MIKAKATI YA KUENDELEZA MPIRA WA MIGUU KWA WANAWAKE
Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam.
Utangulizi:
Awali
ya yote napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya kamati ya utendaji ya
TWFA kuwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu kwa kutupa ridhaa ya kuongoza
chama kwa kipindi cha miaka minne.
Pia
napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wadau wote wa mpira wa miguu
kwa kutuwezesha kufika hapa tulipo. Napenda niwashukuru wadau wote kwa
ujumla wao na pia kuishukuru serikali kwa namna ya pekee zaidi kwa
mchango wake ,na mashirika na makampuni ambayo yamekuwa karibu sana nasi
NMB, SERENGETI, NSSF, PPF, na Bakheresa Group of Companies.
Tunaamini
kabisa kuwa vyombo vya habari ni washirika wetu wakubwa katika
kuendeleza mpira wa miguu wanawake. Napenda kuvishukuru vyombo vyote vya
habari hapa nchini na hata vile vya nje vilivyoweza kutoa nafasi katika
ujenzi wa mpira wa miguu wanawake.
Maendeleo ya mpira
Kutekeleza na kuendeleza mpango wa grassroot.
Kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania,Chama cha Mpira wa Miguu wanawake na vyama vya mikoa na wadau mbalimbali tutaendelea
kuendeleza mradi wa mpira wa miguu kwa watoto wa kike na wa kiume
Grassroot programme.(umri wa miaka 06-12).kwa mwaka 2013 mradi huu
utatekelezwa katika mikoa mitano (5) mikoa hiyo ni Tanga,Pwani.Mwanza,Mtwara
na Lindi. Mradi huu unaendeshwa kupitia shule za msingi.Kwa mwaka 2012
Mradi huu umeendeshwa katika mkoa wa Dar es Salaam na watoto wapatao 8766 (wasichana 4909 na wavulana 3857 ) na walimu 26 wameshirikishwa.
Mafunzo ,semina na makongamano
Kwa mwaka 2013 tunatengemea kuendesha mafunzo mbalimbali katika nyanja kuu nne za maendeleo ya mpira wa miguu yaani Utawala na uongozi,Ualimu(Ukocha) Uamuzi na utabibu katika mpira wa miguu .Katika
mwaka mwaka 2013 mafunzo yatafanyika zaidi katika nyanja ya uongozi ili
kuwajengea stadi za uongozi viongozi wengi ambao wameingia madarakani
katika chaguzi zilizofanyika kwa mwaka 2012/2013.Mafunzo ya utawala na
uongozi yatafanyika katika mikoa nane:Dar es
Salaam,Pwani,Morogoro,Mwanza,Musoma,Shinyanga,Kilimanjaro na
Tanga.Katika mafunzo hayo baadhi ya washiriki watateuliwa kutokana na
uwezo wao kwa kuzingatia vigezo vitakavyowekwa na watahudhuria semina
itakayo andaliwa kwa kushirikiana na shirikisho la mpira wa miguu
Tanzania.
Mafunzo kwa walimu katika ngazi mbalimbali na uratibu wa utekelezaji wa mafunzo yaliyofanyika yatapewa kipau mbele.
Mafunzo
kwa waamuzi yatalenga zaidi kuibua vipaji vya watoto wa kike walioko
mashuleni na wachezaji wanaomaliza/waliomaliza muda wao.Mafunzo
yatafanyika kwa awamu mbili katika mkoa wa Dar es Salaam.
Madaktari wa michezo ni
muhimu sana katika maendeleo ya mpira na afya za wachezaji kwa
kushirikiana na vyombo husika mafunzo kwa mwaka 2013 yatafanyika kwa
awamu mbili na yatafanyika katika mkoa wa Dar es Salaam.
Wanahabari
wenye uweledi katika mpira wa miguu wa wanawake ni chachu ya maendeleo
ya mpira huo.Nafasi ya wanahabari ni kubwa katika kuendeleza mpira wa
miguu ili kuwajengea ujuzi zaidi kutakuwa na mafunzo kwa wanahabari
yatakayofanyika Dar es Salaam.
