapo alisema kuwa Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, kilichofanyika jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, akiagana na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) anayeshughulikia mambo ya kimkakati, Mhe. Dong Ho Kim, baada ya kumaliza kikao kilichojadili ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Korea katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, kilichofanyika jijini Dodoma.

Ujumbe kutoka Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (kushoto) na ujumbe kutoka Jamhuri ya Korea uliyoongozwa na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) anayeshughulikia mambo ya kimkakati, Mhe. Dong Ho Kim ukiwa katika mkutano ulioangazia ushirikiano wa maendeleo, kilichofanyika jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (watano kulia), na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA), anayeshughulikia mambo ya kimkakati, Mhe. Dong Ho Kim (wasita kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe kutoka Wizara ya Fedha na ujumbe kutoka Korea (KOICA), baada ya kikao kilichojadili kuimarisha ushirikiano, kilichofanyika jijini Dodoma.

Na. Saidina Msangi na Peter Haule, WF, Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, amesema Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA), kupitia mpango uliotiwa saini mwaka 2014 limetoa ruzuku ya jumla ya Dola za Kimarekani milioni 139.5 sawa na Sh. bilioni 356.3 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dkt. Mwamba alibainisha hayo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea anayeshughulikia mambo ya kimkakati (KOICA) Don Ho Kim, aliye katika ziara ya kikazi Tanzania.

Alisema kuwa kupitia fedha hizo miradi kadhaa imekamilika na mingine inaendelea ambayo ni pamoja na Mfuko wa sekta ya  Afya na Mpango Jumuishi wa Vijana Walio nje ya Shule (IPOSA).

‘‘Miradi kadhaa iko katika hatua mbalimbali za maandalizi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mifumo ya usambazaji maji kwa maeneo ya mijini na vijijini mjini Dodoma na kuboresha usawa wa kijinsia katika Elimu (STEM) kwa Shule za Sekondari nchini ambapo miradi hii kwa sasa inapitia michakato ya kuidhinishwa ndani ya Wizara husika’’ alisema Dkt. Mwamba.

Alisema tangu 1991, KOICA imesaidia Serikali hasa katika nyanja za afya, elimu, maji na usafiri ili kubadilisha hali ya kijamii na kiuchumi nchini.

Dkt. Mwamba alisema kuwa kupitia mipango mbalimbali ya ufadhili, usaidizi wa kiufundi na programu za kujenga uwezo, KOICA imechochea mabadiliko chanya na yaliyosaidia ukuaji na ustawi jumuishi, kupambana na umaskini na kukuza uchumi.

Aidha alieleza kuwa Agosti 2023, Wizara ya Fedha iliwasilisha ombi la miradi minne ya maendeleo kwa msaada wa KOICA ya jumla ya Dola za Kimarekani milioni 39, sawa na Sh. bilioni  98, inayotarajiwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2025.

Dkt. Mwamba alibainisha miradi hiyo kuwa ni mradi wa kuanzisha  chuo cha ufundi Morogoro,  mradi wa kuimarisha huduma za mama na mtoto jijini Dar es Salaam, mradi wa kuanzisha mifumo ya usambazaji maji katika maeneo ya vijijini vya mkoa wa pwani na mradi wa kuanzisha mpango kabambe wa kitaifa wa barabara kuu na uboreshaji wa uwezo wa rasilimali watu.

Dtk. Mwamba aliishukuru  Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia KOICA kwa kuunga mkono malengo hayo ambapo imekuwa mojawapo ya vyanzo vikuu vya ufadhili wa ruzuku katika kufanikisha miradi ya maendeleo na kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea  kuhakikisha kuwa rasilimali zote zinazopatikana kutoka KOICA zinatumika kwa uangalifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ndani ya muda uliokubaliwa.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) Don Ho Kim, alisema kuwa Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo ya uchumi hasa katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, afya pamoja na kuwezesha wafanyabiashara wadogo kuweza kunufaika na masoko.

Kuhusu miradi iliyowasilishwa na Tanzania alisema kuwa, ipo katika mchakato wa kuidhinishwa na Shirika hilo ambapo kati ya Novemba na Desemba mwaka huu inatazamiwa kuidhinishwa na Bunge la nchi hiyo, aliahidi nchi yake kuendeleza ushirikiano na kuunga mkono mipango ya maendeleo ya  Tanzania