Magari awafunda wasanii chipukizi.

Magari awafunda wasanii chipukizi.

June 02, 2013
Na Oscar Assenga,Lushoto.
MSANII Gwiji wa filamu Tanzania,  
Charles Magari  maarufu kama "Mzee wa Magari" amewaasa wasanii chipukizi wa tasnia hiyo nchini kutambua kuwa sanaa ni kazi kama zilivyo nyingine ambayo inaweza ‘kumtoa’ kijana kutoka kwenye umaskini na kuwa katika hali nzuri ya kimaisha.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye sherehe za uzinduzi wa Filamu  mpya iitwayo “Hulka” iliyofanyika mjini Lushoto, Mkoani Tanga ambapo iliwashirikisha wasanii wengine nguli kama Mzee Jengua, Davina, Birigita na Sekuti.
Magari alisema vijana wengi wanaonekana wakipoteza muda kwenye vijiwe wakipiga porojo zisizo na tija huku wakilalamikia hali duni ya maisha yao wakidai kuwa hawana ajira.
“ Ajira huwezi kuipata kwa kukaa tu na kulalamika kwani fursa ya kujiajiri imepanuka sana”, alisema Magari na kuongeza, tasnia ya sanaa bado inahitaji vijana wengi wenye kujituma.
Alieleza kuwa nia ya kuja kuzindua filamu hiyo ni kutaka kuwapa fursa vijana wa wilaya ya Lushoto kujifunza maudhui yaliyomo katika filamu hiyo na kuchukua hatua ya kujisahihisha.
Katika filamu hiyo washiriki wanaigiza tabia ya kabila fulani ambalo halikutajwa ambapo mwanamke aliyeolewa huona hapendwi asipopigwa na muwe mara kwa mara.
Nafasi ya mume anacheza Sekuti ambapo Biligita anachukua nafasi ya mke,Mume ni mtoto wa Mzee Jengua na mke ni binti ya Mzee Magari.
Akizindua filamu hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto,Majid Mwanga, Ofisa Utamaduni wa wilaya hiyo, Ezekiel Almas alisema wakati sanaa inaanza kukubalika katika jamii, upo umuhimu kwa washiriki hao kujali na kudumisha tamaduni za kiafrika.
Almas aliitaka jamii kuondoa dhana iliyojengeka katika baadhi ya watu kwamba usanii ni uhuni ambapo alieleza uhuni ni tabia ya mtu binafsi sio fani yake.
Meneja wa Creator Entertainment iliyoandaa sherehe hizo, Mwanahawa Chongole alisema kampuni yake ilikubali kuchukua jukumu la kuandaa sherehe hizo kutokana na kutambua umuhimu wa maudhui yaliyomo ndani ya filamu hiyo kwani inatoa ujumbe utakaoelimisha jamii kwa ufasaha.
Mwisho.
Tanga Warriors yaiadhiri City Kings yaibamiza Vikapu 46-37.

Tanga Warriors yaiadhiri City Kings yaibamiza Vikapu 46-37.

June 02, 2013

  Na Oscar Assenga,Tanga.
TIMU ya Mpira wa Kikapu ya Tanga Warriors mwishoni mwa wiki iliifunga City Kings vikapu 46-37 katika bonanza la Michezo ambalo liliandaliwa na Bandari Tanga lengo likiwa ni kuwaweka vijana pamoja na kuinua michezo.

Katika mchezo huo Tanga Warriors walionekana kucheza kwa kujipanga na kupeleka mashambulizi mara kwa mara kwenye lango la City Kings ambapo mpaka mzunguko wa kwanza unamalizika Tanga Warriors walikuwa wanaongoza kwa vikapi 37-22 kwenye mechi hiyo ambayo ilichezwa viwanja vya Bandari jijini Tanga.

Baada ya kumalizika mechi hiyo ilifuatiwa na mchezo wa Pete ambapo timu ya Umiseta Tanga iliweza kuumana na Bandari Tanga na kumalizika kwa Bandari Tanga kuibuka na ushindi wa mabao 24-19,katika mchezo ambao ulikuwa na upinzani wa hali ya juu.

Bonanza hilo ambalo lilikuwa la aina yake kutokana na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa michezo mkoani ambapo kwenye mchezo wa kikapu timu ya  Umiseta Tanga waliweza kuifunga Bandari kwa vikapu 24-17.

Mechi ya mwisho ambayo ilikuwa na upinzani mkubwa ni ya kuvuta kamba ambapo timu ya City Kings iliweza kuibuka kidede baada ya kuwavuta Tanga Warriors seti 2-1 michezo ambayo ilichezwa viwanja vya Bandari jijini Tanga.

Nyota wa bonanza hilo alikuwa ni Adam Mkondo kutoka timu ya Tanga Warriors ambaye alichangia kwa kiasi kikubwa kuipa ushindi timu yao kwenye mechi hiyo .

Akizungumza kabla ya kuanza bonanza hilo mgeni rasmi, Kaimu Meneja wa Bandari Tanga,Moshi Mtambalike Chawala alisema lengo la bonanza hilo lilikuwa kuwapa hamasa vijana kupenda michezo pamoja na kuwataka vijana kupenda kujituma na kucheza kwa moyo kwani michezo ni ajira ambayo inaweza kuwainua katika maisha yao.

Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Bandari ya Tanga, Teckla Malombe alisifu viwango vya wachezaji walioshiriki bonanza hilo na kuwataka vijana kuendelea kupenda michezo na kuipa kipaumbele.

Nae Mratibu wa Bonanza hilo, Dr.Omari Khupe alisema Bonanza hilo ni endelevu ambalo hufanyika kila wiki ya mwishoni mwa mwezi lengo ni kuwakutanisha wanamichezo pamoja na kuinua viwango vya michezo.

Mwisho.

Mashabiki wakifuatilia bonanza hilo jana.

June 02, 2013
Mashabiki wa michezo waliojitokeza kwenye viwanja vya Bandari  wakifuatilia bonanza hilo.

Mcheze vema

June 02, 2013
Afisa Utumishi wa Bandari Tanga,Teckla Malombe akikagua timu kabla ya kuanza bonanza hilo anayefuatia ni mratibu wa bonanza hilo,Dr,Omari Twaha.


Pete nao hawakuwa nyuma

June 02, 2013
Timu za Mchezo wa Pete zikichuana katika bonanza ambalo limeandaliwa na Bandari Tanga nakufanyika jana kwenye viwanja vya Bandari Tanga.

Tunafuatilia.

June 02, 2013
Kaimu Meneja wa Bandari Tanga,Moshi Mtambalike Chawala akishuhudia bonanza hilo na kulia kwake ni Afisa Utumishi wa Bandari Tanga,Teckla Malombe.