Uongozi na utawala bora
Maendeleo
ya mpira wa miguu kwa wanawake yanahitaji viongozi bora na waliopewa
ridhaa na vyombo husika.Chaguzi zimefanyika katika mikoa 16 kati 25 ya mikoa ya Tanzania Bara. Pia tunahimiza mikoa ambayo haijafanya uchaguzi ifanye chaguzi mapema. Mikoa hiyo ni: Dar es salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Rukwa, Arusha, Geita, Simiyu, Njombe, Katavi na Mbeya.
Katika chaguzi hizo kuna baadhi nafasi zote hazikujazwa ni matumaini yetu kuwa zitajazwa katika mikutano ijayo ya vyama husika.
Pia
nichukue nafasi hii kuwahamasisha kina mama wengi wenye sifa kujitokeza
kugombea nafasi mbalimbali katika vyama vya mikoa na taifa pale
uchaguzi utakapoitishwa.
Mashindano
Mashindano mbalimbali ndio moyo wa mpira wa miguu bila mashindano hakuna anayeweza kutambua ubora na kiwango chakena pia ni kipimo cha maendeleo.
Kutakuwa na mashindano mbalimbali katika ngazi ya mikoa,taifa na kimataifa.
Mashindano hayo pia yatahusisha shule za msingi na sekondari na
vyuo mbalimbali.Kwa kushirikiana na vyombo husika kutakuwa na
ufuatiliaji wa karibu wa michezo ya UMISSETA toka ngazi ya mkoa hadi
Taifa na kuwa na mpango endelevu wa kuwaendeleza wale wenye vipaji ambao
wamechaguliwa /wanaweza kuchaguliwa kwenye timu za taifa.
Ligi itachezwa katika ngazi za mikoa na baadaye kuunda kombaini ya mkoa itakayoshiriki mashindano ya taifa.
Kwa mwaka 2013 tunatengemea mikoa kuchezesha ligi isiyopungua timu tano kwa mikoa 15 itakuwa na timu 10 na timu itaruhusiwa kusajili wachezaji 25 kwa mwaka 2013 tunatengemea watoto/wasichana 3750
kushiriki katika mpira wa miguu. Idadi hii ukizidisha mara nne unapata
jumla ya wachezaji 15,000.Endapo tutakuwa na benki ya wachezaji hawa
tutaweza kuunda timu bora za umri tofauti na zenye kiwango cha juu.
Pia
mikoa inahimizwa kuanzisha mashindano mbalimbali yatakayoamsha ari kwa
watoto wa kike na wasichana kushiriki katika mpira wa miguu.
Uratibu wa mikoa
Wajumbe wa kamati ya utendaji pamoja na majukumu yao kama wajumbe watakuwa na jukumu la kuratibu shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu katika mikoa:Uratibu huo utakuwa kama ifuatavyo:
Rose Kissiwa
|
Makamu Mwenyekiti
|
Tabora, Dodoma, Rukwa, Kigoma, Pwani
|
Amina Karuma
|
Katibu
|
Lindi, Mtwara, Iringa, Njombe, Ruvuma
|
Zena Chande
|
Mjumbe
|
Dar es Salaam, Morogoro, Katavi, Shinyanga, Mbeya
|
Triphonia Temba
|
Mjumbe
|
Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Singida
|
Sophia Charles
|
Mjumbe
|
Mara, Kagera, Simiyu, Geita, Mwanza
|
Kwa mujibu wa katiba ya TWFA ibara ya 37 inatoa
nafasi kwa kamati ya utendaji kuunda kamati ndogo za kuendeleza mpira
wa miguu wanawake kamati hizo ni kamati ya Fedha na mipango,kamati ya
Ufundi,kamati ya ngingine itakayoonekana inafaa.Kamati ya utendaji kwa
pamoja ilikubaliana kuunda kamati ya habari na masoko.
Kamati ya Fedha na Mipango
1. Rose Kissiwa - Mwenyekiti
2. Evans Aveva
3. Sophia Tigalyoma
4. Sophia Mukama
5. Asha Baraka
Kamati ya Ufundi
1. Tryphonia Temba – Mwenyekiti
2. Florence Ambonisye
3. Miraji Fundi
4. Dr. Leonia Kaijage
5. Furaha Francis
6. Richard Muhotoli
Kamati ya Habari na Masoko
1. Zena Chande – Mwenyekiti
2. Beatrice Mgaya
3. Mohamed Mkangara
4. Florian Kaijage
5. Somoe Ng’itu
Masoko na Habari
Mpira
wa miguu wanawake hauna udhamini na pia vyanzo rasmi vya kupata
mapato.Kwa kupitia kamati ya habari na masoko ,tunaamini kutakuwa na
mikakakti mbalimbali ya kuelimisha ,kuhamasisha wadau na watanzania wote
kuwiwa na kujitoa kuendeleza mpira wa miguu .
Asanteni
Lina P.Kessy
Mwenyekiti Chama cha Mpira wa miguu wanawake
TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA NCHINI (TFF).
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
"TFF BADO YASISITIZA KUMUONA WAZIRI MUKANGARA"
RAIS
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga
amemshukuru Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela
Mukangara kwa kukubali ombi la Shirikisho la kutaka kukutana naye kwa
mazungumzo na kumsihi asitishe hatua anazodhamiria kuchukua hadi hapo
kikao hicho kitakapofanyika.
Waziri
Mukangara ameiagiza TFF kuitisha Mkutano Mkuu wa marekebisho ya katiba
ifikapo tarehe 15 Aprili 2013 na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi ifikapo tarehe
25 Mei 2013 na kwamba tamko la TFF kutekeleza maagizo hayo liwe
limetolewa katika muda wa siku tano zinazoishia Jumatatu (Machi 11,
2013).
Katika
barua pepe ambayo amemuandikia Waziri ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi,
Rais Tenga ameeleza kuwa alikwenda ofisini kwake tarehe 7 Machi 2013
kujaribu kumuona lakini akaambiwa amesafiri, hivyo kuomba kukutana na
Katibu Mkuu wa Wizara, ambaye pia hakuwepo ofisini na hatimaye akakutana
na Naibu Katibu Mkuu.
Katika
barua hiyo pepe, Rais Tenga ameeleza madhumuni ya kutaka kuonana na
Waziri Mukangara kuwa ni kwanza “kukushukuru kwa kukubali kuonana na
ujumbe wa TFF ulioongozwa na mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji, Bw. Alex
Mgongolwa, akiongozana na Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Angetile Osiah, jana
tarehe 6 Machi 2013.
“Kukushukuru kwa kukubali kukutana nasi tena siku ya tarehe 19 Machi, kwa ajili ya mazungumzo juu ya maagizo yako.
“Kukuarifu kuwa nimepokea maagizo yako uliyoyatoa jana kupitia kwa Mjumbe wetu wa Kamati ya Utendaji na kwa njia ya barua; na
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”
“Kwa heshima na taadhima, kukuomba usitishe hatua yoyote ile unayodhamiria kuchukua hadi hapo tutakapokutana na kupata maelezo yetu, TFF, juu ya maamuzi na maagizo uliyoyatoa.”
Tenga,
ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
la Afrika (CAF) aliondoka jana (Machi 7 mwaka huu) kwenda Marrakech,
Morocco kuhudhuria kikao cha kamati hiyo na pia Mkutano Mkuu wa CAF
ambao umepangwa kufanyika Machi 10 mwaka huu ukihusisha pia ajenda ya
uchaguzi wa rais.
Mwisho.
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
"KAIJAGE KOCHA MPYA TWIGA STARS"
ROGASIAN
Kaijage ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya mpira wa miguu
ya wanawake, Twiga Stars baada ya kocha wa zamani, Charles Boniface
Mkwasa kujiuzulu katikati ya mwaka jana.
Mkwasa,
ambaye alikuwa nyota wa Yanga na Taifa Stars, alijiengua kufundisha
timu hiyo aliyoiongoza kwa muda mrefu, baada ya Twiga Stars kuondolewa
katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza fainali za Afrika
kwa Wanawake (AWC) zilizofanyika nchini Equatorial Guinea.
Twiga
ilipata bao muhimu la ugenini jijini Addis Ababa ilipofungwa na wenyeji
wao Ethiopia mabao 2-1, lakini ikiwa na matumaini ya kutumia vyema bao
la ugenini ilijikuta ikilala bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa katika
mchezo wa marudiano na hivyo kukosa tiketi ya kurudi tena kwenye fainali
hizo.
Kaijage
ambaye kwa sasa anajihusisha na mradi wa vijana (grassroots) pamoja na
programu nyingine za kukuza vipaji zilizo chini ya TFF, aliteuliwa na
Kamati ya Ufundi ya TFF kufanya kazi hiyo na ameita kikosi cha Twiga
Stars kwa mazoezi ya siku kumi kuanzia Machi 10 hadi 23 mwaka huu Uwanja
wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Wachezaji
walioitwa ni Amina Ally (Lord Barden), Asha Rashid (Mburahati Queens),
Aziza Mwadini (Zanzibar), Esther Chabruma (Sayari), Esther Mayalla (TSC
Academy), Etoe Mlenzi (JKT), Evelyn Sekikubo (Mbarahati Queens), Fatuma
Bushiri (Simba Queens), Fatuma Mustafa (Sayari) na Fatuma Omari
(Sayari).
Flora
Kayanda (Tanzanite), Hamisa Athuman (Marsh Academy), Hellen Maduka
(Bujora), Hellen Peter (JKT), Irene Ndibalema (TSC Academy), Maimuna
Said (JKT), Mwajuma Abdallah (Tanzanite), Mwanaidi Tamba (Mburahati
Queens), Mwanahamis Omari (Mburahati Queens) na Mwapewa Mtumwa (Sayari).
Nabila
Ahmed (Marsh Academy), Nasiria Hashim (Zanzibar), Pulkeria Charaji
(Sayari), Rukia Khamis (Sayari), Semeni Abeid (Tanzanite), Sharida
Boniface (Makongo Sekondari), Sophia Mwasikili (Luleburgaz Gucu Spor,
Uturuki), Theresa Yona (TSC Academy), Vumilia Maarifa (Evergreen) na
Zena Khamis (Mburahati Queens).
Mwisho.
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
"YANGA, TOTO AFRICANS KUUMANA DAR"
MICHUANO
ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea
kesho (Machi 9 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo vinara Yanga watakuwa
wenyeji wa Toto Africans kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi
wa mechi hiyo namba 135 atakuwa Andrew Shamba kutoka Pwani akisaidiwa
na Abdallah Mkomwa na Abdallah Rashid pia wote kutoka Pwani. Kamishna ni
Salim Singano kutoka Tanga wakati Mtathmini wa waamuzi ni Alfred Lwiza.
Nayo
Polisi Morogoro itakuwa mgeni wa Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex
ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Azam katika mechi hiyo namba 136 na
nyingine mbili zinazofuata itakuwa bila kocha wake Steward John Hall
ambaye Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imemfungia mechi tatu.
Charles
Komba kutoka Dodoma ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 136
itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani.
Ligi
hiyo itaendelea tena keshokutwa (Machi 10 mwaka huu) ambapo Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam utashuhudia mechi kati ya Simba na Coastal Union ya
Tanga. Waamuzi wa mechi hiyo ni Martin Saanya akisaidiwa na Jesse
Erasmo na Vicent Mlabu wote kutoka Morogoro.
Mwisho.
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
"RHINO, KANEMBWA ZASAKA TIKETI VPL"
KINDUMBWENDUMBWE
cha Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kinaendelea kesho (Machi 9 mwaka huu)
katika makundi yote matatu, lakini macho na masikio ya washabiki wa
mpira wa miguu yakiwa kwenye mechi za Rhino Rangers ya Tabora na
Kanembwa JKT ya Kigoma.
Timu
hizo ndizo ziko katika nafasi nzuri ya kupata tiketi ya kucheza Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao kutoka kundi hilo la C. Tayari Mbeya
City ya Mbeya na Ashanti United ya Dar es Salaam zimeshapata tiketi za
kucheza VPL msimu ujao kutoka kundi A na B.
Rhino
Rangers itaikaribisha Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
mjini Tabora, wakati Kanembwa JKT itakuwa mgeni wa Pamba kwenye Uwanja
wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mechi
nyingine za kundi C ni Mwadui vs Polisi Tabora (Kambarage, Shinyanga),
na Morani vs Polisi Mara (Kiteto, Manyara). Mechi za kundi A ni Majimaji
vs JKT Mlale (Majimaji, Songea), Mkamba Rangers vs Mbeya City (Sokoine,
Mbeya) na Polisi Iringa vs Burkina Faso (Samora, Iringa).
Mshikeshike
ya kundi B ni Ndanda vs Ashanti United (Nangwanda Sijaona, Mtwara),
Villa Squad vs Green Warriors (Karume, Dar es Salaam), Polisi Dar vs
Transit Camp (Mabatini, Mlandizi) wakati Tessema na Moro United
zitacheza Machi 10 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Mwisho.
MABAO 191 na Kadi 163 zapatikana ligi ya wilaya ya Tanga.
Na Mwandishi Wetu,Tanga.
Katika hatua ya mchujo ya Ligi wilaya ya Tanga iliyoanza mwishoni mwa mwezi
septemba mwaka jana na kumalizika Januari 6 mwaka huu jumla ya mabao 191
yalifungwa na timu zilizokuwa zikishiriki ligi hiyo.
Katibu Msaidizi wa Chama cha soka wilaya ya Tanga (TDFA) Salim Carlos
alisema kuwa mabao hayo yalitokana na michezo 64 iliyochezwa kwenye hatua hiyo
ambayo ilikuwa ikishirikisha timu 41 ambazo zilikuwa zimegawanywa kwenye
makundi kumi.
Carlos alisema baada ya kumalizika hatua hiyo kila kundi tiyari limekwisha
kutoa washindi wawili ambao wanaendelea na ligi hiyo katika msimu mpya wa mwaka
2012-2013.
Alisema pia katika hatua hiyo jumla ya kadi zipatazo163 ambapo kati ya hizo
kadi za njano zilikuwa ni 143 wakati kadi nyekundu zilikuwa 20 na timu iliyoongoza kupewa kadi nyingi za njano
ni Raidon ambapo timu hiyo ilipewa kadi 8.
Aidha alisema katika hatua hiyo wachezaji Hussein Salim wa timu ya Donge Fc
Rubein Desideri na wa Younga Rovers waliongoza kwa kufunga mabao ambapo kila
mmoja alifunga mabao 15.
Akizungumzia changamoto ambazo zilijiotokeza katika hatua hiyo, Katibu huyo
alisema uhaba wa fedha za uendeshaji ni moja kati ya vitu ambavyo vilijitokeza
hali iliyopelekea kushindwa kuwalipa waamuzi na pesa za kulipia uwanja kwa
wakati.
Katibu huyo aliwataka wadau mbalimbali wa soka mkoani hapa kukisaidia chama
hicho ili kiweze kufanikisha ligi yao
msimu huu kwani wamedhamiria kuinua kiwango cha soka wilayani hapa.
Mwisho.
|
TIMU 13 kushiriki ligi ya Mkoa wa Tanga"
Na Mwandishi Wetu, Tanga.
JUMLA ya timu 13 zimefunzu kucheza Ligi ya Mkoa wa Tanga mzunguko wa pili
baada ya kufanya vizuri mzunguko wa kwanza na itachezwa kwa mfumo wa nyumbani
na ugenini.
Akizungumza na Blogi hii Katibu wa chama cha soka Mkoa wa Tanga (TRFA), Beatrice
Mgaya alisema maandalizi ya hatua hiyo yamekamilika na mzunguko huo utaanza
Machi 9 mwaka huu.
Mgaya alisema katika ufunguzi wa mzunguko huo, timu za soka Lushoto
Shooting na Korogwe United zinatarajiwa kuonyeshana kazi katika uwanja wa soka
Lushoto na unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa.
Alisema mchezo mwengine utakaochezwa siku hiyo utafanyika
kwenye uwanja wa Mkwakwani ambapo timu ya maafande wa jeshi la magereza
mkoani hapa Small
Prison watakapoikabili Viva Dynamo ya Maramba wilayani Mkinga.
Katibu huyo alizitaka timu zinazoshiriki ligi hiyo kuonyesha nidhamu ya
hali ya juu ili kuweza kuleta ushindani pamoja na kuziasa zifanye maandalizi ya
kutosha kabla ya mechi zao.
Mgaya alizitaja timu zinazoshiriki kuwa ni Lushoto Shooting, Korogwe
United,Halmashauri Fc,Lushoto Star,Small Prison,Viva Dynamo, ,Veteran FC,Monga
Star,African Sports,Black Burn,Eagle Rangers na Moa Original na Makorora Star.
Timu hizo zitachukuana ili kuweza
kupatikana bingwa wa mkoa katika msimu huu ambapo ataweza kushiriki mashindano
ya mabingwa wa mikoa itakayochezwa baada ya kumalizika ligi za mikoa.
Mwisho.
Na Mwandishi Wetu,Handeni
LIGI ya soka kuwania kombe la Diwani kata ya Kwamgwe wilayani hapa,juzi ilifikia tamati kwa mchezo kati ya Bondo United na Mungano FC ambapo matokeo ya mchezo huo Bondo ilitwaa ubingwa kwa njia ya penati kwa kuwanyuka wapinzani wao kwa 3 - 0.
Katika mchezo huo wa fainali uliofanyika uwanja wa Kwedigongo hadi muda wa kawaida unamaizika hakuna mbabe ambapo mwamuzi wa mchezo huo Mohamed Chombo aliongeza muda wa nyongeza dk 15 ambazo pia hazikutoa mshindi hadi hatua ya penati.
Waliofanikiwa kuzikwamisha wavuni penati za Bondo ni Charles Ernest,Hemed Athumani na Hamisi Mohamed wakati ile ya Muungano ilifungwa na mchezaji Enock Juma matokeo ambayo yaliifanya Bondo United kuwa bingwa baada ya penati tano tano kupigwa.
Bingwa wa ligi hiyo ambayo hufanyika kila mwaka aliweza kuzawadiwa kikombe,jezi seti moja na Tsh 100,000, wakati mshindi wa pili timu ya Muungano ilizawadiwa Tsh 70,000 na mshindi wa tatu Tsh 50,000 ambazo zilikwenda jkwa klabu ya soka ya Mbogoni FC.
Mratibu wa mashindano hayo ambaye ni diwani wa kata ya Kwamgwe Sharrifa Abebe akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika alisema,amefurahishwa na wachezaji pamoja na mashabiki wa timu zilizoshiriki kuzingatia suala la nidhamu mchezoni.
Alisema mashindano hayo yameweza kutoa timu ya kata ainayoundwa na wachezaji wapatao 40 ambao watakuwa chini ya mwalimu wao msaidizi aliyemtaja kwa jina la Hamza Manulanula huku jitihada za kumtafuta kocha mkuu zikiendelea kufanywa.
"Nimefurahi ligi kumalizika kwa amani na sasa tunaangalia suala la timu yetu ya kata,mwalimu msaidizi amepatikana...mimi na wafadhili wengine tunasaka kocha mkuu ili kuwanoa vyema vijana wetu,tutakuwa na mechi nyingi za majaribio"alisema Sharrifa.
Alisema,lengo la kuanzishwa ligi hiyo ni kukuza vipaji sanjari na kutengeneza ajira kwa vijana huku akibainisha kuwa kupitia ichezi pia vijana itawasaidia kuepukana na mazingira ambayo yanaweza kuwatumbukiza katika vitendo hatarishi na kuharibu maisha yao.
Mwisho.
Subscribe to:
Posts (Atom)